|
Hii ni rukhsa inayompa msafiri
nafasi ya kuzijumuisha swala mbili na kuziswali
katika wakati wa mojawapo ya swala mbili hizo.
Ushahidi na dalili juu ya rukhsa hii ya
kujumuisha unapatikana katika hadithi nyingi
miongoni mwake ni hadithi hii:- Imepokelewa
kutoka kwa Ibn Abbas–Allah awawiye
radhi-amesema: Alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-akijumisha baina ya swala ya
adhuhuri na ile ya alasiri anapokuwa safarini na
akijumuisha baina ya Maghribi na Ishaa”.
Bukhaariy
Ujumuishaji swala umegawanyika
migawanyiko miwili kama ifuatavyo:-
A/. UJUMUISHAJI WA KUTANGULIZA
Hili ni zoezi la kuzijumuisha
swala mbili; swala ambayo umeingia wakati wake
na ile ambayo haujaingia wakati wake bado na
kuziswali swala mbili hizo pamoja katika wakati
wa swala hii ambayo umeingia wakati wake.
Mathalan kuzijumuisha swala za Adhuhuri na
Alasiri ukaziswali zote mbili katika wakati wa
Adhuhuri. Kwa kujumuisha huku utakuwa
umetanguliza kuiswali Alasiri kabla ya kuingia
wakati wake na huo ndio ‘ujumuishaji wa
kutanguliza’.
B/. UJUMUISHAJI WA KUAKHIRISHA
Hili pia ni zoezi linalohusisha
ujumuishaji wa swala mbili. Swala ya kwanza
tayari umetoka wakati wake na ya pili umeingia
wakati wake. Ukaziswali swala mbili hizi katika
wakati wa swala hii ya pili. Mathalan
kuzijumuisha swala za Adhuhuri na Alasiri,
ukaziswali swala mbili hizi katika wakati wa
Alasiri .Kwa kujumuisha huku utakuwa
umeakhirisha kuiswali swala ya Adhuhuri katika
wakati wake na kuiswali wakati wa Alasiri. Hiyo
ndio maana ya ‘ujumuishaji wa kuakhirisha’.
Ujumuishaji huu wa kutanguliza na ule wa
kuakhirisha unatokana na kitendo cha Mtume.
Imepokelewa kutoka kwa Muaadh–Allah
amridhie–kwamba Mtume–Rehema na Amani
zimshukie–alikuwa katika vita vya Tabuuk.
Anapoanza msafara kabla jua halijapanda
huiakhirisha adhuhuri ili aijumuishe na Alasiri
na kuziswali pamoja (ujumuishaji wa
kuakhirisha). Na unapoanza msafara baada ya
kupinduka jua, huswali Adhuhuri na Alasiri
pamoja (katika wakati wa Adhuhuri), kisha ndio
huenda zake (ujumuishaji wa kutanguliza). Na
alikuwa anapoanza msafara kabla ya Magharibi,
huiakhirisha swala ya Magharibi ili aiswali
pamoja na Ishaa. Na anapoanza msafara baada ya
Magharibi, huiharakisha swala ya Ishaa,
akaiswali pamoja na Magharibi”. Abuu Daawoud,
Tirmidhiy & wengineo.
SWALA ZINAZORUHUSIWA KUJUMUISHWA
Swala zinazoguswa/zinazohusika
na rukhsa hii ya kujumuisha miongoni mwa swala
tano za fardhi ni hizi zifuatazo:-
Adhuhuri na Alasiri, na
Magharibi na Ishaa tu.
Hizi ndizo swala ulizopewa
rukhsa ya kuzijumuisha ukitaka kufanya hivyo. Ni
mamoja kuwe kujumuisha huko ni kwa kutanguliza
au kwa kuakhirisha kama alivyofanya Bwana
Mtume–Rehema na Amani zimshukie. Kwa hivyo
basi haisihi kisheria kuijumuisha swala ya
Sub-hi (Alfajiri) na swala iliyo kabla yake
ambayo ni Ishaa. Au kuijumuisha na swala iliyo
baada yake ambayo ni Adhuhuri. Kadhalika hakuna
kujumuisha baina ya swala ya Alasiri na
Magharibi.
SHARTI ZA KUJUMUISHA
Kila ujumuishaji; ujumuishaji wa
kutanguliza na ujumuishaji wa kuakhirisha una
sharti zake ambazo inatakikana zichugwe ili
ujumuishaji usihi. Hebu sasa na tuzitaje sharti
za kila ujumuishaji tukianzia na:-
a) SHARTI ZA UJUMUISHAJI WA
KUTANGULIZA:
UTARATIBU BAINA YA SWALA MBILI
HIZO
Mjumuishaji wa swala mbili
anatakiwa aanze kuiswali swala ya mwanzo yaani
swala ya wakati ule. Kisha ndio aiswali ile
nyingine ambayo siyo ya wakati ule. Kwa mfano
mtu ameamua kuitumia rukhsa ya kujumuisha kwa
kuzijumuisha swala za Adhuhuri na Alasiri katika
wakati wa Adhuhuri. Kiutaratibu anatakiwa aanze
kuiswali swala ya Adhuhuri, kwani ndio swala ya
wakati ule. Baada ya kumaliza ndio aswali
Alasiri ambayo wakati wake haujaingia bado.
