|
I/.
UBORA WA SIKU YA IJUMAA:
Siku
ya Ijumaa ni siku bora na tukufu miongoni mwa
siku za dunia, Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-ameitaja siku ya Ijumaa kama hivi:
“Bora ya siku uliyochomozewa na jua ni siku ya
Ijumaa, ndani yake ameumbwa Adamu-Amani
imshukie-na ndani yake ametiwa peponi. Na ni
ndani yake (siku hiyo) alitolewa humo (peponi)
na wala hakitasimama kiyama ila ndani ya siku ya
Ijumaa”.
Muslim-Allah amrehemu.
Kwa
hivyo basi, kunamuwajibikia muislamu kuitukuza,
kuienzi na kuiheshimu siku ya Ijumaa kwa
kukithirisha kutenda amali njema na kujiepusha
na madhambi. Katika hadithi nyingine Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema:
“Bwana wa siku mbele ya Allah ni siku ya
Ijumaa (ni bora) kuliko siku ya kuchinja
(Eidil-adh-ha) na siku ya Fitri”.
Shaafiy & Ahmad-Allah awarehemu.
Zimepokelewa
hadithi nyingi kutoka kwa Bwana Mtume zikitaja
fadhila na ubora wa siku hii ya Ijumaa. Hii ni
siku ambayo umo ndani yake wakati (muda fulani)
ambao mja hamuombi Mola wake ndani yake cho
chote cha kheri ila humpa. Ni kwa ajili ya
fadhila hizi tulizozitaja na nyinginezo, Allah
akaichagua siku hii kuwa ni Idi (sikukuu) ya
kila juma (wiki) ya waislamu. Akawaamrisha waja
wake kuipa umuhimu wa pekee siku hii, wajipambe
kama walivyoelekezwa na kufundishwa na Mtume
wao. Waache shughuli zao na waharakie kuiendea
ibada ya swala ya Ijumaa. Wakutanike pamoja
ndani ya siku hii ili iwe ni nembo, alama na
kielelezo cha umoja wao na dalili na ishara ya
nguvu yao. Siku hii ni zawadi kwa umati Muhammad
kwani ni sababu ya kufutiwa dhambi zao na ni
kirudufisho cha ujira na thawabu.
Lakini
kwa masikitiko makubwa, uzoefu unaonyesha kuwa
waislamu wamekuwa ni watu wa kuzembea na kupuuza
kila kitu. Hata kufikia kiasi cha kudharau
matukufu ya dini yao yaliyotukuzwa na Mola
Muumba wao, huu ni msiba mkuu na haya ni
maangamivu. Leo siku ya Ijumaa machoni na
mioyoni mwa waislamu wengi si cho chote na wala
si lo lote ila ni siku tu kama zilivyo baki ya
siku nyingine za juma. Hili halihitaji ushahidi
kwani linashuhudiwa bayana na kila mmoja wetu.
Waislamu tumeipuuza siku yetu tukufu ya Ijumaa,
siku iliyokuwa na nafasi,cheo, daraja na
iliyopewa umuhimu wa pekee na mababu zetu
(wahenga). Wazee wetu hao wema waliutambua
umuhimu, utukufu na ubora wa siku ya Ijumaa,
hivyo wakawa wakiingojea kwa hamu na shauku kuu.
Waliingojea kama mtu mwenye kiu ayangojeavyo
maji baridi au mithili ya mgonjwa aingojeavyo
siku ya kupona na kupoa kwake. Wakawa wanakoga,
wananadhifisha nguo zao, wakajitia manukato na
wakienda mapema msikitini kuhudhuria swala ya
Ijumaa. Wakienda msikitini ilhali wamefunikwa na
staha, heshima, utulivu na unyenyekevu. Nyoyo
zao zikiwa zimesheheni khofu ya Allah Bwana
Mlezi wao na ndimi zao zikiwa majimaji kwa utajo
(dhikri) wa Mola wao. Macho yao yakiwa
yamesitiriwa na maharamisho ya Allah, hata
wakiingia msikitini kila mmoja wao akiwania
kuchukua nafasi iliyo karibu na khatibu; nafasi
ya mbele. Walifanya hivi kutokana na kupupia
kwao kuhodhi fadhila za safu ya kwanza na
kustafidi na khutba. Khatibu anapopanda juu ya
mimbari na kuanza kukhutubu, huwa makini, nyoyo
zao zikizingatia, usikivu (masikio) wao huwa
wazi. Khatibu hamalizi khutba yake ila huwaliza
wote; janibu ya twaa na janibu ya maasi. Janibu
ya maasi hulia kutokana na kuichelea adhabu na
ghadhabu ya Allah. Wakati ile janibu ya twaa
ikilia kutokana na tamaa ya fadhila na thawabu
za Allah.
Enyi
ndugu waislamu, tuchungeni adabu za siku hii
tukufu, tujinadhifisheni, tujipambeni na
tujitieni manukato kwa ajili ya siku hii adhimu.
