Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

C) SUNA ZILIZO (ZINAZOFUATIA) BAADA YA KUMALIZIKA SWALA

 

9:      Takbiyrah za kugura

Tumeshajua katika masomo yaliyotangulia kwamba “Takbiyrah ya kuhirimia swala” ni nguzo ambayo swala haisihi bila ya kuileta. Takbiyrah hii ndio inayoashria mwanzo wa swala na kwamba tayari umo ndani ya swala. Sasa unapokuwa ndani ya swala ndipo inapokuja suna ya “Takbiyrah za maguro”. Hizi ni kusema mwenye kuswali (ALLAAU AKBAR) wakati

-   Anapokwenda rukuu

-   Anapokwenda sijda, na

-   Anapoinuka kutoka sijda aidha kuja katika kitako baina ya sijida mbili au kuja kuanza rakaa nyingine.

 

ANGALIA si suna kuleta “Takbiyrah ya kugura” wakati wa kuinuka kutoka rukuu kuja itidali bali suna ni kusema: SAMIA’ -LLAHU LIMAN HAMIDAH. Haya yote ndiyo maelekezo tunayoyaopata kutokana na hadithi aliyoipokea Abuuu Hurayrah Allah amuwiye radhi amesema Alikuwa Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie anaposimama kwenye swala hukabiri (huleta Takbiyrah) wakati anaposimama (Qiyaamu) na hukabiri anaporukuu, kisha husema: SAMIA’ -LLAHU LIMAN HAMIDAH wakati anapounyoosha mgongo wake kutoka rukuu, halafu ndipo husema akiwa amesimama wima: RABBANAA WALAKAL-HAMDU. Kisha hukabiri wakati anapoporomokea sijida, halafu hukabiri (tena) wakati anapoinua kichwa chake (kutoka sijida ya kwanza. Halafu hukabiri (tena) wakti anaposuiju (sijida ya pili) kisha hukarbiri (tena) wakati anapokiinua kichwa chake (kuja kuanza rakaa nyingine). Halafu hufanya hivi hivi katika swala yote mpaka anapoimaliza na kukabiri (pia) wakati anapoinuka kutoka katika rakaa mbili (za mwanzo) baada ya kjitako (cha tashahudi ya kwanza).” Bukhaary na Muslim.

 

10.    Tasbihi za rukuu na sijida:

Ni suna kwa mwanamume ajiachie wakati wa kurukuu na kusujudu yaani ngoko za mikono yake zisigusane na mbava zake. Ama mwanamke, suna kwake ni kujikusanya, yaani ngoko zake zigusane na mbavu zake bila ya kuachia nafasi. Kisha ni suna aseme ilhali ametulizna katika rukuu: SUB-HAANA RABBIYAL-A’DHIM Mara tatu, na asema katika sijida SUB-HAANA RABBIYAL-A’ALAA Mara tatu. Hivi ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Hudhayfah Ibn Alyamaan Allah amuwiye radhi amesema “Niliswali pamoja na Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie alipoenda rukuu akawa akisema: SUB-HAANA RABBIYAL-A’DHIM Kisha alisujudu na akasema SUB-HAANA RABBIYAL-A’ALAA.” Muslim na Ibn Hibbaan.

 

11.    Kuweka mikono (vitanga) mwanzoni mwa mapaja katika vitako vya tashahudi.

Namna ya uwekaji ni mtu kukitandika/kukikunjua kitanga cha kushoto ilhali amevikusanya pamoja vidole bila ya kuvitawanya kiasi ambacho ncha za vidole zitakuwa zimeelekeana na mwanzo wa goti. Akikunje kitanga cha kulia isipokuwa kidole cha shahada, hiki atakikunjua kwa kukiinamisha mwanzoni mwa tashahudi mpaka atakapofikia kusema ILLA-LLAH ndipo atakiinua kuashiria kwamba Allah ni mmoja. Na ni suna aendelee kukiinua bila ya kukitikisatikisa mpaka mwisho wa swala, yaani kutoa salamu. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar Allah awawiye radhi amesema katika kuuelezea ukaaji wa mtume Rehema na Amani zimshukie Alikuwa anapokaa ndani ya swala huweka kitanga chake cha kulia juu ya paja lake la kulia na akakunja vidole vyake vyote na akaashiria kwa kidole chake ambacho kinachokifuatia kidole gumba (cha shahada) Na huliweka kitanga chake cha kushoto juu ya paja lake la kushoto.” Muslim.

