|
Nyudhuru zinazoweza kumfanya mtu
kutokuhudhuria swala ya jamaa msikitini,
zinagawika katika mafungu mawili makuu kama
ifuatavyo:-
a)
NYUDHURU JUMUIA:
Hizi ni pamoja na mvua kubwa, upepo mkali
wakati wa usiku na matope mengi njiani
kiasi cha kumchafua mtu au kumuangusha.
Imepokelewa kwamba Ibn Umar-Allah awawiye
radhi–aliadhini kwa ajili ya swala katika
usiku wenye baridi na upepo mkali, kisha
akasema: ALAA SWALUU FIR-RIHAAL Maana
yake:“Ehee swalini majumbani mwenu”. Kisha
akasema: Hakika Mtume wa Allah–Rehema na Amani
zimshukie–alikuwa akimuamuru muadhini, uwapo
usiku wenye baridi na mvua kusema: ALAA SWALLUU
FIR-RIHAAL. Bukhaariy & Muslim Leo kutokana
na maendeleo ya miji si rahisi kupatikana
nyudhuru hizi mijini ambamo nyumba zimeungana,
barabara zina lami na mataa yanawaka pia watu
wana makoti ya mvua na miavuli. Kwa hivyo utaona
kama kwamba nyudhuru hizi hazina nafasi mijini
na badala yake zinaweza kutumika zaidi vijijini.
b)
NYUDHURU BINAFSI:
Hizi ni pamoja na maradhi, njaa au kiu
kikali, khofu ya dhalimu kwa nafsi au mali,
kubanwa na haja kubwa au ndogo, kuwekwa
(kutengwa) chakula na mtu akawa na njaa au
anakitamani chakula hicho na kula kitu chenye
kunuka (harufu kali) mithili ya kitunguu thaumu.
Amesema Mtume wa Allah–Rehema na Amani
zimshukie: “Kitapowekwa chakula cha usiku
(Ashaa) cha mmoja wenu na ikakimiwa swala, basi
anzeni na kile chakula na mtu asifanye haraka
mpaka amalize kula (ndio aswali)”. Bukhaariy
& Muslim
“Hapana
swala mbele ya chakula, wala (wakati) yeye
kabanwa na machafu mawili (haja kubwa na
ndogo)”. Muslim
“Atakayekula
kitunguu thaumu, basi na ajitenge nasi”. Au
alisema: “…Na ajitenge na msikiti wetu, na
akae (aswali) nyumbani kwake”. Bukhaariy &
Muslim
Kila
moja miongoni mwa hali hizi tulizozitaja hapa
zinazingatiwa kuwa ni udhuru wa kisheria
unaoweza kumfanya mtu asihudhurie swala ya
jamaa. Nyudhuru hizi zote kama zinaashiria
jambo, basi jambo hilo halitakuwa ila ni wema na
wepesi wa dini hii ya maumbile: “…ALLAH
ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI WALA HAKUTAKIENI
YALIYO MAZITO…”
(2:185)
ix)
SHARTI ZA IMAMU.
Swala ya jamaa huwakusanya pamoja Imamu
mmoja na maamuma mmoja au zaidi ya mmoja.
Imamu ndio kiongozi katika ibada hii ya
swala na maamuma wote walioko nyuma yake
wanalazimishwa kumfuata.
Kwa hivyo basi Imamu anachukua dhima kuu
mbele ya waja na mbele ya Allah, kutokana na
uzito wa dhima hii, imeshurutizwa Imamu awe na
sifa zifuatazo:-
- Mwanamume:
Hausihi uimamu wa mwanamke kuwaswalisha
wanamume ila kwa wanawake wenzake.
- Muadilifu:
Hafai kuwa Imamu mtu fasiki wenye kujulikana
ufasiki wake ila atapokuwa sultani
(kiongozi) mwenye kuchelewa shari yake.
- Mjuzi:
Awe na elimu ihusianayo na swala, tangu
twahara na swala yenyewe pamoja na vipengele
vyake vyote.
Haisihi kuwa Imamu mjinga asiye na
elimu ila kwa watu mfano wake (wajinga
wenziwe).
- Mkubwa:
Imamu asiwe mwana mdogo ambaye hajafikia
baleghe, kwa sababu yeye si katika watu
wenye taklifu.
- Akili:
Mwendawazimu hafai kuwa Imamu, kwa sababu
siyo mukalafu kisheria.
MWENYE
HAKI YA KUWA IMAMU.
Mwenye haki ya kuwa Imamu miongoni mwa
watu ni:-
- Msomi
wao zaidi wa kitabu cha Allah, yaani
aliyehifadhi Qur-ani na kuisoma vizuri
itakiwavyo kwa mujibu alivyofundisha Mtume
wa Allah.
- Kisha
mwenye kuijua vema dini ya Allah, yaani
anajua sheria khususan hukumu za swala na
mambo yote yenye kufungamana nayo.
- Kisha
mwenye wingi wa taq-wa, yaani matendo yake
ya dhahiri yanaonyesha kuwa ni mcha–Mungu.
