Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

V) SWALA NI WAJIBU KWA NANI ?

Faida

Swala imemuwajibikia kila Muislamu aliyebaleghe (mkubwa) mwenye akili timamu. Zitakapopatikana na kutimia kwa mtu sifa tatu hizi:-

       1.         Uislamu.

       2.         Kufikia baleghe (ukubwa) na

       3.         Akili timamu.

Hapo atakuwa amekalifishwa na kuwajibishiwa na sheria kuitekeleza ibada hii ya swala, na si kuitekeleza tu basi, bali kuitekeleza kwa namna aliyoifundisha kwa maneno na matendo Bwana Mtume.

Hebu tuangalie kwa ufafanuzi kidogo sifa tatu hizi ambazo ndizo zinamvika mja taji la kuwajibikiwa na swala. Tuanze na

(i)            UISLAMU. Hii ndio sifa ya kwanza au tuseme ndio sifa mama. Kwa kigezo hiki swala haiwi wajibu kwa kafiri, hii ni kwa sababu kutangulia shahada ambayo ndio tiketi ya kusafiri na gari Uislamu ni sharti ya amri ya swala. Yaani ili mtu awe na sifa ya swala ni lazima kwanza atamke shahada ambayo itamvisha Uislamu, hapo ndipo atawajibikiwa na swala. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipokuwa akimpa maelekezo swahaba wake Muaadh – Allah amuwiye radhi, “Walinganie washuhudie kwamba hapana Mola pasaye kuabudiwa kwahaki ila Allah pekee na kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Allah, ikiwa wao watakutii katika hilo, basi waambie kwamba Allah amewafaradhishia swala tano kila siku, mchana na usiku” Bukhaariy.

 

(ii)            KUFIKILIA BALEGHE (kwa mkubwa),  Hii ndiyo sifa ya pili inayomfanya mtu awe na haki na wajibu wa kushiriki katika ibada ya swala. Sifa hii haimaanishi zaidi ya kuwa swala si wajibu/faradhi kwa mtoto mdogo. Mtoto mdogo kwa mtazamo wa sheria ni yule ambaye hajafikilia baleghe/ hajawa mkubwa. Baleghe kisheria hupatikana kwa mojawapo ya mambo matatu hayo:-

      a)         Mvulana au msichana kufikia umri wa miaka kumi na tano (15) ya mwezi muandamo.

      b)         Kujiotelea usingizini na kutokwa na manii katika umri wa miaka tisa na kuendelea. Hii ni kwa wote, mvulana na msichana.

      c)         Msichana kuanza kupata hedhi kwa kutimiza miaka tisa (9) na kuendelea.

 

Kijana wa kiume na wa kike akitokewa na mojawapo ya mambo matatu haya, kisheria atakuwa amefikia umri wa majukumu . Ambapo hapo atatakiwa kutenda yote aliyoyaamrisha Allah na kuyaacha yote aliyoyakataza, na hapa ndipo dhana ya dhambi na thawabu huchukua nafasi. Sifa hii ya pili tunaipata kupitia kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie, “ Kalamu imeondoshwa kwa aina tatu za watu : kwa mtu aliyelala mpaka atakapoamka, kwa mtoto mapaka atakapobaleghe na kwa mwendawazimu mpaka atakaporudiwa na akili” Abuu Daawaid na Al-Haakim.

Naam, pamoja na kwamba swala haikufaradhishwa na kuwajibishwa kwa mtoto mdogo, lakini ni sunah na imependekezwa na sheria kwa baba, mama au mlezi wa mtoto aanze kumuamrisha mwanae kuswali atakapofikia umri wa miaka saba. Amchape akiacha kuswali wakati akiwa na umri wa miaka kumi. Hizi zote ni hatua za kumjengea mtoto hisia na mazoea ya ibada hii ya swala atakapokuwa mkubwa. Kimaumbile ni rahisi kwa mtoto kukua na kuishi na lile alilolizoea tangu utotoni na ni vigumu mno kwake kulitekeleza ukubwani lile ambalo hakulizoea tangu alipokuwa mtoto. Uzoefu umeuthibitisha na kuukiri ukweli huu, na hii ndio hekima na falsafa ya neno lake Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie, “Waamrisheni watoto wenu kuswali watakapofikia umei wa miaka saba, na wapigeni kwa kuiacha (swala) wakifikia miaka kumi na watengeni katika malazi” Tuimidhiy.

Yaani watoto wa kiume na wale wa kike wasilale pamoja baada ya kufikia umri wa miaka kumi.

(iii)       AKILI TIMAMU: Ili mtu awajibikiwe na swala ni lazima awe na sifa hii ya akili timamu. Kwa mantiki hii swala si wajibu/faradhi kwa mwendawazimu kwa sababu hana nguvu ya kujua alitendalo. Hivyo ndivyo tunavyofahamishwa na kauli ya Bwana Mtume tuliyoitaja katika nukta/kipengele cha pili…”……na kwa mwendawazimu mpaka atakaporudiwa na akili.”

