|
Maana:
Hizi ni zilizomo ndani ya swala ambazo hakukusuniwa kuleta sijida
mbili za kusahau iwapo mwenye kuswali ataacha kuzileta.
1. Kunyanyua
mikono wakati wa kuleta Takbiyra ya kuhirimia, kwenda na kutoka rukuu.
Namna ya
utekelezaji wa suna hii ni mtu kuinyanyua mikono yake na kuyaelekeza kibla
matumbo ya vitanga vya mikono hali ya kuvikunjua vidole. Akivielekezea
vidole gumba vyake ndewe za masikio yake.
Suna hii
ya unyanyuaji wa mikono mwanzoni mwa swala imepokelewa na maswahaba
khamsini, miongoni mwao ni wale kumi walobashiriwa pepo na Bwana Mtume na
hakuna Imamu hata mmoja aliyeipinga suna hii.
i./ Imepokelewa
kutoka kwa Ibn Umar Allah awawiye radhi amesema: Nilimuona Mtume wa Allah
Rehema na Amani zimshukie akiifungua swala kwa takbiyrah, akainyanyua
mikono yao wakati alipoleta takbiyrah mpaka ikawa welekea wa mabega
(mkabala) yake. Na anapoleta takbiyrah ya kwenda rukuu hufanya hivyo
hivyo. Na anaposema:
SAMI’A-LLAHU
LIMAN HAMIDAH
hufanya hivyo
hivyo na akasema RABBANAA WALAKAL-HAMD Wala hafanyi hivyo wakati
anaposujudu wala wakati anapokimyanyua kichwa chake kutoka sijida”.
Bukhaariy na Muslim
ii./
Imepokelewa na Imamu Aliy Ibn Abiy Twaalib Allah amridhie kwamba:
“Alikuwa Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie anaposimama kuswali
swala ya fardhi, huleta takbiyrah na akainyanyua mikono yake mkabala wa
mabega yake. Hufanya kama hvi anapomaliza kisomo chake (cha Al-hamdu na
sura) na akataka kurukuu. Na hufanya hivyo anapoinuka kutoka rukuu. Wala
hainyanyui mikono yake katika sehemu ye yote ya swla yake akiwa amekaa. Na
anapoinuka kutoka katika sijida mbili hizo (kuja kuanza rakaa nyingine)
kadhalika huinyanyua mikono yake na akakabiri (akaleta takbiiyrah)”
Bukhaariy, Tirmidhiy, Abuu Daawoud na Ahmad., kutokana na hadithi sahihi
hizi inatudhihirikia kwamba ni suna kunyanyua mikono kwa sura/namna
tuliyoieleza katika sehemu nne ndani ya swala:-
1. Wakati wa Takbiyra ya kuhirimia swala.
2.
wakati wa kwenda rukuu
3.
wakati wa kuinuka kutoka rukuu (itidali) na
4.
wakati wa kutoka sijida ya pili kuja Qiyaamu (kisimamo cha rakaa
nyingine)
2. Kuweka mkono
wa kulia juu ya ule wa
Baada ya
kuhirimia swala, kuleta takbirah na kuinua mikono kama ilivyobainishwa na
hadithi, ni suna kuweka mkono wa kulia juu ya ule wa kushoto. Namna yake
ni kuweka kitanga cha mkono
wake wa kulia juu ya mgongo wa kitanga cha kushoto chini ya kifua na juu
ya kitovu.
Haya yanatokana
na riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Wail Ibn Hujri Allah amuwiye radhi
kwamba yeye alimuona Mtume wa Allah akiinyanyuua mikono yake anaopingia
ndani ya swala --- kasha akawkea mkono wake wa kulia juu ya ule wa
kushoto.” Muslim.
3.
Kuangalia mahala anaposujudu
Ni karaha kwa
mwenye kuswali kuyapepesa macho yake huku na kule ndani ya swala. Bali ni
suna adumishe kuangalia chini mahala anaposujudu ila wakati wa tashahudi.
Katika tashudhi suna in kukiangalia kidole cheke cha shahada. Imepokelewa
kutoka wa Anas Ibn Maalik Allah amuwiye radhi kwamba amesema mtume wa
Allah Rehema na Amanui zimshukie: “Wana nini watu wanaonyanyua macho yao
kutazama juu ndani ya swala zao, wakomeke (waache) kufanya hivyo au
yatangyakuliwa yatanyakuliwa macho yao.” Bukhaariy na Muslim. Zote
dalili kubwa katika suna zote hizi ni suala zima la kumfuata mtume, kwani
ndiye aliyesema: “Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”.
Na hivyo ndivyo
alivyoonekana Mtume wa Allah akiswali na kunukuliwa kwetu na maswahaba
wake.
