|
Hebu
uchunguze na uuangalie huo mkono wako ambao
unaouinua katika Takbiratul-Ihraam ndani ya
swala. Utaona kama kwamba unayakunja na kuyakata
masafa marefu yaliyo baina yako na Al-Ka’aba.
Bali ukifikiria na kuzivuta sawia fikra zako
utajikuta kama kwamba unatupa kila kitu nyuma
yako na unabakia na Allah Mola Mwenyezi pekee.
Katika hiyo Takbiratul-Ihraam unalisema na
kulitamka neno hili kuu: “ALLAAHU AKBAR” na
kulipiga chapa huko mbali kwenye Al-Ka’aba
Tukufu. Kwa kitendo chako hiki utakuwa
umejihakikishia kuwemo kwako ndani ya swala kwa
moyo (roho), mwili na maana. Hapo utakuwa na
kila sababu ya kufurahi pale ambapo Bwana Mlezi
wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake
anapokuelekea kwa dhati yake mara tu baada ya
kulitamka kwako neno hilo kuu kuliko maneno
yote. Sasa roho yako inaogelea katika bahari ya
ukarimu na utukufu, humo unamwambia Mola wako:
“WEWE TU NDIYE TUNAYEKUABUDU, NA WEWE TU NDIYE
TUNAYEKUOMBA MSAADA”. [1:5]
Na
katika ajabu ya mambo ni kwamba Suratil-Faatihah
(Al-hamdu) unayoisoma katika kila rakaa ya swala
yako ina jumla ya aya saba. Kwa nini saba?!
Namba hii saba (7) inadhihiri na kujirudiarudia
katika viumbe na ishara/dalili za kuwepo Allah
Mola Muumba. Miongoni mwa viumbe/vitu
vinavyoangukia katika idadi ya namba (7) kama
zilivyo idadi za aya za Suratil-Faatihah ni
pamoja na:-
- Mbingu
saba.
- Ardhi
saba.
- Idadi
ya maneno ya kalima ya Tauhidi LAA ILAAHA
ILLAL-LAAHU
Hivi:
LAA (1)
ILAAHA
(2)
ILLA
(3}
LAAHU
(4)
MUHAMMADUN
(5)
RASUULUL
(6)
LAAH
(7)
- Idadi
ya sifa za waumini waliofuzu iliyotajwa
katika Suratil-Muumininun. Hivi:
- HAKIKA
WAMEFUZU WAUMINI AMBAO KATIKA SWALA ZAO
HUWA NI WANYENYEKEVU.
- NA
AMBAO HUJIEPUSHA NA MAMBO YA UPUUZI.
- NA
AMBAO (nguzo ya zakkah) WANAITEKELEZA.
- NA
AMBAO TUPU ZAO WANAZILINDA. ISIPOKUWA KWA
WAKE ZAO AU KWA (wanawake) WALE
ILIYOWAMILIKI MIKONO YAO YA KUUME. BASI
HAO NDIO WASIOLAUMIWA. (Lakini) ANAYETAKA
KINYUME CHA HAYA, BASI HAO NDIO WARUKAO
MIPAKA (ya Allah).
- NA
AMBAO AMANA ZAO
- NA
AHADI ZAO WANAZIANGALIA (wanazitekeleza).
- NA
AMBAO SWALA ZAO WANAZIHIFADHI. HAO NDIO
WARITHI AMBAO WATARITHI PEPO; WAKAE HUMO
MILELE. [23:1-11]
Hebu
sasa tujaribu kuchungulia na kuangalia kwa
makini siri ya aya na sifa hizi tukufu na
njema, ambazo zinawataja waumini waliofuzu.
Aya zimeanza na kuwataja (WANYENYEKEVU KATIKA
SWALA ZAO) na zinakhitimisha na (AMBAO SWALA
ZAO WANAZIHIFADHI). Hebu jaribu kuchunguza
mwanzo na mwisho wa sifa hizi na uzingatie.
Sasa
tuendelee kuishi na tarakimu hii saba (7):-
- Kutufu
Al-Ka’aba mara saba.
- Kwenda
sa’ayi (matiti/jaramba) baina ya vilima
Swafaa na Mar-wa, mara saba.