Tutokeni majumbani mwetu kwa unyenyekevu
kuelekea kwenye nyumba za Allah. Twendeni mapema
na tukiingia msikitini kila mmoja wetu akae kwa
adabu, heshima, staha na utulivu. Tutahadharini
na kufanya kitendo au kusema kauli itakayomuudhi
Allah, Mtume wake na waja wake mithili ya
kukata/kukengeuka shingo za watu. Tueleweni
kwamba kuwaudhi waislamu ni jambo linalopomosha
ujira na kubatilisha thawabu adhimu za Ijumaa.
Atakayeingia msikitini miongoni mwetu na ilhali
khatibu anakhutubu, basi na asikae chini ila
baada ya kuswali rakaa mbili khafifu (nyepesi).
Tunapomaliza kuitekeleza fardhi hii ya swala ya
Ijumaa, tusiwe na haraka ya kutoka msikitini.
Tukae tuswali suna, tulete dua na tumuombe Mola
wetu maghfira, radhi na uongofu. Mola wetu
Mtukufu tunamuomba airejeshe haiba na utukufu wa
siku ya Ijumaa katika nafsi, nyoyo, roho na
miili yetu-Aamiyn.
II/.
KUSHARIIWA (KUWEKWA SHERIA) SWALA YA IJUMAA:
Swala
ya Ijumaa imeshariiwa nayo ni miongoni mwa
fadhila alizoukhusu nazo Allah umati huu.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah
amuwiye radhi-kwamba yeye alimsikia Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Sisi
ndio wa mwisho (kuletwa duniani), wa
mwanzo (kuingia peponi) siku ya kiyama isipokuwa
wao walipewa kitabu (sheria) kabla yetu. Kisha
hii (Ijumaa) ni siku yao ambayo walifaradhiwa
wakakhitalifiana katika siku hiyo. Allah
akatuongoza sisi, basi watu wanatufuata katika
siku hii; Mayahudi kesho (Jumamosi) na Manaswara
kesho kutwa (Jumapili)”.
Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
Swala
ya Ijumaa ilifaradhishwa katika kipindi cha
utume cha Makah, punde kidogo kabla ya Hijrah.
Lakini haikumkinika kuswaliwa kutokana na
udhaifu waliokuwa nao waislamu wakati huo na
kupelekea kushindwa kukusanyika pamoja kwa ajili
ya swala hii. Mtu wa mwanzo aliyewakusanya watu
na kuwaswalisha swala hii ya Ijumaa Madinah
kabla ya Hijrah ya Bwana Mtume, alikuwa ni
As’ad Ibn Zaraarah-Allah amuwiye radhi. Hivi
ndivyo ilivyopokelewa katika riwaya ya Ka’ab
Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-kama alivyopokea
Imamu Abuu Daawoud na wengineo.
III/.
HUKUMU YA SWALA YA IJUMAA NA DALILI YA
UFARADHIFU WAKE:
Wanazuoni
wamekongamana kwamba swala ya Ijumaa ni
FARDHI AYN (faradhi binafsi), HURU ambayo
si badali ya swala ya Adhuhuri. Ila tu pale
inapofutu, basi kunamuwajibikia muislamu kuswali
Adhuhuri rakaa nne. Ufaradhifu na uwajibu wa
swala ya Ijumaa kwa muislamu unatokana na kauli
hii ya Allah: “ENYI MLIOAMINI!
KUKIADHINIWA KWA AJILI YA SWALA SIKU YA IJUMAA,
NENDENI UPESI KUMTAJA ALLAH
NA ACHENI BIASHARA. KUFANYA HIVI NI BORA
KWENU, IKIWA MNAJUA (hivi basi fanyeni)”.
[62:9]
Muradi
wa “KUMTAJA ALLAH” hapa katika aya hii kama
walivyoeleza wanazuoni ni SWALA YA IJUMAA na
KHUTBA yake. Hii ni kwa sababu ndani ya swala na
khutbah hutajwa jina la Allah. Na mapendeleo ya
ibara “ACHENI BIASHARA” ni zile shughuli
zota anazozifanya mwanadamu katika kujipatia
riziki yake ya kila siku. Iwe ni biashara,
kilimo, ajira, uvuvi
na nyinginezo.
Kwa
upande wa hadithi, zipo hadithi nyingi
zilizopokewa katika kutaja uwajibu wa swala hii
ya Ijumaa. Miongoni mwa hadithi hizo ni hizi
zifuatazo:-
v
Twaariq
Ibn Shihaab-Allah amuwiye radhi-amepokea kutoka
kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“Ijumaa ni haki ya wajibu juu ya kila
muislamu...”
Abuu Daawoud-Allah amuwiye radhi.
v
Imepokelwa
kutoka kwa Abuu Hurayrah na Ibn Umar-Allah
awawiye radhi-kwamba wao walimsikia Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema juu ya
mimbari yake: “ Wakome wakome watu
kuacha kwao (swala za) Ijumaa au Allah azipige
mihuri nyoyo zao kisha watakuwa miongoni mwa
walioghafilika”.
Muslim & wengineo-Allah awarehemu.
|