Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

X) YALIYO HARAMU KWA ASIYE NA UDHU

 

Ni haramu kisheria kwa mtu asiyekuwa na udhu kufanya mambo yafuatayo : -

  1. Kuswali swala yeyote ile iwayo; ya faradhi, ya suna, au swala ya maiti, au sijida ya kusoma Qur-ani au sijda ya shukrani. Haya yote yametegemezwa kwenye kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu : "ENYI MLIOAMINI ! MNAPOTAKA KUSWALI, BASI OSHENI NYUSO ZENU, …" [5:6]. Na kwa kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – "Mwenyezi Mungu haikubali swala ya mmoja wenu atakapohuduthi mpaka atawadhe (tena)" Bukhaariy. Na kwa hadithi nyingine "Hana swala mtu asiyekuwa na udhu". Na kwa sababu twahara ya hadathi ni sharti miongoni mwa sharti za kusihi swala, haitosihi swala ila kwa kupatikana twahara ambayo ni udhu.
  2. Kutufu/kuizunguka Al-Kaaba Tukufu, twawafu ya fardhi au ya sunna kwa sababu twawafu ni swala. Hii ni kwa dalili ya riwaya iliyopokelewa na Imam Tirmidhiy katika kitabu chake cha hadithi (SUNAN TIRMIDHIY) kutoka kwa Ibn Abbaas –Allah awawie radhi – kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu –Rehema na Amani zimshukie – amesema : "Twawafu ni swala isipokuwa kwamba Allah mtukufu amehalalisha kuzungumza ndani yake. Basi yeyote atakayezungumza asizungumze ila lile la kheri".
  3. Kuugusa msahafu wote au baadhi yake. Hili ni kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu : "HAPANA AKIGUSAYE ILA WALIOTAKASWA" [56:79]. Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – anatufasiria kauli hii ya Mola Mtukufu anasema : "Asiiguse Qur-ani ila aliye twahara" Na kwa sababu kuitukuza Qur-ani Tukufu ni wajibu miongoni mwa kuitukuza ni muislamu kuigusa il-hali ya twahara. Wamekongomana na kuwafikiana wanazuoni wa fani hii ya fiq-hi kwamba INAJUZU kwa mtu asiyekuwa na udhu kuisoma Qur-ani Tukufu bila ya KUIGUSA. Kama alivoruhusiwa mtoto mdogo kuigusa bila ya udhu kwa lengo la kujifunza, kwa kuwa yeye si MTU MUKALLAF (anayelazimiwa na hukumu za sheria). Pamoja na rukhsa hii bado ni bora azoweshwe kuigusa Qur-ani Tukufu akiwa na udhu ili kuipandikiza heshima na utukufu wa Qur-ani ndani ya moyo twahara wa chipukizi huyu. Akuwe akitofautisha Qur-ani na vitabu vingine.

xi) HALI AMBAZO UDHU HUSUNIWA NDANI YAKE :

Imesuniwa kutawadha katika hali nyingi, miongoni mwa hali ambazo muislamu amesuniwa atawadhe:

