"... BASI SIMAMISHENI SWALA
NA TOENI ZAKA..."(22:78)
Amri hii ya Allah Subhanahu
Wata’alah kama ilivyo ndani ya kitabu chake
kitukufu kinawahusu waumini wote; mwanamume na
mwanammke. Sote tunakiri kuwa Bwana Mtume Rehema
na Amani zimshukie ndiye mwalimu wetu mkuu. Ni
yeye ndiye aliyetufundisha swala na dini kwa
jumla, lau kama si yeye tusingejua swala. Ni
yeye ndiye aliyetufundisha kwamba mwanamke
anatofautiana na mwanamume katika baadhi ya
mambo katika utekelezaji wa amri hio ya Allah ;
amri ya swala. Kwa mujibu mafundisho sahihi ya
mtume, mwanamke anatofautiana na mwanamume
katika mambo 5 yafuatayo ndani ya swala:-
1) Ajikusanye mwili wake katika
sijida.
Zoezi hili hutekelezwa kwa
mwanamke kuvigusisha viwiko vyake vya mikono
katika mbavu zake wakati wa kuitekeleza nguzo ya
sijida. Kadhalika aliambatishe tumbo na mapaja
yake.
Hivi ni kinyume atakiwavyo
mwanamume katika kulitekeleza zoezi hili zima la
kusujudu. Yeye hutakiwa avitenganishe viwiko na
mbavu zake na alinyanyue tumbo lake lisigusane
na mapaja yake.
Haya ndiyo mafundisho
yanayotokana na riwaya: "kwamba Mtume -rehma
na amani zimshukie- aliwapitia wanawake wawili
wakiwa wa naswali akawaambia:"mtakaposujudu
zikusanyeni baadhi ya nyama mnapokwenda ardhini
(kusujudu ), kwani mwanamke katika hilo si kama
mwanamume." Baihaqiy
2) ASHUSHE SAUTI YAKE MBELE ZA
WANAMUME WA KANDO NA KANDO
Mwanamke anatakiwa aishushe
sauti yake, asiitoe kiasi cha kusikika na
wanaume wa kando na kando* wakati wanaposwali
sala ambayo ni sunna kutoa sauti. Hii ni kwa
sababu ya kuchelea fitina inayoweza kuzuka nyuma
ya pazia la sauti yake ambayo kwa mtazamo wa
sheria kamaumbile ni pambo na kivutio tosha kwa
mwanamume. Tusome na tuelewe:".... BASI
MSILEGEZE SAUTI (zenu mnaposoma wa wanamume) ILI
ASITAMANI MTU MWENYE UGONJWA MOYONI MWAKE (
kufanya mabaya na nyie) ...".(33:32)
Tumefahamu kutokana aya hii
kwamba kuna uwezekano sauti ya mwanamke ikazusha
fitna ambayo mwisho wake si mzuri. Hii ndiyo
falsafa ya Uislamu katika kuweka sheria ya
hijabu hata katika eneo la sauti ya mwanamke
akiachilia mbali mavazi na mchanganyiko wa
mwanamume na mwanamke. Kwa mantiki hii Uislamu
unamtaka na kumuamrisha mwanamke muumini
kuteremsha sauti yake mbele za wanamume hata
akiwa ndani ya ibada ya swala. Hiyo ni ndani ya
ibada seuze baki ya hali/ maeneo mengine!.
Hivi ni kinyume na mwanamume,
yeye anatakiwa anyanyue na kutoa sauti mahala
panapohitaji sauti kwa mujibu wa sheria.
3)APIGE KIKOFI AKIPATWA NA JAMBO
NDANI YA SWALA.
Mwanamke atakapopatwa na jambo
ndani ya swala na akataka kumtanabahisha mtu
aliyeko pembeni yake jambo fulani.Yeye
anaelekezwa na sheria apige kikofi hafifu kama
ishara ya kuashiriajambokwa aliye jirani.Namna
ya kupiga ni kutumia tumbo la kitanga chake cha
kulia kupiga juu ya mgngo wa kitanga cha mgongo
wa kulia. Wakati ambapo mwanamume anapopatwa na
jambo/dharura nadani ya swala anatakiwa alete
tasbihi kwa sauti yenye kusikika bila ya
kuikusudia hiyo tasbihi. Hivi ndivyo
ilivyopokelewa kutoka kwa Sahli ibn Saad- Allah
amwie radhi- kwamba Mtume -rehma na amani
zimshukie-amesema,
"atakayepatwa na jambo (linalohitaji
tanbiih) ndani ya swala na alete tasbihi, kwani
atakapoleta tasbihi ataeleweka (na walio jirani
naye). Na hakika si vinginevyo kupiga kofi ni
kwa mwanamke" Bukhariy na Muslim.
4)MWILI MZIMA WA MWANAMKE NI
UTUPU(UCHI)
Kisheria mwli mzima wa mwanammke
ndani ya swala na mbele ya mwanamume wa kando na
kando ni utupu ila uso na viganja vyake. Sehemu
nyingine yote ya mwili wake ukiondoa uso na
viganja ni wajibu ufunikwe na kusitiriwa kama
tulivyo bainisha bayana katika darasa
zilizotangulia ili linatokana na agizo lililoko
katika kauli ya Allah subhana wataallah "WALA
WASIDHIHIRISHE VIUNGO VYA VYAO ISIPOKUWA
VINAVYODHIHIRIKA (navyo ni uso na viganja vya
mikono)" (24:31)
Imepokelewa hadithi kutoka kwa
Ummu Salama Allah amuwie radhi-kwamba yeye
alimuuliza Mtume rehma na amani zimshukie: je,
mwanammke anaweza kusali akiwa amevaa kanzu (ndefu
yenye kufunika mwli mzima) shungi tupu bila ya
shuka ya chini? (mtume)
akijibu:"itakapokuwa kanzu hiyo ndefu yenye
kufunika sehemu ya juu ya miguu yake" Abu
Dawoud.
Ni dhahiri kuwa ikiwa kanzu hii
itafunika kabisa sehemu ya juu ya miguu wakati
wa kusimama na kurukuu, itajivuta wakati wa
kusujudu na hivyo kufunika nyayo
Ama mwanamume ni ile sehemu
iliyo baina ya kitovu na magoti. Lau atasali
akiwa amesitiri sehemu hiyo tu ya mwili wake na
sehemu nyingine ikawa wazi, basi swala yake
itasihi. Hivi ndivyo inavyobainishwa na kauli ya
Mtume kwa Allah rehma na amani zimshikie: "sehemu
iliyo juu ya magoti ni katika utupu na sehemu
iliyo chini ya kitovu ni katika utupu".
Darulkutuniy na Baihaqiy
5)MWANAMKE HANA ADANA ANA IQAMAA
TU.
Haikusuniwa adhana kwa mwanamke
bali kilichosuniwa kwake ni iqama tu.Angalia lau
mwanamke ataadhini kwa sauti ya chini si karaha
na adhana yake hiyo itazingatiwa tu kuwa ni
dhikri ambayo itampatia thawabu na
haitazingatiwa kuwa ni mwito kwa swala. ama
akiinua sauti yake kiasi cha kusikika itakuwa ni
karaha na ikichelea kuamsha fitna itakuwa ni
haramu, elewa!
Hii ni tofauti na mwanamume,
yeye amesuniwa kuleta adhana kwa kila swala ya
fardhi hata kama anaswali peke yake.