|
3.
Maamuma kujua vihamohamo/maguroguro ya Imamu
wake:
Maamuma
ni sharti avijue vihamohamo vya Imamu wake, ama
kwa kumuona yeye mwenyewe akitoka qiyamu kwenda
rukuu, kutoka rukuu kuja itidali na kutoka hapo
kuporomokea sijida na kadhalika. Au kwa kuiona
safu ya mbele yake au kwa kumsikia
mbalighishaji.
4.
Kisiwepo baina ya Imamu na maamuma kitenganishi
eneo kikubwa:
Ikiwa
jamaa inaswaliwa nje; mawandani mahala ambapo si
ndani ya jengo la msikiti. Kumeshurutizwa
kisiwepo baina ya Imamu na maamuma wake
kitenganishi eneo kikubwa. Ama wakiwa ndani ya
msikiti, ufuataji utakuwa ni sahihi vyo vyote
yatakavyombalika masafa baina yao au kuingia
kati majengo yenye kupitika. Yaani mtu anaweza
kutoka jengo moja hadi jingine. Ama Imamu na
maamuma wote wawili wakiwa nje ya msikiti, au
imamu akawa msikitini na maamuma nje yake.
Katika hali na mazingira kama haya
kumeshurutizwa kutombalika masafa baina ya imamu
na maamuma wake.
5.
Maamuma anuie jamaa au kumfuata imamu:
Ni
sharti nia ya jamaa au kumfuata imamu
ikutanishwe pamoja na Takbira ya kuhirimia
swala. Angalia iwapo maamuma ataacha kuleta nia
ya kufuata na kisha akamfuata imamu katika
vihamohamo na matendo, swala yake maamuma huyo
itabatilika ikiwa alikusudia kumfuata. Kwani
ilivyo ndivyo ni amgonjee mgonjeo mwingi kwa
ada, kwa sura ambayo mtazamaji ataona kuwa hizo
ni swala mbili tofauti; haziko katika mtungo
mmoja. Ama kukisadifu kufuatana bila ya
kukusudia au kumngojea kwake imamu kukawa ni
kuchache, swala yake haitabatilika kwa matendo
yake haya.
Kwa
upande wa maamuma, si wajibu kwake kunuia
“uimamu”, bali yapendekeza tu kufanya hivyo
ili aweze kuzihodhi fadhila za jamaa. Kwani kama
hakunuia hatazipata fadhila hizo za jamaa, hili
linatokana na ukweli kwamba mtu hapati ujira ila
wa alilolinuilia. Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-anasema: “Hakika si vinginevyo,
matendo yote yamefungamana na nia, na kwa yakini
kila mtu atapata alilolinuilia...”. Bukhaariy
& Muslim-Allah awarehemu.
Elewa
kuwa maamuma atapata fadhila za jamaa maadam
imamu hajatoa salamu. Na maamuma kuidiriki
takbiratul-ihraam pamoja na imamu wake, kuna
fadhila za pekee kabisa. Fadhila hizi hupatikana
kwa maamuma kujishughulisha kuleta
takbiratul-ihraam mara tu baada ya kuhirimia
imamu wake. Na fahamu kuwa rakaa itamthibitikia
maamuma pale tu atakapomdiriki imamu wake katika
rukuu, nae akarukuu pamoja nae kabla imamu
hajainuka kutoka rukuu (Qiyaamu). Hivi ndivyo
inavyoelezwa na kauli ya Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie: “Mtapoijia swala na
ilhali sisi tumesujudu, basi nanyi sujuduni na
wala msiihesabu hiyo (sijida) kuwa ni sehemu (ya
swala yenu). Na atakayediriki rukuu, hakika
ameidiriki rakaa”. Abuu Daawoud-Allah
amrehemu.
BAADHI
YA MAS-ALA YANAYOFUNGAMANA NA SWALA YA JAMAA:
1.
Kunyoosha safu na kuziba mianya:
Kumesuniwa
kwa Imamu kuwaamrisha maamuma wake kunyoosha
safu zao na kuziba mianya baina yao, hili
lifanyike baada ya Iqaamah na kabla ya kuhirimia
swala. Imepokelewa kutoka kwa Anas-Allah amuwiye
radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alikuwa akituelekea kwa uso wake kabla
hajakabiri (Takbiratul-Ihraam), akituambia: “Kamataneni
barabara na mlingane sawa, na zisawazisheni safu
zenu kwani kusawazika kwa safu ni katika jumla
ya utimilifu wa swala”. Bukhaariy &
Muslim-Allah awarehemu.
