|
MAANA YA
FIQ-HI KATIKA LUGHA NA SHERIA
Fiq-hi ni neno la kiarabu
lenye maana mbili. Maana ya kwanza ni ya kilugha na ya pili ni ya
kisheria. Katika lugha ya kiarabu neno "fiq-hi" maana yake ni
kufahamu na kujua.
Fiq-hi kwa mtazamo wa sheria ni
fani ya elimu inyoshughulikia na kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni
na na taratibu za Uislamu katika maisha ya kila siku kwa ujumla fiq-hi ni
sheria zinazoyatawala maisha ya Muislamu katika nyanja zote za maisha,
kuanzia elimu, ibada, uchumi, ulinzi na usalama, ndoa, mirathi na
kadhalika.
MISINGI YA
FIQ-HI
Misingi ya fiq-hi ni chimbuko
la elimu hii yaani mahala ambamo elimu hii imechukuliwa. Elimu ya fiq-hi
imejiegemeza katika misingi mikuu minne kama ifuatavyo:
Qur-ani
Hadithi(sunnah)
Ijmaa,na
Qiyaasi
Hii ndio misingi na tegemeo la
elimu hii ya fiq-hi.
Maana ya kila msingi
QUR-ANI
Qur-ani Tukufu ni kitabu
kilichokusanya maneno matukufu ya Mwenyezi Mungu alichoshushiwa Mtume wa
mwisho, Nabii Muhammad kupitia kwa Malaika Jibril ili kiwe ni sheria na
muongozo kwa wanadamu wote.
HADITH(SUNNAH)
Hadithi (sunnah) ni tafsiri
sahihi na ufafanuzi kamili wa Qur-ani Tukufu uliotolewa na Bwana Mtume kwa
njia ya vitendo, maneno na "Iqraari"."Iqraari" ni
kitendo cha Bwana Mtume kumuona mtu akitenda jambo fulani, kisha Mtume
asitoe maelekezo yoyote ya kukemea au kukataza. Ukimya huu wa Mtume
hutafsirika kuwa jambo lile linafaa kwani Mtume hawezi kulinyamazia jambo
baya.
IJMAA
Ijmaa ni kongamano na
makubaliano ya wanazuoni wa kiislamu baada ya kuja Mtume juu ya jambo au
suala ambalo halikuelezwa kwa uwazi ndani ya Qur-ani au hadithi
QIYAASI
Qiyaasi ni mizani ya kulipima
jambo au suala ambalo halina ufafanuzi ndani ya Qur-ani au hadithi na
jambo au suala lililotajwa ndani ya Qur-ani au Hadith, kwa kulingana
sababu.
Kwa ufupi hizi ndizo maana
nyepesi na za awali za misingi hii minne ambayo ndio chimbuko la elimu hii
ya sheria ya Kiislamu, elimu ya fiq-hi.
FAIDA YA
FIQ-HI
Umuhimu na faida itokanayo na
elimu hii ya fiq-hi unajidhihirisha katika maisha ya kila siku ya
Muislamu, jamii na ummah mzima wa Kiislamu. Fiq-hi humsaidia Muislamu
kujua:-
- Maamrisho ya Mola wake,
akayafuata ikawa ni sababu ya kupatia mafanikio ya Duniani na Akhera.
- Makatazo ya Mola wake,
akayaepuka ikawa pia ndio sababu ya kusalimika na maafa ya Duniani na
Akhera.
- Namna ya kutekeleza lengo la
kuumbwa kwake ambalo ni ibada. Vipi na jinsi gani atamuabudu Muumba
wake katika maisha yake yote.
- Uhusiano wake na Mola wake,
uhusiano wake na wanadamu wenziwe, uhusiano wa taifa na taifa jingine.
- Halali na haramu. Fiq-hi ndio
humbainishia ni lipi halali kutenda, kusema au kula na ni lipi haramu
kutenda, kusema au kula.
- Hukumu za makosa mbalimbali.
Fiq-hi humuongoza Muislamu kutoa hukumu na adabu za makosa mbalimbali
kuanzia yale madogo mpaka ya jinai.
Hizi ni baadhi ya faida
zipatikanazo katika fani hii ya fiq-hi, kwa kuziangalia na kuzizingatia
utaona na kufahamu kuwa Uislamu hauwezi kutekelezeka bila ya kuwa na elimu
hii na hapo ndipo unapoonekana umuhimu wa fiq-hi.
HUKUMU YA
SHERIA KATIKA FIQ-HI
Baada ya kuona faida na
umuhimu wa fiq-hi hatuna budi kujua hukumu ya sheria katika elimu hii.
Kila elimu katika Uislamu ina hukumu yake, elimu ya uchawi kwa mfano ni
haramu kujifunza, elimu ya udaktari ni fardhi ya kutoshelezeana ndani ya
mji, kama hakuna mwenye elimu hiyo ndani ya mji mzima basi wakazi wote wa
mji ule huwa na madhambi.
