|
Swala ni miongoni mwa ibada
tukufu kabisa, kwa hivyo inamuwajibikia kila
muislamu wakati wa kuitekeleza ibada hii,
kujipamba na ikhlaaswi, unyenyekevu na utulivu
mkubwa kabisa. Na kuyaelekeza mawazo, akili na
fikira zake zote humo ndani ya swala. Mafaqihi
wametaja mambo mengi ambayo yakitokea ndani ya
swala huibatilisha na kuifisidi, miongoni mwa
mambo hayo ni haya yafuatayo:-
- KUZUNGUMZA
KWA MAKUSUDI:
Maneno
yanayokusudiwa hapa ni yale yasiyo Qur-ani,
dhikri na dua za swala.
Imepokelewa
kutoka kwa Zayd Ibn Arqam-Allah amuwiye
radhi-amesema: Tulikuwa tukizungumza ndani ya
swala, mmoja wetu akizungumza na mwenziwe katika
haja yake mpaka iliposhuka aya hii: “ANGALIENI
SANA SWALA(zote kuziswali, khasa jamaa) NA
(khasa) ILE SWALA YA KATI NA KATI. NA SIMAMENI
KWA UNYENYEKEVU KATIKA KUMUABADU ALLAH”.
[2:238] Bukhaariy & Muslim.
Imepokewa
kutoka kwa Muaawiyah Ibn Hakam Assulamiy-Allah
amuwiye radhi-kwamba Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-alimwambia- alipomshemua mpiga chafya
ndani ya swala yake: “ Hakika ya hii swala
hakifalii ndani yake cho chote miongoni mwa
maneno ya watu. Hakika si vinginevyo hiyo ni
tasbihi, takbira na kisomo cha Qur-ani”.
Muslim.
Na
maneno yanayobatilisha swala ni yale
yaliyotungika kuanzia na herufi mbili na
kuendelea, hata kama hayana maana. Au yakawa
yanawakilishwa na herufi moja tu yenye maana,
mithili ya neno ‘QI’ linalomaanisha
‘kinga’ na neno ‘i’ lenye maana ya
‘hifadhi/tunza’ na neno ‘fi’ ambalo
maana yake ni ‘tekeleza’.
Ama
ikiwa atazungumza kwa kujisahau kuwa yumo ndani
ya swala au akawa hajui kuwa ni haramu
kuzungumza ndani ya swala, kwa kuwa ndio kwanza
ameingia uislamuni . katika hali na mazingira
haya atasamehewa maneno machache, na haya ni
yale yasiyozidi maneno sita.
- MATENDO
MENGI:
Muradi
na mapendeleo ya matendo mengi ni yale yote
yanayopingana na matendo ya swala kwa sharti
yawe mengi na yafuatane. Haya yanabatilisha
swala kwa sababu ya kule kupingana kwake na
nidhamu (utaratibu) ya swala. Na kipimo cha
wingi ni haraka tatu na kuendelea na kipimo cha
mfuatano ni matendo kwa mujibu wa ada/desturi.
Ama
matendo machache mithili ya mtu kuweka vizuri
kilemba chake, kupiga hatua moja mbele kwa ajili
ya kuziba pengo (nafasi) lililo katika safu ya
mbele. Au kukinyooshea mkono kitu haraka moja,
haya yote hayabatilishi swala. Kwa sababu ya
riwaya sahihi iliyothibiti kutoka kwa Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwamba yeye
alimnyanyua Umaamah na kumuweka chini na ilhali
akiwa ndani ya swala akiwaswalisha watu.
Bukhaariy.
Umaamah
ni mtoto wa kike wa Bibi Zaynabu Binti ya Mtume
wa Allah.
- NGUO
AU MWILI KUGUSANA/ KUKUTANA NA NAJISI:
Makusudio
ya kugusana/kukutana na najisi ni hiyo nguo au
mwili kupatwa na sehemu ya najisi, kisha
mswaliji hasifanye haraka kuikung’uta pale
pale. Kwa sababu hiyo ni hadathi inayopingana na
mojawapo ya sharti za swala ambayo ni twahara ya
mwili na nguo kutokana na najisi. Najisi
ikimpata kwa kupeperushwa na upepo au mfano wake
na akaweza kuiondosha haraka na ikawa ni kavu,
swala yake haibatiliki.
- KUFUNUKA
UTUPU (UCHI):
Umekwishajua
mpaka wa uchi kwa mwanamke na mwanamume ndani ya
swala katika masomo yaliyotangulia. Sehemu yo
yote ya utupu wa mswaliji ikifunuka kwa
makusudi, swala yake itabatilika kwa hali yo
yote ile. Ama ukifunuka bila ya kukusudia na
akafanya haraka kujisitiri, swala haitabatilika.
Na akitojisitiri pale pale utupu ulipomfunuka,
swala yake itabatilika kwa sababu ya kukosekana
mojawapo ya sharti za swala katika mojawapo ya
sehemu za hiyo swala.
- KULA
AU KUNYWA:
Kula
au kunywa makusudi ndani ya swala kunabatilisha
swala kwa sababu kunapingana na mfumo na
utaratibu wa ibada hii. Na kipimo cha chenye
kubatilisha ni kiasi cho chote cha chakula au
kinywaji hata kama ni kichache.
