|
MILANGO
MITANO YA FAHAMU.
Milango
mitano ya fahamu uliyonayo hukuwezesha kumjua
Allah Mola Muumba wako. Ni milango hii pia
ambayo huithibitisha imani yako iliyomo moyoni,
nayo milango hii ndio chimbuko na chemchem ya
elimu na maarifa uliyonayo. Ziada ya yote haya,
milango mitano hii ya fahamu hukukumbusha zile
nguzo tano za uislamu ambazo juu yake umejengwa
uislamu, zingatia. Hebu tuichunguze kwa pamoja
milango mitano hii ya fahamu na dhima yake
katika maisha yetu ya kila siku.
- MLANGO
WA UONI (MACHO):
Mlango
huu wa fahamu, mbali na kazi zake nyingine
ambazo hukusaidia katika maisha yako ya kila
siku, una dhima/jukumu jingine mama.
Ukiizingatia kauli hii ya Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie: “...Nimewekewa burudani
(tuzo) ya macho yangu ndani ya swala...”
Nasaai
Hutoshindwa
kutambua kuwa uoni (macho) hukulingania
(hukuita) kusimamisha swala. Kauli hii tukufu ya
Mtukufu Bwana Mtume ikiwa inaashiria jambo, basi
si jingine bali inaashiria kuwa hakuna burudani
kama swala. Ndani ya swala ndimo mahala pekee
ambamo mja hupata fursa ya kunong’ona na Allah
Bwana Mlezi na Muumba wake. Je, iko burudani
nyingine kushinda hii kwa watu wenye akili ya
kuelewa?!
- MLANGO
WA UGUSI (MKONO):
Mlango
huu wa fahamu una faida adida (nyingi) na
mchango mkubwa katika kuyafanikisha maisha yako
ya kila siku. Ni mikono ambayo hukuwezesha
kushika, kubeba, kutoa, kupokea
na...na...Ukiachilia mbali faida na manufaa
haya, mlango huu wa fahamu ugusi (mkono), una
dhima nyingine kuu. Dhima hii ikitekelezwa vema
huchangia kwa asilimia tisini na tisa kama sio
mia moja kuboresha hali ya maisha ya jamii ya
kiislamu. Mkono una dhima mama ya kukulingania
wewe kutoa zaka na sadaka katika vile
ulivyoruzukiwa na Allah Mmiliki halisi wa mbingu
na ardhi na vyote vilivyomo humo. Hebu tuitegee
sikio la usikivu kauli hii ya Allah: “YULE
ANAYETOA (zakah, sadaka na vinginevyo) NA KUMCHA
ALLAH. NA KUSADIKI JAMBO JEMA (akalifuata)
TUTAMSAHILISHIA NJIA YA KWENDA PEPONI”.
[92:5-7]
Hiyo
ndio faida na jazaa ya aliyeutumia vema mlango
huu wa fahamu ugusi (mkono). Akautumia mkono
wake katika kutoa vile alivyoruzukiwa na Allah
Mola Mruzukuji, katika kuisadia jamii na
kuupeleka mbele uislamu. Amesema Allah katika
amri hii ya kutoa zakkah, tusome pamoja:
“CHUKUA SADAKA (zakah) KATIKA MALI ZAO,
UWASAFISHE NA KUWATAKASA KWA AJILI YA HIZO
(sadaka zao)...” [9:103]
Hapana
shaka kwamba uchukuaji na utoaji wa zakah
hufanyika kwa msaada mkubwa wa mlango huu wa
fahamu ugusi, yaani mkono.
Ni vema ukakumbuka kwamba kutoa katika
mambo ya kheri ni katika kuishukuru neema ya
Allah. Ambako hakumaanishi ila kuzidishiwa
neema, tusome kwa mazingatio: “NA (kumbukeni)
ALIPOTANGAZA MOLA WENU (kuwa); KAMA MKISHUKURU,
NITAKUZIDISHIENI...” [14:7]
- MLANGO
WA UONJO (ULIMI):
Kama
milango ya fahamu iliyotangulia, mlango huu pia
ambao hukiusisha kiungo ulimi una manufaa
makubwa katika maisha ya kila siku ya mja.
