|
HII
NDIYO DAWA, PONYO (POZO) LIKO WAPI?
Allah
Mola Mwenyezi anasema: “SOMA ULIYOLETEWA WAHYI
KATIKA KITABU (hiki ulicholetewa) NA ISIMAMISHE
SWALA. BILA SHAKA SWALA (ikiswaliwa vilivyo)
HUMZUILIYA HUYO (mwenye kuswali na) MAMBO
MACHAFU NA MAOVU, NA KWA YAKINI KUMBUKO (utajo)
LA ALLAH (lililomo ndani ya swala) NI JAMBO
KUBWA KABISA (la kumzuilia mtu na mabaya) NA
ALLAH ANAJUA MNAYOYATENDA”. [29:45]
Huenda
ukajiuliza: Mbona/kwa nini yameamrishwa mambo
mawili katika kauli hii ya Allah; kusoma kitabu
(Qur-ani) na kusimamisha swala?
Jawabu
sawia kwa swali lako hilo ni kuwa yameamrishwa
mambo mawili hayo. Kwa kuzingatia kwamba ibada
inayotekelezwa na mja imegawanyika katika
vigawanyo (sehemu) vikuu vitatu:-
IBADA
YA MOYO: Hii inahusisha itikadi ya haki na kweli
juu ya Allah Mola Muumba wa ulimwengu na vyote
vilivyomo; tuvijuavyo na tusivyovijua.
IBADA
YA ULIMI: Hii inahusisha kumdhukuru Allah na
kumsifia kwa utajo (dhikri) mwema.
IBADA
YA KIWILIWILI: Hii inajihusisha na utendaji wa
amali (matendo) njema kwa mujibu wa itikadi
iliyomo moyoni mwa mja.
Katika
mgawanyiko huu wa ibada, itikadi kwa maana ya
imani ndio ibada pekee isiyojikariri na
kujirudiarudia. Hii ni kwa sababu mtu akiitakidi
kitu/jambo, haiingii akilini
kuliitakidi/kuliamini kwa mara nyingine tena.
Kwani itikadi (imani) ile ya mwanzo huendelea
kuishi na kudumu moyoni, akilini na katika fikra
zake. Kwa mantiki hii itikadi ni kitu cha mara
moja, kikishakita mizizi moyoni ndio kimekita.
Pamoja na kukubali kuwa itikadi (imani) ni kitu
kisichohitaji kurudiwarudiwa. Lakini hatuna budi
kuukubali ukweli kuwa imani (itikadi)
huzidi/hukua au hupungua/hudumaa.
Hapa
sasa ndio tunabakiwa na vitu viwili; dhikri
(utajo) ambayo ni ibada ya ulimi na ibada ya
kiwiliwili. Ibada mbili hizi ndizo zinazokubali
zoezi la kujirudiarudia, kama lilivyo wazi hili
kwa kila mmoja wetu. Hii ndio sababu/falsafa ya
kutajwa mambo mawili haya tu; kusoma kitabu
(ibada ya ulimi) na kusimamisha swala (ibada ya
kiwiliwili) katika aya hii. Maswahaba Ibn Masoud
na Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-wamesema: Ndani
ya swala kuna kinga na kizuizi kinachomzuia mja
kumuasi Allah. Basi mtu ambaye swala yake
haimuamrishi kufanya mema na wala haimkatazi
kufanya maovu. Swala yake hiyo haimzidishii ila
kuwa mbali zaidi na Allah na kuwa ni msiba na
janga kwake yeye.
MARADHI
YA MOYO/ROHO:
Elewa
na ufahamu ewe muislamu kwamba kama ambavyo
mwili huugua na kupatwa na maradhi mbali mbali.
Ambayo pengine husababisha kifo kwa mwili huo au
udhaifu wa mwili, kama maradhi hayo
hayakudirikiwa kwa tiba muafaka. Hivi ndivyo
zilivyo roho za wanadamu ambazo uhai wa
kiwiliwili unazitegemea, kwani bila ya roho
kiwiliwili hakina uhai. Roho nazo hushambuliwa
na maradhi ya kiroho, kinafsi na kimoyo. Maradhi
haya ni kathiri (mengi) katika roho (nafsi) za
wanadamu kuliko tunavyoweza kufikiri na kuwaza.
