|
Muislamu hatayamamu kwa sababu tu amejisikia kufanya hivyo,
akaacha kutawadha. Bali uislamu umeweka hali na mazingira maalumu, ambamo humo ndimo mtu
anaruhusiwa kuitumia na kuitekeleza sheria hii ya tayamamu. Hali na mazingira haya ndio
yanayojulikana kisheria kama sababu za kutayamamu. Sababu zinazomuhalalishia muislamu
kutayamamu ni nne kama ifuatavyo;
- Kukosa maji. Mtu anaweza kuyakosa maji kinadharia au kisheria. Kuyakosa maji
kinadharia ni kama vile mtu kuwa safarini na akayakosa maji au akawa na maji
yasiyomtosheleza kutawadhia. Ama kuyakosa maji kisheria ni mtu kuwa na maji lakini akawa
anayahitajia kwa kunywa yeye mwenyewe au hayawani mwingine ambaye ni muhtaramu. Ni mamoja
anataka kuyanywa sasa hivi au baadaye. Kutayamamu kwa sababu ya kukosa maji ni ruhusa
itokanayo na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu
NA
HAMKUPATA MAJI, BASI KUSUDIENI (TAYAMAMUNI) UDONGO (MCHANGA) ULIO SAFI (TWAHARA)
.. (5:6)
Katika sunnah, kukosa au
kutokupata maji ni sababu inayomuhalalishia mtu kutayamamu kutokana na hadithi hii;
Imepokelewa kutoka kwa Imraan Ibn Huswain amesema; Tulikuwa safarini pamoja na Mtume
Rehema na Amani zimshukie akawaswalisha watu (maswahaba), tahamaki kuna mtu
mmoja amejitenga na watu wale (hakuswali pamoja nao). Mtume akamwambia "Ni jambo gani
lililokuzuia usiswali pamoja nasi ? Akajibu mtu yule; Ewe mtume wa Mwenyezi Mungu,
limenipata janaba na (hapa) hapana maji (ya kukoga). Mtu akamwambia; Tumia mchanga, kwani
huo unakutosheleza. Bukhaariy na Muslim.
- Maji kupatikana mbali. Mtu atakapokuwa mahala ambapo hakuna maji karibu. Kutokea
hapo alipo mpaka kuyafikia maji ni umbali wa kilometa mbili na nusu (2.5km) na
kuendelea/na zaidi. Katika mazingira haya mtu anaruhusiwa kutayamamu na wala
haimuwajibikii kuhangaika kuyatafuta maji kwa sababu ya taabu, shida inayoweza kumpata
katika utafutaji huo.
- Kushindwa kuyatumia maji. Kushindwa kunaweza kuwa kinadharia au kisheria. Kushindwa
kutumia maji kinadharia ni kama vile maji yanapatikana karibu na mahala alipo, lakini
baina ya mahala alipo na yalipo maji kuna adui kama vile majambazi wanaopora na
kunyanganya mali na pengine kuua au kuna mnyama hatari kama vile simba au chui.
Katika hali na mazingira kama haya, muislamu anapewa ruhusa ya kutayamamu ili asiitie
hatarini nafsi yake, kwa sababu tu ya kutafuta maji ya kutawadhia. Tusome;
WALA MSIJITIE KWA MIKONO YENU KATIKA MAANGAMIZO ... (2:195) Ama kushindwa kuyatumia
maji kisheria kunapatikana katika sura hizi;
- Kuchelea kuzuka kwa maradhi kwa sababu ya kutumia maji.
- Kuzidi kwa maradhi ikiwa mtu atatumia maji.
- Maradhi kuchelewa kupona iwapo atatumia maji. Ni mamoja ikiwa mtu atayajua haya
kutokana na uzoefu alionao au kwa kuambiwa na daktari bingwa.
Katika hali zote hizi mtu anaruhusiwa kutayamamu na wala
haimuwajibikii kutawadha. Haya ndio mafundisho na eleweko linalopatikana katika hadithi
hii ya Bwana Mtume; Imepokelewa kutoka kwa Jaabir -Allah amuwiye radhi amesema;
Tulisafiri, mtu mmoja miongoni mwetu alipatwa na jiwe likampasua kichwa chake. Kisha
(majeruhi huyu) akajiotelea (usiku). Akawauliza wenzake; Je, mnanipatia ruhusa ya
kutayamamu (kutokana na jeraha nililo nalo ?) Wakamwambia hatukupatii ruhusa ilhali
unaweza kutumia maji. Mtu yule akaoga (ili apate uhalali wa kuswali) akafa (kutokana na
kudhuriwa na maji). Tuliporudi safari na kufika kwa Mtume - Rehema na Amani zimshukie
akaelezwa habari ile (ilivyokuwa). (Mtume) akasema "Wamemuua, Allah awauwe na
wao!! Kwa nini wasiulize kama hawajui, hakika dawa ya ujinga ni kuuliza. Hakika si
vinginevyo ilikuwa inamtoshea kutayamamu na kufunga kitambaa kwenye jeraha lake, kisha
akapakaza juu yake (maji) na akaosha sehemu nyingine ya mwili wake. Abuu Daawoud.