NIA YA KUJUMUISHA KABLA YA
KUMALIZIKA KWA SWALA YA MWANZO:
Mjumuishaji anapaswa kunuia
kuijumuisha swala ya pili (Alasiri) na hii ya
mwanzo (Adhuhuri) kabla hajatoa salamu kuashiria
kumalizika kwa swala hii ya mwanzo aliyoanza
kuiswali. Lakini inapendelewa kuwa nia hiyo ya
kujumuisha pamoja na Takbira ya kuhirimia swala
ya mwanzo.
KUFULULIZA BAINA YA SWALA MBILI
HIZO.
Mjumuishaji hapaswi kuacha
mwanya mkubwa baina ya swala mbili hizi
anazozijumisha kwa kuleta dua au kuswali suna
katikati yake. Bali anatakiwa baada ya kutoa
salamu ya swala ya mwanzo, ainuke na kuanza
kuswali swala ya pili. Angalia ikiwa ataacha
mwanya mkubwa na ukubwa wa mwanya utarejea
katika ada. Au iwapo ataichelewesha swala ya
pili bila ya sababu yo yote (dua/suna)
utabatilika ujumuishaji wake huo na
kutamuwajibikia kuiakhirisha swala hiyo ya pili
mpaka uingie wakati wake na aiswali ndani ya
wakati wake huo na sio sasa. Haya yote ni kwa
kumfuata Bwana Mtume–Rehema na Amani
zimshukie. Imepokelewa kutoka kwa Ibn
Umar–Allah awawiye radhi– amesema: Nilimuona
Mtume–Rehema na Amani zimshukie– anapokuwa
na safari ya haraka huiakhirisha swala ya
Magharibi na kuiswali rakaa tatu (kama kawaida),
kisha hutoa salamu. Halafu hakai kitambo kirefu
ila hukimu (Iqaamah) Ishaa na kuiswali rakaa
mbili (Qaswru), kisha hutoa salamu”. Bukhaariy
KUWEMO SAFARINI MPAKA KUVAANA NA
SWALA YA PILI.
Ni sharti swala mbili zote
zinazojumuishwa ziswaliwe na il-hali mjumuishaji
angali safarini, hii ni kutokana na kufungamana
kwa rukhsa ya kujumuisha na safari. Yaani rukhsa
hii hutumika safarini, kwa mantiki hii basi
isitokee mojawapo ya swala jumuisho kuswaliwa
safarini na nyingine nje ya safari.
b) SHARTI ZA UJUMUISHAJI WA
KUAKHIRISHA:
Kujumuisha swala kwa kuakhirisha
kunatawaliwa na sharti mbili zifuatazo:-
KUNUIA KUJUMUISHA SWALA YA
MWANZO NDANI YA WAKATI WAKE.
Msafiri anayekusudia
kuzijumuisha swala za Adhuhuri na Alasiri
mjumuisho wa kuakhirisha,
mathalani. Inamapasa kutia nia ya kuijumuisha
swala hii ya mwanzo inayoakhirishwa (Adhuhuri)
ili iswaliwe pamoja na Alasiri ndani ya wakati
wa Alasiri. Atie nia ya kuijumuisha Adhuhuri
ndani ya wakati wake, yaani wakati wa Adhuhuri.
Angalia ikiwa hakutia nia ya kujumuisha Adhuhuri
na Alasiri kwa kuakhirisha mpaka ukatoka wakati
wa Adhuhuri na kuingia Alasiri. Swala hii ya
Adhuhuri itakuwa katika dhima yake kwa njia ya
“kadhaa” inayoambatana na dhambi ya kuiswali
nje ya wakati wake.
KUWEMO SAFARINI MPAKA KUMALIZA
KUZISWALI SWALA ZOTE MBILI PAMOJA
Kama tulivyotangulia kueleza
kuwa rukhsa hii ya kujumuisha inafungamana na
safari. Ni sharti swala mbili hizi
zinazojumuishwa kwa kuakhirishwa ziswaliwe zote
ndani ya safari. Katika ujumuishaji huu wa
kuakhirisha haikupokelewa sharti ya utaratibu,
bali mjumuishaji ana khiyari ya kuanza na swala
yo yote miongoni mwa mbili hizo aitakayo.
|