|
Inampasa muumini kuwa mtulivu na
makini awapo ndani ya swala. Hii ni kwa sababu
haijuzu kuitekeleza ibada kwa harakati (matendo)
za haraka haraka; zenye kutoa sura tu ya ibada.
Elewa utekelezaji wa ibada bila ya kuwa makini
na mtulivu unaweza kukupelekea kufanya makosa
ndani ya ibada husika. Mfano wa wale
wanaozifisidi na kuziharibu ibada zao kutokana
na haraka zao zisizo na msingi na upungufu wa
sharti na nguzo. Ni kama mfano wa mgonjwa
aliyepewa dawa na tabibu (daktari), akamueleza
jinsi ya kutumia na kiasi cha kutumia. Mgonjwa
huyu akayapuuza maelekezo ya tabibu wake,
akazidisha au kupunguza kipimo cha dawa. Hili ni
kosa kubwa na baya linaloweza kumgharimu huyu
mgonjwa maisha yake au siha (afya) yake. Dawa
ikimdhuru au isipomsaidia (isipomponya), mgonjwa
huyu aseme dawa hii mbaya au haifai. Au aseme
tabibu yule hajui kazi yake?! Tabibu na dawa
wote hawapaswi kulaumiwa, bali wa kulaumiwa ni
nafsi yake mwenyewe kwa kuyakhalifu maelekezo ya
tabibu wake ambaye ndiye mjuzi wa dawa.
Angalia ewe mwenye kughafilika,
ndani ya swala unakuwa mbele ya nani?
Unanong’ona na kuwasiliana na nani? Hebu ona
haya kunong’ona na Mola wako kwa moyo
ulioghafilika na kifua kilichosheheni wasiwasi
wa shetani na fikra za matamanio mabaya. Hivi
huamini kuwa Allah Mola Muweza anaichomozea siri
yako? “(Allah) ANAJUA KHIYANA YA MACHO NA
YAFICHWAYO NA VIFUA (nyoyo)”. [40:19]
Hukubali kuwa Allah anauangalia
moyo wako na kuyajua yote yaliyomo? Kwa nini
basi unajidhihirisha kuwa unaswali kwa kuyafanya
matendo ya swala na ilhali ukweli wa mambo
huswali?! Unamdanganya nani, elewa hudanganyi
ila nafsi yako.
FAIDA (MATUNDA) ZA SWALA.
Hakika ni ukweli usio na shaka
ndani yake kwamba swala kamili, swala iswaliwayo
kwa namna airidhiayo Allah:-
Huutia nuru ya twaa moyo wa mja.
Huiweka sawa na kuirekebisha
tabia.
Humfundisha mja wajibu na adabu
za uja kwa Bwana Mlezi wake.
Hii ni kutokana na utukufu na
ukubwa wa Allah unaopandwa moyoni mwake na zoezi
zima la swala. Swala humvika mtu taji la tabia
njema kama vile ukweli, uaminifu, kukinahi,
unyenyekevu, upole, uadilifu na wema. Swala
humuelekeza mja kwa Mola wake na humuonyesha mja
njia ya kumfika Mola wake. Swala humfanya
akipatwa na jambo limtatizalo aone hana msaada
ila kukimbilia ndani ya swala. Akiamini kuwa
humo ndimo umo msaada wake: “ENYI MLIOAMINI!
JISAIDIENI (katika mambo yenu) KWA SUBIRA NA
SWALA, BILA SHAKA ALLAH YU PAMOJA NA
WANAOSUBIRI”. [2:153]
Swala humfanya mja amuone Mola
wake yu pamoja naye po pote alipo na analiona
kila alitendalo, kulisema au hata kulifikiria.
Hisia hizi humfanya kumcha na kuogopa kumuasi
Allah, kwa hivyo swala kwake inakuwa ni askari
wa kumchunga. Swala huitakasa nafsi yake na hapo
ndipo utamuona mtu aswaliye vilivyo hana sifa ya
uongo, khiyana, shari, ghadhabu, kibri na uadui.
