Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

IV/. FALSAFA (HEKIMA) YA SWALA YA IJUMAA:

Faida

Katika kushariiwa swala ya Ijumaa kuna hekima na faida kathiri (nyingi). Katika jumla ya faida hizo ni kule kukutana waislamu katika ngazi ya mji, kitongoji au kijiji mahala pamoja. Ambapo ni ndani ya msikiti wa Ijumaa, mara moja kila juma, mara nne kila mwezi na mara khamsini takriban kila mwaka. Hii ni fursa muhimu na ya pekee ambayo huwaunganisha waislamu na kuzidisha nguvu yao kama ambavyo huwazidishia kuzoeana, kufahamiana na kusaidiana. Ijumaa ni idhaa ya waislamu yenye dhima kuu ya kuwapasha waislamu matukio ya kila juma yanayojiri katika ulimwengu wao. Idhaa hii huwanganisha waislamu na matukio haya na kuwaonyesha nafasi yao kama waislamu nyuma ya matukio hayo. Ni kwa kiasi gani matukio hayo yanawadhuru au kuwanufaisha waislamu na wao kama waislamu wafanye nini kuyaboresha manufaa au kuyaondosha madhara yatokanayo na matukio hayo. Ijumaa ni chuo cha nidhamu kinachowafundisha waislamu kuwa ni lazima wawe nyuma ya kiongozi wao mmoja, wakimtii na kumsikiliza katika maamrishi na makatazo, ikiwa wanataka kufaulu kama walivyofaulu maswahaba nyuma ya kiongozi wa uma; Bwana Mtume. Ijumaa ni chuo cha usawa kinachoondosha tofauti za rangi, lugha, hadhi na hali za kimaisha baina ya waislamu. Katika swala ya Ijumaa utamuona tajiri bilionea amekaa pembeni ya masikini hohehahe, kiongozi yuko bega kwa bega na raia wake duni, mkubwa amekaa sambamba na mdogo na hata mweupe na mweusi pia hukaa pamoja. Hakuna nafasi maalum kwa tabaka la watu fulani, bali kila muislamu ana haki ya kukaa po pote na hakuna mwenye haki ya kumuondoa. Ila aamue yeye mwenyewe kwa khiari yake kusogea au kumpisha nduguye muislamu, hili ni suala binafsi la matashi ya mtu. Hii ni sehemu ya falsafa kuu ya swala hii ya siku ya Ijumaa.

 

V/. SHARTI ZA KUWAJIBISHA SWALA YA IJUMAA (WANAOWAJIBIKIWA NA IJUMAA):

Swala ya Ijumaa kwa mujibu wa sheria ni wajibu kwa mtu ambaye zimepatikana kwake sharti saba zifuatazo:-

  1. Uislamu: Swala ya Ijumaa ni wajibu kwa muislamu tu na wala haimuwajibikii kafiri kwa kuwa hana sifa ya Ijumaa, ambayo ni Uislamu.
  2. Baleghe: Swala ya Ijumaa inamuwajibikia mtu mzima aliyefikia umri wa baleghe. Kwa maana hiyo, swala ya Ijumaa si wajibu kwa mtoto mdogo; aliye chini ya umri wa baleghe.
  3. Akili timamu: Inamuwajibikia swala ya Ijumaa mtu mzima mwenye akili timamu. Kwa hivyo basi, mwendawazimu hawajibikiwi na swala hii ya Ijumaa.
  4. Uhuru kamili (Uungwana): Swala ya Ijumaa si wajibu kwa mtumwa anayezingatiwa na sheria. Hii ni kwa sababu ya kushughulishwa kwake na haki ya utumwa kwa bwana wake. Haki hii ya bwana wake ndio inayomnyima uwajibu wa swala ya Ijumaa.
  5. Uanamume: Ijumaa si wajibu kwa wanawake wa Kiislamu kwa sababu ya kushughulika kwao na ulezi wa watoto na shughuli za nyumbani. Pia Ijumaa si wajibu kwao kutokana na imkani (uwezekano) ya kupatikana mashaka kwao kwa sababu ya ule uwajibifu wa kuhudhuria katika wakati na mahala maalum.
  6. Siha (afya) ya kiwiliwili: Swala ya Ijumaa si wajibu kwa mgonjwa ambaye anapata maumivu (machungu) kutokana na harakati za kuhudhuria msikitini au kukaa msikitini mpaka kumalizika kwa swala. Pia anapewa hukumu ya mgonjwa mtu ambaye anamuuguza na kumtumikia mgonjwa na pakawa hapana mtu wa kumshikia zamu wakati wa kwenda msikitini. Huyu bila ya kuangalia mgonjwa ni ndugu au si ndugu yake wa nasabu, haimuwajibikii swala ya Ijumaa maadam mgonjwa anahitajia huduma yake.
  7. Ukazi wa mahala pa Ijumaa: Ijumaa si wajibu kwa msafiri aliyesafiri safari ya halali ijapokuwa ni ile inayohusisha rukhsa ya kukusuru. Hukumu hii ni iwapo safari yake ilianza kabla ya kuchomoza kwa alfajiri ya siku ya Ijumaa.

