|
10. KUTOKUTETEA: Ni suna kuacha
kutoa adhana kwa kutetea, yaani kuvuta mno sauti
kiasi cha kupelekea kuharibika kwa maana au
kutokueleweka maneno. Adhana isigeuzwe nyimbo
ambapo mtu hughani upeo wa sauti yake, hilo ni
karaha.
11. WAADHINI WAWILI: Ni suna
msikiti kuwa na waadhini wawili kwa ajili ya
swala ya alfajiri. Mmoja ataadhini kabla ya
kuingia kwa alfajiri na mwingine baada ya
alfajiri. Suna hii imethibiti kutokana na
hadithi (riwaya) ya Abdullah Ibn Amrou-Allah
amuwiye radhi: “Hakika Bilali huadhini usiku,
basi kuleni na kunyweni mpaka muisikie adhana ya
Ibn Ummu Maktuum”. Bukhaariy & Muslim
Falsafa ya adhana nje ya wakati
ni kwa ajili ya kuwaamsha watu kujiandaa na
kujitayarisha kwa ajili ya swala, hiyo ndio
ilikuwa adhana ya Bilali. Lakini kunatakikana
kwa muadhini huyu anayeadhini nje ya wakati kuwa
na wakati mmoja ili kuepuka kuwatatiza na
kuwachanganya watu. Kama ada yake ni kuadhini
saa kumi kamili, basi siku zote aadhini ndani ya
wakati huo. Sio leo kaadhini saa kumi, kesho saa
tisa na keshokutwa saa kumi na nusu.
12. KUNYAMAZA (KUKAA KIMYA): Ni
suna kwa mwenye kusikia adhana kukaa kimya na
kuisikiliza adhana hiyo na kusema mithili ya
anavyosema muadhini. Dalili ya usuna huu ni
kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie: “Mtapousikia wito (wa swala), basi
semeni mithili ya asemavyo muadhini”.
Bukhaariy & Muslim
Lakini wakati muadhini
ataposema: “HAYYA ALAS-SWALAAT X2, HAYYA
ALAL-FALAAH X2”. Yeye mwenye kumsikia atasema:
“LAA HAWLA WALAA QUWWATA ILLA BILLAAH”. Haya
ni sehemu ya mafundisho ya hadithi: “Na
(muadhini) ataposema: Hayya alas-swalaah, aseme
(anayemsikia): Laa hawla walaa quwwata illa
billaah. Na ataposema: Hayya alal-falaah, aseme:
Laa hawla walaa quwwata illa billaah”.
Bukhaariy & Muslim.
Ama katika “Tathwiybu”-
yaani muadhini anaposema: “Asswalaatu khayrun
mina-naumu” katika swala ya alfajiri, ni suna
amjibu kwa kusema: “Swadaqta wabararta”.
13. KUOMBA DUA NA KUMSWALIA
MTUME BAADA YA ADHANA: Kunasuniwa kwa wote
wawili; muadhini na mwenye kumsikia muadhini
kumswalia Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-mara tu baada ya kumalizika kwa
adhana. Kisha waombe dua iliyopokewa kutoka kwa
Mtume na akatuhimiza sana kuisoma kila baada ya
adhana. Haya yote ni kwa mujibu wa hadithi
iliyopokewa na Abdullah Ibn Amrou-Allah amuwiye
radhi-kwamba yeye alimsikia Bwana Mtume-Rehema
na Amani zimshukie-akisema: “Mtakapomsikia
muadhini, basi semeni mithili ya asemavyo kisha
niswalieni. Kwani hakika mwenye kuniswalia mimi
swala moja (tu), Allah atamswalia (mtu huyo kwa
swala moja) hiyo swala kumi. Kisha niombeeni
“wasiyla” kwa Allah, kwa sababu hiyo wasiyla
ni daraja/cheo cha peponi. Haitakikani
daraja/cheo hicho ila kwa mja miongoni mwa waja
wa Allah na ninataraji kuwa mimi ndiye (mja
huyo). Basi ye yote atakayeniombea wasiyla huo,
umemuhalalikia (ameupata) uombezi wangu (siku ya
kiyama)”. Muslim & wengineo
Na dua inayotakiwa kusomwa baada
ya adhana ni kama ilivyopokelewa na swahaba
Jaabir-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Atakayesema wakati (anapomaliza) kusikiliza
adhana: ALLAAHUMMA RABBA
HAADHIHID-DA’AWATIT-TAAMMAH,
WASSWALAATIL-QAAIMAH, AATI SAYYIDANAA MUHAMMADAN
AL-WASIYLAH WAL-FADHWIYLAH, WAB-ATH-HU MAQAAMAN
MAHMUUDANIL-LADHIY WA’ADTAHU, umemuhalalikia
uombezi wangu siku ya kiyama”. Bukhaariy &
wengineo.
