Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

SOMO LA NNE

 

SIJIDA YA KUSAHAU (SIJIDATIS–SAH–U).

 AINISHO/MAANA YA KUSAHAU:

Neno “Kusahau” lina maana mbili kama ifuatavyo:-

             I.      KUSAHAU KILUGHA:
Katika lugha ya kawaida kusahau kunamaanisha kupoteza kumbukumbu za kitu/jambo au kughafilika na jambo. Bila ya kujali kuwa upotezaji huu wa kumbukumbu ni wa muda tu au ni wa milele.

            II.      KUSAHAU KISHERIA (KIFIQ-HI):
Muradi  na  mapendeleo ya neno “kusahau”  katika somo letu  hili ni yale makosa  (kunguwao)  anayoyafanya mwenye kuswali ndani ya swala  yake. Bila ya kuangalia amefanya makosa  hayo kwa bahati mbaya  (kwa kusahau) au kwa  makusudi mazima.

 

FALSAFA/HEKIMA YA SIJIDA YA KUSAHAU: 

Sheria ya Kiislamu  imeyazingatia maumbile ya mwanadamu na kumuona  kuwa ni kiumbe  dhaifu anayesahau  na kukumbuka kwa kuyazingatia maumbile haya ya mwanadamu ndipo  sheria  ikamuwekea kiumbe huyu  “Sijida ya  kusahau” katika swala yake ili:-

Amfukuzilie mbali shetani anayemtia  katika  wasiwasi  huu wa kusahu.

Ayazibe makosa ambayo kwa namna moja au nyingine anaweza kuyatenda ndani ya  swala  yake.

iii)HUKUMU YA  SIJIDA YA KUSAHAU:

      Sijida hii ya kusahau inaweza kuwa  ama ni wajibu au  ni suna.

Wakati gani sijida ya kusahau inakuwa ni WAJIBU?                     Sijida ya kusahau inakuwa wajibu wakati ambapo mwenye  kuswali anapokuwa  maamuma nyuma ya Imamu  wake. Imamu wake  huyu atakaposahau na kusahu kwake huku kukampelekea kusujudu kwa sababu ya kusahau huko. Akasujudu  sijida ya kusahau katika hali hii kutamuwajibikia maamuma  aliye nyuma ya Imamu huyu kumfuata Imamu wake katika kusujudu huko hata  kama yeye  (maamuma) hakusahau. Angalia  maamuma huyu atapomkhalifu Imamu wake  asimfuate katika huko kusujudu swala  yake itabatilika na kutamuwajibikia kuirejea  tena  (kuiswali upya.

 

Wakati gani sijida ya kusahau inakuwa SUNA ?

Sijida ya kusahau itakuwa ni suna  wakati ambapo mwenye kuswali atapoacha  cho chote ambacho si katika jumla ya  nguzo za swala  kama kuacha kuleta Qunuut katika  swala  ya Sub-hi au swala ya Witri ya Ramadhani.

 

DALILI/USHAHIDI WA SIJIDA YA KUSAHAU: 

Sijida ya  kusahau imethibiti  katika  Suna ya Mtume. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah–Allah amuwiye radhi– amesema: “Mtume wa Allah-Rehema  na Amani zimshukie: Alituswalisha swala ya Adhuhuri au ya Alasiri, akatoa salamu. Dhul-yadaini akamwambia: Swala  ewe Mtume wa Allah, je imepunguzwa  (idadi ya rakaa zake)? Mtume akauliza: “Ni kweli ayasemayo (Dhul-yadaini)? (Maswahaba) wakasema: Naam, (Mtume) akaswali rakaa mbili nyingine, kisha  akasujudu sijida mbili”. Bukhaariy

Tutazitaja dalili nyingine wakati tutakapotaja sababu za kusujudu sijida ya kusahau.

 

MGAWANYO WA MATENDO YANAYOWEZA KUACHWA NA MWENYE KUSWALI NDANI YA  SWALA YAKE:

Matendo ya  swala ambayo mwenye  kuswali anaweza kuyaacha ndani ya swala yake ama kwa makusudi au kwa kusahau,  yanagawika katika mafungu matatu. Ima  mwenye kuswali atakuwa ameacha tendo  linalloitwa:-

FARDHI na pia huitwa NGUZO, au

2. SUNAH na sunah ikusudiwayo hapa ni ile  inayoitwa    “Ba’adh”.

SUNAH isiyo “Ba’adh”, yaani suna iitwayo  “Haiah”. Hii ni kama vile Takbira za  maguroguro (kuhama kutoka Qiyaamu kwenda  rukuu, kutoka Itidali kwenda  sijida na  kadhalika) na kunyanyua/kuinua mikono  wakati wa kuleta Takbira ya kuhirimia  swala.

 

HUKUMU  ZINAZOANDAMIA MATENDO HAYA:

FARDHI: Tendo la fardhi/nguzo lililoachwa  kwa makusudi HUBATILISHA swala  na lile lililoachwa kwa makusudi halikaliwi badali, yaani haliungwi na sijida ya kusahau.

