|
Swala
ndio nguzo ya pili miongoni mwa nguzo tano za
Uislamu. Kwa hivyo basi kuihifadhi swala kwa
kuiswali namna itakiwavyo na kwa wakati
uliowekwa na sheria ni kielelezo kinachoonyesha
nguvu ya imani ya mja. Kama ambavyo ni nembo ya
ukweli wa Uislamu wa mja huyo na ni ishara ya
mafungamano na mawasiliano yasiyokatika ya kila
siku baina ya mja na Allah Mola Muumba wake.
Uislamu kama mfumo sahihi wa maisha ni dini ya
maumbile inayoyatambua fika maumbile ya waumini
wake na wanadamu kwa ujumla. Uislamu unatambua
kwamba muislamu/mwanadamu hupitia vipindi
mbalimbali vya mpito, sambamba na mabadiliko ya
kimaumbile kulingana na hatua za uhai
anazozipitia. Miongoni mwa vipindi vya mpito
anavyovipitia mwanadamu ni uzima (siha) na
ugonjwa na hivi ni vitu/mambo yaliyo nje ya
uweza wake. Kwa kuizingatia hali na mazingira
haya anayoyapitia mwanadamu na ili mgonjwa
asikatikiwe na mawasiliano na Mola wake, Uislamu
umemuwekea utaratibu maalumu wa kuitekeleza
ibada hii mama (swala). Uislamu ukakariri na
kutangaza kwamba ye yote miongoni mwa waislamu
waliopasiwa na swala atakayekuwa mgonjwa.
Mgonjwa huyu akawa hawezi kuswali swala tano za
fardhi kwa kusimama. Kusimama wima ambako ni
miongoni mwa nguzo za swala ambazo swala haisihi
ila kwa kuzitekeleza zote ipasavyo. Huyu
anaruhusiwa kuiswali swala hiyo ya fardhi kwa
KUKAA KITAKO, na kama hawezi kuswali kwa kukaa
ataswali kwa kulala ubavu na kuotezea
(kuashiria) rukuu na sijida. Ili kutofautisha
baina ya nguzo mbili hizi; rukuu na sijida,
anatakiwa kuotezea zaidi katika sijida kuliko
rukuu. Tuitegee sikio la usikivu Qur-ani Tukufu:
“AMBAO HUMKUMBUKA ALLAH WAKIWA WIMA NA WAKIKAA
NA WAKILALA...” [3:191]
Imekuja
riwaya kutoka kwa Imraan Ibn Huswayn-Allah
amuwiye radhi-amesema: Nilipatwa na maradhi ya
bawasiri (Hemorrhoids), nikamuuliza Mtume-Rehema
na Amani zimshukie-kuhusiana na swala (niswali
vipi), akanijibu: “Swali kwa kusimama, ikiwa
huwezi basi (swali) kwa kukaa na iwapo huwezi
basi (swali) kwa kulalia ubavu wako”.
Bukhaariy
Linalozingatiwa
(kipimo) katika kutokuweza au kushindwa kusimama
au kukaa ni ugumu, uzito au shida inayoweza
kumpata mgonjwa kutokana na ama kusimama au
kukaa. Pia kushindwa huzingatiwa kwa ama kuzidi
maradhi au kuchelewa kupona iwapo atakaa au
kusimama. Tumia vipimo hivi katika kupimia mambo
mengine ambayo yanayoweza kupelekea kuzidi
maradhi au kuchelewa kupona au kumtia mtu
machungu. Namna ya mkao ambao unakuwa badali ya
kusimama ni mkao wa ‘Tarabui’-(cross
legged), yaani mkao wa kukalia tako na kupitisha
mguu chini ya mwingine mithili ya herufi
“X”. Hivi ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa
mama wa waumini (mkewe Mtume); Bi. Aysha-Allah
amuwiye radhi-amesema: “Nilimuona Mtume-Rehema
na Amani zimshukie-akiswali kwa kukaa mkao wa
Tarabui”. Nasaai
Pia
kunajuzu kukaa mkao wa tashahudi au mkao
mwingine wo wote auwezao, hivi ni iwapo hawezi
mikao hii tuliyoitaja. Ama namna ya kuswali kwa
mtu ambaye aliyeshindwa kusimama na kukaa, huyu
anapewa ruhusa ya kuswali kwa kulala ubavu kama
tulivyotangulia kueleza. Akitoweza hivyo, basi
na aswali kwa kulala chali (kimangalimangali)
ilhali miguu yake ameilekezea Qiblah kwa kiasi
cha uweza wake. Amesema Sheikh Abdurahmaan
AL-jazaairiy-Allah amrehemu-katika kitabu chake
kiitwacho (AL-FIQ-HU
‘ALAL-MADHAAHIBIL-‘ARBAA) juzuu ya kwanza:
“Na kama mgonjwa hawezi kufanya cho chote
miongoni mwa matendo ya swala ila kwa kuashiria
(kitendo) hicho kwa macho yake. Au kuyapitisha
matendo hayo moyoni mwake, kutamuwajibikia
kuswali hivyo awezavyo na wala swala haimpomokei
(haimuondokei) maadam ana akili timamu”.
|