|
8.
Baada ya Kuitikia “Aamiyn”, soma sura
nyingine au sehemu ya sura yoyote lakini bora ni
kusoma sura kamili. Hiyo ndiyo swala ya Mtume
kama alivyotupokelea Abuu Qataadah-Allah amwie
radhi- “Kwamba Mtume Rehema na Amani
zimshukie- alikuwa akisoma katika swala ya
Adhuhuri katika rakaa mbili za mwanzo Ummul
Kitaab (Al-hamdu) na sura mbili (nyingine) na
katika zile rakaa mbili nyingine (za mwisho
akisoma) Ummul-Kitaab pekee …” Bukhariy
9.
Kisha nyanyua vitanga vyako mpaka mkabala wa
mabega na uende rukuu il-hali ukisema ALLAHU
AKBAR, na kufanya hivyo ni kuitii kauli ya Mola
wako isemayo “MLIYOAAMINI! RUKUUNI NA SUJUDUNI
NA MWABUDUNI MOLA WENU NA FANYENI MEMA ILI MPATE
KUFAULU” [22:77]. Katika rukuu weka vitanga
vyako magotini, nyoosha mgongo wako na
utulizane. Hivi ndivyo alivyosema Mtume
wako-Rehema na Amani zimshukie- wakati alipokuwa
akimfundisha swala yule mtu aliyekuwa akiswali
sivyo, akamwambia : …Halafu rukuu mpaka
utulizane il-hali umerukuu …” Bukhaariy. Ama
uwekaji wa vitanga magotini, imepokelewa kwa
Saalim Al-Barraad Al-kuufiy amesema :
Tulimwendea Abu Mas-oud, tukamwambia :
-Tuhadithie kuhusiana na swala ya Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie, akasimama mbele
yetu akakabbbir, aliporukuu akaweka vitanga
vyake juu ya magoti yake na vidole vyake
akaviweka chini ya hapo …” Nasaai.
Ukishatulizana katika rukuu ndipo useme mara
tatu au zaidi : SUBHAANA RABBIYAL-ADHIIM. Hii
ndiyo swala ya Mtume kama ilivyopokelewa kutoka
kwa Hudhayfah Ibn Al-yamaan – Allah amwie
radhi – amesema : “Niliswali pamoja na Mtume
wa Allah – Rehema na Amani zimshukie –
aliporukuu akawa akisema : SUBHAANA
RABBIYAL-ADHIIM … Muslim na Ibn Hibbaan.
10.
Baada ya Kukamilisha rukuu, inuka kutoka rukuu
il-hali ukisema SAMIA’-LLAHU LIMAN HAMIDAH na
usimame ukiwa umetulizana. Hayo ndiyo mafundisho
ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
alipomfundisha yule mtu aliyekuwa akikosea
katika swala yake : “… Kisha rukuu mpaka
utulizane hali ya kurukuu, kisha inuka mpaka
utulizane hali ya kusimama …” Ibn Maajah.
Kisha ukilingana sawa hali ya kusimama sema
katika itidali hiyo RABBANAA LAKAL-HAMDU. Haya
yote yamepokewa kutoka kwa Abuu Hurayrah –
Allah amuwie Radhi - : “… Kisha husema
SAMIA’L-LAHU LIMAN HAMIDAH wakati
anpounynanyua uti wa mgongo wake kutoka rukuu,
kisha husema naye akiwa amesimam : RABBANAA
LAKAL-HAMDU …” Bukhaariy
11.
Halafu poromoka kwenda kusujudu il-hali ukisema
(Allahu Akbar), usujudu kwa viungo saba.
Hakikisha uso, vitanga (viwili) magoti (mawili)
na miguu (nyayo mbili) vyote hivi viguse ardhi
(busati/mkeka). Kusujudu kunatokana na kauli ya
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-wakati
akifundisha swala : “..kisha usujudu mpaka
utulizane hali ya kusujudu …” Bukhariy na
Muslim.
Ama
kuhusiana na viungo vinavyohusika na sijida,
imepokelewa na Ibn Abbaas – Allah awawiye
radhi – kwamba Mtume wa Allah – Rehema na
Amani zimshukie – amesema : “Nimeamrishwa
kusujudu juu ya viungo saba, juu ya paji la uso,
akaiashiria pua yake kwa mkono (kidole) na
mikono (miwili) na magoti (mawili) na ncha (za
vidole) vya miguu …” Bukhaariy na Muslim.