2.
Imamu kufanya takhfifu:
Kumesuniwa
imamu awakhafifishie swala maamuma wake,
asitwawilishe (asirefushe) swala kiasi cha
maamuma kuona dhiki mioyoni mwao. Hivi ndivyo
anavyotuagiza Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-katika hadithi iliyopokelewa na Abuu
Hurayrah-Allah amuwiye radhi: “Atapowaswalisha
mmoja wenu watu basi na akhafifishe (asifanye
swala kuwa ndefu kupita kiasi), kwani miongoni
mwao (hao maamuma) kuna walio dhaifu, wagonjwa
na watu wazima. Na mtu akiswali peke yake na
atwawilishe atakavyo (awezavyo)”.
Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
3.
Imamu
atwawilishe rakaa ya kwanza na amsubiri
anayemuhisi kutaka kuunga jamaa ili aweze
kuidiriki jamaa:
Imamu
ameruhusiwa na sheria kutwawilisha rakaa ya
kwanza kwa ajili ya kumngojea mwenye kutaka
kuunga jamaa ili kumpa fursa ya kudiriki fadhila
za jamaa. Kama ambavyo kumesuniwa kwa imamu
kumngojea mtu aliyemuhisi kuingia naye akiwa
katika rukuu au katika kikao cha mwisho.
Imepokelewa hadithi kutoka kwa Abuu
Qataadah-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa
akitwawilisha rakaa ya kwanza. (Akasema Abuu
Qataadah): Tukadhania kwamba yeye amewakusudia
kwa hilo watu waidiriki rakaa ya kwanza. Na
imepokewa na Abuu Said-Allah amuwiye
radhi-amesema: Swala ilikuwa ikikimiwa, mtu
akaenda ‘Baqiy’ akakidhi haja yake,
akatawadha kisha akaja na ilhali Mtume wa Allah
akiwa (bado) katika rakaa ya kwanza kutokana na
jinsi anavyoitwawilisha. Ahmad, Muslim, Ibn
Maajah & Nasaai-Allah awarehemu.
4.
Mtanguliwa (masbuuq) kujiunga na imamu:
Mtu
atapoingia msikitini na kukuta swala imesimama
tayari, kutamuwajibikia kujiunga upesi na imamu
katika hali yo yote aliyomkuta. Ni mamoja
akimkuta katika rukuu, sijida, kitako au qiyamu
(kisimamo). Hivi ndivyo inavyoeleweka kutokana
na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie: “Mmoja wenu atapoijia swala na
imamu akiwa katika hali fulani, basi na afanye
kama afanyavyo Imamu”. Tirmidhiy-Allah
amrehemu.
5.
Hakujuzu (hakuruhusiwi) swala ya suna
itakapokimiwa swala ya faradhi:
Si
rukhsa mtu kuswali swala ya suna ikimiwapo swala
ya faradhi. Angalia swala hiyo ya faradhi
ikikimiwa na tayari mtu yumo ndani ya swala ya
suna, ataikata swala hiyo ya suna na kwenda
kujiunga na swala ile ya faradhi. Ukataji huu ni
iwapo haijafungamana rakaa kwa kuinuka kutoka
rukuu na iwapo imeshafungamana ataitimiza katika
hali ya ukhafifu. Yote haya yamekusanywa na
kauli ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Itapokimiwa
swala, basi hapana (rukhsa ya kuswali) swala (ya
suna) ila ile ya fardhi tu”. Muslim-Allah
amrehemu.
Mpenzi
msomaji wetu, ni vema ukafahamu kwamba swala ya
jamaa ina vipengele chungu nzima ambavyo
kunakupasa kuvijua. Hivi tulivyovigusia kwa
mukhtasari ni vichache tu miongoni mwa hivyo
kathiri (vingi). Kwa kulizingatia hili, Website
yako; WEBSITE UISLAMU inakushauri kujiunga na
masomo ya dini katika eneo unaloishi. Ili uweze
kuipata kokwa ya elimu na khasa kwa kujifunza
lugha ya Qur-ani Tukufu (Kiarabu). Endelea kuwa
nasi na zidi kutuombea taufiq kwa Allah ili
tuzidi kukutumikia.
|