Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

SHARTI ZA KUSIHI ADHANA

 

Ili adhana iweze kusihi na kuzingatiwa kisheria kuwa ni adhana kumeshurutizwa kupatikana sharti zifuatazo:-

  1. UISLAMU: Kisheria haisihi adhana kwa kafiri kutokana na kutokuwa kwake na utayarifu/ustahiki wa ibada (ahliyah). Kwa mantiki hii ni lazima muadhini awe ni muislamu.
  2. UPAMBANUZI (discrimination): Haisihi adhana kwa mtoto mdogo ambaye bado hajafikia umri wa upambanuzi. Kutokusihi huku kwa adhana ya mtoto kunatokana na kutokuwa kwake na utayarifu wa ibada na udhibiti wa wakati.
  3. UANAMUME: Haisihi adhana ya mwanamke, kwa sababu adhana haikushariiwa wala haikusuniwa kwake bali imeharamishwa. Hii ni kutokana na kuwepo uwezekano wa kufitinika wanaume na sauti yake. Na hii pia ni mojawapo ya sababu nyingi zinazomnyima uimamu mbele ya mwanamume. Kama isivyosihi adhana ya mwanamke, kadhalika haisihi adhana ya “khuntha”-(Hermaphrodite) kwa sababu ya kutokujulikana uanamume au uanamke wake. Kwa mantiki hii ni lazima muadhini awe mwanamume.
  4. UTARATIBU: Ni sharti matamko ya adhana yaletwe kwa mtungo na utaratibu wake kama yalivyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Hii ni kwa sababu kuacha utaratibu kunatuhumisha kufanya mchezo na kupunguza uzito wa tangazo hili la kuingia kwa wakati wa swala.
  5. MFULULIZO: Ni sharti upatikane mfululizo baina ya matamko ya adhana, kiasi cha kutopatikana mwanya mkubwa baina ya tamko la kwanza na lile la linalofuatia.
  6. KUINGIA WAKATI WA SWALA: Haisihi adhana na ni haramu kuadhini kabla ya kuingia wakati wa swala husika, hili linatokana na kongamano (Ijmaa) la mafaqihi. Kongamano hili linatokana na kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Itakapohudhuria swala, basi na akuadhinieni mmoja wenu”.
  7. Bukhaariy & Muslim

    Ni dhahiri kuwa swala haihudhurii ila kwa kuingia wakati wake.

    Ikiwa adhana itatolewa nje ya wakati, kutalazimu kuadhini tena utakapoingia wakati wa swala. Hii ni kwa sababu adhana nje ya wakati inakosa falsafa ya adhana ambayo ni kufahamisha kuingia kwa wakati wa swala. Kwa mantiki hii ni haramu kuadhini kabla ya kuingia kwa wakati wa swala husika kutokana na kuwatatiza (kuwachanganya) watu. Na kuwaongopea kwa kungia wakati wa swala na ilhali bado haujaingia.

    TANBIHI: Adhana ya swala ya Sub-hi haiguswi na sharti hii ya kuingia kwa wakati. Kwani inajuzu kuadhini baada ya kupita nusu ya usiku (usiku wa manane) kama inavyofanywa leo Makkah na Madinah. Hili ni natija ya riwaya ya Abdallah Ibn Amrou-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisema: “Hakika Bilali huadhini usiku, basi kuleni na kunyweni mpaka muisikie adhana ya Ibn Ummu Maktuum”. Bukhaariy & Muslim

  8. IWE KWA KIARABU: Ni sharti matamko yote ya adhana yaletwe kwa lugha ya Kiarabu kama yalivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allah. Haijuzu kutolewa adhana kwa lugha nyingine yo yote isiyo Kiarabu, kwani hiyo haitakuwa adhana bali tarjamah (tafsiri ya neno kwa neno) ya adhana.
  9. KUWASIKILIZISHA BAADHI YA WATU: Ni sharti adhana ya jamaa itolewe kwa sauti inayoweza kusikiwa na watu walio jirani na mahala inapotolewa. Ama ikiwa ni adhana ya mtu anayeswali peke (Munfarid) si sharti kunyanyua sauti, bali adhana hiyo itolewe kwa sauti ya chini kiasi cha kusikia muhusika pekee. Imepokewa kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia Abuu Said Al-Khudriy-Allah amuwiye radhi: “Mimi ninakuona wewe ni mpenzi wa mifugo na kuishi mashambani. Utapokuwa pamoja na mifugo yako au kitongojini kwako na ukaadhini kwa ajili ya swala, basi inyanyue sauti yako kwa wito huo (wa swala). Kwani hausikii upeo wa sauti ya muadhini jini wala mwanadamu ila (sauti hiyo) itamshuhudia siku ya Kiyama”.

Bukhaariy

TANBIHI: Haikusuniwa adhana kwa jamaa ya wanawake, kwa sababu ya fitina inayoweza kupatikana kutokana na kusikilizika sauti zao na wanamume. Iliyosuniwa kwao ni Iqaamah tu, kwa sababu hekima (falsafa) yake ni kuwainua waliohudhuria swala kuswali. Na haina kuinua sauti kama ilivyo kwa adhana.

 

VIII/. SUNA ZA ADHANA.

