Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

RUKHSA YA KUJUMUISHA ....Inaendelea

 

3. SHARTI ZA SAFARI ILIYORUHUSIWA KUKUSURU NA KUJUMUISHA NDANI YAKE.

Msafiri hapati rukhsa ya kukusuru au kujumuisha swala ndani ya safari mpaka kwanza safari yake hiyo itimize sharti tatu zifuatazo:-

             I.      MASAFA YA KILOMETA THEMANINI NA MOJA (80km) NA KUENDELEA: Ni sharti safari iwe ndefu inayoanzia kilometa themanini na moja na kuendelea. Kwa matazamo wa sheria haiwi ni safari, safari iliyo chini ya masafa haya. Hiyo haitakuwa ni safari inayopata rukhsa hii ya kujumuisha au kukusuru. Imepokelewa kwamba Ibn Umar na Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-walikuwa wakikusuru swala na wakifuturu (wakila mchana wa Ramadhan) katika (safari ya umbali wa) ‘burudi’ nne, ambazo ni sawa na ‘farsakh’ kumi na sita (zilizo sawa na kilometa themenini na moja takriban). Walikuwa wakifanya hivyo kutokana na elimu/ujuzi walioupata kutoka kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie.

           II.      MUELEKEO WA SAFARI (DESTINATION): Rukhsa ya kukusuru au kujumuisha haitapatikana mpaka safari husika iwe na muelekeo maalumu. Kwamba mtu anasafiri kutoka sehemu fulani kwenda sehemu fulani, yaani kuwepo kituo cha kuanzia na kumalizikia safari. Isiwe mtu yumo safarini anakwenda tu bila ya kujua safari itakomelea wapi. Mfano wa mtu anayemtafuta mtu/kitu kilichopotea au askari anayemfuata kamanda wake bila ya kujua anakwenda wapi. Hawa na kama hawa hawapati rukhsa ya kukusuru/kujumuisha mwanzoni mwa safari yao ila baada ya kusafiri umbali wa kilometa themanini na moja. Katika umbali huo ndio wataanza kupata rukhsa ya kujumuisha/kukusuru swala.

        III.      UHALALI WA SAFARI: Ili safari iambatane na rukhsa hii ya kujumuisha/kukusuru swala ni lazima iwe na malengo halali. Lengo la safari lisiwe limefungamana na maasi kwa namna yo yote ile iwayo. Ikiwa mtu anasafiri kwa ajili ya biashara haramu (kama  kuuza/kutangaza ulevi), kwenda kupokea riba/rushwa au kufanya unyang’anyi njiani na kadhalika. Huyu/hawa kisheria sio wasafiri na hiyo sio safari.

 

KIAMBATISHI.

KUJUMUISHA SWALA KWA SABABU YA MVUA.

Sheria inampa muislamu rukhsa ya kujumuisha swala mbili mjumuisho

wa kutanguliza kwa sababu ya mvua. Rukhsa hii ni zao la riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliswali Madinah rakaa saba na rakaa nane: Adhuhuri na alasiri (rakaa nane), na maghribi na ishaa (rakaa saba) bila ya kuwepo khofu wala safari. Bukhaariy & Muslim.

Na katika riwaya aliyopwekeka nayo Imamu Bukhaariy: Alisema Ayoub-mmoja wa wapokezi wa hadithi hii: Huenda ilikuwa katika usiku wa mvua? Akasema (Ibn Abbas): Labda/huenda.

Rukhsa hii ya kujumuisha kwa sababu ya mvua inahusisha tu ujumuishaji wa kutanguliza na si ujumuishaji wa kuakhirisha. Hii ni kutokana na kuwepo uwezekano wa kukatika kwa mvua wakati ule wa swala ya pili na hivyo kumfanya kuwa ameitoa swala ya kwanza katika wakati wake bila ya udhuru. Ujumuishaji huu kwa sababu ya mvua umeshurutiziwa sharti zifuatazo:-

1)     Swala inayojumuishwa iwe ni swala ya jamaa inayoswaliwa katika msikiti wa mbali. Msikiti ambao kama mtu ataamua kuuendea  atafika akiwa ametota kabisa au kuchafuka kutokana na tope la njiani au kupata maudhi ya aina yo yote ile. Marejeo ya umbali, yanaachiwa ada/desturi ya mahala husika.

2)     Kudumu/kuendelea kunyeesha kwa mvua mwanzo wa swala mbili hizo na wakati wa kutoa salamu ya swala ya kwanza. Kwa maneno mengine hivi ni sawa na kusema kuwa swala ya mwanzo miongoni mwa swala mbili hizo zinazojumuishwa iswaliwe yote ndani ya mvua yaani wakati mvua ikiendelea kunyeesha.

