|
I.
MAANA YA SWALA YA JAMAA:
Muradi
na mapendeleo ya swala ya jamaa ni ile swala ya
fardhi au ya suna iliyosuniwa kuswaliwa jamaa.
Inayoswaliwa kwa pamoja na zaidi ya mtu mmoja
ndani ya msikiti au nje ya msikiti. Hii ndio
swala ya jamaa tutakayohusika nayo katika somo
hili.
II.
HISTORIA FUPI YA SWALA YA JAMAA:
Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alianza
kusimamisha swala ya jamaa Madinah baada ya
Hijrah. Katika kipindi chote cha utume alichokaa
Makah, kipindi kisichopungua miaka kumi na tatu
hakupata kuswali jamaa. Hili lilitokana na
unyonge waliokuwa nao maswahaba wakati huo na
hivyo kusababisha kila mmoja wao kuswali pekee
nyumbani kwake. Mtume alipohamia Madinah na
Uislamu ukawa na nguvu ndipo swala ya jamaa
ikaanza na akaidumisha mpaka anaondoka duniani.
III.
HUKUMU YA SWALA YA JAMAA:
Ilivyo
sahihi ni kwamba jamaa isiyokuwa ya swala ya
Ijumaa ni FARDHI KIFAAYAH.
Hauwapomokei/hauwaondokei ufaradhi wake watu wa
mji ila pale mahala ambapo inapodhihiri
nembo/alama yake. Iwapo swala ya jamaa
haikuswaliwa kabisa katika mji au ikaswaliwa kwa
uficho, watu wote wa mji husika watapata dhambi
na kutamuwajibikia Imamu (kiongozi) kuwapiga
vita mpaka waisimamishe jamaa.
Asili
na chimbuko la swala hii ya jamaa ni kauli yake
Allah Mola Mtukufu: “NA UNAPOKUWA PAMOJA NAO
(waislamu katika vita) UKAWASWALISHA (jamaa),
BASI KUNDI MOJA MIONGONI MWAO WASIMAME PAMOJA
NAWE (waswali)...”. [4:102]
IV.
FADHILA/UBORA WA JAMAA:
Swala
ya jamaa ina fadhila kubwa na ujira adhimu.
Zimepokewa hadithi nyingi sahihi katika kutaja
na kueleza fadhila na ubora wa swala ya jamaa.
Mbali na kutaja fadhila za jamaa, hadithi hizo
kwa upande mwingine pia ni ushahidi wa swala ya
jamaa. Miongoni mwa hadithi hizo ni hizi
zifuatazo, amesema Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie:-
1)
“Swala ya jamaa inaizidi swala ya mtu
pweke (munfaridi) kwa daraja ishirini na
saba”. Bukhaariy & Muslim
2)
“Hapana watu watatu kijijini au
kitongojini haisimamishwi miongoni mwao swala ya
jamaa ila shetani huwatawala na kuwageuzia
kwake. Hakika si vinginevyo mbwa mwitu humla
kondoo aliye mbali na kundi”. Abuu Daawoud
& Ibn hibbaan.
3)
“Ninamuapia yule ambaye nafsi yangu imo
mikononi mwake, kwa yakini niliazimia kuamrisha
zikusanywe kuni, kisha niamrishe swala
iadhiniwe. Halafu nimuamrishe mtu awaswalishe
watu, kisha mimi niwaendee watu wasiohudhuria
swala ya jamaa nikawachomee nyumba zao”.
Bukhaariy & Muslim
V.
FALSAFA/HEKIMA YA SWALA YA JAMAA:
Hakika
si vinginevyo nguzo hii ya Uislamu husimama juu
ya msingi wa kufahamiana waislamu na kuwa ndugu
wenye kusaidiana katika kuithubutisha haki na
kuiondosha batili. Kufahamiana na kuunga udugu
huku hakutimii katika kumbi zilizo bora zaidi
kuliko kumbi za misikiti ambamo waislamu
hukutana humo mara tano kila siku kwa ajili ya
kutekeleza fardhi ya swala. Misikitini ndimo
mahala ambamo tofauti za watu kimaslahi, chuki
binafsi na mifundo huondoshwa
kutokana na
kukutana kwao mara tano kila siku katika
swala ya jamaa.