 

12. Mkao wa “Tawaruki” katika kikazi ha mwisho na mkao wa “Iftiraashi katika vikazi vingine vyote.

“Tawaruki” huu ni aina ya mkao ambao mwenye kuswali hulikalia tako lake la kushoto na akaunyoosha mguu wake wa kulia na kuutolea ule wa kushoto chini yake (ule wa kulia) Na “Iftiraahsi” ni mkao ambapo mtu hukikalia kisigino cha mguu wake wa kushoto na kuunyoosha ule wa kulia kwa kuziweka chini ncha za vidole. Imepokelewa kutokana na hadithi ya Abuu Humayd Allah amuwiye radhi amesema: Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie kuliko nyie (na akasema katika sehemu ya hadithi hiyo): Na anapokaa katika zile rakaa mbili (za mwanzo) huukalia mguu wake wa kushoto na kuukunjua ule wa kulia (Tawaruki). Na anapokaa katika ule mkao wa mwisho huutanguliza mguu wake wa kushoto (yaani chini ya mguu wake wa kulia aliounyoosha) na akaunyoosha ule mwingine na akayakalia makalio (matako) yake.” Bukhaariy

 

13.    Kumswalia Mtume kwa kutumia “Swalaatu Ibraahimiyyah” kasha kumba dua baada ya Tashahudi ya mwisho.

Tayari umekwishafahamikiwa katika masomo yaliyotangulia kwamba kumswalia Mtume ni nguzo miongoni mwa nguzo za swlaa ambazo swala haisihi kama hazikuletwa: Nguzo hii hutekelezwa kwa kumswalia mtume kwa tamko lo lote lile linalobeba maana ya kumswalia. Lakini suna kumswalia kwa kuleta “Swalaatu Ibraahimiyyah,” hii ni kusema

 

ALLAHUMMA SWALLI ALAA MUHAMMAD WA ‘ALAA AALI MUHAMMAD KAMAA SWALLAYTA ALAA IBRAHIM WA ‘ALAA AALI IBRAHIM, WABARIK ALAA MUHAMMAD WA ‘ALAA AALI MUHAMMAD KAMAA BAARAKTA ‘ALAA IBRAHIM WA ‘ALAA AALI IBRAHIM INNAKA HAMIIDUN MAJIID

Bukhaariy

 

Akimaliza kumswalia mtume kwa tamko hili au kwa matamko mengine ni suna amuombe Mola wake amkinge/amuepushe na adhabu ya kaburi, na adhabu ya moto. Au aombe dua yo yote aitakayo kwa shariti asitwawilishe (asiirefushe) dua hiyo zaidi ya muda ule anaoutumia kusoma tashahudi na kumswalia mtume.

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah Alah amuwiye radhi amesema: Amesema Mjume wa Allah Rehema na Amani zimshukie:- “ Atakapomaliza mmoja wenu (kusoma) Tashahudi ya mwisho, basi na ajilinde kwa Allah dhidi ya mambo manne: adhabu ya moto wa Jahanamu, adhabu ya kaburi, na fitina ya uhai na kifo na shari ya masihi Dajali.” Muslim

 

14.    Salamu ya pili

Tumeeleza katika darasa zilizopita kwamba salamu ya kwanza katika swala, ambayo hii ndio huashiria kumalizika kwa swala ni nguzo. Hii ni ile inayoambatana na kugeuka upande wa kulia wakati wa kuitoa. Pamoja na kwama salamu hii ya kwanza inamaanisha kumalizika kwa swala lakini ni suna kuongezea kutoa salamu ya pili huku ukigeukia upande wa kushoto. Hivi ndivyo alivyopokea Ibn Masoud Allah amuwiye radhi kwamba Mtume wa Allah Rehema na amani zimshukie alikuwa akitoa salamu kuliani na kushotoni kwake mpaka unaonekana weupe wa shavu lake ASSALAAM ‘ALEYKUM WARAHMATULLAH, ASSALAAM ‘ALEYKUM WARAHMATULLAH

Abuu Daawoud

 

Miongoni mwa dua alizokuwa akiomba Bwana mtume ni ile iliyopokelewa na Imamu Aliy Allah amuwiye radhi kwamba Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie “Alikuwa akisema baina ya Tashahudi na salamu.

ALLAHUMMA-GHFIR LII MAA QADDAMTU WAMAA AKHHARTU WAMAA ASRARTU WAMAA A’LANTU WAMAA ASRAFTU WAMAA ANTA A’LAMU BIHI MINNIY ANTALMUQADDIM WA ANTALMUAKHHIR LAA ILAHA ILLA ANTA

Muslim

 

Hizi zote kwa ujumla ndizo suna zinazoitwa “hay-aata”, suna hizi kama tulivyotangulia kueleza mwenye kuswali akiacha ye yote miongoni mwake si suna kwake kuiunga kwa kuleta “sijidat sahau”.



Forum | Guestbook | Tuandikie |