|
Mtu akipatwa na janaba kwa maana ya janaba kama tulivyoeleza katika maelezo yetu
ya awali yanamuharimikia kwa mujibu wa sheria mambo yafuatayo:-
- Kuswali swala ya fardhi au ya sunnah. Hili ni kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu: "ENYI MLIOAMINI! MSIKARIBIE SWALA, HALI MMELEWA MPAKA MYAJUE MNAYOSEMA WALA
HALI MNA JANABA ISIPOKUWA MMO SAFARINI (mnapita njia) MPAKA MKOGE
" [4:43]
Muradi na makusudio ya neno SWALA katika aya hii ni MAHALA PA KUSWALIA (msikiti)
kwa sababu kupita njia hakupatikani ndani ya swala. Ikiwa mwenye janaba anakatazwa kupita
msikitini, basi kukatazwa kuswali ni aula zaidi.
Amepokea Imam Muslim kutoka kwa Ibn Umar- Allah awawiye radhi- amesema : Hakika
nimemsikia Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie- akisema "Haikubaliwi
swala bila ya twahara".
Twahara iliyotajwa katika hadithi ni pamoja na twahara ya hadathi ndogo na janaba
(hadathi kubwa). Hadathi hii inafahamisha uharamu wa kuswali kwa mwenye hadathi zote hizo;
hadathi ndogo na hadathi kubwa(janaba).
- Kukaa msikitini. Ama kupita njia tu bila ya kukaa si haramu. Haya yanafahamika
kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu : "
WALA HALI MNA JANABA,
ISIPOKUWA MMO SAFARANI(mnapita njia)
". Yaani msiikurubie swala wala mahala pa
kuswali (msikiti) mtakapokuwa mna janaba bila kukurubia kwa nia ya kupita njia, huku
hakukukatazwa. Naye Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Msikiti si halali kwa mwenye
hedhi wala mwenye janaba". Abu Daawoud
- Kutufu Al-Kaaba , twawafu ya nguzo/fardhi au ya sunna. Hii ni kwa sababu twawafu
iko katika daraja ya swala, kwa hiyo nayo imeshurutizwa twahara kama ilivyo kwa swala.
Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie- aliposema:
"Kutufu al-Kaaba ni swala, isipokuwa kwamba Allah amekuhalalishieni kuzungumza ndani
yake (twawafu), basi atakayazungumza na asizungumze ila la kheri". Al-Hakim
- Kusoma Qur-ani. Amesema Nabii Muhammad Rehema na Amani zimshukie: "Asisome
mwenye hedhi wala mwenye janaba chochote katika Qur-ani". Tirmidhiy
ANGALIA: Inajuzu kwa mwenye janaba kuisoma Qura-ani moyoni bila ya kuitamka kwa
ulimi, kama ambavyo inavyomjuzia kuutazama Msahafu bila kuushika. Kadhalika inamjuzia
kusoma dhikri/nyiradi za Qur-ani kwa kukusudia ile dhikri na sio Qur-ani yenyewe. Dhikri
ya Qur-ani ni kama vile mtu kusema:
(RABBANAA AATINAA FID-DUN-YAA HASANATAN WAFIL AAKHIRATI HASANATAN WAQINAA
ADHAABAN-NAAR)[2:201] kwa kuikusdua aya hii kama dua. Na kama vile kusoma
anapokipanda kipando (chombo cha usafiri)
("SUB-HANNAL-LADHIY SAKHARA LANNA HAADHA WA MAA KUNNAA LAHU MUQRINIYN")
[43:13] kwa kuisudia hii dua na sio dhati ya Qur-ani yenyewe. Allah ndiye mjuzi mno.
- Kuugusa au kuubeba /kuuchukua msahafu au karatasi/kataa la msahafu au ngozi/jalada
lake au kuuchukua msahafu ukiwa ndani ya mfuko au sanduku. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"HAPANA AKIGUSAYE ILA WALE WALIOTAKASWA" [56:79]
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie- anatufasiria aya hiyo kwa kusema :
"Asiiguse Qur-ani ila aliye twahara ". Daaruqutuniy na Maalik.
ANGALIA: Inajuzu kwa mwenye janaba kuubeba msahafu ukiwa pamoja na mizigo au ndani
ya nguo sandukuni na wala hakuukusudia kuubeba ule msahafu bali mizigo/nguo. Kadhalika
inamjuzia kuvichukua vitabu vya tafsiri ya Qur-ani iwapo ile tafsiri ni nyingi kuliko
Qur-ani. Allah ndiye mjuzi mno wa lililo la sawa na haki.