- Idadi
ya siku za juma.
- Idadi
ya rangi za upinde wa mvua.
- Idadi
ya makundi ya watu ambao Allah atayaweka
chini ya jivuli la Arshi yake siku ya
Kiyama. Kama ilivypokelewa katika hadithi
sahihi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie:-
- Imamu/kiongozi
muadilifu.
- Kijana
aliyeinukia/aliyekulia katika kumuabudu
Allah.
- Mtu
ambaye moyo wake umefungamana na misikiti.
- Watu
wawili waliopendana kwa ajili ya Allah;
wakakutana juu ya pendo hilo na kutengana
kwalo.
- Mtu
aliyetoa sadaka kiasi cha kutokujua
kushoto kwake kile kitolewacho na kulia
kwake.
- Mtu
aliyeitwa na mwanamke mwenye cheo na uzuri
(afanye naye machafu), yeye akasema:
Hakika mimi ninamuogopa Allah.
- Mtu
aliyemdhukuru Allah faraghani yakabubujika
machozi macho yake.
Bukhaariy
& Muslim
Ichunguze/izingatie
hadithi pale iliposema (Na mtu ambaye moyo wake
umefungamana na misikiti), utaona hadithi hii
ina mafungamano ya moja kwa moja na swala.
Swala
kama tulivyotangulia kusema katika darsa
iliyotangulia ni kiungo baina ya mja (kiumbe) na
Allah Mola Muuumba wake. Kwa mantiki hii, mtu
anapokuwa haswali huwa ameyakata mwenyewe tena
kwa khiari yake mawasiliano baina yake na Mola
wake. Hali hii ya kukata mawasiliano na Mola
wake ni kitendo kinachoashiria kuwa yeye (mja)
anajitosheleza na hamuhitajii Muumba, jambo
ambalo si kweli. Imepokelewa kutoka kwa Abuu
Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia
Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akisema: “Amesema Allah Mtukufu
nimeigawa swala baina yangu na mja wangu nusu
mbili na mja wangu atapata akiombacho. Basi
atakaposema mja: “SHUKURANI ZOTE ANASTAHIKI
ALLAH, MOLA WA WALIMWENGU WOTE”, Allah husema
amenihimidi (amenisifu na kunishukuru) mja
wangu. Na atakaposema: “MWENYE KUNEEMESHA
NEEMA KUBWA KUBWA NA MWENYE KUNEEMESHA NEEMA
NDOGO NDOGO”, Allah husema amenisifia mja
wangu. Na atakaposema: “WEWE TU NDIYE
TUNAYEKUABUDU NA WEWE TU NDIYE TUNAYEKUOMBA
MSAADA”, Allah husema hili ni baina yangu na
mja wangu na atapata mja wangu atakachokiomba.
Na mja atakaposema: “TUNGOZE NJIA ILIYONYOOKA.
NJIA YA WAKE ULIOWANEEMESHA; SIO (ya wale)
WALIOKASIRIKIWA, WALA (ya) WALE WALIOPOTEA”,
Allah husema hili ni la mja wangu na atapata
aliombalo mja wangu”.
Muslim
SWALA
TANO.
Sote
tunatambua kwamba swala za fardhi ni tano. Kwa
nini tano, nini maana ya utano huu?!
Tarakimu/nambari tano (5) inawakilisha
mambo/vitu vingi. Hebu uangalie mkono wako
unaouinua ndani ya swala, una jumla ya vidole
vingapi? Bila shaka utasema kuna idadi ya vidole
vitano. Vidole vitano hivi vina maana na manufaa
makubwa sana kwa mtu mwenye kuyatazama
mambo/vitu kwa mazingatio. Vidole vitano hivi
vinauwakilisha utano mkuu na mkubwa ukiongozwa
na:-
- Nguzo
za uislamu ni tano kama alivyosema Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Uislamu
umejengwa juu ya nguzo tano:
- Shahada
kwamba hapana apasaye kuabudiwa kwa haki
ila Allah na Muhammad ni Mtume wa Allah.
- Kusimamisha
swala.
- Kutoa
zakkah.
- Kufunga
Ramadhani.