VI.
UCHACHE WA JAMAA:
Jamaa
hufungamana kwa watu wawili; imamu na maamuma na
kuendelea. Hivyo ndivyo ilivyokuja katika
hadithi kadhaa za Bwana Mtume. Amesema Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Watu wawili
na kuendelea ni jamaa hiyo”. Katika hadithi
nyingine Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alimwambia Maalik Ibn al-Huwayrith na
mwenziwe: “Na aadhini mmoja wenu (wawili nyie)
na akuswalisheni aliye mkubwa kati yenu”.
Imepokelewa
na Abuu Said Al-Khudriy-Allah amuwiye
radhi-kwamba mtu mmoja aliingia msikitini wakati
ambapo tayari Mtume alikuwa ameshawaswalisha
maswahaba wake. Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akasema: “Nani atampa sadaka huyu,
akaswali pamoja nae? Akasimama mtu mmoja
akaswali pamoja nae (jamaa)”. Ahmad, Abuu
Daawoud & Tirmidhiy
Na
kila idadi ya watu inapozidi ndio hupendeza
zaidi kwa Allah, haya ni kwa mujibu wa kauli
yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:
“Swala ya mtu pamoja na mtu hupendeza zaidi
(nzuri zaidi) kuliko swala yake pekee. Na swala
yake pamoja na watu wawili hupendeza zaidi
kuliko swala yake na mtu mmoja. Na swala yenye
idadi kubwa (ya watu) hupendeza mno kwa
Allah”. Ahmad, Abuu Daawoud, Nasaai & Ibn
Hibbaan.
Na
kuwa swala ya jamaa msikitini ni bora zaidi
kuliko kuswaliwa nyumbani. Na jamaa ya msikiti
wa mbali ni bora zaidi kuliko ile ya msikiti wa
karibu. Hili linatokana na kauli ya Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Hakika mtu
mwenye ujira mkubwa katika swala kuliko wote ni
yule wa mbali wao zaidi kuiendea swala”.
Muslim
TANBIHI:
Kunajuzu
kwa wanawake kuhudhuria swala ya jamaa
misikitini kwa sharti ya kujiepusha na
mambo/vitu vinavyoweza kuamsha matamanio na
kupelekea kuzuka kwa fitna. Yaani watoke kwenda
huko misikitini hali ya kuwa wamejistiri kwa
mujibu wa sheria, hawakujipamba wala kujitia
manukato. Imepokelewa kutoka kwa Abuu
Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Msiwazuilie vijakazi wa Allah na misikiti ya
Allah na watoke (kwenda huko) bila ya kujitia
manukato”. Ahmad & Abuu Daawoud.
Akasema
tena Bwana Mtume: “Mwanamke ye yote
aliyejifukiza udi asihudhurie pamoja nasi swala
ya Ishaa”. Muslim, Abuu Daawoud & Nasaai.
Pamoja
na wanawake kuruhusiwa kuswali jamaa misikitini
lakini ilivyo bora kwao ni kuswali majumbani
mwao. Imepokewa kutoka kwa Ummu Humayd
As-saaidiyah-kwamba yeye alimuendea Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia: Ewe
Mtume wa Allah, hakika mimi ninapenda kuswali
pamoja nawe (jamaa). Bwana Mtume akamwambia:
“Kwa yakini ninalitambua hilo, (lakini) na
swala yako chumbani kwako ni bora kwako wewe
(swala hiyo) kuliko swala yako katika msikiti wa
jamaa zako (kitongojini mwako).
Na swala yako katika msikiti wa jamaa
zako ni bora kwako kuliko swala yako katika
msikiti wa jamaa”. Ahmad & Twabaraaniy
VII.