Ukishatulizana katika sijida sema : SUBHAANA
RABBIYAL-A’LA mara tatu au zaidi. Hivyo ndivyo
alivyoswali Mtume wa Allah kama anavyotueleza
Hudhayfah Ibn Al-yamaan –Allah amuwie radhi
– “Niliswali pamoja na Mtume wa Allah –
Rehema na Amani zimshukie- aliporukuu akawa
akisema : SUBHAANA RABBIYAL-ADHIIM kisha
akasujudu na akasema : SUB-HAANA RABBIYAL-A’LA
..” Muslim.
Pia
imethibiti kwamba wakati mwingine Mtume wa Allah
– Rehema na Amani zimshukie – alikuwa
akisema katika sijida yake : SUB-HAANA
RABBIYAL-A’LA WA BIHAMDIH na katika rukuu
(akisema) SUB-HAANA RABBIYAL-ADHIM WABIHAMDIH.
Hivyo ndivyo alivyopokea Daaruqutwniy.
12.
Kisha inuka kutoka sijida il-hali ukisema
(Allahu Akbar) ukae kitako mkao wa iftiraashi na
useme : ALLAHUMMAGHFIR LII WARHAMNII WA
A’AFINIY WAHDINII WARZUQNII Hivyo ndivyo
alivyoelekeza Mtume wa Allah – Rehema na Amani
zimshukie - : “…Kisha usujudu mpaka
utulizane hali ya kusujudu, halafu inuka mpaka
itulizane hali ya kukaa …Bukhariy na Muslim.
Ama
dhikri hiyo ya kitako inatokana na ile hadithi
ya Ibn Abbaas – Allah awawie radhi – amesema
: “Alikuwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani
zimshukie – akisema baina ya sijida mbili :
ALLAHUMAGHFIR LII WARHAMNII WA A’FINIY
WAHDINIY WARZUQNIY” Abu Daawud, Tirmidhiy na
Muslim. Na katika riwaya ya Baihaqiy kuna ziada
: WAJBURNIY WARFA’NIY.
Kisha
sema Allahu Akbar huku ukienda kusujudu sijida
ya pili kama ulivyosujudu ile ya kwanza. Sijida
hii ya pili imo katika ile kauli ya Mtume –
Rehema na Amani zimshukie – “…Kisha sujudu
mpaka utulizane hali ya kusujudu (sijida ya
kwanza), halafu inuka mpaka utulizane hali ya
kukaa (kitako baina ya sijida mbili), kisha
sujudu (tena) mpaka utulizane hali ya kusujudu
(sijida ya pili) … Bukhariy na Muslim.
Kwa
kufuata utaratibu huu tulioutaja, mpaka hapo
itakuwa imetimia na kukamilika rakaa ya kwanza.
Sasa inuka kutoka kutoka sijida il-hali ukisema
Allahu Akbar mpaka usimame wima tayari kuanza
rakaa ya pili. Hii rakaa ya pili utaiswali kama
ulivyoiswali ile ya kwanza. Isipokuwa katika hii
rakaa ya pili hakuna tena kuleta nia ya
Iftitaahi (Dua ya ufunguzi). Kadhalika rakaa hii
ya pili isiwe ndefu kama ile ya kwanza, hivi
ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Abuu Qatadah
– Allah amuwie radhi - : “…na
akiitwawilisha (akirefusha) katika rakaa ya
kwanza asivyotwawilisha katika rakaa ya pili
…”Bukhaariy.
13.