ii) HEDHI
A/. MAANA YA HEDHI
Hedhi katika lugha ya kiarabu, maana yake ni KUCHURIZIKA. Ama hedhi kwa mtazamo wa
sheria ni DAMU YA MAUMBILE yaani damu hii ni sehemu/ni katika jumla ya maumbile ya
mwanamke, mwanamke kaumbwa hivyo kwa lengo maalum. Damu hii kutoka ndani kabisa ya tumbo
la uzazi kila mwezi baada ya mwanamke kutimiza kwa uchache umri wa miaka tisa
B/. DALILIYAKE
Dalili na ushahidi juu ya kuwa hadhi huwajibisha josho la kisheria ni Qur-ani
Tukufu na sunnah(hadithi). Ama katika Qur-ani ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu :
"NA WANAKUULIZA JUU YA HEDHI , WAAMBIE HUO NI UCHAFU. BASI JITENGENI NA WANAWAKE
WAKATI WA HEDHI (zao). WALA MSIWAKARIBIE MPAKA WATWAHARIKE. WAKISHATWAHARIKA BASI
WAENDEENI KATIKA PALE ALIPOKUAMRISHENI ALLAH
"[2.222]
Ama dalili yake katika sunnah ni kauli ya Bwana Mtume Rehema na Amani
zimshukie kumwambia Fatmah Bint Abiy Hubayshi Allah amuwiye radhi-: "Itapokujia hedhi
, basi acha kuswali na itakapomalizika (kutoka) basi ikoshe damu (twaharisha) na
uswali" Bukhaariy na Muslim.
B/. MUDA WA HEDHI
TunAkusudia kwa ibara (Muda wa hedhi) kile kipindi ambacho mwanamke hutumika yaani
huwamo hedhini. Kipindi hiki tunaweza kukigawa katika sehemu tatu,kama ifuatavyo:-
- Kipindi kifupi;
- Kipindi kirefu na
- Kipindi cha ghalibu (ada)
KIPINDI KIFUPI Hii ndio muda wa chini kabisa wa kutoka damu ya hedhi hiki
ni kipindi cha masaa ishirini na nne (24). Hii inaamaanisha kuwa mwanamke anaweza kuingia
hedhini mchana na usiku wake tu, kisha damu ikakatika
KIPINDI KIREFU-Huu ndio muda wa juu kabisa wa kutoka damu ya hedhi. Hiki ni
kipindi cha siku kumi na tano (15), mchana na usiku
KIPINDI CHA GHALIBU- Huu ndio muda wa ada na desturi kwa wanawake walio wengi,
yaani wanawake wengi hutumika katika kipindi hiki. Huu ni muda wa siku sita au saba
Muda wa chini wa twahara, yaani kipindi cha chini ambacho mwanamke anakuwa katika
twahara ni siku kumi na tano(15). Hakuna ukomo (limit) wa wingi wa twahara kwani
inawezakana kabisa mwanamke asipate hedhi kwa muda wa mwaka, miaka miwili au miaka kadhaa
na hili limethibiti kwa majaribio
Mwanamke atakapoiona damu chini ya kipindi kifupi cha hedhi yaani chini ya masaa
ishirini na nne au aliiona damu baada ya kule kipindi kirefu cha hedhi, yaani baada ya
siku kumi na tano, damu hii itazingatiwa kisheria kuwa ni damu ya ISTIHAADHA na sio damu
ya hedhi
C/. NINI ISTIHAADHA?
Istihaadha ni damu ya ugonjwa damu hii hutoka katika mshipa ulio ndani kabisa ya
tumbo la uzazi. Damu hii hutengua udhu lakini haiwajibishi josho kama ilivyo kwa damu ya
hedhi. Kadhalika damu hii haitoi fursa ya kuacha kuswali na kufunga. Mwanamke mwenye
maradhi haya ya Istihaadha anatakiwa aioshe damu na afunge utepe mahala itokapo, kisha
atawadha na halafu aswali. Imepokelewa riwaya kutoka kwa Fatmah Bint Abiy Hubaysh
Allah amuwiye radhi kwamba yeye alikuwa akitokwa na istihaadha. Bwana Mtume
Rehema na Amani zimshukiae- akamwambia: "Ikiwa ni damu ya hedhi, basi itakuwa
ni damu nyeusi ijulikanayo. Itakapokuwa hivyo, basi acha kuswali, ikiwa ni nyingine basi
tawadha na uswali, hakika si vingenevyo huo ni mshipa ". Abu Daawoud.
D/. MAMBO YALIYO HARAMU KWA MWENYE HEDHI
- Kuswali- kwa ushahidi wa hadithi hiyo ya Fatmah Bint Abiy Hubaysh tuliyoitaja hapo
katika Istihaadha.
- Kusoma Qur-ani na kugusa na kuuchukua msahafu kwa ushahidi tulioutaja katika yakiyo
haramu kwa mwenye janaba (namba 4 na 5)
- Kukaa msikitini si kupita njia kwa ushahidi uliotajwa katika yaharamikayo kwa
mwenye janaba (namba 2). Miongoni mwa dalili zinazoonyesha kuwa nafsi ya kupita
hakukuharamishwa, mbali na ushahidi uliopita ni hii riwaya iliyopokelewa na Imam Muslim
kutoka kwa Bi: Aysha Allah amuwiye radhi- amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-aliniambia: "Niletee mswala msikitini" Nikamwambia: Mimi nimo
hedhini.akaniambia. "Bila shaka hedhi yako hiyo hunayo mkono mwako ".
