Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

VI/. SHARTI ZA KUSIHI KWA SWALA YA IJUMAA:

Faida

 

3. Iswaliwe katika wakati wa swala ya Adhuhuri:

Ni sharti swala ya Ijumaa iswaliwe ndani ya wakati wa Adhuhuri ndipo iweze kusihi. Wakati wa swala ya Adhuhuri ukidhikika kiasi cha kutosalia kitambo cha kutosha kuiswali swala ya Ijumaa ndani ya kipindi hicho kabla ya kuingia kwa wakati wa swala ya Alasiri. Katika hali kama hii kutawawajibikia hawa waliodhikiwa na wakati kuiswali Ijumaa adhuhuri rakaa nne badala ya mbili kama ambavyo ingeswaliwa ndani ya wakati. Lau watu wataingia kuiswali swala ya Ijumaa, wakati wa Adhuhuri ukatoka na ilhali wao bado wangali ndani ya swala hiyo; hawajaimaliza. Hapa wataigeuza swala ya Ijumaa kuwa Adhuhuri na kutimiza rakaa nne kwa nia ile ile ya Ijumaa waliyoanza nayo.

Dalili ya sharti hii:

Dalili na ushahidi huu wa sharti hii ya tatu ya kusihi kwa Ijumaa ni kitendo chake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuiswali swala ya Ijumaa ndani ya wakati huo wa Adhuhuri. Haya ni kama yanavyofahamika kupitia hadithi zifuatazo:-

              I.      Imepokelewa kutoka kwa Anas-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiswali swala ya Ijumaa wakati jua linapopinduka”. (Na huo ni wakati wa Adhuhuri kwani jua halipinduki ila wakati huo). Bukhaariy-Allah amrehemu.

           II.      Imepokelewa kutoka kwa Salamah Ibn Al-Ak-waa-Allah amuwiye radhi-amesema: “Tulikuwa tukiswali pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-swala ya Ijumaa. Kisha tukiondoka (kurudi majumbani) na ilhali kuta zikiwa hazina kivuli tunachoweza kujikinga nacho”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

         III.      Imepokelewa kutoka kwa Sahli Ibn Sa’ad-Allah amuwiye radhi-amesema: “Hatukuwa tukipata lepe la mchana (hatulali usingizi mdogo wa mchana) wala chakula cha mchana ila baada ya (kuswaliwa) swala ya Ijumaa”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Hadithi zote hizi zinafahamisha kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa haiswali swala ya Ijumaa ila ndani ya wakati wa Adhuhuri. Na si tu ndani ya wakati wa Adhuhuri bali ndani ya wakati wa mwanzo wa Adhuhuri, elewa na ufahamu hivi. Kwa mantiki hii basi, hakusihi kuiswali swala ya Ijumaa kabla ya wakati huu wa Adhuhuri wala baada yake, yaani baada ya kumalizika na kuingia Alasiri.

 

        IV.      Ijumaa iwe moja tu katika mji ila kwa dharura:

Kumeshurutizwa kutoidadika (kutokuwa nyingi) swala za Ijumaa katika mji au kitongoji kimoja muda wa kumkinika hilo. Hii ni kutokana na ule wajibu wa kukutana watu wa mji mmoja mahala pamoja ili kuonyesha nembo ya swala tukufu ya Ijumaa.

Angalia:

a)      Iwapo watu watakithiri (watakuwa wengi) kiasi cha kushindikana kukusanyika mahala pamoja kutokana na ufinyu wa mahala hapo. Katika hali na mazingira haya kutajuzu kuwepo na Ijumaa nyingi kwa kiasi cha kukidhi haja tu.

b)      Lau swala za Ijumaa zitakuwa nyingi katika mji mmoja bila ya kuwepo na haja ya kisheria ya kufanya hivyo. Haitasihi miongoni mwa Ijumaa hizo ila ile iliyozitangulia nyingine. Na mazingatio na marejeo katika kutangulia ni katika kuanza na sio katika kumalizika. Kwa mantiki hii basi, ile swala ya Ijumaa ambayo imamu wake ataanza kuswali kabla ya zile nyingine, hiyo ndiyo itakayokuwa sahihi. Na nyingine zote zilizobakia zitakuwa ni batili na kutawapasa watu waliozihudhuhuria kuswali Adhuhuri mahala pa Ijumaa.