VI.            SWALA ZA FARDHI NA NYAKATI ZAKE.

Swala za fardhi ambazo Muislamu amefaradhiwa na Mola wake kuziswali kila siku, mchana na usiku ni swala tano. Kila moja miongoni mwa swala tano hizi ina wakati wake maalum ambao muislamu anawajibikiwa kuiswali ndani ya wakati huo.

Hii ndiyo amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani Tukufu. “……..KWA HAKIKA SWALA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA NYAKATI MAKHSUSI (maalumu) “. (4:103). Tumejua kutokana na aya hii kwamba kumbe kuswali kwa wakati ni nembo na alama ya Imani ya mja. Haisihi  na wala haijuzu kwa muislamu kuiswali swala kabla ya kuingia wakati kama isivyofaa kuiswali bada ya kutoka wakati wake ila kwa dharura ya kisheria. Suala la wakati wa kila swala halikuwa mikononi mwa Bwana  Mtume - Rehema na Amani zimshukie – bali lilitawaliwa na wahyi (ufunuo) kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Imethibiti katika hadithi nyingi sahihi kwamba Jibril – Amani imshukie – alimjia Bwana Mtume – baada ya kufaradhishwa swala tano kumfahamisha nyakati za swala, swala ipi inaingia wakati gani na kumalizika wakati gani. Kisha naye Bwana Mtume akaubainishia umma wake nyakati hizo kwa maneno na matendo.

Hadithi iliyokusanya kwa pamoja nyakati za swala zote tano ni ile iliyopokelewa na Imam Muslim ikiwa ni riwaya ya Abuu Muusa Al-Ash-ariy-Allah amuwiye radhi -kutoka kwa Mtume Rehema na Amani zimshukie kwamba yeye Mtume alijiwa na mtu akimuuliza juu ya nyakati za swala (Mtume) hakumjibu chochote Na katika riwaya nyingine Mtume alisema: “Njoo uswali pamoja nasi. Akasema (Abuu Muusa): (Mtume) akaisimamisha Alfajiri (Swala ya Alfajiri) wakati ilipochimbuka Alfajiri na ilhali watu wanakurubia kutofahamiana (kutokana na muangaza hafifu). Kisha akamuamrisha kuisimamisha Adhuhuri wakati jua lilipopinduka na il-hali akisema msemaji: Mchana umegawika nusu, naye alikuwa ni mjuzi mno wa hilo (la nyakati) kuliko wao. Halafu akawaamrisha, akaisimamisha Al-asri na ilhali jua likiwa limepanda. Kisha akamuamrisha akaisimamisha Maghribi wakati jua lilipotua/lilipozama. Kisha akamuamrisha akaisimamisha Isha wakati yalipozama mawingu (mekundu) kisha kesho yake akaichelewesha Alfajiri, mpaka akamaliza kuiswali na msemaji akisema: Jua limechomoza au limekurubia (kuchomoza). Kisha akaiakhrisha Adhuhuri mpaka ikawa karibu na wakati wa Al-asiri ya jana. Kisha akaichelewesha Al-asiri mpaka akamaliza kuiswali na ilhali akisema msemaji: Jua limekuwa jekundu. Halafu akaiakhirisha Maghribi mpaka ikawa wakati wa kuzama mawingu mekundu. Kisha akaiakhirisha Ishaa mpaka ikafika theluthi ya kwanza ya usiku. Kisha kulipopambazuka akamuita yule muulizaji na kumwambia: “Huo wakati (uliokuwa ukiuulizia) uko baina (ya nyakati) mbili hizi (ule wa juzi na wa jana).

Zipo hadithi nyingine ambazo zimekuja kutoa tafsiri na ufafanuzi juu ya kauli jumla zilizomo ndani ya hadithi hii. Zikiitaja kila swala na wakati wake. Tufuatane pamoja na tujifunze.

WAKATI WA ALFAJIRI.

Wakati wa swala ya Alfajiri huingia kwa kuchomoza Alfajiri ya kweli (Alfajiri halisi) na huendelea mpaka kuchomoza kwa jua. Amesema Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie: “Wakati wa swala ya Sub-hi ni tangu kuchomoza Afajiri maadamu jua halijachomoza.” Muslim

WAKATI WA ADHUHURI.