- Kutufu Al-Kaaba kwa ushahidi uliopita katika yaliyoharamishwa kwa mwenye janaba
(namba 3). Imepolewa na Bi Aysha-Allah amwiye radhi amesema :Tulitoka hali ya
hatujidhani ila ni wenye kuhirimia hija, tulipofika sehemu iitwayo sarafu nikaanza kutokwa
na hedhi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie- akaingia kwangu na il-hali nikilia
akaniuliza: "Una nini, umeigia hedhini?" nikamjibu: Naam. Akaniambia : Hakika
hili ni jambo ambalo Mwenyezi Mungu amewaandikia (amewafaradhishiya) mabinti wa Adam
(wanawake). Fanya/tekeleza ibada azifanyazo hujaji isipokuwa usifanye twawafu katika
al-kaaba". Na katika riwaya nyingine "mpaka utwahirike".
- Kupita msikitini kwa sababu damu ni najisi na ni haramu kuuchafua msikiti kwa
najisi na uchafu mwingineo. Ikiwa mwanamke atajiaminisha kutokuuchafua msikiti, basi
anaweza kukatiza na kupita msikitini
- Kufunga, haijuzu kwa mwenye hedhi kufunga swaumu ya fardhi au ya suna, haya ni kwa
mujibu wa riwaya ya Abiya Said-Allah amuwiye radhi. Kwamba Mtume wa Mwenyezi Allah
Rehema na Amani zimshukie alisema kuhusiana na mwanamke wakati alipoulizwa
juu ya maana ya upungufu wa dini yake (mwanamke): "Je, hakuwa aingapo hedhini,
haswali na hafungi?". Bukhariy na Muslim
Atakidhi/atalipa mwenye hedhi swaumu iliyomfutu katika kipindi cha hedhi baada ya
kutwahirika kwake. Wala hawajibikiwi kukidhi swala zilizompita katika kipindi hicho.
Itakapokatika hedhi yake, itamuwajibikia funga hata bado hajakoga. Impokelewa kutoka kwa
Bi Muaadhah, amesema : nilimuuliza Bi Aysha Allah amuwiye radhina akasema: kwa
nini mwenye hedhi anakidhi swaumu na wala hakidhi swala ? Akasema: "hayo yalikuwa
yakitupata tulipokuwa pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimeshukie, basi
tukiamrishwa kukidhi swaumu na wala hatukuamrishwa kukidhi swala"Bukhariy na Muslim
- Kuingiliwa yaani kufanya naye tendo la ndoa. Haya yanatokana na kauli ya Allah:
"BASI JITENGENI NA WANAWAKE WAKATI WA HEDHI (zao) WALA MSIWAKARIBIE MPAKA
WATWAHARIKE. WAKISHAKUTWAHIRIKA BASI WAENDEENI KATIKA PALE ALIPOKUAMRISHENI
ALLAH
" [2:222].
Muradi na makusudio ya kujitenga na wanawake ni kuacha kuingiliana nao kimwili.
Imepokelewa kutoka kwa Abdillah Ibn Saad. Allah Amuwiye radhi kwamba yeye alimuuliza
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie: Ni kipi kinachonihalalikia kwa mke wangu
wakati awapo hedhini? (Mtume) akamjibu: "Ni halali yako kilicho juu ya ya shuka
(gaguro). Abu Daawoud.
NYONGEZA KATIKA KUTAJA UMRI WA KUBALEGHE
Tamaanisha na kukusudia kwa neno "baleghe" ule umri ambao atakapoufika
mtu mwanamume au mwanamke hupata sifa ya kuwa ni mtu MUKALLAFU. Yaani sasa anatakiwa
kuyatekeleza yale yote aliyoamrishwa au kukatazwa na sheria; tangu swala, swaumu, hijah na
ibada nyingenezo.
Baleghe hujulikana kwa kupatikana mojawapo ya mambo matatu haya :-
- kujitolea na kutokwa na manii. Hili hushirikiana msichana na mvulana yaani msichana
naye hujitolea usingizini kama ajiotoleavyo mvulana.
- Msichana kuanza kutokwa na damu ya hedhi kipindi cha mwanzo ambacho msichana
anaweza kujiotelea au kutokwa na damu ya hedhi ni miaka tisa ya mwezi muandamo. Kuchelewa
au kuwahi kupata hedhi hutofautiana baina ya nchi na nchi, mtu na mtu na hali za kimaisha.
- Mvulana au msichana kutimiza umri wa miaka kumi na tano kwa mwaka wa mwezi
mwandamo. Hili ni iwapo hajajitolea au kupata hedhi mpaka kufikia umri huo
|