|
Najisi kwa mtazamo wa sheria zimegawanywa katika aina tatu zifuatazo :
- NAJISI NZITO : Hii ni najisi ya mbwa na nguruwe na mnyama aliyezaliwa kutokana nao
au mmoja wao (mbwa na nguruwe). Najisi hii imeitwa najisi nzito kutokana na uzito
unaompata mtu katika kuiondosha
- NAJISI KHAFIFU : Hii ni mkojo wa mtoto mchanga wa kiume aliye chini ya miaka miwili
na hali ila maziwa ya mama tu. Najisi hii imeitwa Najisi khafifu kwa sababu ya wepesi
unaopatikana katika uiondosha.
- NAJISI YA KATI NA KATI : Hii imekusanya baki ya najisi nyingine ukiondoa najisi ya
mbwa na nguruwe na mkojo wa mtoto mchanga wa kiume. Najisi hii imeitwa Najisi ya kati na
kati kwa kuwa haiko kwenye uzito na wala haikufika kwenye ukhafifu.
JINSI/NAMNA YA KUZIONDOSHA NAJISI HIZI :
Ni muhimu tukakumbuka kuwa ni haramu kujipakaza najisi na ni wajibu kuiondosha
mara tu inapoingia mwilini, nguoni au mahala pake mtu.
Hutwahirishwa mahala palipoingiwa na najisi ya mbwa na nguruwe kwa kupaosha mahala
hapo paliponajisika kwa kupaosha mara saba na mojawapo wa mara saba hizo iwe kwa kusugua
na mchanga. Bwana Mtume -Allah amrehemu na amshushie amani- amesema :
"Twahara ya chombo cha mmoja wenu atakapokiramba mbwa ni kukiosha mara saba, ya
kwanza yake ( hizo mara saba) iwe ni kwa mchanga" Muslim
Najisi khafifu hutwahirishwa mahala paliponajisika kwa kuingiwa/kupatwa na najisi
khafifu kwa kuimwagia maji sehemu hiyo, maji yaenee. Imepokewa hadithi kutoka kwa Ummu
Qays Bint Mihswan-Allah amridhie- kwamba alimpeleka Mtume wa Allah mtoto wake mdogo wa
kiume ambaye hajala chakula (ananyonya) akamkojolea (mtume) nguoni, akaagizia maji na
kuyamiminia palipokojolewa na hakuifua (nguo)". Bukhaariy na Muslim.
Najisi ya kati na kati, mahala paliponajisika kwa kuingiwa na najisi hii
hutwaharishwa kwa kupaosha na maji twahara mpaka iondoke rangi, utamu na harufu ya najisi
hiyo. Haidhuru kubakia kimojawapo rangi au harufu ziloshindikana kuondoka.
TANBIHI : Usiitumbukize nguo iliyonajisika ndani ya maji machache kama vile ndoo
ukadhani kuwa umeitwahirisha bali itakuwa bado imenajisika na kunajisisha maji yote na
hivyo kuyafanya yasifae tena kutwahirishia. Unachopaswa kufanya ni kutumia kata au kilicho
mfano wa kata, uteke maji na kuitwahirishia nguo hiyo pembeni ambapo maji yanayochuruzika
kutoka katika nguo iliyonajisika hayaingii tena chomboni.
TWAHARA YA ARDHI :
Ardhi ikipatwa na najisi, hutwahirishwa kwa kumwagiwa maji juu yake mpaka najisi
iondoke, hivyo ndivyo alivyoagiza Bwana Mtume. Imepokelewa riwaya kutoka kwa Abuu
Hurayra-Allah amridhie- kwamba amesema : Alikuja bedui mmoja akakojoa msikitini, watu
(maswahaba) wakamuinukia ili wamuadhibu, Mtume akawaambia : "Mwacheni (amalize haja
yake) na (kisha) mumwagie mkojo wake ndoo ya maji" Bukhaariy na Muslim.
Msikiti wa Bwana Mtume Allah amshushie rehma na amani- ulikuwa haukusakafiwa
kama ilivyo misikiti yetu ya leo bali ulikuwa na sakafu ya udongo/mchanga kama zilivyo
nyumba zetu za vijijini.
Ardhi pia hutwahirika kwa kukauka yenyewe kutokana na kupigwa kwa jua au
kunyeshewa mvua na kuondoka athari ya najisi.
TWAHARA YA SAMLI, JIBINI, SIAGI NA MFANO WA VITU HIVYO
Samli, jibini siagi na vitu vinavyofanana navyo vikiingiwa na najisi na vikiwa
katika hali ya ugumu na vimeganda na si hali ya kumiminika, hutwahirika kwa kuitoa najisi
iliyoingia pamoja na sehemu zinazozunguka/zilizojiranikiana na najisi ile.
Bwana Mtume-Allah amshushie rehema na amani- aliulizwa kuhusiana na (hukmu ya)
panya aliyetumbukia (na kufia) ndani ya samli, akajibu "Mtupeni na sehemu
inayomzunguka na kuleni samli yenu". Al-Bukhariy.
Ama itakapokuwa samli, siagi, jibini na chochote chenye kufanana navyo katika hali
ya kumiminika/maji maji na ikaingiwa na najisi itanajisika yote na haitofaa tena kwa
matumizi ya binadamu.
TWAHARA YA NGOZI
Ngozi ya mnyama hutwahirishwa kwa kudabighiwa. Dabghu ni kuondosha damu, mafuta na
mabaki ya nyama zilizosalia katika ngozi baada ya mnyama kuchunwa. Uondoshaji huu
hufanyika ka kutumia vitu vikali vyenye muonjo wa asidi, baada ya hapo ndipo ngozi
hutwahirishwa na maji na kufaa kutumika kwa matumizi mbali mbali ya binadamu. Imepokelewa
na Ibn Abbas Allah amridhie- kwa Bwana Mtume-Allah amshushie rehema na amani-
amesema "Ngozi itakapodabighiwa imetwahirika" Bukhaariy na Muslim.
|