Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

NGUZO  ZA SWALA

 

3.          TAKBIRA YA KUHIRIMIA

Takbira ya kuhirimia ya swala ndio nguzo ya tatu ya swala, hii ni kusema wakati wa kuingia ndani ya swala  ALLAAHU AKBAR. Hili linatokana na tendo lake mwenyewe Bwana Mtume na ni yeye  ndiye aliyetuagiza: “Swalini kama mlivyoniona nikiswali”. Bukhaariy.

Takbira ya kuhirimia katika suna

1.    Imepokelewa na Sayyidna Abdullah Ibn Umar-Allah amuwiye radhi – amesema: “ Alikuwa Mtume wa Allah- Rehema na Amani zimshukie- anaposimama kwa ajili ya kuswali, hunyanyua mikono yake mpaka ikawa mkabala wa mabega yake kisha akasema ALLAHU AKBAR………” Muslim.

2.    Imepokelewa na Sayyidna Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema: “Alikuwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – anaposimama kwenye swala kusema ALLAAHU AKBAR wakati anaposimama……..” Muslim.

3.    Imepokelewa na Imam Aliy – Allah amuwiye radhi amesema: Amesema  Mtume wa Allah – Rehma na Amni zimshukie: “Ufunguo wa swala ni udhu, na kiharamisha chake (swala) ni takbiria na kihalalisha chake ni salamu” Turmidhiy na Ibn Maajah

Mwenye kuswali atakapohirimia swala kwa kusema ALLAAHU AKBAR, inamuharamikia kusema kauli au kutenda tendo lililo nje ya matendo au kauli zinazoijenga swala mpaka atakapotoa salamu. Kwa hivyo utaona kuwa Takbira ya kuhirimia ndio ufunguo wa kuifungulia swala na salamu inaashiria mwisho wa swala.

Tamko la Takbira

Tamko la Takbira ya kuhirimia swala kama lilivyopokelewa kutoka kwa Bwana Mtume ni ALLAAHU AKBAR. Mtume hakuwahi kuifungua swala kwa kutumia tamko lingine zaidi ya hili na kumfuata yeye ni wajibu kwetu sisi.

Sharti za Takbiria ya kuhirimia.

Ili Takbiri isihi, kumeshurutizwa kuchunga mambo yafuatayo

  1.  Mwenye kuswali alitamke tamko la Takbira akiwa amesimama wima na hatembei. Hili linatokana na maelekezo ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alipomwambia yule swahaba aliyemuona haswali itakiwanvyo, akamwambia: “Unaposimama kwenye swala leta Takbiriia (sema ALLAAHU AKBAR)” Bukhaariy na Muslim.   Katika hadithi hii Bwana Mtume anamshrutizia swahaba huyu kuhirimia akiwa amesimama.

  2. Alitamke akiwa ameelekea Qiblah.

  3. Tamko la Takbira litamkwe kwa lugha ya Kiarabu. Hili lni kwa mujibu wa agizo lililotolewa na Mtume – Rehema na Amani zimshukie:” Swalini kama mlivyoniona mimi nikiswali”. Haikupokelewa riwaya yeyote kwamba Mtume alilitamka tamko hili la Takbira kwa lugha isiyo ya kiarabu, kwa hivyo ikatuwajibika nasi tulitamka kama alivyolitamka mwalimu wetu huyu.

Mas-ala: Inamuwajibikia mtu asiyejua kiarabu ajifunze mpaka aweze kulitamka tamko la Takbira ya kuhirimia kwa kiarabu. Kadhalika inamlazimu ajifunze kutamka dhikri zote za wajibu katika swala kwa kiarabu. Fahamu na uelewe, akishindwa kabisa, basi inamjuzia kuzitamka hizo dhikri kwa lugha yake aiwezayo ila Qur-ani tu ndio haitamkwi ndani ya swla ila kwa Kiarabu pekee.

Mahala pa kusoma Qur-ani katika swala anaweza kuleta dhikri nyingine kama tasbiyh, tahmiyd, tahliyl na takbiyr. Hivi ndivyo tunavyoelekezwa na Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie. Imepokelewa na Ibn abiy Awfaa-kwamba mtu mmoja alisema, Ewe Mtume wa Allah, nifundishe kitu kitakachonitosheleza na Qur-ani (Mtume) akamwambia: “Sema: sub-haanallah (Tasbiyh), Wal-hamduli llaah (Tahmiyd) wa laa Illaha illal – laah (Tahilyl) wallaahu akbar (Takbiyr)” Ibn Hibbaan.

 

(iv)    Tamko hili likutanishwe na nia, yaani usiwepo mwanya baina ya nia na Takbira hii ya kuhirimia swala.

 

4.    KUSOMA AL-HAMDU (Suuratul-faatihah).

Inakupasa ufahamu kwamba kusoma Al-hamdu, ndio nguzo ya nne ya swala yeyote ile iwayo ya suna au ya fardhi na ni katika kila rakaa. Nguzo hii inamuwajibikia Imamu, maamuma na hata mwenye kuswali pekee (Munfaridu). Nguzo hii haisamehewi ila kwa maamuma aliyemdiriki Imamu katika rukuu. Huyu atanuia na kuhirimia, halafu aungane na Imamu katika rukuu na atahesabiwa kuwa ameipata rakaa hii ijapokuwa hakuisoma al-hamdu.