Hapo ndipo itakuwa imethibiti juu yake kauli ya
Mola wake isemayo: “…BILA SHAKA SWALA
HUMZUILIA (huyo mwenye kuswali na) MAMBO MACHAFU
NA MAOVU…” [29:45]
Lau waislamu wa leo
wangelizihifadhi swala zao kwa kuziswali katika
nyakati zake zilizowekwa na sheria.
Wakazisimamisha na kuzitekeleza kama
alivyowaamrisha Mola wao. Bila shaka yo yote
bishara ya Allah ingelitimia kwao, wangelikomeka
na mambo machafu na maovu. Wangeliepukana na
majanga mbali mbali yanayotokana
(yanayosababishwa) na madhambi na matendo yao
maovu ya uasi kwa Bwana Muumba wao: “…NA
KAMA WANGALIFANYA WALIYOAMBIWA INGALIKUWA BORA
KWAO NA YANGEKUWA YANATHIBITISHA ZAIDI (Uislamu
wao). NA (ingekuwa hivyo) TUNGEWAPA MALIPO
MAKUBWA KUTOKA KWETU. NA TUNGEWAONGOZA NJIA
ILIYONYOOKA (ya kuwafikisha peponi)”.
[4:66-68]
NANI MWENYE KUSWALI NA
KUSIMAMISHA SWALA? (SIFA ZA MWENYE KUSWALI
KIKWELI).
Mtu mwenye kuihifadhi na
kuiswali swala itakiwavyo, mtu huyo:-
Hawi mzinifu na wala haijui
kabisa zinaa: “HAKIKA WAMEFUZU WAUMINI AMBAO
KATIKA SWALA ZAO HUWA NI WANYENYEKEVU. NA AMBAO
HUJIEPUSHA NA MAMBO YA UPUUZI. NA AMBAO (nguzo
ya) ZAKA WANAITEKELEZA. NA AMBAO TUPU ZAO
WANAZILINDA. ISIPOKUWA KWA WAKE ZAO AU KWA
(wanawake) WALE ILIYOWAMILIKI MIKONO YAO YA
KUUME. BASI HAO NDIO WASIOLAUMIWA” [23:1-6]
Hawi mla riba na wala haitambui
riba kwa sababu: “HIKI NI KITABU KISICHOKUWA
NA SHAKA NDANI YAKE; NI UWONGOZI KWA WAMCHAO
ALLAH”. [2:2]
Ni kina nani basi hao
wacha-Mungu? “AMBAO HUYAAMINI YASIYOONEKANA
(Maadamu tu yamesemwa na Allah na Mtume wake) NA
HUSIMAMISHA SWALA NA HUTOA KATIKA YALE
TULIYOWAPA. NA AMBAO WANAAMINI YALIYOTEREMSHWA
KWAKO, NA YALIYOTEREMSHWA KABLA YAKO NA
WANAAMINI (kuwa iko) AKHERA”. [2:3-4]
Kwa kuwa mwenye kuswali ni
Mcha-Mungu na anaiamini Qur-ani, vipi umtazamie
kula riba na ilhali tayari imeshamshukia kauli
ya Allah: “ENYI MLIOAMINI! MSILE RIBA,
MKIZIDISHAZIDISHA; NA MCHENI ALLAH ILI MPATE
KUTENGENEKEWA. NA OGOPENI MOTO AMBAO UMEWEKEWA
WENYE KUKANUSHA AMRI ZA ALLAH (Na katika hizo ni
huku kutokula riba)”. [3:130-131]
Hawi mtu mwenye mfundo na
kinyongo na wala hawi hasidi. Vipi atajasiri na
kuthubutu kuyafanya hayo na ilhali anayaamini
yaliyoteremshwa kwa Nabii Muhammad?! Mola wake
anamwambia: “…NA ANACHOKUPENI MTUME BASI
POKEENI, NA ANCHOKUKATAZENI BASI JIEPUSHENI
NACHO. NA MUOGOPENI ALLAH; KWA YAKINI ALLAH NI
MKALI WA KUADHIBU”. [59:7]
Na miongoni mwa aliyotukataza
Bwana Mtume: “Msibughudhiane, msihusudiane na
wala msikatane pande kwa uadui, na kueni ndugu
enyi waja wa Allah. Na wala si halali kwa
muislamu kumuhama nduguye muislamu zaidi ya siku
tatu”. Anas
Hawi mzito kutekeleza haki za
watu na wala hachupi mpaka katika mali ya mtu.
