|
ADHANA
NA IQAAMA.
A:
ADHANA
i)
MAANA YA ADHANA:
Adhana
ni neno la Kiarabu lenye maana mbili; maana ya
kilugha na maana ya kisheria (kifiq-hi). Kilugha
neno adhana lina maana ya “tangazo” kama
lilivyotumika ndani ya Qur-ani Tukufu: “NA NI
TANGAZO (adhana) LITOKALO KWA ALLAH NA MTUME
WAKE, KUJUVYWA WATU SIKU YA HIJA KUBWA KWAMBA
ALLAH YU MBALI NA WASHIRIKINA…..” (9:3)
“NA
(tukamwambia): UTANGAZE (uadhini) KWA WATU
HABARI ZA HIJA….” (22:27)
Ama
maana ya adhana kisheria ni dhikri (utajo)
maalum iliyowekwa na Uislamu kwa ajili ya
kutangaza kuingia kwa wakati wa swala ya fardhi
na kuwaita waislamu kuja kuswali.
- HUKUMU
YA ADHANA:
Adhana
ni suna kwa swala ya sasa (ya wakati huu) na
swala iliyofutu (inayoswaliwa nje ya wakati
wake). Kwa upande wa swala inayoswaliwa kwa
jamaa adhana inakuwa ni SUNA KOKOTEZWA
(Muakadah) kwa anjia ya kutoshelezeana. Yaani
akiadhini mmoja miongoni mwao atakuwa
amewatoshelezea wengine wote na suna hii, kwa
hivyo haitalazimu kutolewa adhana nyingine.
Ama kwa mtu anayeswali peke yake, yeye
mwenyewe tu bila ya kuwa na wa pili yake,
kwake huyu adhana itakuwa ni SUNA AINIYAH
(yenye uzito wa fardhi).
Adhana
ina umuhimu mkubwa na uzito wa pekee katika
kudhihirisha alama za kuadhimisha dini ya
Allah.
- FADHILA
ZA ADHANA:
Zimepokelewa
hadithi kadhaa kutoka kwa Mtume wa Allah
– Rehema na Amani zimshukie –
zinazofahamisha fadhila na thawabu
adhimu zinazopatikana ndani ya adhana.
Miongoni
mwa hadithi hizo ni kama zifuatavyo:
- Imepokewa
kutoka kwa Abuu Hurayrah – Allah
amuwiye radhi kwamba Mtume wa Allah
– Rehema na Amani zimshukie –
amesema: “Lau watu wangelijua
yaliyomo katika wito (adhana) na safu
ya kwanza (ya swala ya jamaa) (yaani
fadhila na thawabu adhimu
zinazopatikana humo). Kisha wasipate
(fursa hizo) ila kwa kupiga kura, basi
wangelipiga kura.”
Bukhaariy
& Muslim
- Imepokelewa
kutoka kwa Abuu Said Al-khudriy- Allah
amuwiye radhi – amesema: Amesema
Mtume wa Allah – Rehema na Amani
zimshukie: “Utapokuwa katika (kundi
la) mbuzi na kondoo wako (malishoni)
au (utapokuwa) kitongojini mwako,
ukaadhini kwa sababu (ya kuingia
wakati wa) swala. Basi inyanyue sauti
yako kwa wito huo (adhana) kwani
hakika haisikii sauti ya muadhini jini
wala mwanadamu wala kitu cho chote ila
(sauti hiyo) itamshuhudia (mtu huyo)
siku ya kiyama.”
Bukhaariy
- Amesema
Mtume wa Allah- Rehema na Amani
zimshukie: “Bora ya waja wa Allah ni
wale wachungao jua, nyota na vivuli
(waadhini) kwa ajili ya dhikri ya
Allah (swala).” Al-Haakim
- DALILI
NA USHAHIDI WA ADHANA:
Adhana
inapatikana ndani ya Qur-ani Tukufu na suna ya
Mtume. Katika Qur-ani adhana inapatikana
katika kauli ya Allah: “ENYI MLIOAMINI!
KUKIADHINIWA KWA AJILI YA SWALA SIKU YA
IJUMAA, NENDENI UPESI KUMTAJA ALLAH NA ACHENI
BIASHARA….” (62:9) Na katika kauli ya
Allah: “NA MANAPOITA KWENDEA SWALA
(mnapoadhini) WANAIFANYIA MZAHA NA MCHEZO.
HAYO NI KWA SABABU WAO NI WATU WASIO NA
AKILI.” (5:58)
Katika
suna ya Mtume, adhana inaelezewa na kauli ya
Mtume – Rehema na Amani zimshukie:
“Unapoingia wakati wa swala, basi na
akuadhinieni mmoja wenu na akuswalisheni aliye
mkubwa wenu.” Bukhaariy & Muslim
Kutokana
na nukuu hizi za kitabu (Qur-ani) na Sunah
(hadithi) uma wa Kiislamu umekongamana juu ya
kwamba adhana imeshariiwa kwa swala tano za
fardhi ili kuwajulisha waislamu kuingia kwa
wakati wa swala husika.
- HISTORIA
YA ADHANA (MWANZO WA ADHANA):
Kwa
mujibu wa kauli zenye nguvu, adhana
imeshariiwa katika mwaka wa kwanza wa Hijrah.