- KUZUKIWA
NA HADATHI KABLA YA KUTOA SALAMU YA KWANZA:
Mtu
akihuduthi kwa kutokwa na ushuzi mathalan, swala
itabatilika bila ya kuangalia ni makusudi au ni
kwa kujisahau (kushindwa kujizuia). Swala
itabatilika kwa sababu ya kukosekana mojawapo ya
sharti za kusihi swala kabla ya kutimia kwake,
nayo ni twahara ya hadathi.
Ama
ikiwa mtu atahuduthi baada ya kutoa salamu ya
kwanza na kabla ya kutoa ile ya pili, swala yake
itakuwa sahihi na imetimia na hili ni kongamano
la wanazuoni. Hii ni kwa kuzingatia kwamba
mwanzo wa swala ni takbira ya kuhirimia
na mwisho wake ni salamu ya kwanza ambayo ndiyo
nguzo.
- KUJIKOHOZA,
KUCHEKA,KULIA NA KUUGULIA (KUDIHA):
Yote
haya yatabatilisha swala iwapo tu zitadhihiri
herufi mbili kutokana na kuyatenda, hata kama
hazifahamishi maana. Hivi ni iwapo alifanya kwa
makusudi, ama ikiwa ni kwa kushindwa kama vile
kujiwa na kikohozi cha nguvu au kulipukwa na
kicheko, swala haitabatilika. Kadhalika swala
itabatilika kwa kuleta dhikri au dua kwa
kukusudia kumsemeza mtu kwa dua au dhikri hiyo.
Kama vile mtu kusema ndani ya swala:
YARHAMUKAL-LAAHU-(Allah akurehemu), hii ni
dhikri ambayo wakati huo itazingatiwa kuwa ni
kuzungumza na mtu. Na umekwishajua kwamba haifai
kuzungumza ndani ya swala. Ama kutabasamu
hakubatilishi swala.
- KUBADILI
NIA:
Iwapo
mswaliji ataazimia kutoka ndani ya swala au
akakutungikia huko kutoka na jambo fulani kama
vile ujaji wa mtu. Akasema moyoni mwake fulani
akija nami sijamaliza kuswali nitaikata swala
yangu. Au simu ikilia nitakata swala na kwenda
kuipokea. Kwa kufanya hivi swala yake
itabatilika pale pale atakapotia nia ya kuikata.
Kwa sababu swala haisihi ila kwa nia ya kutinda
(ya moja kwa moja). Na azma au kusudi hili la
kuikata swala kwa jambo fulani, linakinzana na
nia ya kutinda.
- KUKIPA
MGONGO QIBLAH/KUKENGEUKA NA QIBLAH:
Swala
itabatilika iwapo mswaliji atakengeuka na Qiblah
kwa kukipa mgongo, kwa sababu kuelekea Qiblah ni
sharti ya msingi ya swala. Swala itabatilika
bila ya kujali kuwa alifanya hivyo kwa makusudi
au alikengeushwa na mtu kwa nguvu. Angalia ikiwa
atarudia kuelekea Qiblah haraka, swala yake
haitakuwa ni batili.
- KULETA
ZIADA YA MFANO WA SWALA KWA KUSAHAU:
Mswaliji
akijisahau akaswali adhuhuri rakaa nane badala
ya nne au akaswali magharibi rakaa sita badala
ya tatu. Swala yake itakuwa batili kwa sababu
kusahau kwake kumevuka mpaka kiasi cha kuleta
ziada ya mfano wa swala. Na hii ni dalili ya
wazi ya kutokuwemo kwake ndani ya swala kwa
moyo, fikra, akili na mawazo yake yote
(unyenyekevu).
- KUKUMBUKA
KUTOKUSWALI SWALA YA KABLA YA SWALA HII YA
SASA:
Ikiwa
mswaliji ataingia kuswali Alasiri na akakumbuka
ndani ya swala hiyo ya Alasiri kwamba hajaswali
swala ya Adhuhuri. Swala ya Alasiri itabatilika
pale pale mpaka kwanza aswali adhuhuri, kwa
sababu utaratibu baina ya swala tano ni FARDHI.
Kwa kule kupokewa kwake
kutoka kwa Bwana Mtume kwa mtungo na
utaratibu maalum wa fardhi baada ya fardhi. Kwa
mantiki hii, swala haisihi kabla ya kuswali ile
ya kabla yake.
- KUACHA
MOJAWAPO YA NGUZO ZA SWALA:
Mswaliji
akiacha nguzo mojawapo miongoni mwa nguzo za
swala kama vile kuacha rukuu. Kisha hasiidiriki
kwa kuileta ndani ya swala, swala yake itakuwa
ni batili. Ubatili huu unatokana na kauli yake
Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-alipomwambia yule mkosaji wa swala
yake. Wakati alipoacha kutulizana na itidali
ambazo hizo ni nguzo mbili: “Rejea ukaswali
tena kwani hakika wewe bado hujaswali”.
Muslim.
- KUMTANGULIA
IMAMU:
Iwapo
maamuma atamtangulia imamu wake kwa makusudi,
kama vile akarukuu kabla ya imamu hajarukuu. Au
akasujudu kabla ya kusujudu imamu wake, katika
hali hii swala yake itabatilika. Ubatili huu
unatokana na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie: “Hakika si vinginevyo, imamu
amewekwa ili afuatwe”. Bukhaariy & Muslim. |