- Kisha
mwenye umri mkubwa kuliko wote.
Huu
ndio utaratibu kama alivyoupanga mwenyewe Bwana
Mtume– Rehema na Amani
zimshukie–katika kauli yake:
“Awaswalishe watu (awe Imamu wao) msomi wao
wote wa kitabu cha Allah, wakilingana sawa
katika huo usomaji (wa kitabu cha Allah) basi
(awe imamu) mjuzi wao wa suna (ya Mtume).
Wakilingana sawa katika kuijua suna, basi (awe
imamu) mtangulizi wao kwa Hijrah. Na wakilingana
sawa katika Hijra basi (awe imamu) mkubwa wao
kwa umri”. Muslim
TANBIHI:
Akiwepo kiongozi, basi yeye ndiye mwenye haki
zaidi ya kutawalia uimamu katika mamlaka yake.
Haimfalii mtu mwingine ye yote kumtangulia ila
kwa idhini yake. Kadhalika atapokuwepo Imamu
aliyechaguliwa na watu wa sehemu husika na
kupewa jukumu na watu wa sehemu hiyo na kupewa
jukumu hilo la uimamu. Haisihi mtu mwingine
kumtangulia imamu huyu ila kwa idhini yake.
Pia haifai mtu mwingine kumtangulia
mwenye nyumba nyumbani kwake ila kwa idhini
yake. Haya ndiyo mafunzo yatokanayo na kauli ya
Mtume wa Allah– Rehema na Amani zimshukie:
“Mtu asiwe asiwe imamu wa mtu kwa watu wake
(nyumbani kwake) wala katika mamlaka yake ila
kwa idhini yake”.
MAS–ALA.
Ni vema mtu kuyajua mas-ala haya katika
suala zima la uimamu:-
- UIMAMU
WA MWANAMKE:
Inasihi mwanamke kuwa Imamu akawaswalisha
wanawake wenzake. Kiutaratibu yeye hasimami
mbele yao kama asimamavyo Imamu mwanamume, bali
yeye atasimama katikati yao katika safu.
Hili linatokana na idhini ya Mtume wa
Allah Rehema na Amani zimshukie– aliyompa Ummu
Waraqah Bint Naufal.
Idhini ya kujiwekea muadhini wake
nyumbani mwake, aadhini kisha yeye (Ummu
Waraqah) apate kuwaswalisha watu wake wa
nyumbani. Haya
ni kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa na Imamu
Abuu Daawoud.
- UIMAMU
WA KIPOFU:
Inasihi kipofu kuwa imamu kwa sababu
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alimpa Ibn
Ummu Maktuum ukhalifa wa Madinah mara mbili.
Nae–Allah amuwiye radhi–akawa anawaswalisha
watu na
ilhali yeye ni kipofu. Hivi ndivyo
inavyoeleza riwaya ya Abuu Daawoud.
- UIMAMU
WA ALIYE CHINI KATIKA DARAJA YA UIMAMU:
Inasihi
kuwa imamu mtu aliye chini katika daraja ya
uimamu pamoja na kuwepo aliye bora kuliko yeye.
Hili linatokana na kitendo cha Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie–kuswali nyuma
ya Sayyidna Abuu Bakri na nyuma ya Abdur-rahmaan
Ibn Auf na il-hali yeye Bwana Mtume ni bora
kuliko wao bali kuliko viumbe wote.
Hivyo ndivyo ilivyokuja katika riwaya ya
Imamu Bukhaariy.
- UIMAMU
WA MTU ALIYETAYAMAMU:
Inasihi mtu aliyetayamamu kumswalisha mtu
aliyetawadha. Hii ni kwa sababu Amrou Ibn Al-Aaswi alikiswalisha kipote
(kikundi) cha vita (sariyah) nae akiwa
ametayamamu na maamuma wake wakiwa wametawadha.
Khabari hii ikamfikia Bwana Mtume nae
hakukanusha wala kulikemea hilo na hivyo
kufahamika kuwa amelikiri.
Hivi ndivyo ilivyo katika riwaya ya Abuu
Daawoud.
- UIMAMU
WA MSAFIRI:
Inasihi msafiri kuwa imamu wa mkazi
(asiye msafiri) isipokuwa itamlazimu huyu mkazi
kuitimiza swala yake baada ya imamu wake msafiri
kutoa salamu.
Hili linatokana na kitendo cha Mtume wa
Allah– Rehema na Amani
zimshukie–kuwaswalisha watu wa Makah nae akiwa
msafiri, na akawaambia: “Enyi watu wa Makah,
timizeni swala zenu kwani sisi ni wasafiri”.
Imam Maalik
Na
kama msafiri ataswali nyuma ya mkazi, atatimiza
pamoja nae.
Aliulizwa Ibn Abasi–Allah awawiye
radhi–kuhusiana na suala la kutimiza msafiri
nyuma ya mkazi, akasema: “Hiyo ni sunah ya
Abul-Qaasim (Mtume)”.
Ahmad
|