|
Mswaliji
anaruhusiwa kisheria kufanya baadhi ya mambo
akiwa ndani ya swala, kwa sharti kwamba kuwe na
dharura ya kufanya hivyo. Anaruhusiwa kuyafanya
mambo hayo katika hali hiyo ya dharura bila ya
swala yake kubatilika. Mambo hayo ni kama
yafuatavyo:-
- Ni
halali kufanya kitendo kichache/chepesi.
Kitendo hiki ni kama vile mtu kufunga
shuka/msuli wake uliolegea ambao kama
hakuufunga (hakuukaza) utamuanguka. Na
kumuacha utupu na hivyo kupelekea kubatilika
kwa swala yake.
- Kujikohoza
wakati wa haja. Ni jambo lililoruhusiwa mtu
kujikohoza ikiwa kapaliwa na kitu au kohozi
limemkaa kohoni.
- Kumuweka
sawa mtu katika safu. Ni rukhsa kumvutia
mbele au nyuma mtu aliye nje ya safu ili
akae sawia katika safu. Kadhalika ni rukhsa
Imamu kumzungushia maamuma kuliani kwake
ikiwa atakuja na kusimama kushotoni kwake,
wakati ambapo wako wawili tu yeye na imamu.
Hivi ndivyo mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alivyofanya kwa Ibn Abbas-Allah
amuwiye radhi-aliposimama kuswali pembeni
yake usiku. Haya ni kwa mujibu wa riwaya ya
imamu Bukhaariy.
- Kupiga
mwayo na kufunika kinywa kwa kiganja cha
mkono. Mswaliji anaruhusiwa kufunika kinywa
chake kwa kiganja cha mkono wake atakapopiga
mwayo ndani ya swala.
- Kumfungua/kumzindua
Imamu wake atakaposahau au kukwama katika
kisomo. Ni halali kwa maamuma kumfungua
Imamu wake anapokwama katika kisomo cha
Qur-ani. Kama ambavyo pia ni halali
kumzindua atakapoacha au kuzidisha nguzo kwa
kutamka: (Sub-haanallah). Rukhsa hii
inatokana na kauli yake Bwana Mtume-Rehema
na Amani zimshukie: “Atakayepatwa na jambo
ndani ya swala yake na aeme:
Sub-haanallah”. Bukhaariy & Muslim
- Kumzuia
mtu apitaye mbele yake. Mswaliji anaruhusiwa
kumzuia kidogo na hata kwa nguvu mtu apitaye
mbele yake. Uhalali huu anaupata kutokana na
kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie: “Atakaposwali mmjoa wenu
kuelekea kitu kinachomsitiri na watu,
atakapotaka mtu kupita mbele basi na amzuie.
Akikataa basi na amzuie kwa nguvu, kwani
huyo ni shetani”. Bukhaariy & Muslim
- Kumuua
nge au nyoka. Ikiwa mswaliji atatokewa na
nge au nyoka akiwa ndani ya swala yake,
sheria inamruhusu kumuua nge au nyoka huyo.
Lakini anachotakiwa kufanya ni kitendo cha
kuua tu na sio kutamka maneno yaliyo nje ya
swala. Kwani kufanya hivyo kutapelekea
kubatilika kwa swala. Matendo yote
atakayoyatenda mpaka kumuua nge au nyoka
huyo yatasameheka na ataendelea na swala
yake bila ya kubatilika. Rukhsa hii ni
natija ya kauli yake Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie: “Viuweni vyeusi viwili
ndani ya swala; nyoka na nge”. Tirmidhiy
- Kujikuna,
mswaliji anaruhusiwa kujikuna panapomuwasha
katika mwili wake. Kwa sababu kujikuna ni
katika matendo machache/mepesi yenye
kasameheka ndani ya swala.
- Kumuashiria
kwa mkono mtu aliyemtolea salamu, hili
linatokana na kitendo cha Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie. Kama ilivyo
katika riwaya ya Imamu Tirmidhiy.
Kauli
jumla ni halali kufanya kila tendo ambalo
halipingani/halikinzani na adabu, suna au
unyenyekevu wa swala. Kama vile mtu kutoa
machozi anaposoma aya inayotoa onyo kali au
inayofanya adhabu.
|