  1. Wakati wa kumdhukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwani Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – alikuwa akipenda kumdhukuru Mola wake katika hali ya twahara. Ni bora ikafahamika kwamba Bwana Mtume alikuwa akimdhukuru Mola wake katika hali zote, akiwa amekaa au amesimama, akiwa ana udhu au hana, akiifanyia kazi kauli ya Mola : "NA LIKUMBUKE (litaje) JINA LA MOLA WAKO ASUBUHI NA JIONI" [76:25]. Udhu ni silaha ya muumini, kwa hivyo ni vema saa zote akawa anatembea na silaha yake hiyo, khasa khasa wakati wa kumdhukuru Mola wake.
  2. Wakati wa kulala. Zimepokelewa hadithi nyingi zinazoeleza ubora wa mtu kulala akiwa na udhu. Miongoni mwa hadithi hizo ni hii iliyopokelewa na Albaraai bin Aazib – Allah amuwie radhi – amesema : Aliniambia Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – "Unapokiendea kitanda chako (unapotaka kulala) tawadha udhu wako wa swala, kisha ulalie upande wa kulia, halafu useme : ALLAHUMMA INNIY ASLAMTU NAFSIY ILAYKA, WAWAJJAHTU WAJ-HIY ILAYKA, WAFAWWADHTU AMRIY ILAYKA, WA ALJA-TU DHWAHRIY ILAYKA RAGHBATAN WA RAHBATAN ILAYKA, LAA MALJAA WALAA MANJAA MINKA ILLAA ILAYKA. ALLAHUMMA AAMANTU BIKITABIKAL-LADHIY ANZALTA, WABINABIYYIKAL-LADHIY ARSALTA" Bukhariy.
  3. Ni sunna kutawadha kwa mtu aliye na janaba anapotaka kula, kunywa au kulala. Imepokelewa kutoka kwa Ammaar bin Yaasir –Allah amuwie radhi – kwamba Mtume – Rehema na Amani zimshukie – amemruhusu mwenye janaba anapotaka kula, kunywa au kulala atawadhe udhu wake wa swala (ndipo ayafanye hayo yaliyotajwa)" Tirmidhiy. Hii ni iwapo haikumwepesikia kuoga mapema, na ikiwa ni wepesi, basi ni bora akaharakia kuoga, ZINGATIA.
  4. Imesuniwa kutia udhu kabla ya kukoga josho la janaba. Imepokewa kutoka kwa Bi Aysha – Allah amuwie Radhi – amesema : Alikuwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – anapotaka kukoga, huanza kwa kuosha mikono (vitanga) vyake, halafu humimina maji kwa mkono wake wa kulia na huukosha utupu wake kwa mkono wa kushoto. Halafu hutawadha udhu wake wa swala, kisha ndipo hukoga baada yake" Bukhaariy na Muslim.
  5. Wakati wa kumbeba maiti. Imepokelewa katika hadithi tukufu : "Mwenye kumuosha maiti na mwenye kumbeba (pia) akoge"
  6. Wakati mtu aghadhibikapo sana, ni suna akatawadhe kwa sababu udhu husaidia kuzima mfumuko na mchemko wa ghadhabu na humrejesha mtu kwenye hali ya utulivu. Imepokelewa kutoka kwa Atwiyah Al-aufaa kwamba Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – amesema : "Bila ya shaka ghadhabu hutokana na shetani, na huyo shetani amuembwa na moto na hakika si vinginevyo moto huzimwa na maji. Basi ashikwapo na ghadhabu mmoja wenu na akatawadhe" Abuu Dawoud.
  7. Ni suna kujadidi udhu (kutawadha udhu juu ya udhu) kwa kila swala. Tunasoma katika hadithi tukufu : "Lau si kuwaonea taabu umati wangu ningaliwaamrisha kutawadha kwa kila swala na kupiga mswaki kwa kila udhu". Ilikuwa ni ada ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kutawadha kwa kila swala na baadhi ya nyakati akiswali zaidi ya swala moja; yaani swala nyingi kwa udhu mmoja, yaani ule ule maadam haujatenguka.

xii) UDHU WA MWENYE UDHURU

Tunakusudia kusema kwa istilahi (wenye udhuru) wale watu ambao ambao wana maradhi yanayowafanya wasiweze kuuhifadhi udhu wao kama wanavyoweza watu wengine katika hali ya kawaida. Hawa ni pamoja na mtu mwenye maradhi ya mchuchuro wa mkojo, hawezi kuuzuia mkojo, saa zote hutokwa na mkojo au anatokwa na upepo (ushuzi) mara kwa mara. Au mwanamke aliyepatwa na maradhi ya kutokwa na damu ya mbobo/ugonjwa, hii ni damu itokayo kwa wingi katika wakati usiokuwa wa damu ya ada ya kila mwezi (hedhi). Hukumu ya udhu wa watu hawa ni kwamba wanatakiwa watawadhe kila unapoingia wakati wa kila swala, wasitawadhe kabla ya kuingia wakati kwa kuwa wanatakiwa kufululiza baina ya udhu na swala. Hii ni kwa sababu kisheria hawana udhu kwani wana hadathi ya kudumu na udhu wao ni wa ruhusa maalum waliyopewa na sheria ili waweze kuyatekeleza yale yote yasiyotekelezeka bila ya udhu, kama vile swala, tawafu na kadhalika. Wataswali kwa udhu huo swala wazitakazo za suna au za fardhi. Udhu wa watu hawa utabatilika na kutenguka mara tu unapoingia wakati wa swala nyingine. Akitaka kuswali basi itamlazimu kutawadha tena. Haya yote yanaonyesha wepesi wa sheria ya Kiislamu ambayo imejengwa juu ya misingi ya wepesi na kuondosha uzito na ugumu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu : "WALA HAKUWEKA JUU YENU MAMBO MAZITO KATIKA DINI. (Nayo dini hii) NI MILA YA BABA YENU IBRAHIMU …" [22:78].

 



Forum | Guestbook | Tuandikie |