Mlango huu wa fahamu hukulingania kuacha kuonja
kinywaji na chakula, kwa ajili tu ya kutekeleza
nguzo ya nne ya uislamu (swaumu). Hali kadhalika
mlango huu wa fahamu hukulingania kuacha kusema
maneno ya fedhuli na badala yake kuutumia ulimi
katika kusema maneno ya kheri na uongofu. Zaidi
ya yote hayo, mlango huu wa fahamu hukulingania
kumdhukuru na kumtaja kwa wingi Allah sambamba
na kukithirisha kumswalia Bwana Mtume: “ENYI
MLIOAMINI! MKUMBUKENI (mdhukuruni) ALLAH KWA
WINGI NA MTUKUZENI ASUBUHI NA JIONI”. [33:41-42]
Ni
kheri kwako ikiwa utakumbuka kwamba KUMKUMBUKA
ALLAH ni KUJIKUMBUKA wewe mwenyewe, amini
ukitaka: “BASI NIKUMBUKENI (kwa kunishukuru
kwa hii neema niliyo kuneemesheni ya kukuleteeni
Mtume, nami) NITAKUKUMBUKENI NA NISHUKURUNI WALA
MSINIKUFURU”. [2:152]
- MLANGO
WA USIKIVU (MASIKIO):
Mlango
huu wa fahamu una mchango mkubwa sana katika
kufanikisha mawasiliano yako ya kila siku na
wanadamu wenzako, sambamba na viumbe wengine.
Hukuwezesha wewe kusikia yasemwayo na wenzio;
yote mema na mabaya, yenye madhara na manufaa.
Kama ambavyo huwawezesha wengine kusikia ujumbe,
maoni, ushauri, nasaha na maonyo kutoka kwao.
Mbali na manufaa haya ya mlango huu wa fahamu,
ambao hulihusisha sikio katika utendaji kazi
wake. Mlango huu una dhima kuu ya kukulingania
kwenda kufanya ibada ya hijah na kuliitikia
tangazo la ibada hiyo. Sikio ndio hukukumbusha
kauili/agizo la Allah kwa Nabii Ibrahim-Amani
imshukie: “NA (tukamwambia) UTANGAZE KWA WATU
KHABARI ZA HIJAH, WATAKUJIA (wengine) KWA MIGUU
NA (wengine) JUU YA KILA MNYAMA ALIYEKONDA (kwa
machofu ya njiani) WAKIJA KUTOKA KATIKA KILA
NJIA YA MBALI”. [22:27]
- MLANGO
WA KUNUSA (PUA):
Mlango
huu wa fahamu ni kiungo muhimu sana kinachotoa
mchango mkubwa sana katika uhai wa kila siku.
Kiungo hiki ndio njia kuu ya kuingiza hewa safi
mwilini na kuitoa nje ile chafu. Kadhalika
humsaidia mwanadamu kuweza kutofautisha harufu
za vitu mbali mbali vizuri na vibaya. Ukiyaweka
kando manufaa haya ya mlango huu wa fahamu,
utaona kuwa mlango huu wa kunusa una dhima
nyingine. Mlango huu hukulingania kuvuta pumzi
za kumpwekesha Allah Mola Mwenyezi kwamba kila
pumzi inayoingia au kutoka mwilini mwako, itoke
au iingie nawe ukiwa katika hali na mazingira ya
tauhidi. Pumzi yako isitoke au kuingia mwilini
mwako ikakupa uhai wa kimwili tu bila ya kukupa
uhai wa kiroho. Kadhalika mlango huu wafahamu
unakukumbusha kisa kilicho sheheni elimu,
hekima, busara na nasaha njema. Hiki si kingine
bali ni kile kisa cha Mtume wa Allah Yousuf Ibn
Ya’akuub-Amani ya Allah iwashukie, pale mzee
Ya’akuub aliposema: “NA ULIPOONDOKA MSAFARA
(katika Misri) BABA YAO (huku Shamu) ALISEMA:
NASIKIA HARUFU YA YUSUFU; LAU SI KUWA MNAITAKIDI
NIMEHARIBIKA AKILI (mngenisadiki. Allah
alimfanyia muujiza huo wa kusikia harufu ya ile
kanzu ya mwanawe kabla haijafika)”. [12:94]
Kwa
ujumla swala tano za fardhi unazowajibika
kuzitekeleza kila siku, daima zinakukumbusha
hakika na ukweli usiopingika wala kuepukika.