4. Kusoma dua ya
ufunguzi wa swala;
Alikuwa Mtume wa
Allah Rehema na Amani zimshukie akimuomba Mola wake kwa aina mbalimbali za
dua baada ya takbiyrah ya kuhirimia na kabla ya kuanza kusoma Suuratil
Faatiyhah (Al-hamdu). Miongoni mwa dua alizokuwa akiziomba ni ile iliyomo
katika riwaya iliyopokelewa na Aliy Ibn Abiy Twaalib Allah amuwiye radhi
kwamba Mtume wa Allah Rehema na amani zimshukie alikuwa anaposimama ndani
ya swla shukie alikuwa anaposmama ndani ya swala husema:
WAJJAHTU
WAJHIYA LILLADHI FATARASSAMAWATI WAL-ARDHI, HANIIFAN WAMAA ANA
MINALMUSHRIKIIN. INNA SWALAATIY WANUSUKIY WAMAHYAAYA WAMAMAATIY LILLAHI
RABBIL-‘ALAMIIN, LAA SHARIKA LAHU WABDIHALIKA UMIRTU WA ANA
MINAL-MUSLIMIIN
Muslim
Kutokana
na hadithi hii na nyinginezo imethibiti kuwa ni suna kusoma dua ya
ufunguzi wa swala katika swala ya fardhi au ile ya suna. Suna hii
inawahusu wote, Imamu, maamuma na hata yule mwenye kuswali pekee. Mahala
pa kuilete suna hii ni kabla ya kuanza kuisoma suuratil Faatihah. Akianza
tu kuisoma, basi suna hii itakuwa imefutu na hatakiwi kuikata Alhamdu na
kurudi kuisoma dua hii ya ufunguzi hata kama alifanya hivyo kwa kukosea au
kusahu. Pia ni vema ikakumbukwa kwamba ni suna kuleta dua ya ufunguzi
katika swala ya maiti wala katika swala ya fardhi wakati
utakapodhiki/utakapokuwa finyu kiasi cha kuchelea kutoka kwa wakati
5.
Istiaadha.
Ni suna thabiti
kutoka kwa Mtume, mwenye kuswali alete “Istaadha” baada ya kumaliza
kusoma dua ya ufunguzi na kabla ya kuanza kusoma suuratil aatihah.
Istiaadhah ni kusema.
AUDHU BILLAHI
MINASHHAITAANIR-RAJIIM kwa kulitekeleza agizo la Allah: “NA UKITAKA
KUOSMA QURANI PIGA AUDHU (kwanza, jikinge) KWA ALLAH (akulinde) NA SHETANI
ALIYEFUKUZWA (katika rehema yake Allah).” [16 : 98]
6.Kujihirisha
na kusirisha kisomo katika sehemu zake:
Sehemu/mahala
ambamo ni suna kujihirisha kisomo (kusoma kwa sauti yenye kusikika) ni:-
i.
Rakaa mbili za swala ya Alfajiri.
Hili
linatokana na hadithi ya Ibn Abbaas Allah amuwiye radhi alipokuwa
akisimulia kuhudhuria kwa majini na kuisikiliza Qurani kwa Mtume Rehema na
Amani zimshukie sehemu ya hadithi inasema Na ilhali yeye (Mtume)
akiwaswalisha maswahaba wake swalatil fajri, waliposikia (majini) Qur-ani
hiyo (iliyokuwa ikisomwa na Mtume] walikaa kusikiliza.” Bukhaariy na
Muslim
Imepokelewa
na Ubaadah Ibn Swaamit Allah amuwiye radhi tulikuwa nyuma ya Mtume Rehema
na Amani zimshukie katika swala ya Alfajiri, kisomo kikamuwiya uzito
(akakwama). Alipomaliza swala akasema: “Huenda nyinyi mnasoma nyuma ya
imamu wenu.” Akasema (ubaadah) tukasema ewe Mtume wa Alah, ndiyo wallah.
Akasema: “Msisome ila Ummul Qurani (Suuratul faatihah), kwani hana swala
asiyeisoma.” Abuu Daaoud na Nasaai. Na katika riwaya nyingine:
“Msisome cho chote katika Qurani nitakapojihirisha kusoma (Qurani) ila
(someni) Ummul Qurani
Hadithi
hizi zinafahamisha kwamba Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie alikuwa
akijihirisha kisomo chake (cha Qurani) kiasi cha kusikiwa na maamuma wake.
ii.
Rakaa mbili za mwanzo za swala za magharibi na Ishaa.
Haya
ni kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Baraa Allah amuwiye radhi
amesema Nilimsikia Mtume Rehema na Amani zimshukie akisoma: “Wattiyn
waz-zaytuun”. Katika swala ya Ishaa. Na sikupatapo kumsikia mtu mwenye
sauti nzuri kuliko yeye” Bukhaariy na Muslim
iii. Swala
za Ijumaa, Eid mbili, ya mfunguo mosi na mfunguo tatu, swala ya kupatwa
kwa mwezi, swala ya kuomba mvua, swala ya taraweh, swala ya witri ya
Ramadhan.
Humu
ndimo mahala ambamo ni suna mtu kusoma Qurani kwa sauti ndani ya swala kwa
ushahidi wa hadithi nyingi sahihi zilizothibiti kutoka kwa Bwana mtume
sehemu nyingine zote ambazo hatukuzitaja atasoma kwa kusirisha (bila ya
kutoa sauti).