Sharti saba hizi za uwajibifu wa swala ya Ijumaa ambazo ni: Uislamu, baleghe, akili timamu, uungwana, uanamume, siha ya mwili na ukaazi wa mji. Zote hizi zinatokana na kauli hizi za Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:-

ü      “Ijumaa ni haki ya wajibu juu ya kila muislamu katika/pamoja na jamaa ila watu wanne:

·        mtumwa aliyemilikiwa, au

·        mwanamke, au

·        mtoto mdogo, au

·        mgonjwa”. Abuu Daawoud-Allah amrehemu.

ü      “Ye yote mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho (muislamu), basi imemuwajibikia Ijumaa ila mwanamke, msafiri, mtumwa na mgonjwa”. Daaruqutwniy na wengineo-Allah awarehemu.

 

VI/. SHARTI ZA KUSIHI KWA SWALA YA IJUMAA:

 

Zikipatikana sharti saba hizi tulizozitaja, swala ya Ijumaa itakuwa tayari ni wajibu kwa muhusika ila tu itakuwa haisihi ila kwa kupatikana sharti nne zifuatazo:-

  1. Kuwa ndani ya mipaka ya mji: Ili Ijumaa isihi kisheria ni wajibu isimamishwe ndani ya mipaka ya mji, kitongoji au kijiji chenye wakazi wasiopungua arobaini [40] ambao kwao swala ya Ijumaa ni wajibu. Kwa mantiki hii, swala ya Ijumaa haisihi mawandani, kambini (mahala walipopiga makhema) wala katika kijiji ambacho kina watu walio chini ya idadi ya wanaopasiwa na Ijumaa. Lakini watu wa kijiji hiki wakisikia adhana ya swala ya Ijumaa inayotolewa katika kijiji kilicho jirani yao, kutawawajibikia kutoka kwenda kuswali swala ya Ijumaa katika kijiji jirani hicho. Na kama hawaisikii adhana ya kijiji jirani, basi Ijumaa itaendelea kuwa sio wajibu kwao.

Dalili/ushahidi wa sharti hii:

Swala ya Ijumaa katika zama zake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na pia katika zama za makhalifa waongofu-Allah awawiye radhi-haikuswaliwa ila ndani ya mipaka ya mji. Pembezoni mwa Madinah yalikuwepo makabila ya mabedui, haikuthibiti hata katika hadithi dhaifu kwamba waliswali Ijumaa au Bwana Mtume aliwaamrisha kuswali. Kadhalika pamoja na kukithiri kwa safari za Mtume wa Allah nje ya Madinah, katu haikuthibiti kwa riwaya sahihi kwamba aliiswali swala ya Ijumaa safarini. Huu ndio ukweli, zingatia!

  1. Kupatikana watu arubaini:

Idadi ya watu wanaojumuika kwa ajili ya swala ya Ijumaa na ambao kwao Ijumaa ni wajibu isipungue watu arubaini. Watu arubaini hawa wawe ni wanamume, watu wazima, wakazi wa mji husika.

Dalili ya sharti hii ya pili:

v     Imepokelewa kutoka kwa Jaabir Ibn Abdillah-Allah amuwiye radhi-amesema: Suna ya Mtume imepita kwamba katika kila (idadi ya watu) arubaini na kuendelea ni Ijumaa (hiyo).

v     Imepokelewa na Ka’ab Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-kwamba wa mwanzo aliyewaswalisha Ijumaa ni As’ad Ibn Zaraarah-Allah amuwiye radhi-na wakati huo walikuwa ni watu arubaini.

 

TANBIHI: Elewa na ufahamu ewe mpenzi ndugu msomaji wetu kwamba kuna makindano baina ya wanazuoni katika kadhia hii ya idadi ya watu inayofungamana nayo Ijumaa. Ni arubaini, ama ni kumi na mbili au ni watu watatu, rejea vitabu vya Fiq-hi kwa ufafanuzi wa kina na rejea vema dalili za kila upande.

 

 


TUJIFUNZE NA TUKUBALI:

“Atakayetawadha na akaufanya vema udhu wake, kisha akaiendea (swala ya) Ijumaa na akanyamaza (kwa ajili ya kuisikiliza khutba). Ataghufiriwa madhambi yaliyo baina ya Ijumaa hiyo na Ijumaa nyingine na ziada ya siku tatu. Na atakayegusa kijiwe, huyo kafanya mchezo”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Riwaya: Muslim


Forum | Guestbook | Tuandikie |