Baada ya kutoka katika sijida ya pili ya rakaa
ya pili, kaa kitako usome tashahudi ya kwanza
ikiwa swala uiswaliyo ni ya rakaa tatu au au nne
kama Magharibi na Isha. Hivi ndivyo
iliyopokelewa katika hadithi ya yule mtu
aliyekuwa akiswali sivyo ndivyo, Mtume –
Rehema na Amani zimshukie – akamwambia :
“…utakapokaa kitako katikati ya swala, basi
tulizana na (ukae mkao wa Iftiraashi) ulitandike
paja lako la kushoto, kisha ulete tashahudi
…” Abu Daawoud. Na tashahudi ni kama
ilivyopokelewa kutoka kwa Ibn Abbaas – Allah
awawie radhi – kwamba yeye amesema : Alikuwa
Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie –
akitufundisha Tashahudi kama anavotushinda sura
ya Qur-ani, alikuwa akisema : ATTAHIYYATU
ALMUBARAKATU, ASSWAALAWATU ATTAYIBAATU LILLAHI,
ASSALAAMU ALAYKA AYYUHANNABII WARAHMATULLAHI
WABARAKATUH, ASSALAAMU ALAYNA WA A’LAA
IBADILLAHI SSWALIHIIN, ASH-HADU AN LAA ILAHA
ILLALLAH, WA ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN
RASULULLAH” Muslim
Baada
ya kumaliza kusoma tashahhudi kama ilivyopokewa
kutoka kwa Bwana Mtume, sasa inuka huku ukisema
Allahu Akbar, uiinue mikono yako mkabala wa
mabega, funga swala. Hivi ndivyo ilivyopokelewa
kutoka kwa Abuu Humayd As-saaidiy : “ …
Kisha hukabiri anapoinuka kutoka katika rakaa
mbili (za mwanzo) na huinyanyua mikono yake
mpaka mkabala wa mabega yake …” Abu Daawoud.
Swali
rakaa ya tatu na ya nne kama rakaa mbili za
mwanzo. Lakini katika rakaa mbili hizi za mwisho
baada ya Al-hamdu husomi sura nyingine wala
husomi Al-hamdu kwa sauti ikiwa swala uiswaliyo
huswaliwa kwa kutoa sauti.
14.
Baada ya sijida ya pili ya rakaa ya tatu ya
swala ya Magharibi au sijida ya pili ya rakaa ya
nne ya swala za adhuhuri, alasiri, na ishaa.,
kaa mkao wa tawaruki na usome tashahudi ya
mwisho. Lete tashahudi kama tulivyokwisha itaja,
halafu umswalie Bwana Mtume kabla ya kutoa
salamu. Kumswalia Bwana Mtume ndani ya swala na
kulitekeleza agizo la Allah : HAKIKA ALLAH
ANAMSWALIA MTUME (anamteremshia rehema) NA
MALAIKA WAKE WANAMSWALIA (wanamuombea dua).
BASI, ENYI MLIOAMINI MSWALIENI (Mtume, muombeeni
rehema) NA MUOMBEENI AMANI” [33:56].
Imepokelewa kutoka kwa Abdulrahman ibn Abiy
Laylaa, amesema : Nilikutana na Ka’bu ibn
Ujrah akaniambia : Je, nikupe hidaya (zawadi)
niliyoisikia kutoka kwa Mtume –Rehema na Amani
zimshukie - ? Nikasema : Kwani, nipe, akasema :
Tulimuuliza Mtume wa Allah – Rehema na Amani
zimshukie – tukasema : Ewe Mtume wa Allah,
tukuswalieni vipi enyi Ahlul-bayti, kwani Allah
ametufundisha jinsi ya kukuombeeni amani.
Akasema (Mtume) : “Semeni : ALLAHUMMA SWALLI
ALAA MUHAMMAD WA A’LAA
AALI MUHAMMAD KAMAA SWALLAYTA ALAA
IBRAHIM WA A’LAA AALI IBRAHIM INNAKA HAMIDUN
MAJIID. ALLAHUMMA BAARIK ALAA MUHAMMAD WA
A’LAA AALI MUHAMMAD KAMAA BAARAKTA ALAA IBRAHIM WA A’LAA AALI
IBRAHIM INNAKA HAMIDUN MAJIID. Bukhaariy, Muslim
na Baihaqiy.
15.
Kisha toa salamu kwa kusema : ASSALAAMU ALAYKUM
WARAHMATULLAH huku ukigeukia kuliani na toa
salamu ya pili huku ukigeukia kushoto.
Imepokelewa na Bi Aysha – Allah amwie radhi
– amesema : “Alikuwa Mtume wa Allah –
Rehema na Amani zimshukie – akiifungua swala
kwa Takbiyrah na kuikhitimisha kwa salamu.”
Abu Daawoud na Baihaqiy. Imepokelewa kutoka kwa
Sa’d ibn Abiy Waqqaaswi – Allah amuwie
radhi- amesema : “Nilikuwa nikimuona Mtume wa
Allah – Rehema na Amani zimshukie – akitoa
salamu kuliani na kushotoni kwake mpaka nikiuona
weupe wa kitefute (shavu) chake.” Muslim.
