|
11.
KUMSWALIA MTUME BAADA YA TASHAHUDI YA MWISHO.
Hii ndio nguzo ya kumi na
moja ya swala. Nguzo hii yaani
kumswalia Bwana Mtume, huchukua nafasi mara tu
bada ya kukamilka kwa tashahudi na kabla ya kutoa salamu. Hapo ndipo mahala
pake nguzo hii.
Dalili ya swala ya Mtume.
Kumswalia Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie
– ndani ya swala ni katika kulitekeleza agizo na amri ya Allah isemayo
“HAKIKA ALLAH ANAMTEREMSHIA REHEMA MTUME (anaswalia) NA MALAIKA WAKE
(wanamuombea dua) BASI, ENYI WAUMINI MSWALIENI (Mtume, muombeeni rehema) NA
MUOMBEENI AMANI” (33:56).
Wanazuoni wamekongamana na kuwafikiana kwamba
kumswalia Mtume si WAJIBU ila ndani ya swala tu. Uwajibu huu unatokana na
riwaya nyingi sahihi ikiwemo hii iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Masoud – Allah
amuwiye radhi – katika (kueleza) swali aliloulizwa Bwana Mtume – Rehema na
Amani zimshukie – juu ya kuswaliwa kwake. Tukuswalieje ndani ya swala?
Akajibu, Semeni.
ALLAHUMMA SALLI ALAA MUHAMMAD WA ALAA AALI
MUHAMMAD KAMAA SALLAYTA ALAA IBRAHIM WA AALI IBRAHIM WABAARIK ALAA MUHAMMAD
WA ALAA AALI MUHAMMAD KAMAA BAARAKTA ALAA IBRAHIM WA ALAA AALI IBRAHIM
FIL-AALAMINA INNAKA HAMIDUN MAJID Bukhariy na Muslim
Riwaya hii ndio inayoanisha kwamba mahala pa
wajibu pa kumswalia Bwana Mtume ni ndani ya swala.
Uchache wa matamko ya kumswalia Mtume ni kusema: ……………ALAAHUMMA SALLI ALAA
MUHAMMAD
Matamko kamili ni kamili ni kama hayo yaliyomo
ndani ya hadithi tuliyoitaja. Katika baadhi ya riwaya kuna zaida au pungufu.
Sharti za swala ya Mtume.
Kumeshurutizwa
katika kumswalia Mtume ndani ya Swala, kuchunga mambo yafuatayo:-
(i)
Ajisikilizishe mwenyewe matamko yake, iwapo hana matatizo ya usikivu.
(ii)
Iwe ni kwa tamko la “ Muhammad” au Rassul” au “An-nabiy”. Lau mtu
atamswalai kwa kusema mathalan “Alaa Ahmad”, haitamjuzia.
(iii)
Iwe ni kwa Kiarabu.
Akishindwa, ataleta
tafsiri yake kwa lugha yeyote aiwezayo LAKINI afahamu bado inamuwajibikia na
kumlazimu kujifunza upesi imkinikavyo.
(iv)
Mtungamano (Utaratibu) wa matamko yake. Asiyacheleweshe matamko
yaliyotangulia na kuyatanguliza yaliyocheleweshwa, bali ayatamke kama
yalivyopokewa katika hadithi.
(v)
Mtungamano baina yake (swala ya Mtume) na Tashahudi. Haisihi
kuanza kumswalia Mtume kabla ya
kusoma Tashahudi.
12.
SALAMU YA KWANZA.
Kutoa salamu ni ule
ugeukaji wa kutumia shingo tu wa
mwenye kuswali kuliani kwake il-hali
akisema…………ASSALAAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH
Nguzo hii ni natija ya kauli ya Bwana Mtume –
Rehema na Amani zimshukie “ Ufunguo wa swala ni Twahara na Ihramu yake ni
Takbiyra na ufunguzi wake ni Kutoa salamu”. Turmidhiy, Abuu Daawoud na wengineo.
Uchache wa salamu ni mtu kusema mara moja:
……………………………………… ASSALAAMU ALAYKUM
Ama ukamilifu wake ni kusema.
………………………………………. ASSALAAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH
Mara mbili, mara ya kwanza kuliani na ya pili
kushotoni.
Imepokelewa hadithi kutoka kwa Sa’ad – Allah
amuwiye radhi – amesema : Nilikuwa nikimuona Mtume wa Allah – Rehema na Amani
zimshukie – akitoa salamu kuliani kwake na kushotoni kwake mpaka ninaona
weupe wa kitefute (shavu) chake” Muslim.
13.
MTUNGAMANO (UTARATIBU) WA NGUZO HIZI KAMA ZILIVYOTAJWA.
