Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

X/. SHARTI ZA KUSIHI KUFUATA (SHARTI ZA MAAMUMA)

 

Maamuma anayeswali nyuma ya imamu kumeshurutizwa sharti kadhaa ili kumfuata kwake imamu kusihi. Miongoni mwa sharti muhimu ni kama zifuatavyo:-

1)     Mfuataji (maamuma) asijue kubatilika kwa swala ya imamu wake au kuitakidi hivyo.

Mfano: Watu wawili wamefanya jitihadi katika kujua upande kilipo Qiblah. Kila mmoja wa wawili hawa akaitakidi kwamba Qiblah kiko upande ule auonao yeye na wala hakiko upande auonao mwenzake. Katika hali kama hii hakujuzu kwa mmojawapo wa wawili hawa waliokhitalifiana katika upande kilioko Qiblah, jambo ambalo ni mojawapo ya nguzo za swala. Hakumjuzii kumfuata mwenzake  akamfanya kuwa ndio imamu wake na yeye akawa maamuma nyuma yake. Kutokujuzu huku kunatokana na ile itikadi ya kila mmoja wa wawili hawa kwamba mwenzake amekosea welekea/upande wa Qiblah. Sasa basi, maadam amekosea Qiblah basi na swala yake anayoiswali kuelekea upande huo itakuwa sio sahihi, ni batili tu na si vinginevyo kwa itikadi yake hiyo.

2)    Imamu asiwe umiyi (asiyejua kusoma wala kuandika) na ilhali maamuma ni msomi:

Muradi wa makusudio ya “umiyi”, hapa ni mtu asiyeweza kuisoma vizuri Suratil-faatihah (Al-hamdu) kwa hukumu zake za usomaji kama zilivyotajwa katika vitabu vya fani ya “Tajweed”. Angalia ikiwa imamu na maamuma wote ni maumiyi, basi kutamjuzia kila mmoja wao kumfuata mwenzake.

3)    Imamu asiwe mwanamke na maamuma akawa ni mwanamume:

Mwanamke hana mamlaka kisheria kumtangulia mwanamume katika swala, akawa ndio imamu  wa mwanamume. Hili ndilo agizo la Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika kauli yake: “Mwanamke asimswalishe mwanamume”. Ibn Maajah-Allah amrehemu.

 

XI/. NAMNA YA KUFUATA:

 

Kufuata kulikoelezwa na sheria hakutathibiti ila kwa sharti na namna ambazo inatakikana kwa mwenye kufuata (maamuma) kuzichunga. Sharti hizi ni nyingi, tunazifupiliza kama ifuatavyo:-

1)     Maamuma asimtangulie imamu wake katika mahala pa kusimama (masimamo):

Ili ufuataji usihi ni sharti maamuma asimtangulie imamu wake katika masimamo. Akimtangulia, ufuataji wake umebatilika kwa mujibu wa kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Kwa yakini imamu amewekwa ili afuatwe” – (na sio kutanguliwa). Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Ni dhahiri kuwa kufuata hakupatikani ila atakapokuwa mfuataji (maamuma) yu nyuma ya afuatwaye (imamu). Lakini haidhuru maamuma kulingana sawa na imamu wake katika masimamo, ijapokuwa ni karaha kufanya hivyo kwani suna ilivyo ni kuwa nyuma yake kidogo. Maamuma akimtangulia imamu wake, akawa yeye ndio yuko mbele na imamu nyuma, hapo swala yake itabatilika tu na si vinginevyo. Na mazingatio katika suala la  kutangulia au kuakhirika ni kisigino. Hiki ndicho kinachoangaliwa, kisigino cha maamuma kikiwa mbele ya kisigino cha imamu, maamuma huyo atazingatiwa kuwa kamtangulia imamu wake. Na kikiwa nyuma, huyo anazingatiwa kumfuata imamu wake.

 

Namna ya kusimama nyuma ya imamu:

 

Maamuma wakiwa ni wawili na kuendelea , watapiga safu nyuma ya imamu wao. Maamuma akiwa ni mmoja, ni yeye tu na imamu wake, anatakiwa kusimama kuliani kwa imamu nyuma kidogo. Akiongezeka mtu wa pili, huyu atasimama kushotoni kwa imamu, kisha maamuma wawili hawa watarejea nyuma walingane sawa. Au imamu wao atasogea mbele kidogo ili kuwapa wao nafasi ya kulingana sawa. Imepokelewa kutoka kwa Jaabir-Allah amuwiye radhi-amesema: “Niliswali nyuma ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-nikasimama kuliani kwake. Halafu akaja Jaabir Ibn Swakhri akasimama kushotoni kwake (Mtume). (Bwana Mtume) akatushika mikono sote na kutusimamisha nyuma yake”. Muslim-Allah amrehemu.