c)      Ikiwa haijulikaniwi ni Ijumaa ipi iliyotangulia, basi Ijumaa zote hizo zitakuwa ni batili. Na kutawalazimu watu wa Ijumaa hizi kukusanyika mahala pamoja iwapo hilo linamkinika na wakati ukawa unaruhusu, waswali tena Ijumaa upya. Iwapo hili halitawezekana, wote watalazimika kuswali Adhuhuri kwa ajili ya kuunga mapungufu yaliyojitokeza.

Dalili ya sharti hili:

Sharti hili la nne la kusihi kwa swala ya Ijumaa linatokana na ukweli kwamba si tu katika zama za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Bali hata katika zama za makhalifa waongofu-Allah awawiye radhi-na pia katika zama za Taabiina. Ijumaa haikuswaliwa ila mahala pamoja tu katika mji/kitongoji kizima. Zama/enzi hizo ulikuwepo katika mji/kitongoji msikiti mkubwa kushinda misikiti yote iliyopo katika mji/kitongoji husika. Msikiti huu ulijulikana kama “AL-MASJIDUL-JAAMII”-yaani “MSIKITI WA IJUMAA”, inamoswaliwa ndani yake Ijumaa ya mji/kitongoji hicho. Na misikiti mingine ilibaki ikitumiwa kwa swala tano nyingine, yaani zile za kila siku na sio Ijumaa. Hivi ndivyo tunavyoweza kufahamu kupitia hadithi zifuatazo:-

              I.      Imepokelewa kutoka kwa mama wa waumini; Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: “Watu walikuwa wakija mara kwa mara siku ya Ijumaa kutoka majumbani mwao na kutoka (pande) za ‘AWAALIY” (Hizi ni sehemu/vitongoji vya mashariki mwa Madinah. Kilichokuwa karibu zaidi na Madinah kilikuwa umbali wa maili tatu au nne kutokea  mjini Madinah palipokuwa pakiswaliwa hiyo Ijumaa)”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

           II.      Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kwamba amesema: Hakika Ijumaa ya mwanzo iliyoswaliwa baada ya ile Ijumaa (iliyoswaliwa) katika msikiti wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-(ilikuwa) katika msikiti wa Abdili-Qaysi huko Juwaathaa (hiki kilikuwa ni kimojawapo ya vitongoji vya nchi ya Bahrein enzi hizo) pande za Bahrein”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Falsafa ya sharti hili ni kwamba kitendo cha kutosheka na mahala pamoja watu wote kinapelekea zaidi kufikiwa kwa lengo la swala hii ya Ijumaa inayowakusanya watu wengi kwa pamoja mara moja kila juma. Na lengo hili si lingine bali ni kule kuwa wamoja waislamu na kuonyesha mshikamano utakaowaogofya na kuwatisha maadui wao. Na kitendo cha kutapanyika huku na huko bila ya haja, hutengeneza na kujenga mazingira ya kugawika na kutengana na hivyo kutoa mwanya kwa adui kuingia kati yetu kirahisi na kutugonganisha wenyewe kwa wenyewe.  

 


TUJIFUNZE NA TUKUBALI:

“Atakayekoga siku ya Ijumaa na akajitia manukato ya mkewe ikiwa anayo na akavaa nguo zake nzuri. Kisha asizikengeuke shingo za watu (huko msikitini) na asifanye mchezo wakati wa mawaidha (khutba). Itakuwa (Ijumaa hiyo) ni kafara (ya madhambi) baina ya (Ijumaa) mbili. Na atakayefanya mchezo na akazikengeuka shingo za watu  itakuwa kwake ni Adhuhuri”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Riwaya: Abuu Daawoud & Ibn Khuzaymah-Allah awarehemu.


Forum | Guestbook | Tuandikie |