Kutungamanisha nguzo za
swala ni kuziratibisha kwa utaratibu wake kama zilivyo moja baada ya nyingine
kila moja ikachukua nafasi yake bila ya kuitangulia nyingine. Kwa mantiki
hii, mwenye kuswali analazimika kuianza swala yake kwa nia, halafu Takbiyra ya
kuhirimia, kisha, asome Suratil-Faatiha, halafu arukuu, aitadili,
asujudu……..na kuendelea kama hivi Angalia ikiwa mtu ataihamisha nguzo kwa
makusudi kuitoa mahala pake ilipowekwa na sheria na kuipeleka mahala si pake,
swala yake nzima itabatilika,
haikubaliwi. Ama akitenda hivyo bila ya kukusudia, basi swala yake itakuwa
imebatilika kuanzia katika ile nguzo aliyoitenda mahala si pake na
itamuwajibikia kuirudia swala yake tokea pale alipokosea tu. Kwa mantiki,
iwapo mtu ataendela na swala yake baada ya kuwa ameshabadili utaratibu wa
nguzo mpaka akafikia mahala alipopabadilisha katika rakaa iliyotangulia.
Mathalann rukuu mpaka rukuu nyingine ya rakaa nyingine, nguzo shaihi ya rakaa
hii ya sasa itakaa mahala pa nguzo
fasidi ya ile rakaa iliyotangulia. Kwa hivyo basi, itamuwajibikia azidishe
rakaa moja, katika swala yake ili kuifidia ile rakaa iliyofisidika kwa
kufisidika utaratibu wa nguzo.
(Allah ndiye Mjuzi mno wa
lililo la sawa.)
Hizi ndizo nguzo za swala
ambazo swala haisihi ila kwa kuzileta zote, tena kwa utaratibu huu
tulioubainisha. Ni wajibu kwa mwenye kuvaana na ibada hii awaye yeyote,
mwanamume wau mwanamke aihifahdi ibada hii kwa kuiteleza kwa ikhlasi,
ufanisi na unyenyekevu.
X/.
SUNA
ZA SWALA.
Muradi
na makusudi ya suna za swala ni zile: kauli na matendo ambayo atakapoyasema
au kuyatenda mwenye kuswali, atapata thawabu kutoka kwa Allah na kama
hakuzisema kauli hizo au kuyatenda matendo hayo humfutu (hapati) thawabu. Na
atastahili kulaumiwa kwa kuziacha kauli au matendo hayo kwa sababu Bwana Mtume
– Rehema na Amani zimshukie – alikuwa akiyasema na kuyatenda.
Kama ambavyo swala ina nguzo na sharti
zinazomlazimu mwenye kuswali kuzitekeleza kwa njia ya uwajibu ili swala yake iweze kusihi. Kadhalika inazo
suna ambazo mwenye kuswali anatakiwa azitekeleze LAKINI sio kwa njia ya
UWAJIBU/ULAZIMA. Bali kuzitenda suna hizo hakutamaanisha kingine zaidi ya
kurudufika na kuzidi thawabu za swala zake na kuacha hakumaanishi kupata
dhambi: Suna hizi za swala ni nyingi baadhi ya Mafaqihi wamezichambua mpaka
kufikia idadi yake khamsini . Suna zote hizi kwa ujumla wake zinagawanyika
katika matapo/mafungu matatu yafuatayo:-
a.
Suna zilizo kabla ya Swala.
b.
Suna zilizo ndani ya swala.
c.
Suna zilizo baada ya swala.
a./.
SUNA
ZILIZO KABLA YA SWALA.
Haya ni mambo ambayo mwenye kuswali anatakiwa
kuyatenda kabla hajaingia ndani ya swala, haya hayazidi mambo matatu ambayo
ni:
(i)
Adhana
(ii)
Iqaamah.
Inshaalah, tutazielezea adhana na Iqaamah kwa
ufafanuzi wa kutosha katika somo la pili.
(iii)
Kuweka sitara mbele.
Ni suna kwa mwenye kuswali kuweka kitu mbele yake
kitakachokuwa ni sitara baina yake na wale wapitao mbele yake. Sitara hii
inaweza kuwa ni ukuta au nguzo ya msikiti, akaswali karibu na ukuta au nyuma
ya nguzo. Au anaweza kuweka fimbo mble yake au kitu kingine mithili ya hivyo.
Kama hakupata sitara kabisa, basi anaweza kuchora/kupiga mstari. Imepokelewa
kutoka kwa Ibn Umar- Allah awaridhie kwamba Mtume wa Allah – Rehema na Amani
zimshukie – alikuwa anapotoka siku ya Eid (kwa ajili ya swala) huamrisha (uletwe) mkuki wake na huwekwe mbele yake, naye huswali kwa
kuuelekea na il-hali watu (wakiswali) nyuma yake. Na hivyo ndivyo alivyokuwa
akifanya awapo safarini. Bukhaariy na Muslim.
Na ni bora sitara ikawa
karibu na mahala pake pa kusujudia. Hili linatokana na riwaya iliyopokelewa
kutoka kwa sahli Ibn Sa’ad –
Allah amuwiye radhi – amesema: Ulikuwa (Umbali) wa baina ya muswala (mahala
pa kusujudia) wa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie na ukuta wa
msikiti ni (kama) mapito ya mbuzi (nafasi awezayo kupita mbuzi). Bukhaariy na Muslim.
|