Kumesuniwa kutokuzidi umbali ulio baina ya imamu na maamuma wake zaidi ya dhiraa tatu na hivi ndivyo itakiwavyokuwa baina ya kila safu mbili. Angalia maamuma wakiwa ni mchanganyiko unao wachanganya pamoja wanamume na wanawake. Katika hali hii maamuma wanamume watasimama nyuma ya imamu na wanawake watakuwa nyuma ya wanamume. Haya ni katika jumla ya mafundisho ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kama yalivyo katika kauli zake zifuatazo:-

v     “Bora ya safu za wanamume ni ile ya kwanza yao na shari (mbaya) yake ni ile ya mwisho yao (hizo safu za wanamume). Na bora ya safu za wanawake ni ile ya mwisho yao na shari yake ni ile ya mwanzo yao (inayoifuatia ile ya mwisho ya wanamume)”. Muslim-Allah amrehemu.

v     Anas-Allah amuwiye radhi-amesema kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimswalisha yeye na mama yake. Akanisimamisha mimi kuliani kwake na akamsimamisha  mwanamke (mama yangu) nyuma yetu”. Muslim-Allah amrehemu.

 

TANBIHI:

Ama jamaa ya wanawake, yaani jamaa inayowahusisha wanawake watupu tu peke yao bila ya kuwemo miongoni mwao mwanamume. Imamu wao; mwanamke mwenziwao atasimama katikati yao, kama lilivyothibiti hili kutoka kwa bibi Aysha na bibi Ummu Salamah-Allah awawiye radhi.

Ni karaha maamuma kusimama peke yake katika safu, yaani kuanza safu peke yake bila ya kuwa na mwenzake. Imepokelewa na Waabiswah kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimuona mtu akiswali nyuma ya safu peke yake, akamwambia: “Ewe mswali pweke, kwani usiunge safu (ya mbele yako) ukaingia katikati yao au ukamvutia kwako mtu mmoja ikiwa mahala pamekudhikikia akasimama pamoja nawe! Wewe huna swala (swali tena)”. Twabaraaniy-Allah amrehemu.

Kwa hivyo basi utaona kuwa ni suna kwa huyu aliye pweke kumvuta mtu mmoja kutoka katika safu iliyo mbele yake baada ya kuhirimia ili aje kusimama pamoja nae. Kadhalika ni suna kwa huyu mwenye kuvutwa kumsaidia ndugu yake kwa kurejea nyuma kusimama naye ili apate fadhila za kusaidiana katika wema: “...NA SAIDIANENI KATIKA WEMA NA TAQWA...” [5:2]

 

2)    Maamuma amfuate imamu wake katika vihamohamo (maguroguro) vyake na katika baki ya nguzo vitendo nyingine.

Maamuma kumfuata imamu maana yake ni kuchelewa kuanza kwa kitendo chake, yaani kitendo chake kitanguliwe na kile cha imamu wake. Hivi ndivyo alivyotufundisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kupitia kauli yake: “Kwa yakini imamu amewekwa ili afuatwe, akikabiri (akileta takbir) basi nanyi (ndipo) mkabiri na wala msikabiri mpaka (kwanza) akabiri yeye. Na akirukuu nanyi rukuuni na wala msirukuu mpaka arukuu yeye. Na ataposujudu nanyi sujuduni na wala msisujudu mpaka asujudu yeye”. Ahmad & Abuu Daawoud-Allah awarehemu.

Na kauli yake hii: “Enyi watu! Mimi ndio imamu wenu, basi msinitangulie kwa kurukuu, wala kwa kusujudu wala kwa kusimama, wala kwa kukaa na wala kwa kutoa salamu”. Ahmad & Muslim-Allah awarehemu.

Angalia na uzingatie kwamba kumtangulia imamu ni jambo lililokemewa vikali sana na Mtume wako, hata akafikia kusema: “Ehee hachelei mmoja wenu anaponyanyua kichwa chake kabla ya imamu, Allah kukigeuza kichwa chake kuwa kichwa cha punda. Au Allah kuigeuza sura yake sura ya punda”. Bukhaariy & Muslim-Allah amrehemu.

Lakini maamuma akiwa nyuma ya imamu wake kwa nguzo moja, hilo litakuwa ni karaha. Na iwapo atachelewa nyuma ya imamu wake kiasi cha nguzo mbili ndefu, sura ya hili ni kama vile imamu kurukuu, kuitadili, kisha akasujudu na kuinuka kutoka sijida ya kwanza. Akayafanya yote haya na ilhali maamuma ameendelea kusimama bila ya udhuru wo wote, swala yake itabatilika. Ama ikiwa kuchelewa kwake huko ni kwa sababu ya udhuru mithili ya uzito katika kusoma Al-hamdu. Basi kunamuelea kuwa nyuma ya imamu wake kwa nguzo tatu. Iwapo nguzo tatu hizi hazitoshi kumpa nafasi ya kukamilisha  kisomo chake cha Al-hamdu na kisha kumfuata imamu wake. Hapa sasa kutamuwajibikia kukata hapo alipofikia na amfuate imamu wake, kisha atadiriki kilichobakia baada ya imamu wake kutoa salamu.

 


 

 


Forum | Guestbook | Tuandikie |