 

Kumesuniwa katika adhana kufanya mambo yafuatayo:-

  1. KUELEKEA QIBLAH: Ni suna muadhini kuelekea Qiblah wakati wa kuadhini, kwa sababu bora ya pande za kuelekewa kwa ajili ya ibada ni upande uliyoko Qiblah. Na hakuna hata mmoja anayeweza kuthubutu kukanusha uibada wa adhana. Na isitoshe imethibiti kwamba waadhini wa Bwana Mtume-Allah awawiye radhi-walikuwa wakielekea Qiblah wakati wa kuadhini.
  2. TWAHARA YA HADATHI NDOGO NA KUBWA: Ni suna mtu kuadhini hali ya kuwa yu katika hali ya twahara, yaani hana hadathi ndogo inayompasishia udhu wala ile kubwa inayompasishia josho. Kwa maana hii, ni karaha kuadhini mtu mwenye hadathi ndogo (asiye na udhu). Na ukaraha unazidi zaidi kiasi cha kuelekea kwenye uharamu kwa mtu mwenye janaba (hadathi kubwa). Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Nachukia (sipendi) kumdhukuru Allah Mtukufu ila niwe na twahara”.
  3. Abuu Daawoud & wengineo

  4. KUSIMAMA WIMA: Ni suna mtu kuadhini hali ya kuwa amesimama, hili linatokana na kauli ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Ewe Bilali simama unadi swala (uadhini)”.
  5. Bukhaariy & Muslim

    Ikiwa mtu ana udhuru kama ugonjwa akisimama ataanguka au maumivu yatazidi, basi ataadhini kwa kukaa kwa sababu: “ALLAH HAIKALIFISHI NAFSI YO YOTE (kutenda) ILA YALIYO SAWA NA UWEZA WAKE...” [2:286]

  6. KUGEUZA SHINGO KULIANI NA KUSHOTONI: Miongoni mwa suna za adhana kama zilivyothibiti kutoka kwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Ni pamoja na muadhini kugeuza shingo yake kuliani wakati wa kusema: (Hayya alas-swalaah) na kushotoni anaposema: (Hayya Alal-falaah). Imepokewa kwamba Abuu Juhayfah-Allah amuwiye radhi-amesema: “Nilimuona Bilali akiadhini, nikawa ninaufuatilia mdomo (kinywa) wake huku na huko. (Akageuka) kuliani na kushotoni (wakati wa kusema): Hayya Alal-swalaah, Hayya Alal-falaah”.
  7. Bukhaariy

  8. KUFANYA TARJI’I: Ni suna muadhini kuleta matamko ya shahada mbili. Yaani (Ash-hadu An-laa Ilaaha Illal-laahu) na (Ash-hadu Anna Muhammadan Rasuulullaah) kwa siri (sauti ya chini), kabla ya kuyajihirisha (kuyatamka wazi/kwa sauti). Suna hii imethibiti katika hadithi ya Abuu Mahdhuurah-Allah amuwiye radhi-kama ilivyopokelewa na Imamu Muslim-Allah amrehemu: “...Kisha hurudia (hufanya Tarji’i) akasema: Ash-hadu An-laa Ilaaha Illal-laah...”
  9. KURATILI MANENO YA ADHANA (KUYALETA KWA NJIA/MTINDO WA TARTIYLI): Ni katika jumla ya suna mtu kuadhini kwa “Tartiyli”. Yaani ayatamke maneno ya adhana kwa mtungo wa utuvu mithili ya mtu aimbaye kidogo. Na si kutetea kwa kuivuta mno sauti kiasi cha kutokueleweka maneno au kuharibika herufi. Hili linatokana na kuizingatia adhana kuwa ni tangazo la kuwajulisha walio mbali kuingia kwa wakati wa swala. Ikawa mtindo huu wa “Tartiyli” ni fasaha zaidi katika kufikisha tangazo kwa walengwa.
  10. KULETA “TATH-WIYBU” KATIKA ADHANA YA ALFAJIRI: “Tath-wiybu” ni muadhini kusema baada ya (Hayya alal-falaah x2); ASWALAATU KHAYRUN MINAN-NAUM, mara mbili.
  11. Amesema Bilali-Allah amuwiye radhi: Aliniamrisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuleta “Tath-wiybu” katika adhana ya Alfajiri”.

    Ahmad, Abuu Daawoud & wengineo

  12. SAUTI KALI (INAYOFIKA MBALI) NA NZURI: Ni suna muadhini kuwa na sauti kali na nzuri itakayomudu kuulainisha moyo wa msikilizaji na kumpelekea kuuitika wito huo. Suna hii inatokana na kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomwambia Abdullah Ibn Zayd-Allah amuwiye radhi-ambaye ndiye aliyeiona adhana usingizini: “Inuka/simama pamoja na Bilali, umtamkishe (maneno) uliyoyaona (usingizini) na aadhini kwayo. Kwani yeye ana sauti kali kuliko wewe”.
  13. Abuu Daawoud & wengineo

  14. TABIA NJEMA: Muadhini anapaswa kutangaa baina ya watu kwa tabia njema na uadilifu. Hii ni kwa sababu tabia njema na uadilifu huwapelekea watu kumsadiki anapowapa khabari ya wakati (adhana).

 


 

 


Forum | Guestbook | Tuandikie |