Swala tano hizi hukuambia kila siku kwa ulimi wa
matendo ya kwamba sasa umelikaribia kaburi lako
masafa ya siku moja, hivyo zidisha maandalizi.
Na swala ya Ijumaa mpaka Ijumaa nyingine
inakueleza kuwa mpaka Ijumaa hiyo ya pili tayari
umekwisha upoteza umri wako kwa kipindi cha juma
zima. Yaani tayari siku saba zimekwisha pungua
katika umri wako. Na Ramadhani ya mwaka jana
mpaka hii ya mwaka huu inakukumbusha kuwa tayari
umeshaponyokwa na mwaka mzima katika umri wako
ambao hauujui ni miaka mingapi. Kwa kuukiri
ukweli huu, hebu tuizingatie kwa pamoja kauli
hii ya Allah: “NAAPA KWA ZAMA (zako ewe nabii
Muhammad). KUWA BINADAMU YUMO KATIKA KHASARA.
ISIPOKUWA WALE WALIOAMINI NA WAKAFANYA VITENDO
VIZURI, NA WAKAUSIANA (kufuata) HAKI NA
WAKAUSIANA (kushikamana) NA SUBIRA”. [103:1-3]
Ewe
mwenye kuswali ni vema ukakumbuka na kukiri kuwa
hakika Allah Mola Mwenye hekima na utukufu
amekuwekea vitu/mambo maalumu. Ambayo
yanakufahamisha na kukuashiria juu ya mauti na
mwisho wa uhai huu. Vinakukumbusha ufufuo,
kiyama, hisabu, adhabu, tuzo (thawabu) na bila
ya kusahau kukumbusha juu ya neema au adhabu za
kabri. Maisha na amali zako katika ulimwengu huu
wa mpito na mtihani ndio yatakayoamua ama kaburi
lako liwe ni bustani ya pepo au liwe ni shimo la
jahanamu. Huu hapa usingizi (kulala) ni dalili
ya wazi juu ya mauti, tusome kwa mazingatio:
“ALLAH HUTAKABADHI ROHO WAKATI WA MAUTI YAO.
NA ZILE (roho) ZISIZOKUFA (bado, pia Allah
anazitakabadhi) KATIKA USINGIZI WAO. BASI
HUZIZUIA ZILE ALIZOZIKIDHIA MAUTI
(alizozihukumia kufa) NA HUZIRUDISHA ZILE
NYINGINE MPAKA (ufike) WAKATI ULIOWEKWA. BILA
SHAKA KATIKA HAYA YAMO MAZINGATIO KWA WATU
WANAOTAFAKARI”. [39:42]
Lakini
kwa huzuni na khasara kuu, sisi hatutafakari,
hatuzingatii na wala hatuyatii akilini kama
kwamba (Allah atulinde na hali hiyo) tumekuwa
katika wale ambao: “WANAJUA HALI YA DHAHIRI YA
MAISHA YA DUNIA, NA WAMEGHAFILIKA NA AKHERA, JE,
HAWAFIKIRI KATIKA NAFSI ZAO (wakaona kuwa):
ALLAH HAKUUMBA MBINGU NA ARDHI NA VILIVYOMO
NDANI YAKE ILA KWA HAKI NA KWA MUDA ULIOWEKWA?
NA KWA YAKINI WATU WENGI HAWAKUBALI YA KWAMBA
WATAKUTANA NA MOLA WAO”. [30:7-8]
TUJIFUNZE
NA TUKUBALI: Kuwa “SIKUWAUMBA MAJINI NA WATU
ILA WAPATE KUNIABUDU”. [51:56]
Tukubali
au tukatae, swala ndio ibada mama, ibada
nyingine zote zinaitegemea. |