Imepokelewa
kutoka kwa Ibn Mas-oud – Allah amwie radhi –
amesema : “Sijasahau mambo, kwani mimi bado
sijaisahau utoaji salamu wa Mtume wa Allah –
Rehema na Amani zimshukie – kuliani na
kushotoni kwake : ASSALAAMU ALEYKUM
WARAHMATULLAH ASSALAAMU ALEYKUM WARAHMATULLAH.
Ibn Hibbaan na wengineo.
Hiyo
ndio swala ya Mtume na kwa kuswali hivyo utakuwa
umeikubali na kuitekeleza kivitendo kauli na
agizo la Mtume : “Swalini kama mlivyoniona
mimi nikiswali” Bukhariy.
HITIMISHO
(KIJALIZO):
Huenda
wewe msomaji wetu mpenzi ukawa unajiuliza kama
wanavojiuliza wengine na kusema :
Allah-Subhanahu Wa Ta’ala anasema
ndani ya Qur-ani : “…BILA SHAKA SWALA
HUMZUILIYA (huyo mwenye kuswali na) MAMBO
MACHAFU NA MAOVU …” [29:45].
Ikiwa
ndivyo hivi, mbona tunawaona baadhi ya watu
wanaswali kila siku na bado wana mambo machafu
na maovu ?! Tabia zao mbaya, maneno yao machafu
na mienendo yao miovu !
Jawabu
sahihi la swali hili ni kwamba watu hawa
hawajaisimamisha swala kwa namna sahihi
itakiwayo ambayo iliyopokelewa kutoka kwa Mtume
wa Allah – Rehema na Amani zimshukie.
Hawajaswali bado kama alivyoamrisha Mtume na
kuwafundisha maswahaba wake watukufu – Allah
awawiye radhi. Hawa wamepuuza kujifunza fiq-hi
ya swala na mchanganuo wake sahihi. Wametosheka
na kutekeleza matendo (harakati) ya dhahiri
(nje) kwa kuwaiga tu watu. Hawa ndio mithili ya
yule mtu ambaye aliyeingia msikitini akaswali na
il-hali Mtume wa Allah – Rehema na Amani
zimshukie – akimuangalia. Alipomaliza kuswali
swala yake hiyo, Mtume akamwambia : “rejea
uswali tena kwani hakika wewe bado hujaswali”
Bukhariy na Muslim. Mtu anaswali na bado Mtume
anamwambia mara tatu kaswali tena. Chini ya
kivuli cha kauli hii ya Mtume kuna ufumbulizo wa
wazi kwamba kuna baadhi ya watu wanatenda
matendo ya swala; wanasimama, wanarukuu,
wanaitadili, wanasujudu na kukaa lakini
hawaswali. Hawa hawaswali kwa maana ya kuswali
kwa sababu ya kutokuwa na elimu ya kutosha na
sahihi juu ya swala. Elimu na maarifa ambayo
yatawapelekea kuswali kama alivyofundisha Bwana
Mtume na si kama watakavyo na kupenda wao. Kwa
mantiki hii swala yao inakuwa fasidi
(isiyokubalika) na wanahesabika kama
hawajaswali, japokuwa wao watajihesabu
wameswali. Kama wanadai wameswali, tunawauliza
mbona swala zenu hazijakufikisheni katika lengo
: “…BILA SHAKA SWALA HUMZUILIA (huyo mwenye
kuswali na) MAMBO MACHAFU NA MAOVU…” Zinduka
na utambue kwamba yule atakayeswali kwa kuijua
swala, kuanzia nguzo, suna, sharti, karaha na
yabatilishayo na baki ya mambo mengine
yafungamanayo na swala. Akayajua yote hayo
kupitia elimu sahihi, huyu ndiye ambaye Allah
humuumbia kinga ndani ya moyo wake. Kinga hii
ndio humfanya aamrike katika mema na akatazike
katika maovu na machafu. Kinga hii ndio
humpendezesha mambo ya twaa na kumchukizishia
mambo ya maasi na kuifanya njema tabia yake. Hi
ndio falsafa ya amri ya kwanza kumshukia Mtume
kuwa ni KUSOMA na sio KUSWALI. Ataswali vipi
bila ya kuijua hiyo swala yenyewe ?! (ALLAH
NDIYE MJUZI MNO) |