Suna na usomaji wa Al-hamdu.

1.  Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Hana swala mtu asiyesoma Faatihatul-kitaab” (Al-hamdu)”. Bukaariy na Muslim

Tanbihi:

Bismillah ni miongoni mwa aya za Suuratil-faatihah. Haisihi suuratil–faatihah bila ya mwenye kuswali kusoma (Bismillahir_Rahmaanir-Rahiym). Haya ni kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa na Ibn khuzaymah-kutoka kwa Ummu Salamah-Allah amuwiye radhi – kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie – aliihesabu (Bismillahri – Rahamaanir – Rahiym) kuwa ni aya katika Suuratil-Faatihah.

Sharti za kusihi Al-hamdu.

Mwenye kuswali, hana budi kuchunga sharti zifuatazo anapoisoma Suuratil-Faatiha:.

i)       Msomaji ajisikizishe Suuratil-Faatihah iwapo hana matatizo ya kusikia.

ii)    Akitungamanishe kisomo cha Suuratil-Faatihah, yaani azisome aya zake kwa utaratibu kama ilivyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume na ilivyonakiliwa leo msahafuni. Aisome huku akichunga matokeo ya herufi na hukumu zote za usomaji.

iii)  Katika usomaji wake, hasifanye kosa linaloweza kuharibu maana mathalan neno(An-amta) akalitamka (An-amtu) hapo maana itakuwa imeharibika. Kwani badala ya maana kuwa “Umeneemesha wewe Allah” itakuwa “Nimeneemesha mimi”. Lakini akifanya kosa lisilo na athari katika maana swala yeke haitabatilika bali itamuwajibikia ajifundishe matamshi sahihi. Kosa hili ni kama vile kusoma“Al-Hamdu Lillahi Rabbul-Aalamin”

Badala ya “Al-Hamdu Lillahi Rabbil-Aalamin” Akaweka harakati ya dhummah katika neno “rabbu” badala ya harakah ya kasra “rabbi” ambayo ndiyo stahiki ya neno hilo hapo lilipo. Makosa kama haya hayaharibu maana ijapokuwa yanabakia kuwa ni makosa ya kisarufi.

iv)  Aisome kwa lugha ya Kiarabu, haisihi kuisoma kwa lugha nyingine kwa sababu hiyo haitakuwa Qur-ani bali tafsiri ya Qur-ani.

v)     Aisome akiwa amesimama. Akienda rukuu huku anakamilisha  kuisoma, usomaji wake huo utabatilika na itamuwajibikia kurudi katika kisimamo na kusoma tena.

 

5.    RUKUU.

Nini rukuu.

Katika sheria, rukuu ni kuinama mwenye kuswali kiasi cha vitanga vyake kugusa magoti yake. Huu ndio uchache wa rukuu. Ama ukamilifu wake ni kuinama kiasic ha mgongo kulingana sawa na kufanya mfano wa pembe mraba (90o).

Rukuu  ndani ya Qur-ani.

Rukuu ndani ya Qur-ani inatajwa katika kauli tukufu ya Allah. “ENYI MLIDAMINI RUKUUNI NA SUJUDUNI NA MUABUDUNI MOLA WENU NA FANYENI MEMA ILI MPATE KUFAULU (22:77).

Rukuu katika kivuli cha Sunnah:

Rukuu inatajwa katika kauli ya Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – aliposema kumfundisha mtu swala: “….Kisha rukuu  mpaka utulizane ukiwa umerukuu……”  Bukhaariy na Muslim.

Sharti za rukuu.

Ili rukuu ya mwenye kuswali isihi kisheria ni lazima ajilazimishe kufuata yafuatayo

i)        Ainame kama tulivyoeleza katika kuainisha rukuu, yaani ainame mpaka vitanga viguse magoti.

Imepokelewa  na swahaba Abu Humayd – Allah amuwiye radhi – alipokuwa akitaja namna alivyokuwa akiswali Mtume wa Allah- Rehema na Amani zimshukie:” …. Na anaporukuu huimanikinisha (huiweka) mikono yake magotini mwake……” Bukhaariy.

ii)       Asikusudie katika kurukuu kwake kitu kingine zaidi ya rukuu (kisichokuwa rukuu). Mathalan, iwapo mtu atainama kwa kuchelea kitu Fulani, akaendelea kuinama kwa kujaalia kuwa hiyo ndiyo rukuu,  rukuu hiyo haitoshi kwa hali hii kwa sababu haikukusudiwa kuwa ndio rukuu, bali ilikusudiwa kitu kingine. Katika mazingira kama haya itamuwajibikia asimame na alingane sawa, kisha ndipo arukuu kwa kuikusudia rukuu.

 

Atulizane katika rukuu kwa kadri ya Tasbihy moja kwa uchache. Hili linatokana na kauli ya Mtume iliyotangulia: “……Mpaka  utulizane ukiwa umerukuu….” Pia imepokewa kutoka kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie kwamba amesema “Mwizi  muovu kuliko wote ni yule anayeiba ndani ya swala yake” (Maswahaba) wakauliza: Ewe Mtume wa Allah, mtu anawezaje kuiba katika swala yake? Akawajibu “Hazitimizi rukuu zake (hiyo swala) wala sijida zake” Ahmad/Twabaraaniy.


Forum | Guestbook | Tuandikie |