Ataanza vipi kuyafanya hayo na ilhali swala
inamfanya ayaamini yaliyoteremshwa kwa Mtume,
ambayo ni pamoja na : “WALA MSILIANE MALI ZENU
KWA BATILI NA KUZIPELEKA KWA MAHAKIMU ILI MPATE
KULA SEHEMU YA MALI YA WATU KWA DHAMBI NA ILHALI
MNAJUA (kuwa si haki yenu)”. [2:188]
Hawi muongo na wala hajui
kuongopa. Vipi atasema uongo na ilhali swala
inamfanya kuwa muumini na kusema uongo si sifa
ya muumini: “WANAOZUA UONGO NI WALE
WASIOZIAMINI AYA ZA ALLAH; NA HAO NDIO
WAONGO”. [16:105]
Hawi mwenye
kupoteza/kuzuia/kunyima haki za wazazi, watu
wake wa nyumbani, jamaa na jirani zake.
Atajasiri vipi kuyafanya hayo na ilhali swala
inamfinyanga kuyaamini yote aliyoshushiwa Nabii
Muhammad, ambayo ni pamoja na: “MWABUDUNI
ALLAH WALA MSIMSHIRIKISHE NA CHO CHOTE. NA
WAFANYIENI IHSANI WAZAZI WAWILI, NA JAMAA NA
MAYATIMA NA MASIKINI NA JIRANI WALIO KARIBU NA
JIRANI WALIO MBALI, NA RAFIKI WALIO UBAVUNI
(mwenu)…” [4:36]
Haachi kuwaangalia na kuwasadia
mayatima, masikini na wasiojiweza wengine.
Atathubutuje kuwatupa watu hao na ilhali Qur-ani
anayoiamini inamwambia: “JE, UMEMUONA
(unamjua) YULE ANAYEKADHIBISHA DINI (asiyeamini
malipo ya akhera)? HUYO NI YULE ANAYEMSUKUMA
YATIMA. WALA HAJIHIMIZI KUWALISHA MASIKINI (wala
hawahimizi wenziwe). BASI ADHABU ITAWATHUBUTUKIA
WANAOSWALI. AMBAO WANAPUUZA (maamrisho ya) SWALA
ZAO (kama kuwafanyia wema viumbe wenzao). AMBAO
HUFANYA (amali zao ili wawaone tu) RIYAA. NAO
HUNYIMA MISAADA (basi swala zao hazina faida
kubwa nao)”. [108:1-7]
Kwa ujumla mwenye kusimamisha
swala huipenda haki na wanahaki, sambamba na
kuichukia batili na wanachama wake. Wala
hamkandamizi mtu wala yeye hakubali
kukandamizwa/kuonewa. Hadhulumu na wala hayuko
tayari kudhulumiwa na hawapendi madhalimu na
mafisadi. Huyu ndiye mwanadamu kamili
anayejengwa na swala mara tano kila siku. Ni mtu
ambaye jamii imesalimika na shari/uovu wake na
inaneemeka na kunufaika na kheri/wema wake.
Ewe muislamu, swala ni mazoezi
ya viungo (mwili) yanayokuweka katika hali ya
siha njema. Swala ni kiungo cha mawasiliano
baina yako na Allah Mola Muumba wako. Tambua
kuisimamisha swala ni miongoni mwa nembo kuu za
imani na ni katika alama za kuadhimisha dini ya
Allah. Swala ni dhihirisho tukufu la uja
(utumwa) wako kwa Mola wako, dhihirisho la
shukurani kwa neema za Allah Bwana Mlezi wako
zisizodhibitika. Swala ndio miraji ya roho, na
siri ya kimungu ambayo hawaijui hakika na ukweli
wake ila wale waliozama katika elimu na
ucha-Mungu.
|