|
KUKUSURU
NA KUJUMUISHA.
UTANGULIZI:
Allah
Mola Mwenyezi anasema ndani ya Qur-ani Tukufu
(muongozo sahihi wa wanadamu) “….WALA
HAKUWEKA JUU YENU MAMBO MAZITO KATIKA
DINI….” (22:78)
Maana
sahali ya kauli hii tukufu ya Allah ni kwamba
waislamu hawakuwekea katika dini hii hukumu
zisizotekelezeka kutokana na ugumu wake. Bali
hukumu zote za sheria ya Kiislamu zimezingatia
maumbile na mazingira ya mwanadamu ili
kumuwepesishia utekelezaji wake. Uislamu
unaizingatia safari kuwa ni kipande cha adhabu
ambacho kinamkosesha mtu utulivu wake wa kawaida
na kumyima mapumziko yanayohitajika na mwili
wake. Mtizamo huu wa Uislamu umeizingatia nafsi
ya safari bila ya kuangalia chombo kinachotumika
kusafiria. Bali kiislamu safari ni safari tu
hata kama ikiwa ni kwa ndege chombo ambacho kina
uchovu kidogo tu, ukilinganisha na vyombo
vingine vya usafiri. Pia Uislamu haukuzingatia
lengo la safari, safari yo yote itapewa hukumu
ya safari muda wa kuwa si safari ya maasia na
imefikisha umbali unaozingatiwa na sheria. Kwa
mtizamo huu juu ya safari ndipo Allah
akamkhafifishia msafiri nyingi miongoni mwa
hukumu za dini yake. Katika jumla ya hukumu hizo
alizokhafifishiwa na swala. Sasa kwa msaada wake
Allah na tuanze kubainisha kaifia ya takhfifu
hii sambamba na sharti zake na jinsi msafiri
anavyofaidika nayo. Tuanze kwa kujiuliza:
1.
SAFARI NI NINI?
Kisheria
safari ni zile harakati/kitendo cha mtu kugura
(kuhama/kuondoka) katika makazi yake ya asili
kwenda mahala pengine ambapo umbali wake ni
zaidi ya kilometa themanini na moja au maili
khamsini (81km.150m) takriban. Tunakusudia kwa
neno letu (makazi ya asili) mahala ambapo
alipozaliwa mtu na akakusudia/akaamua kuishi
hapo. Hii ndiyo safari tunayoikusudia katika
darsa yetu hii.
SWALA
YA MSAFIRI HUWAJE?
Allah
amempa msafiri rukhsa mbili kama ifuatavyo:-
RUKHSA
YA KUKUSURU (SHORTENING): Hii ni rukhsa
inayohusisha upunguzaji wa idadi ya rakaa za
swala ambapo msafiri huruhusiwa kuziswali swala
za rakaa nne nne kama Adhuhuri, Alasiri na Ishaa
rakaa mbilimbili badala ya nne za kawaida.
Rukhsa hii hujulikana kisheria kama
“QASWRU.” Rukhsa hii ya kukusuru swala za
rakaa nne inatokana na kauli ya Allah: “NA
MNAPOSAFIRI KATIKA ARDHI, SI VIBAYA KWENU
MKIFUPISHA SWALA (mkikusuru)…” (4:101)
Imepokelewa
kutoka kwa Ya’alaa Ibn Umayyah–Allah amuwiye
radhi–amesema: Nilimuambia Umar Ibn
Al-Khatwaab– Allah amuwiye radhi (kwamba Allah
anasema): “….SI VIBAYA KWENU MKIFUPISHA
SWALA (mkikusuru) IWAPO MNAOGOPA YA KWMABA WALE
WALIOKUFURU WATAKUTAABISHENI….” Watu tayari
wamo katika amani (vita hakuna, kukusuru huku ni
kwa nini?) Akaniambia: Mimi nae nilistaajabu
kama unavyostaajabu wewe (leo) nikamuuliza Mtume
wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-juu ya
suala hili, akanijibu: “(Rukhsa) hii ni
swadaka mliyopewa na Allah, basi ipokeeni
swadaka yake hiyo.” Muslim & wingeneo.
Hadithi
hii ndio inayofahamisha kuwa kukusuru swala
hakukukhusishwa na khofu tu pekee, bali muislamu
anayo rukhsa ya kukusuru swala kwa sababu ya
safari.
SHARTI
ZA KUSIHI KUKUSURU.
Rukhsa
hii ya kukusuru swala aliyopewa msafiri
imeambatana na sharti ambazo anatakiwa azitimize
ili kukusuru kwake kusihi. Sharti za kusihi
kukusuru ni hizi zifuatazo kama zilivyobainishwa
katika vitabu vya fiq-hi:-
Dhima
na utekelezaji wa swala husika viwe ndani ya
swala.