NAMNA YA KUTOKA KWENDA MSIKITINI
KUHUDHURIA SWALA YA JAMAA:
Kumesuniwa
kwa mtu mwenye kutoka nyumbani kwake kwenda
msikitini kuhudhuria swala ya jamaa, atangulize
mguu wake wa kulia na aseme wakati wa kutoka:
“BISMILLLAAHI TAWAKKALTU ‘ALAL-LAAH, WALAA
HAULA WALAA QUWWATA ILLA BILLAAH, ALLAAHUMMA
INNIY ‘AUDHUBIKA AN ADHWILLA AU UDHWALLA, AU
AZILLA AU UZALLA, AU ADHWLIMA AU UDHWLAMA, AU
AJ-HALA AU UJ-HALA ‘ALAYYA. ALLAAHUMMA INNIY
AS-ALUKA BIHAQQIS-SAAILIYNA ‘ALAYKA WA BIHAQQI
MAMSHAAYA HAADHA, FAINNIY LAM AKHRUJ ASHARA
WALAA BATWARAA, WALAA RIYAA WALAA SUM’AH,
KHARAJTUT-TIQAA SUKHTWIKA WABTIGHAA
MARDHWAATIKA. AS-ALUKA AN TAHGFIRA LIY DHUNUUBIY
JAMIY’AN, FAINNAHU LAA YAGHFIRUD-DHUNUUBA ILLA
ANTA. ALLAAHUMMAJ-‘AL FIY QALBIY NUURA, WA FIY
LISAANIY NUURA, WA FIY SAM’IY NUURA, WA FIY
BASWARIY NUURA, WA ‘AN YAMIYNIY NUURA, WA
‘AN SHIMAALIY NUURA, WA MIN FAUQIY NUURA,
ALLAAHUMMA A’ADHWIM FIYYA NUURA”.
Dua
hii ni mkusanyiko wa matamko ya riwaya tofauti
zilizopokewa na maimamu Tirmidhiy, Bukhaariy
& Muslim
Kisha
aanze kupiga khatua kuelekea huko msikitini kwa
ushwari, utulivu, heshima na staha. Imepokelewa
kutoka kwa Abuu Qataadah-Allah amuwiye
radhi-amesema: Wakati ambapo sisi tukiswali
pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-mara akasikia ghasia za watu.
Alipomaliza kuswali akauliza: “Mna nini
nyinyi”. Wakajibu tulikuwa tunaikimbilizia
swala. Mtume akawaambia: “Msifanye hivyo,
mnapoiendea swala basi umekulazimuni utulivu
(ushwari). Po pote mtapoidiriki swalini na
kilichokufutuni (katika hiyo swala) basi
kitimizeni (baada ya imamu kutoa salamu)”.
Bukhaariy, Muslim & wengineo. Akishafika
msikitini, autangulize mguu wake wa kulia wakati
wa kuingia na aseme: “BISMILLAAH,
‘AUDHUBILLAAHIL-‘ADHWIYM,
WABIWAJIHIHIL-KARIYM WASULTWAANIHIL-QADIYM
MINAS-SHAYTWAANIR-RAJIYM, ALLAAHUMMA SWALLI
‘ALAA NABIYYINAA MUHAMMADIN WA AALIHI
WASALLAM, ALLAAHUMMMAGH-FIRLIY DHUNUUBIY, WAFTAH
LIY ABWAABA RAHAMATIKA”. Dua hii ya kuingia
msikitini imepokewa na Imamu Ahmad & Ibn
Maajah
Akishaingia
msikitini basi asikae kitako mpaka aswali rakaa
mbili za suna ijulikanayo kama
‘Tahiyyatul-Masjid’. Haya ndio maelekezo ya
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-katika
kauli yake: “Atapoingia mmoja wenu msikitini
basi na asikae kitako mpaka aswali (kwanza)
rakaa mbili”. Muslim
Ila
kama ataingia msikitini wakati wa kuchomoza au
kuzama kwa jua, wakati huo atakaa bila ya
kuswali, kwa sababu Bwana Mtume amekataza
kuswali ndani ya nyakati mbili hizo. Na wakati
wa kutoka msikitini kurudi nyumbani, atoke kwa
kutanguliza mguu wa kushoto na aisome dua hii
tuliyoitaja hapo juu. Ila badala ya kusema:
WAFTAH LIY ABWAABA RAHMATIKA, atasema: WAFTAH
LIY ABWAABA FADHWLIKA.
|