 2. SUNAH BA’ADH: Tendo la Sunah  mithili ya Tashahudi   ya mwanzo, mkao wake, Qunuut. Mwenye kuswali akisahau kuleta cho chote miongoni mwa matendo haya, atapaswa  kusujudu sijida ya kusahau.

 SUNA HAIAH: Tendo linaloingia chini ya  sunah hii ni mithili ya Tasbihi za  rukuu,  sijida na kadhalika.  Mwenye  kuswali  hawajibikiwi kusujudu kwa kusahau bila ya  kuangalia kuwa aliacha makusudi au kwa  kusahau.

 

SABABU ZA  SIJIDA YA KUSAHAU:

Mambo yafuatayo ndio yatakayo mpelekea mwenye kuswali  kuleta sijida ya  kusahau:

  •       Mwenye kuswali kuacha  mojawapo  miongoni  mwa suna za swala zinazoitwa “Ab-aadh”, mithili ya Tashahudi ya mwanzo na Qunuut  (kwa ufafanuzi wa kina juu ya suna hizi, rejea SURA YA PILI, SOMO LA KWANZA, SWALA {x} Suna za swala). Imepokewa kutoka kwa Abdullah Ibn Buhaynah-Allah amuwiye radhi–kwamba yeye amesema:  Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-alituswalisha rakaa mbili za  swala fulani. Na katika upokezi mwingine: “Aliinuka  kutoka katika  rakaa mbili za  swala ya Adhuhuri, kisha akasimama na  wala hakukaa            (Tashahudi  ya mwanzo), watu (maamuma)  nao wakainuka pamoja nae. Alipomaliza swala yake  (kwa kuswali rakaa mbili za mwisho), (wakati) tukiingojea salamu yake,  akakabiri  (akasema  Allahu  Akbar) kabla ya kutoa salamu. Akasujudu  sijida mbili na il-hali amekaa,  kisha (ndio) akatoa salamu. Bukhaariy &  Muslim.

Imepokelewa  kutoka kwa Al-Mughiyrah Ibn  Shu’ubah–Allah amuwiye radhi–amesema: Amesema Mtume wa Allah–Rehema na Amani  zimshukie: “Atapoinuka mmoja wenu kutoka  (katika) rakaa mbili        (za mwanzo) na  akawa hajatimia hali ya  kusimama , basi na akae (kwa   ajili ya Tashahudi ya mwanzo. Na atapotimia  hali ya kusimama, basi na asikae (aendelee na  swala yake)  na atasujudu sijida mbili  za  kusahau”. Ibn  Maajah, Abuu Daawoud & wengineo.

 

  •       Mtu kuwa na shaka ya  idadi ya rakaa alizoziswali. Katika hali hii, mwenye shaka anatakiwa aishike idadi ya chini na atimize rakaa  zilizobakia.  Kisha  atasujudu  sijida ya kusahau  kwa ajili ya kuunga imkani ya kwamba yeye  amezidisha kitu katika swala yake. Lau mtu  atakuwa  na  shaka je,  ameswali  Adhuhuri rakaa  tatu au nne? Shaka hii ikamtokea akiwa  bado ndani  ya swala, basi atachukulia kuwa  ameswali rakaa tatu na aongeze rakaa moja  nyingine ili zitimie rakaa nne zitakiwazo. Halafu  tena  akimaliza asujudu sijida mbili za kusahau  kutokana na imkani ya kuwa kaswali  rakaa  tano na hivyo kuwa amezidisha  kitu katika  swala yake.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Said–Allah   amuwiye radhi–amesema: Amesema Mtume wa  Allah–Rehema na Amani zimshukie: “Atapotia  shaka  mmoja wenu ndani ya swala yake,  na asijue ameswali rakaa ngapi, tatu au nne? Basi (cha  kufanya) ni kuitupa  shaka hiyo na ajengee  alicho na yakini  nacho. Kisha asujudu sijida mbili kabla  ya kutoa salamu.  Akiwa ameswali  rakaa tano, (kusujudu huko)  kutaifanya   swala  yake  kuwa jozi  (ya  rakaa   mbili za  mwanzo  na mbili za  mwisho).  Na   akiwa ameswali    kutimiza rakaa nne, zitakuwa  (sijida  mbili) hizo zimemdhalilisha na  kumghadhibisha shetani”. Muslim.

Ama lau mtu alitia shaka   nje  ya swala  (baada ya kutoka  ndani ya swala) kwa yakini shaka yake hii  haitaathiri usahihi na ukamilifu wa swala  yake. Ila kama shaka hiyo itakuwa ni   katika nia na  Takbira ya kuhirimia swala,  shaka hii itamlazimisha  kuirudia (kuiswali  tena) swala yake.

 

TANBIHI:

Kusahau kwa maamuma wakati wa kumfuata Imamu wake, kama vile kusahau Tashahudi ya  mwanzo. Kusahau kwake huku kutachukuliwa na Imamu wake na wala haitamlazimu kusujudu sijida mbili za kusahu baada ya  salamu ya Imamu wake. Dalili ya  haya ni kauli   yake    Bwana  Mtume–Rehema na Amani zimshukie: “Imamu ni mdhamini    (wa  maamuma)”. Ibn Hibbaan

 


 

 


Forum | Guestbook | Tuandikie |