Kuna maradhi ya unyonge, dharau, unafiki, kibri
na riyaa. Kadhalika roho/nyoyo zinaugua maradhi
ya ubakhili, hasadi, wivu mbaya, choyo, uroho,
tamaa (uchu) wa mali na madaraka na mengi
mengineyo. Yote haya ni maradhi ambayo huyafanya
maisha ya mwanadamu kuwa mithili ya Jahanamu
isiyokalika hata kwa sekunde moja. Unaitazamia
vipi nafsi ( roho) ya mnafiki kupata neema ya
kutulia kupumzika wakati ambapo lengo la unafiki
ni fisadi na uharibifu?! Vipi itapata utulivu na
makini nafsi ya mtu bakhili wakati ambapo maisha
yake yamezungukwa na kutoa na kutumia. Na yeye
hupenda kukusanya na kulimbikiza bila ya kutaka
kutoa wala kutumia?! I wapi basi dawa ya maradhi
haya hatari, maovu na machafu yanayouangamiza
utu wa mwanadamu?
Aya
tukufu tuliyoifungulia somo letu hapo juu
inatueleza na kutupa dawa na tiba pekee na
sahihi ya maradhi haya chukivu kwa Allah. Lakini
wapi, yu wapi mwanadamu wa kuitumia dawa hii
imponye na kumkinga na maradhi haya yanayomvua
ubinadamu wake na kumvika unyama. Sote
tumeghafilika na dawa hii kama kwamba
hatuihitajii na tutaishi milele katika ulimwengu
huu. Tambua na ujue kuwa muislamu kamili, mwenye
akili timamu ni yule anayeweza kuiepusha na
kuitakasa nafsi yake na maradhi haya hatari ya
moyo (roho). Atafanya hivyo kwa kukisoma kitabu
kitukufu cha Mola wake mara kwa mara na
kuyatekeleza yote yaliyomo ndani yake kivitendo.
Kwa kuzisimamisha swala tano kama itakiwavyo
sambamba na kumtaja (kumdhukuru) Bwana Mlezi
wake. Na kumtakia rehema na amani Mtume wake
(kumswalia) asubuhi, mchana, jioni na usiku.
Hakika Qur-ani Tukufu na dhikri (utajo) ya Allah
ni mizizi mitatu ambayo kwa pamoja hutengeneza
dawa mujarabu ya kiroho. Ambayo hutoa tiba isiyo
shaka kwa maradhi yote ya moyo/roho. Ikiwa hivi
ndivyo hebu na tujiulize: Kwa nini leo dawa hii
imepoteza nguvu yake miongoni mwetu na haiwatibu
ila wachache tu, pamoja naukweli kuwa tupo
wagonjwa wengi tuihitajiayo?! Ni kwa nini leo,
dawa hii haina athari kwetu, haitutibu pamoja na
kuitumia kwetu japo kimatatizotatizo?! Leo tuna
wasomaji wazuri tu wa Qur-ani ambao wamehifadhi
sehemu kubwa tu ya Qur-ani kama si Qur-ani
nzima. Mbona hawa hawana tofauti na watu wengine
katika mwenendo, matendo na kauli na kuzama
katika ulimwengu?! Huzioni kabisa adabu za
Qur-ani waisomayo au kuihifadhi katika utendaji
wao wa kila siku, uwe ni ule wa kibinafsi au wa
kijamii. Ni nadra sana kumuona fundi,
mfanyakazi, mfanyabiashara na…na…, swala
yake imemzuilia na ghushi (udanganyifu/utapeli).
Uvunjaji wa ahadi, viapo vya uongo na utendaji
mbaya wa majukumu yake. Wala hatujamshuhudia mtu
mwenye mwenendo mbaya akiingia msikitini
kuswali, kisha akatoka akiwa kabadilika kwa
kuuacha mwenendo mbaya huo. Swala ikamfunganisha
na Allah Muumba na Mruzuku wake, akamcha na
kumuogopa kutokana na mwenendo wake huo mbaya na
akarudi katika njia ya haki na sawa. Tunawaona
watu wengi wakitenga wakati maalumu wa mchana
nausiku wao kwa ajili ya dhikri, nyiradi na
kusoma Qur-ani. Hulipupia hili sambamba na
kuchunga utekelezaji wake bila kuchelewa wala
kuzembea. Wako pia wanaokwenda na kurudi katika
halaqah (daira/vikao) za dhikri na elimu. Kisha
pamoja na juhudi zao zote hizi, bado ibada zao
hizi haziwapi nafuu ya kuyaepa na kuyaepuka
maasi. Kwa upande mmoja wanaonekana wanamtii
Mola wao na kwa upande mwingine wanamuasi bila
ya haya wala soni.
Ni
kwa nini basi watu hawa hawanufaiki na ibada zao
hizi wanazozifanya usiku na mchana?! Wana nini
wagonjwa hawa, dawa wanatumia lakini hawaponi
bali pengine maradhi yao ndio huzidi! Wamepata
dawa lakini wamenyimwa kupona! Ni kweli kuwa
dawa kazi yake ni kuponya, lakini vipi umtazamie
kupona mtu atumiaye dawa bila ya kupata
virutubisho vyote muhimu vihitajikavyo mwilini!