Baridi kali. Hii ndio sababu ya nne inayomuhalalishia mtu
kutayamamu badala ya kutawadha. Iwapo mtu atakuwa na yakini kuwa atadhurika kutokana na
kutumia maji katika mazingiria ya baridi kali sana na ikawa hana njia yoyote ya
kumuwezesha kuchemsha maji, ataruhusika kisheria kutayamamu. Hii ni kwa sababu swahaba wa
Mtume Amri Ibn Al-aaswi- Allah amuwiye radhi- alitayamamu kutokana na janaba lililompatia,
akaacha kuoga kwa kuchelewa kuangamia (kufa) kutokana na baridi. Bwana mtume Rehema
na Amani zimshukie-akalikiri hili na wala asilipinge, kwa hivyo likawa ni miongoni mwa
mambo/sababu zinazomuhalalishia mtu kutayamamu. Riwaya hii imepokewa na Abuu Daawoud na
kusahihishwa na Ibn Hibaan na Al-Haakim.
TANBIHI:
Ni vema ikakumbukwa kwamba katika hali hii ya kutayamamu kwa
sababu ya baridi itamuwajibikia mtu huyo kuzikidhi na kuzirudia kuziswali swala zote
alizoziswali kwa tayamamu iliyotokana na sababu hiyo. Hili lifanyike mara tu atakapoweza
kuyatumia maji.
Muislamu atakapotokewa na mojawapo ya mambo manne hayo
tuliyoyataja, ndio anapata ruhusa na kibali cha kutayamamu badala ya uoga au kutawadha kwa
mujibu wa sheria.
VI) SHARTI ZA KUSIHI KUTAYAMAMU
Sharti za kusihi kutayamamu, haya ni mambo ambayo sheria
imelazimisha na kuwajibisha yapatikane kwanza kabla mtu hajaanza kutayamamu. Kusihi kwa
tayamamu sambamba na ibada itayofanywa kwa tayamamu hiyo, kutategemea sana upatikanaji wa
mambo yafuatayo:
- Kujua kuingia wakati wa swala anayoitayamamu. Tayamamu hisihi kabla ya kuingia
wakati wa swala.
- Kutafuta maji baada ya kuingia wakati wa swala. Sharti hili ni iwapo anatayamamu
kwa sababu ya kukosa maji.
- Mchanga twahara usio na vumbi la mkaa, unga, (wa nafaka kama vile mahindi) au vumbi
la chokaa na kadhalika.
- Aondoe najisi kabla ya kuanza kutayamamu
- Ajitahidi kuelekea Qibla kabla ya kuanza kutayamamu.
FAIDA: SHARTI ZA KUWAJIBISHA KUTAYAMAMU
Ili mtu apate ruhusa na kibali cha kutayamamu ni lazima
yapatikane mambo/sifa zifuatazo:
- Uislamu: Tayamamu ni sheria inayomuhusu muislamu peke yake. Kwa mantiki hii asiye
muislamu hana tayamamu.
- Baleghe: Hana tayamamu na wala haisihi kwa mtoto mdogo.
- akili timamu: hana tayamamu mwendawazimu kwa sababu ya kutokulitambua alitendalo,
jambo ambalo ni sharti kubwa katika kusihi na kukubalika utendaji na utekelezaji wa ihada
zote za mja katika uislamu.
vii/. NGUZO ZA TAYAMAMU:
Nguzo za tayamamu, haya ni mambo ya msingi kabisa mabayo kuwepo /
kupatikana kwa tayamumu kunayategemea, na haya ni mambo yanayofanyika ndani ya tayamamu
yenyewe. Mambo yenyewe ni kama yafuatavyo:
- Nia: Hii ndiyo nguzo ya kwanza na ya msingi ya tayamamu. Anuie moyoni mwake
kuondosha hadathi ndogo au hadathi kubwa.
- Kupaka (vumbi) uso wote na mikono mpaka vifundoni kwa mapigo mawili. Nguzo hii
hutekelezwa kwa kupiga viganja juu ya fungu la mchango twahara wenye vumbi na kuupaka za
uso kwa vumbi lililomo kwenye viganja hivyo. Kisha vipigwe viganja kwa mara ya pili juu ya
lile fungu la pili la mchanga na kuipakaza mikono hadi vifundoni kwa vumbi lililomo
viganjani. Haya ni kwa mujibu wa hadithi iliyopokelewa na Ibn Umar-Allah amuwiye radhi
amesema : Amesema Mtume Rehema na Amani zimshukie Tayamamu ni mapigo
mawili, pigo moja ni la uso na pigo jingine ni la mikono mpaka vifundoni
Daaruqutwniy.
ZINGATIA: Ni lazima mtu ahakikishe kiungo
chote cha tayamamu, ambacho ni uso na mikono, kimeenea vumbi kama kinavyoenea maji katika
kutawadha. Iwapo amevaa pete kidoleni, basi itamuwajibikia kuivua wakati wa pigo la pili
ili vumbi liweze kufika mahala hapo.
- Utaratibu: Hii ndiyo nguzo ya mwisho ya tayamamu. Mtu aanze kutayamamu kwa
kupangusa uso na amalizie na kupangusa mikono hadi vifundondoni. Hii ni kwa sababu
tayamamu ni badala ya udhu, na utaratibu ni nguzo miongoni mwa nguzo za udhu kama
ulivyokwisha jifunza katika masomo yaliyopita. Kwa mantiki hii utaratibu unakuwa ni nguzo
katika tayamamu ambayo ni badala ya udhu.
|