Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

2. HALI YA MAPAMBANO

Faida

Hii ndio hali ya pili ya swala ya khofu. Katika hali hii ya kuuma kwa vita, hakuna namna maalumu ya swala iliyopokelewa, bali kila mtu anatakiwa kuswali kwa namna inavyomkinikia. Ataswali huku akipigana akienda kwa miguu au akiwa amepanda mnyama. Kadhalika anaweza kuswali akiwa anatembea bila ya kupigana au akiwa amesimama. Katika hali hii anaruhusiwa kuswali kwa kuelekea upande inakotokea khatari, ni mamoja imesibu kuwa ndio upande wa Qiblah au la. Na atayafanya matendo ya rukuu na sijida kwa kuotezea yaani kwa kukitukutisha kichwa chake hali ya kushiria hiyo rukuu na sijida. Yatakikana kuotezea kwa sijida kuwe ni zaidi kuliko kuotezea kwa rukuu ili kufarikisha au kutofautisha baina ya viwili hivyo; sijida na rukuu. Ikiwamkinikia kufuatana na kuswali jamaa pamoja itakuwa ni bora hata kama watakhitalifiana kimuelekeo, huyu kaelekea huku na yule kaelekea kule au maamuma akamtangulia imamu wake. Kuhusiana na haya tunasoma: “ANGALIENI SANA SWALA (zote kuziswali, khasa jamaa) NA (khasa) ILE SWALA YA KATI NA KATI. NA SIMAMENI KWA UNYENYEKEVU KATIKA KUMUABUDU ALLAH. NA KAMA MKIWA NA KHOFU (kuswali kidasturi; mmo katika kupigana, basi swalini) NA HALI YA KUWA MNAKWENDA KWA MIGUU AU MMEPANDA (wanyama). NA MTAKAPOKUWA KATIKA AMANI, BASI MKUMBUKENI ALLAH (swalini) KAMA ALIVYOKUFUNZENI YALE MLIYOKUWA HAMUYAJUI”. [2:238-239]

Imamu Bukhaariy amepokea riwaya kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-katika kuitaja kwake swala ya khofu. Baada ya kuzitaja aina mbili zilizotangulia (kuelezwa katika darsa iliyopita) akasema: Na khofu ikiwa bado ni kubwa kushinda hivyo, waliswali hali ya kuwa wanakwenda kwa miguu au hali ya kupanda (wanyama), wakiwa wameelekea Qiblah au wakiwa hawakuelekea. Imamu Maalik akasema: Amesema Naafii: Simuoni Abdullah Ibn Umar kuwa kayataja hayo (aliyoyataja) ila ni kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Katika hali hii ya mapambano husamehewa harakati na matendo anayoyafanya mwenye kuswali kwa kulazimishwa na hali hiyo ya vita, matendo na harakati ambazo hazisameheki katika hali ya amani. Maneno na ukelele, hivi havisameheki kwa sababu hakuna dharura inayohitajisha kufanya hivyo. Katika hali hii mtu akipatwa na najisi isiyosameheka kama vile damu na mfano wake, swala yake itakuwa ni sahihi lakini kutamuwajibikia kuikidhi baadae akiwa katika hali ya amani.

Ni vema ukatambua kwamba aina hii ya swala tuliyoitaja imeruhusiwa kuswaliwa kwa kaifia hii katika kila vita vya kisheria. Na katika mazingira ambayo mtu anakuwa na khofu kubwa, kama wakati anamkimbia adui au mnyama mkali. Kilichozingatiwa katika kuwekwa sheria ya kuswali kwa namna hii iliyokhalifiana na ada/dasturi ya swala ni kuchunga kuitekeleza swala katika wakati wake uliowekwa na sheria. Hii yote ikiwa ni kuamrika na kauli yake Allah isemayo: “...KWA HAKIKA SWALA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA NYAKATI MAKHSUSI”. [4:103]

 

FALSAFA/HEKIMA YA KUSHARIIWA (KUWEKWA SHERIA) SWALA YA KHOFU.