- Kuhiji
kwa mwenye uwezo”.
Bukhaariy,
Muslim, Tirmidhiy & Nasaai.
- Herufi
za neno RAMADHAN (kwa Kiarabu) ambao ni
mwezi mtukufu uliofaradhishwa ndani yake
swaumu na kushushwa Qur-ani. Ukizihisabu
herufi hizi utakuta idadi yake ni tano:
REE
– MIYM – DHWAAD – ALIFU – NUUN
{RA
- MA - DHWA - A - N}
Kila
mojawapo ya herufi tano hizi, inawakilisha
maana maalumu kama ifuatavyo:-
- RA
– Rahmah (rehema) yaani Ramadhani ni
mwezi wa rehema.
- MIYM
– Maghfirah (msamaha) yaani Ramadhani ni
mwezi ambao Allah huwasamehe waja wake kwa
wingi; mwezi wa toba kama tuuitavyo.
- DHWAAD
– Dhwamaanuun Liljannah (dhamana ya
pepo) yaani mwezi huu unampa mja dhamana
ya kuingia peponi kutokana na amali njema
azifanyazo ndani yake.
- NUUN
– Nuurun minal-laah (nuru itokayo kwa
Allah) yaani Ramadhani ni mwezi wenye nuru
kwa sababu ya kushushwa Qur-ani ndani yake
ambayo yenyewe ni nuru.
- ALIF
– Amaanun-minan-naari (amani kutokana na
moto). Yaani mwezi wa Ramadhani ukitumiwa
vema humpa mja amani kwa kumuepusha na
adhabu ya moto.
3).
Waumini wana sifa tano kama zilivyotajwa
katika Suratil-Anfaal:
- “HAKIKA
WANAOAMINI KWELI NI WALE AMBAO ANAPOTAJWA
ALLAH NYOYO ZAO HUJAA KHOFU.
- NA
WANAPOSOMEWA AYA ZAKE HUWAZIDISHIA IMANI.
- NA
WAKAMTEGEMEA MOLA WAO TU BASI.
- AMBAO
WANASIMAMISHA SWALA.
- NA
WANATOA KATIKA YALE TULIYOWAPA. HAO NDIO
WANAOAMINI KWELI KWELI. WAO WANA VYEO
(vikubwa) KWA MOLA WAO, NA MSAMAHA NA
RIZIKI BORA (kabisa huko Akhera)”.
[8:2-4]
4).
Hali kadhalika vidole vitano vinakukumbusha
kauli yake Allah: “...ALLAH ANATAKA
KUKUONDOLEENI UCHAFU, ENYI WATU WA NYUMBA
(ya Mtume-“Ahlul-Bayt”) NA (anataka)
KUKUTAKASENI KABISA KABISA”. [33:33]
Amesema
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:
“Aya hii ilishushwa kwetu sisi Ahlul-Bayt;
Aliy, Fatmah, Hassan na Hussein”.
Rejea
tafsiri Ibn Kathiyr na Sunan Tirmidhiy.
5).
Milango mitano ya fahamu (hisia) “Five Common
Sense”. Kila mmoja wetu ana milango mitano ya
fahamu:-
- Uoni
(macho).
- Kugusa
(ngozi).
- Kuonja
(ulimi).
- Usikivu
(masikio).
- Kunusa
(pua).
Ni
kupitia milango mitano hii ya fahamu ndipo
unapoweza kuutambua ulimwengu huu na aliyeuumba;
Muumba Mshindi Mwenye nguvu. Unapoinyanyua
mikono yako ndani ya swala na vidole vyako
vitano, unazikumbuka neema za Allah zilizo juu
yako. Unaukumbuka uwezo, hekima (busara) na
utukufu wake. Basi ni fardhi juu yako
kumuhimidi, kumshukuru na kumsifia: “NEEMA
ILIYOTOKA KWETU. HIVYO NDIVYO TUWALIPAVYO
WANAOSHUKURU”. [54:35]
“...KAMA
MKINISHUKURU NITAKUZIDISHIENI...” [14:7]
“...NA
KAMA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH, HAMTAWEZA
KUZIHISABU...” [14:34]
|