Huanza wakati wa swala ya Adhuhuri kwa kukengeuka jua nusu ya mbingu kuelekea upande wa Magharibi, huku ndiko kunakoitwa kutenguka/kupondoka jua. Wakati huu kivuli cha kitu huonekana kidogo tu, kinachoanza kuelekea upande wa Mashariki, na hiki ndicho kinachoitwa kivuli cha kitu mfano (Mithili) wa kitu chenyewe. Amepokea Imam Muslim kwamba Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie amesema “Wakati wa Adhuhuri ni zama litakapotenguka jua na kikawa kivuli cha mtu kama mfano wa urefu wake (Mtu huyo) muda wa kuwa haijaingia Al-asiri.”

WAKATI WA AL-ASIRI.

Huanza wakati wa swala ya Al-asiri kwa kumalizika wakati wa Adhuhuri na huendelea mpaka kuzama kwa jua. Haya tunayafahamu kutokana na kauli ya Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie. “Na atakayeidiriki (atakayeiwahi) rakaa moja ya Al-asiri kabla ya kuzama jua, hakika ameidiriki Al-asiri” Bukhaariy na Muslim.

Lakini ni bora mtu asiicheleweshe swala ya Al-asiri mpaka wakati huu, bali apupie kuiswali mwanzo wa wakati.

WAKATI WA MAGHRIBI:

Wakati wa swala ya maghribi huanza kwa kuzama jua na huendelea mpaka kuzama kwa mawingu mekundu bila ya kubakia athari yake upande wa Magharibi. Mawingu (makungu) mekundu ni matokeo ya kubakia athari ya mwangaza wa jua ambayo hudhihiri upande wa Mashariki wa pambizo za mbingu wakati jua linapozama. Hatimaye giza huyafukuzia upande wa Magharibi kidogo kidogo mpaka hupotea/hutoweka kabisa. Kiza kikifunga na kuenea pambizo la Magharibi na kutoweka kabisa kwa athari ya mawingu mekundu, hali hii humaanisha kumalizika kwa wakati wa swala ya Magharibi na kuingia kwa wakati wa swala ya Ishaa. Hivyo ndivyo tulivyofahamu kutokana na hadithi jumla ya nyakati za swala tuliyoitaja huko nyuma pamoja na kauli ya Mutume isemayo: “Wakati wa Maghribi ni muda wa kuwa hayajazama mawingu mekundu.

WAKATI WA ISHAA.

Huingia wakati wa swala ya Ishaa kwa kuisha/kumalizika wakati wa swala ya Magharibi na huendelea mpaka kudhihiri kwa Alfajiri ya kweli. Lakini ni bora isicheleweshwe mpaka kupita theluthi ya kwanza ya usiku. Hizi ndizo nyakati za swala tano. Inapendeza au imependekezwa kwa Muislamu kuiswali swala mwanzoni mwa wakati wake kwa sababu jambo hili huonyesha ukomavu wa Imani ya mja na kuijali kwake ibada ya swala. Pia si vema kuichelewesha kwa makusudi ukaiswali ukingoni mwa wakati kwa hoja ya ukunjufu wa wakati, kwa sababu uchelewashaji huu unaweza kusababisha kuiswali nje ya wakati wake. Na pengine huweza kusababisha kuzembea na kuacha kuiswali kabisa. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie  - aliulizwa ni amali ipi iliyo bora kuliko zote ? Akajibu ! “ Ni kuswali kwa wakati wake”. Bukhaary na Muslim.

Yaani kuswali mwanzo na wakati.

FAIDA!

Jua na ufahamu kwamba mtu iliyotuka baadhi/sehemu ya swala yake ndani ya wakati na baadhi nyingine nje ya wakati wake. Angalia akiipata mtu rakaa moja ndani ya wakati, swala hiyo, itakuwa ni ADAA – yaani itahesabika kuwa imeswaliwa ndani ya wakati. Na iwapo hakuwahi kuipata rakaa moja ndani ya wakati, yaani kaipata sehemu tu ya rakaa, basi swala hiyo itakuwa ni KADHAA, yaani imeswaliwa  nje ya wakati. Ushahidi wa haya ni ile hadithi iliyopokelewa na Abu Hurayrah – Allah amuwiye radhi – kwamba Mtume wa Allah – Rehema na  Amani zimshukie – amesama; “Atakayediriki katika (swala ya ) Sub-hi rakaa moja kabla ya kuchomoza jua, hakika ameidiriki sub – hi. Na atakayeidiriki rakaa moja katika  swala ya Alasiri kabla ya kuzama jua, hakika atakuwa amediriki Alasiri”.

Na kauli ya Mtume isemayo:

“Atakayeidiriki rakaa moja katika swala, hakika ameidiriki swala hiyo”. Bukhaariy na Muslim.


TUJIFUNZE NA TUKUBALI kuwa: Kuiswali swala kwa  wakati wake ni kielelezo cha ukomavu wa  imani ya mja na kuswali nje ya wakati bila ya udhuru wa kisheria ni uduni wa kiimani/ni kufilisika kiimani.  


Forum | Guestbook | Tuandikie |