Ni wazi kuwa dawa hii itageuka na kuwa sumu, kwa
hivyo badala ya kutibu itaua tu na si
vinginevyo. Hali kadhalika ibada na twaa zote
haziwezi kumfikisha muhusika katika lengo
lililokusudiwa. Ambalo ni kumpa manufaa na
kumuondoshea madhara kama hazikutekelezwa kwa
usahihi kwa mujibu wa muongozo na sheria.
Utekelezaji sahihi wa ibada kama alivyoamrisha
Allah na kufundishwa kimatendo na kauli na Mtume
wake. Ndio chakula kinachotakiwa kitumike pamoja
na dawa ili mgonjwa aweze kupona. Kwa hivyo
linalodhihirika ni kwamba hao Dhaakirina (wenye
kumdhukuru Allah), waswaliji na wasomaji wa
Qur-ani. Wao wenyewe ndio wamejidhulumu faida
(dawa) na matunda ya ibada zao. Kwa nini, kwa
sababu ya utekelezaji wao mbovu, kuacha adabu na
mambo ya wajibu (msingi) katika ibada zao.
Maadamu msomaji wa Qur-ani hajishughulishi na
kukifahamu akisomacho na kisha kukifanyia kazi.
Vipi Qur-ani hii itakuwa dawa ya kumponya
maradhi yake ya roho/nafsi! Na muda wa kuwa
swala leo imekuwa kwa watu wengi ni ada na
mazoezi tu ya viungo kuliko kuwa ibada. Leo
utamuona mtu akiswali haraka haraka, amejawa na
fadhaa, hana utulivu wala unyenyekevu. Akirukuu,
kusujudu na ilhali kichwa chake kimejaa wasiwasi
na shughuli zake. Hafahamu na wala hazingatii
anachokisema ndani ya swala yake. Ni vipi basi
mtu huyu aingiaye ndani ya swala kwa mwili wake
tu, na moyo na akili yake vikiwa nje ya swala.
Kisha swala hii ndio iwe dawa na tiba kwa mtu
huyu?! Ni vipi swala hii iliyokosa roho yake,
imkanye na kumkinga mwenye kuiswali na mambo
maovu na machafu?! Unaitazamia vipi swala hii
iwe ni kiungo baina ya mja na Mola wake? Hali ni
hii kwa dhikri inayofanywa kwa ulimi tu na moyo
na akili vikawa mbali na dhikri hiyo. Dhikri ya
namna hii ni: “…NI KAMA MAVUMBI
YALIYOTAPANYWA (yaliyotawanywa)”. [25:23]
Yana
faida gani basi mavumbi hayo isiyokuwa madhara!
Hivi ndivyo zilivyo ibada zote, ziwe ni za
fardhi au zile za suna, zote zinatakiwa ziwe na
kiwiliwili na roho. Ama kiwiliwili cha ibada ni
zile harakati (matendo) zake za kimaumbile
zinazoambatana na kanuni/misingi ya Fiq-hi
katika kutengenea na kusihi kwake. Na roho ya
ibada yo yote ile ni moyo kuwa hadhiri kiasi cha
kumuona au kuwa na hisia kuwa Allah yu mbele
yake. Akili izingatie na kujua yote yasemwayo na
kutendwa kwa muongozo na amri yake. Kwa hivyo
utaona kiwiliwili hakikamiliki bila ya kuwa na
roho na roho pia ili iweze kutambulika
inahitajia kiwiliwili. Muislamu analazimika
kutambua anapoinua mikono yake na kuleta
Takbiratul-Ihraamu ambayo huashiria kuwemo ndani
ya swala. Atambue kwamba kitendo chake hicho
kinamaanisha kuitupa nyuma ya mgongo wake dunia
na vyote vilivyomo ndani yake. Na kwamba amekuja
mbele ya yule ambaye ni Mtukufu na Mkubwa kuliko
vitu vyote. Muumini atambue kwamba swala
haikuitwa “swala” ila ni kutokana na kuwa
kwake “swila”-kiungo cha mawasiliano baina
ya mja kiumbe na Mola Muumba wake. Faida na
matunda ya swala yatakuja kwa kadri ambavyo mja
anavyoijua swala na jinsi anavyozitekeleza
nguzo, sharti na suna zake. Sambamba na
kujiepusha na yenye kuibatilisha na kuifisidi.
Mja hapati jazaa ya swala yake ila kwa kadri
atakavyokuwemo ndani ya swala. |