 

4. SWALA YA KADHAA (KUKIDHI SWALA ZILIZOPITA).

Miongoni mwa nembo na alama ambazo ni kielelezo cha muumini wa kweli ni kuswali swala katika nyakati zake zilizowekwa na sheria. Kwa kuitekeleza kauli ya Allah Mola Muumba wake: “...KWA HAKIKA SWALA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA NYAKATI MAKHSUSI”. [4:103] Kwa mujibu wa kauli hii ya Allah, muislamu atakapoiakhirisha swala mpaka ukatoka wakati wake bila ya kuiswali ndani ya wakati wake huo, atakuwa amefanya dhambi kubwa. Nini kinachofuatia baada ya mtu kupitwa na swala? Mafaqihi wamekongamana na kuwafikiana kwamba itakayemfutu (itakayempita) swala, kunamlazimu kuikidhi (kukidhi swala ni kuiswali nje ya wakati wake). Kwa mfano mtu iliyomfutu swala ya adhuhuri na ukaingia wakati wa alasiri, kutamlazimu mtu huyo kuswali swala ya adhuhuri iliyomfutu kabla ya kuiswali ile ya alasiri. Hii ni kwa sababu utaratibu katika swala tano za fardhi ni suala la wajibu. Kwa maana hii basi, kumalizika kwa wakati wa swala iliyofutu (adhuhuri) hakuupomoshi utaratibu baina yake na swala ya sasa (alasiri). Angalia  utaratibu hautafuatwa wala kuzingatiwa iwapo tu swala ilimfutu kwa sababu ya kusahau kunakozingatiwa na sheria. Au kwa kudhikika (kuwa finyu) wakati wa swala ya sasa (alasiri), kiasi kwamba kama ataanza kuswali adhuhuri, wakati wa alasiri utakuwa umetoka na kuingia maghribi na hivyo kuifanya hii alasiri nayo kuwa ni kadhaa ya pili. Au kuwa swala zilizofutu ni zaidi ya swala sita au mtu kukumbuka kuwa hajaswali alasiri mathalan, wakati yumo ndani ya swala ya maghribi. Katika hali na mazingira yote haya utaratibu hautazingatiwa.

Ni haramu kwa mtu ambaye anawiwa na swala za fardhi zilizomfutu kujishughulisha kuswali swala za suna, bali anapaswa kuutumia muda huo wa kuswali suna kuzikidhi swala hizo za fardhi zilizomfutu. Angalia anaweza kuswali suna andamizi za swala (Qabliyah na Ba’adiyah) na suna kokotezwa (Muakadah) kama witri na rakaa mbili za kabla ya alfajiri. Kadhalika anaweza kuswali swala ya Eid na swala zote za suna zilizopata hukumu ya ‘suna kokotezwa’.

Kadhalika kunampasa mtu aliyefutiwa swala na wakati wake kutoka, kuiswali swala hiyo wakati wa kuikidhi kwa namna yake iliyopasa. Ikiwa ni swala ya jahriyah ataiswali kwa jahra (kwa kutoa sauti) na ikiwa ni swala ya siriyah ataiswali kwa kuisirisha (bila ya kutoa sauti).

 

HITIMISHO:

Imekongamana na kuwafikiana Jumuhuri ya ulamaa wa madhehebu zote kwamba mtu mwenye kuacha swala anakalifishwa kuikidhi swala hiyo aliyoiacha. Taklifu hii itamuandama bila ya kujali kuwa aliiacha swala kwa kusahau au kwa makusudi lakini pamoja na upambanuzi wa hali mbili hizo; kusahau na kusudi. Iwapo mtu aliiacha swala kwa udhuru unaozingatiwa kisheria kama kulala au kusahau. Huyu hapati dhambi na wala hakumlazimu kukidhi haraka bila ya kuchelewa. Ama yule mwenye kuiacha bila ya udhuru, yaani kaacha kuswali kwa makusudi tu, huyu pamoja na kupata dhambi kutamuwajibikia kukidhi haraka bila ya kuchelewa.

Dalili/ushahidi wa kukidhi swala ni kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Atakayelala (akapitwa) na swala au akaisahau, basi na aiswali atakapoikumbuka, haina kafara (swala iliyoachwa) ila hiyo”. Bukhaariy, Muslim & wengineo.

Kauli ya Bwana Mtume (haina kafara ila hiyo), ndio inayofahamisha kwamba hapana budi kuikidhi swala ya fardhi iliyofutu, kwani hiyo ndio njia pekee ya kumvua mja na dhima ya swala iliyomfutu.

 

 



Forum | Guestbook | Tuandikie |