Hii
maana yake ni kwamba swala anayotaka kuikusuru
mtu iwe imemkuta tayari yumo safarini na
aikusuru humo humo safarini. Kwa mantiki hii mtu
haruhusiwi kukusuru swala iliyomuwajibikia kabla
hajavaana na safari. Kisha akasafiri kabla
hajaiswali, basi haimjuzii mtu huyu kuiswali
swala hii kwa kuikusuru. Hii ni kwa sababu
wakati swala hii ilipomuwajibikia na kuwa katika
dhima yake hakuwa msafiri bado, kwa hiyo swala
hii haiwezi kupewa hukumu ya safari. Kadhalika
haihusiani na rukhsa hii ya kukusuru, swala
ambayo uliingia wakati wake naye akiwa safarini
lakini hakuiswali mpaka akarejea mjini kwake.
Basi haitamjuzia kuiswali swala hiyo kwa
kukusuru, kwa sababu wakati wa kuitekeleza
atakuwa si msafiri tena na kukusuru ni rukhsa
aliyopewa msafiri.
Kuvuka
ukuta wa mji anaotoka au maamirisho (majengo)
yake ikiwa hauna ukuta.
Kisheria
mtu ataanza kuhesabika kuwa ni msafiri baada ya
kuuvuka ukuta wa mji wake anaosafiri kutokea
humo. Au baada ya kuvuka maamirisho (majengo) ya
mji huo iwapo haukuzungukwa na ukuta (ngome)
kama ilivyokuwa miji mingi ya kale. Kwa maneno
mengine tunaweza kusema kuwa safari inaanza kwa
kuvuka ukuta/maamirisho ya mji anaotoka mtu Na
hapo ndipo inapoanza kutumika ile rukhsa ya
kukusuru swala aliyopewa msafiri. Imepokelewa
kutoka kwa Anas Ibn Maalik Allah-amuwiye
radhi-amesema: Niliswalai Adhuhuri pamoja na
Mtume–Rehema na Amani zimshukie–rakaa nne
tukiwa Madina (mjini). Na alasiri tukaswali
Dhul-Hulayfah rakaa mbili (Qaswra)”. Bukhaariy
& Muslim
Ikumbukwe
Dhul-Hulayfah ni kitongoji kilichoko nje ya
maamirisho ya Madinah.
Msafiri
kutonuia ukazi wa siku nne mahala anakokwenda,
ukiziondoa zile siku mbili; siku ya kuingia
anakokwenda na siku ya kurudi anakotoka.
Msafiri
akinuia ukazi wa siku nne mahala anakokwenda,
kwa nia yake hii mji huo alionuia kukaa siku nne
utakuwa kisheria katika hukumu ya makazi na
mahala pake pa kuishi. Kwa mantiki hii
ataandamiwa na hukumu za mkazi na sio msafiri,
kwa hivyo haitamjuzia kukusuru ndani ya mji huo.
Atabakia na haki ya kukusuru njiani tu, yaani
wakati wa safari ya kwenda katika mji huo au
kurudi mjini kwake.
Ama
atakaponuia ukazi wa chini ya siku nne,
atabakiwa na rukhsa ya kukusuru mpaka atapoamua
kurejea mjini kwake. Na ikiwa msafiri huyu hajui
atakaa muda gani huko ugenini ambako ameenda kwa
shughuli/haja fulani na hajui ataikamilisha lini
shughuli hiyo/haja yake hiyo. Katika mazingira
haya atapewa rukhsa ya kukusuru swala kwa
kipindi cha siku kumi na nne tu, ukiziachilia
mbali zile siku mbili; siku ya kuingia na ile ya
kuondoka.
Imepokelewa
kutoka kwa Imraan Ibn Huswayn–Allah amuwiye
radhi–amesema: “Nilipigana vita pamoja na
Mtume wa Allah– Rehema na Amani zimshukie-na
nilikuwa pamoja nae wakati wa Fat-hi Makah.
Akakaa mjini Makah siku kumi na nane, haswali
(katika kipindi chote hicho) ila rakaa mbili.”
Abuu Daawoud
Bwana
Mtume–Rehema na Amani zimshukie-alikaa Makah
kipindi chote hiki katika mwaka ule wa Fat-hi
Makah kwa ajili ya kupambana na kabila la
Hawaazin. Akawa anakusuru swala, kwa sababu
hakuwa akijua mapambano hayo yatamchukua muda
gani hadi kumalizika na hali kuwa shwari.
Msafiri
asimfuate mkazi katika swala yake, yaani asiwe
maamuma anayeswali nyuma ya Imamu mkazi.
Msafiri
mwenye rukhsa ya kukusuru, kwa kuiswali rakaa
mbili swala ya rakaa nne hawezi kumfuata mkazi
anayeiswali swala hiyo hiyo kwa kutimiza rakaa
nne zote. Angalia akiamua kumfuata mkazi huyo,
swala yake itasihi na itamuwajibikia kumfuata
pia katika kutimiza na hivyo kujiondoshea yeye
mwenyewe rukhsa ya kukusuru.
|