Elimu ya fiq-hi ni fardhi kwa
muislamu kujifunza kwani kwa kupitia elimu ndiyo huweza kutekeleza
maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Lakini ufaradhi huu unatofautiana baina ya
mtu na mtu. Kwa mwengine huwa ni fardhi ya lazima kujua vipengele fulani
na kwa mwengine huwa ni fardhi kifaaya.
FARADHI YA
LAZIMA:
Kujifunza, kuijua na kutumia
elimu hii ya fiq-hi inakuwa ni faradhi ya lazima kwa kila Muislamu
mwanamume na mwanamke katika mambo ya ibada ya kila siku, kwa mfano sala
na funga. Kujua kutoa zaka, au kujua jinsi ya kuhiji wakati hana uwezo si
fardhi ya lazima bali ni faradhi kifaaya, ama kwa mwenye uwezo ni fardhi
ya lazima kujua elimu hizo.
Kwa mantiki hiyo hiyo, mwenye
kufanya biashara ni fardhi ya lazima kujua vipengele vya kufanya biashara
ndani ya fiq-hi ili biashara yake iwe kwa mujibu wa sheria ya kiislamu, na
kama hajafanya hivyo atakuwa na makosa mawili, kosa la kwanza ni
kutojifunza hukmu ya uislamu ndani ya kazi yake na kosa la pili ni
kutokufanya biashara yake kwa mujibu wa sheria kwa hivyo fahamu.
FARADHI
YA KUTOSHELEZEANA
Elimu hii inakuwa ni faradhi
ya kutoshelezeana katika masuala ya mirathi, elimu ya ukadhi, elimu ya
kutoa fat-wa na elimu nyingine zinazofanana na hizo. Sasa ikiwa ndani ya
mji hakuna anayejua masuala ya mirathi, wakazi wote huwa na madhambi kwa
kutojifunza elimu hiyo.
Huu ndio mgawanyo wa hukumu ya
sheria kuhusiana na fani hii ya elimu ya fiq-hi.
HUKUMU
ZA SHERIA YA KIISLAMU
Jambo lolote lile katika
maisha ya kila siku ya Muislamu linaangukia kwa mujibu na mtazamo wa
sheria katika mafungu yafuatayo ya hukumu:-
Faradhi/Wajibu
Sunnah
Haramu
Mubah
Makuruuh
Hizi ndizo hukumu tano
zinazoitawala sheria ya kiislamu, na ifuatayo ni maana na ufafanuzi mdogo
wa kila hukumu:-
FARADHI/WAJIBU
Faradhi au Wajibu ni jambo
ambalo mtu baleghe, mwenye akili timamu amelazimishwa na sheria kulitenda.
Mtu mwenye sifa hizo tulizozitaja akilitenda la faradhi kama vile swala,
funga n.k. kwa kumtii Mola wake hupata thawabu na akiacha kutenda bila ya
udhuru wowote unakubalika kisheria anastahiki kupata dhambi na adhabu ya
Mola.
SUNNAH
Sunna kwa mtazamo wa fiq-hi
ni kinyume cha faradhi. Kwa hivyo basi sunnah ni jambo ambalo sheria
haikumlazimisha mtu kulitenda bali imempa khiyari kutenda au kutotenda.
Mfano wa sunnah ni kama vile kuanza kutoa salamu, kuwapa sadaka masikini,
kufunga Al-khamisi na Jumatatu na kadhalika. Atakayelitenda jambo la
sunnah atalipwa thawabu na atakayeacha hatopata dhambi wala kuadhibiwa.
HARAMU
Haramu ni kila jambo ambalo
sheria imekataza kabisa kulitenda kama vile kuiba, kusema uwongo, kunywa
pombe na kadhalika. Mtu aliye baleghe na mwenye akili timamu akilitenda
lililoharimishwa kwa kuvunja amri ya Mola atastahiki kupata dhambi na
adhabu na akiacha kutenda haramu kwa kufuata amri ya Mola atapata thawabu.
MUBAAH
Mubaah ni jambo ambalo sheria
haikulazimisha mtu kulitenda na wala haikumkataza kulitenda. Mfano wa
mubaah ni kama vile kuvaa nguo nzuri mno au kula vyakula vizuri vizuri.
Hapana thawabu wala dhambi ndani yake.
UZINDUSHI:
Mtu akitenda jambo la Mubaah
kama vile kula na akatia nia ya kupata nguvu ya kufanya ibada, atapata
thawabu na kinyume chake akinuia kwa jambo hilo hilo la Mubaah kumuasi
Mwenyezi Mungu basi atapata dhambi.
MAKURUUH:
Makuruuh ni kila jambo ambalo
linachukiza kulitenda kwa mtazamo wa sheria. Hastahiki mtu kupata adhabu
ya Mola kwa kulitenda bali akiacha atapata thawabu.
|