Imepokelewa
kutoka kwa khabaab Allah amuwiye radhi alipoullizwa na muulizaji: Je,
Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie alikuwa akisoma katika swala ya
Adhuhuri na Alasiri akajibu. Nido tukamuuliza tena mlikuwa mkilijuaje hilo
(kwamba yeye anasoma). Akajibu kutokana na kuchezacheza kwa ndevu zake
Bukhaariy.
7. Kuitikia
Aamiyn inaposomwa suuratil faatihah
uitikjiaji huu
ni kuifuatishia kauli ya Allah iliyoko mwishoni mwa suuratil faatihah na
tamko “Aaamiyn.”
Kuitikia
“Aaamiyn” mara tu baaada ya kumaliza kusoma suuratil Faatihah ni suna
kwa kila anaye swali, Imamu, maamuma na mwenye kuswali pekee. Ataitikia
kwa sauti katika swala inayoswaliwa kwa kutolewa sauti na bila ya kutoa
sauti katika swala iswaliwayo bila ya kutolewa sauti. Na maana ya kiitikio
hiki “Aamiyn” ni tukubalie itupokelee swala/dua yetu hii ewe Bwana
Mlezi wetu. Uitikiaji huu wa “Aaamiyn” tunaupata kutokana riwaya
zilizopokelewa na Abuu Hurayrah Allah amuwiye radhi amesema
“Atakapoitikia Imamu “Aaamiyn” nanyi itikieni, kwani mwenye
kuwafikiana Aamiyn yake na Aamiyn ya malaika hughufiriwa dhambi zake
zilizotangulia.” Bukhaariy na Muslim.
Amesema
Abuu Huayrah alikuwa Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie anaposoma
WALADHWAALIIN husema/huitikia: Aaamiyn, mpaka huweza kumsikia
wanaomfuatia, yaani watu wa safu ya kwanza.Abuu Daawoud.
Imamu Ibn
Maajah akazidisha katika riwaya yake: “--- Na msikiti mzima ukaripuka
kwa kuitikia Aaamiyn.”
8. Kusoma
sehemu ya Qur-ani baada ya suuratil Faatihah:
suna hii
huthibiti kwa kusoma sura ye yote ndani ya Qur-ani hata ikiwa ni fupi au
kwa kusoma aya tatu zenye kufuatana. Suna hii hutekelezwa katika rakaa
mbili za mwanzo za kila swala, kwa imamu na mwenye kuswali pekee
(munfarid). Pia suna hii humuhusisha maamuma katika swala inayoswaliwa
bila ya kutoa sauti au, maamuma anapokuwa mbali, mahala ambapo hakisikii
kisomo cha imamu wake.
Ni suna
kwa mwenye kuswali asome “sura ndefu kiasi” kama vile Hujuraat {49},
Rahmaan {55} na kadhalika katika swala za Alfajiri na Adhuhuri, katika
swala za alasiri na Ishaa, asomo “Sura za kati na kati” kama vile
As-shamshi {91}, Al-layli {92} na kushuka chini, katika swala ya Maghribi
asome “sura fupi” kama vile Ikhalaaswi {112}. Hivi ndivyo
tunavyojifunza kutokana na hadithi iliyopokelewa na Sulayman Inb Yasaari
nae akipokea kutoka kwa Abuu Hurayrah Allah awawiye radhi amesema Sijapata
kuswali nyuma ya mtu yeyote swala inayoshabihiana kabisa na ya Mtume wa
Allah Rehema na Amani zimshukie kuliko mtu Fulani. Tuliswali nyma ya mtu
huyu (akisoma sura ndefu) katika rakaa mbili za mwanzo za swala ya
Adhuhuri na kaikhafifisha katika zile mbili nyingine. Na akikhafifisha
(akisoma sura fupi) katika swala ya Alasiri na akisoma katika swala ya
Maghribi sura fupi. Na akisoma katika swala ya Ishaa “Was-shamsi
wadhuhaa” na mfano wake, na katika swala ya sub-hi akisoma sura mbili
ndefu.” Nasaai
Faida
i./ Ni suna
kusoma katika swala ya sub-hi ya siku ya Ijumaa Suuratis Sajidah (32)
katika rakaa ya kwanza na Al-insaan (76) katika rakaa ya pili. Hili
linapatikana katika riwaya ya Abuu Hurayrah Allah amuwiye radhi amesema:
Mtume Rehema na Amani zimshukie alikuwa akisoma katika swala ya Alfajiri
ya siku ya Ijumaa ALIF LAAM MIIM TANZIIL As-sajidah na Al-insaan.
Bukhaariy na Muslim
ii./
Kadhalika ni suna katika swala zote kuirefusha rakaa ya kwanza kuliko ile
ya pili kama ilivyopokelewa: “mtume Rehema na Amani zimshukie alikuwa
akirefusha katika rakaa ya kwanza na kufupisha katika rakaa ya pili.”
Bukhaariy na Muslim
|