Sababu ya kuanza kutumika kwa adhana ambayo
haikuwepo katika kipindi chote cha utume
Makah. Inatajwa kwamba baada ya Mtume wa Allah
– Rehema na Amani zimshukie – kufika
Madinah, iliwawia uzito waislamu kujua nyakati
za swala. Bwana Mtume akawataka shauri
maswahaba wake wafanyeje ili swala ya jamaa
isije ikawafutu. Baadhi ya maswahaba
wakashauri ipigwe kengele kila unapoingia
wakati wa swala. Wengine wakasema lipulizwe
tarumbeta (baragumu) ili kuashiria kuingia kwa
wakati wa swala. Na pia wako waliotoa ushauri
uliokhitilafina na huu, lakini katika
majumuisho yote ya ushauri uliotolewa hakuna
uliompendeza Bwana Mtume. Akapendezwa na
ushauri uliotolewa na Umar Ibn Al-Khatwaab –
Allah amuwiye radhi. Imepokelewa kutoka kwa
Naafi, kwamba Ibn Umar Allah awawiye radhi –
alikuwa akisema: Waislamu walikuwa wakikutana
na kukadiria nyakati za swala na hakukuwepo ye
yote anayeita kwendea swala (anayeadhini).
Siku moja wakalizungumzia suala hilo. Wakasema
baadhi yao: Jifanyieni kengele kama wafanyavyo
Manaswara. Na wengine wakasema: Bali tupulize
baragumu kama Mayahudi. Basi (hapo ndipo) Umar
aliposema: Kwa nini hamumpeleki mtu akanadi
swala? Mtume wa Allah – Rehema na Amani
zimshukie – akasema: “Ewe Bilali inuka
unadi swala.
Bukhaariy
Imamu
Ahamd – Allah amrehemu – amepokea kwamba
mmoja wa maswahaba nae ni Abdullah Ibn Zayd
– Allah amuwiye radhi – alimuona malaika
usingizini akamfundisha adhana na Iqaamah.
(Alipoamka) akampa Mtume khabari ya ndoto yake
hiyo. Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
akasema: “Bila shaka hiyo ni ndoto ya haki
(kweli) pindipo akitaka Allah, basi inuka
umfundishe Bilali maneno uliyoota ndotoni nae
aadhini kwayo, kwani yeye ana sauti kali
kuliko wewe”. Umar Ibn Al-Khatwaab akiwa
nyumbani kwake akaisikia adhana hiyo, akatoka
wanguwangu kuja kwa Mtume na kumwambia,
namwapia yule aliyekutuma kwa haki, hakika
nimeona usingizini haya haya aliyoyaona
Abdullah Ibn Zayd”.
- TAMKO
LA ADHANA (NAMNA YA KUADHINI):
Tamko
na umbo la adhana ambayo Mtume wa Allah
– Rehema na Amani zimshukie –
alimfundisha Abuu Mahdhuurah ni:-
ALLAAHU
AKBAR X 4
ASH-HADU
AN-LAA ILAAHA ILLAL-LAAH X 2
ASH-HADU
ANNA MUHAMMADAN RASUULULLAAH X 2
(Kisha
hufanya Tarjii (1) )
HAYYA
ALAL-SWALAAH X 2
HAYYA
ALAL-FALAAH X 2
Ikiwa
ni adhana ya Alfajiri ataongeza:
AS-SWALAATU
KHAYRUN MINAN-NAWM X 2
ALLAAHU
AKBAR X 2
LAA
ILAAHA ILLAL-LAAH X 1
Abuu
Mahdhuurah – Allah amuwiye radhi
amesema: Hakika Mtume wa Allah –
Rehema na Amani zimshukie –
alinifundisha adhana: Allaahu Akbar
Allaahu Akbar Allaahu Akbar Allaahu
Akbar, Ash-hadu An-laa Ilaaha
Illal-laah, Ash-hadu An laa Ilaaha
Illal-laah, Ash-hadu Anna Muhammadan
rasuulullaah, Ash-hadu
Anna
Muhammadan Rasuulullaah. Kisha hurudia
akasema: Ash-hadu Ilaaha illal-laah
(mara mbili) Ash-hadu Anna Muhammadan
Rasuulullaah (mara mbili). Hayya
Alas-swalaah (mara mbili) Hayya
Alal-Falaah (mara mbili). Ikiwa ni swala
ya Sub-hi nilisema: As-swalaatu khayrun
minan-nawm. As-swalaatu khayrun
minan-nawm. Allaahu Akbar Allaahu Akbar,
Laa Ilaaha illal-laah”.
Tirmidhiy,
Bukhaariy, Muslim & wengineo
MAANA
YA MATAMKO YA ADHANA
Allaahu
Akbar - Allah ni Mkubwa kuliko kila kitu.
Ash-hadu
An-laa Ilaaha Illal-laah- Ninashuhudia kwamba
hapana afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah
pekee.
Ash-hadu
Anna Muhammadan Rasuulullaah – Ninashuhudia
kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah.
Hayya
Alas-swalaah – Njooni kuswali.
Hayya
Alal-falaah – Njooni kwenye kufaulu.
Asswalaa
tu khayrun Minan-nawm – Swala ni bora kuliko
usingizi.
Allaahu
Akbar – Allah ni Mkubwa kuliko kila kitu.
Laa
Ilaaha Illal-laah – Hapana aabudiwaye kwa haki
ila Allah.
(1)
Tarji’i ni kuyarudia tena matamko hayo kwa
sauti ya chini kidogo.
|