MAANA YA MATAMKO YA DUA:
Allaahumma: Ewe Mola wa haki
wee!
Rabba
haadhihid-da’awatit-taammah: Bwana wa wito huu
(wa Tauheed) uliotimia (usoingiliwa na
mabadiliko).
Aati sayyidanaa Muhammadan:
Ninakuomba umpe Bwana wetu Muhammad.
Al-wasiylah: Wasila (Ukaribu na
Allah/daraja peponi).
Wal-fadhwiylah: cheo chenye
kuzidi viumbe wote.
Wab-ath-hu: na umpe
Maqaaman mahmuudah: uombezi
mkubwa siku ya kiyama.
Alladhiy wa’adtahu: ambao
uliomuahidi.
Ahadi hii ya Allah kwa mtume
aliye kipenzi chake imo katika kauli yake:
“...HUENDA MOLA WAKO AKAKUINUA CHEO
KINACHOSIFIKA”. [17:79]
Muadhini anatakiwa kumswalia
Bwana Mtume na kuomba dua kwa sauti ya chini na
sio kwa sauti kama ile aliyoitumia katika
kuadhini. Isije kuchukuliwa na kudhaniwa kwamba
hiyo swala ya mtume na dua ni sehemu ya adhana.
Ni vizuri kwa muadhini mwenye kutumia kipaaza
sauti kumswalia Bwana Mtume na kuomba dua baada
ya kuzima kipaaza sauti hicho.
14. UUNGWANA, UKUBWA, WEMA NA
UJUZI WA WAKATI:
Kumesuniwa Muadhini kuwa:-
Muungwana (huru), yaani asiwe
mtumwa anayeweza kuzuiwa na bwana wake kutoka
kwenda kuadhini.
Mkubwa (mtu mzima) mwenye akili
timamu anayejua anachokifanya, asiwe mtoto mdogo
ambaye hajabaleghe bado.
Mtu mwema, mwenye tabia njema,
anayekubalika na jamii, asiwe mtu fasiki mwenye
mambo ya hovyo hovyo.
Mjuzi wa nyakati za swala.
Suna hii ni kama ilivyothibiti
katika hadithi ya Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi:
“Akuadhinieni aliye mbora wenu na
akuswalisheni msomi wenu zaidi wa Qur-ani”.
TANBIHI: Isieleweke kwamba
haisihi adhana ya mtumwa wala mtoto mdogo,
wakiadhini adhana yao itasihi lakini si suna
kwao kuadhini kama wapo watu wenye sifa.
15. UONI WA MUADHINI: Ni suna
muadhini kuwa mtu mwenye kuona, asiwe kipofu
kwani kipofu hajui wakati ila kwa msaada. Lakini
kipofu akiadhini adhana yake itasihi kwa sababu
Ibn Ummu Maktuum (swahaba wa Mtume aliyekuwa
kipofu) alikuwa akimuadhinia mtume wa Allah.
Amesema Ibn Amrou katika riwaya iliyopokelewa na
Imamu Bukhaariy: “(Ibn Maktuum) alikuwa ni mtu
kipofu, hanadi swala mpaka aambiwe: kumekucha
kumekucha”.
16. KUWEKA VIDOLE MASIKIONI:
Kumesuniwa kuweka vidole masikioni wakati wa
kutoa adhana, kwa sababu kufanya hivyo kuna
msaada mkubwa katika kunyanyua sauti. Usuna huu
wa kuweka vidole masikioni wakati wa kuadhini
unatokana na riwaya iliyopokewa na Imamu Abuu
Haniyfah-Allah amrehemu-“Kwamba Bilali
aliadhini na akaweka vidole vyake masikioni”.
Bukhaariy & Muslim.
Kadhalika imepokelewa kutoka kwa
Sa’ad; muadhini wa Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-“Kwamba Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie-alimuamrisha Bilali kuweka
vidole vyake katika masikio yake na akasema:
Hakika kufanya hivyo kunaiinua zaidi sauti
yako”. Ibn Maajah, Al-Haakim, Twabaraaniy
& Ibn Adiy.
17. KUJITOLEA (KUTOKUADHINI KWA
UJIRA): Ni suna mtu kuadhini kwa kutaraji ujira
kutoka kwa Allah, asichukue ujira kwa kazi hiyo.
Hili ndilo kongamano la wanazuoni wote, hii ni
kwa sababu Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alimwambia Uthmaan Ibn Abul-Aaswi:
“Na umuweke muadhini asiyechukua ujira kwa
adhana yake”. Abuu Daawoud, Ibn Maajah &
Tirmidhiy.
TANBIHI: Ikiwa watu wataifanya
adhana kuwa ni kazi maalumu kama zilivyo kazi
nyingine, basi kutajuzu kuchukua ujira kwa kazi
hiyo kwa mujibu wa makubaliano ya uongozi wa
msikiti husika na muadhini aliyeajiriwa.
|