Falsafa/hekima pekee ya kushariiwa swala ya khofu ni kumfanyia mja wepesi ili aweze kuitekeleza nguzo hii kuu ya dini katika hali na mazingira yo yote yale. Ili kuonyesha kuwa Uislamu ni dini inayokwenda sambasamba na maumbile ya mwanadamu: “BASI UELEKEZE USO WAKO KATIKA DINI ILIYO SAWA SAWA-NDILO UMBILE ALLAH ALILOWAUMBIA WATU (yaani dini hii ya Kiislamu inawafikiana barabara na umbo la binadamu) HAKUNA MABADILIKO KATIKA MAUMBILE YA VIUMBE VYA ALLAH. HIYO NDIO DINI ILIYO HAKI, LAKINI WATU WENGI HAWAJUI”. [30:30]

Kadhalika swala hii ya khofu ni kielelezo cha wazi kinachoonyehsa wepesi wa dini hii ya Kiislamu kama alivyosema Allah: “...ALLAH ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI WALA HAKUTAKIENI YALIYO MAZITO....” [2:185]

“...WALA HAKUWEKA JUU YENU MAMBO MAZITO KATIKA DINI (nayo dini hii) NI MILA YA BABA YENU IBRAHIMU...” [22:78]

Pia kwa kuzingatia kuwa swala ni mawasiliano na kiungo baina ya mja na Mola wake ikawekwa swala hii ya khofu ili mja asikatikiwe na mawasiliano na Mola wake katika kipindi hiki kigumu ambacho anayahitajia zaidi mawasiliano hayo. Kupitia mawasiliano hayo amuombe Mola wake nusra na ushindi dhidi ya maadui wake aliojisabilia maisha yake katika kupambana nao. Ndani ya mawasiliano hayo atamtaja Bwana Mlezi wake, utajo ambao utampa utulivu wa moyo na makini ya akili, vitu ambavyo ni nyenzo muhimu sana katika uwanja wa mapambano. Ni utulivu na umakini huu ndivyo vitakavyomuwezesha kupanga mikakati na mbinu zitakazomsaidia na kumuhakikishia ushindi. Tusome na tuamini: “...SIKILIZENI! KWA KUMKUMBUKA (kumtaja/kumdhukuru) ALLAH NYOYO HUTULIA”. [13:28] Isitoshe kumdhukuru Allah katika hali ngumu hii ya vita ni sababu kuu ya ushindi na nusra, tusome na tuamini tukitaka: “ENYI MLIOAMINI! MKUTANAPO NA JESHI (la makafiri) KAZANENI BARABARA (wala msikimbie) NA MUMKUMBUKE ALLAH KWA WINGI ILI MPATE KUFAULU”. [8:45]

 

HITIMISHO:

SWALA HAIPOMOKI KWA HALI YO YOTE ILE IWAYO.

Inabainika kutokana na maelezo yote haya yanayoitaja swala ya khofu kwamba swala haipomoki kwa hali yo yote ile iwayo maadam mtu ana akili timamu. Si mwendawazimu na ni mkubwa si mtoto mdogo. Hivi ndivyo kusema kuwa mja hana udhuru wo wote utakaompa kibali cha kuacha kuswali, hilo lingelikuwepo basi angelikipata kibali hicho katika hali ya vita. Kilichoruhusiwa si kuacha kuswali bali ni wepesi wa kuswali kwa mujibu wa mazingira na hali aliyomo mtu. Msafiri kwa mfano ameruhusiwa kujumuisha swala mbili iwe ni mjumuisho wa kutanguliza au ule wa kuakhirisha na kukusuru yaani kuziswali swala za rakaa nne, rakaa mbili mbili badala ya nne. Hakuambiwa asiswali eti kwa kuwa tu yumo safarini bali Uislamu kwa kuutambua uzito na taabu ya safari ukampa wepesi wa namna fulani katika kuitekeleza nguzo hii ya swala.

 

 

 


TUJIFUNZE NA TUKUBALI: Kuwa swala ipo kwa maslahi na manufaa yetu sisi wenyewe na ina msaada mkubwa kwetu, tusome kwa mazingztio: “NA JISAIDIENI (katika mambo yenu) KWA KUSUBIRI NA KWA KUSWALI; NA KWA HAKIKA JAMBO HILO NI GUMU ISIPOKUWA KWA WANYENYEKEVU AMBAO WANA YAKINI YA KWAMBA WATAKUTANA NA MOLA WAO NA YA KWAMBA WATAREJEA KWAKE”. [2:45-46]

Tukizidi kuzingatia: “...BILA SHAKA SWALA (ikiswaliwa vilivyo) HUMZUILIA (huyo mwenye kuswali na) MAMBO MACHAFU NA MAOVU, NA KWA YAKINI KUMBUKO LA ALLAH (lililomo ndani ya swala) NI JAMBO KUBWA KABISA (la kumzuilia mtu na mabaya) NA ALLAH ANAYAJUA MNAYOYATENDA”. [29:45]

 

 


Forum | Guestbook | Tuandikie |