|
Kustanji/Kuchamba ni kusafisha na kuondoa najisi iliyotoka katika mojawapo ya tupu
{uchi}mbili au zote mbili; tupu ya mbele na ya nyuma kwa kutumia maji twahara au
kinachosimama memo/mahala pa maji wakati wa kukosekana maji kama vile mawe, karatasi,
kitambaa, majani na kadhalika. Mchambaji ahakikishe amejisafisha vema kiasi cha kutobakia
athari ya najisi iliyotoka; ikiwa ni mkojo au mavi.
Kustanji/Kuchamba baada ya kukidhi haja ni WAJIBU/FARADHI kama tutakavyoona katika
kauli za Mtume Rehma na Amani zimshukie katika maelezo yajayo.
VITU VITUMIKAVYO KATIKA KUSTANJI
Inajuzu/inafaa kustanji (kuchamba) kwa kutumia maji mutlaq (maji halisi) ambayo
ndiyo asili katika kujitwahirisha na najisi. Pia inajuzu kustanji kwa kila kitu chenye
sifa zifuatazo :
- Kigumu (kigogofu)
- Chenye Kuparuza (kisichoteleza)
- Kinachoweza kuondosha najisi.
Vitu vyenye sifa hizi ni kama mawe, karatasi, kitambaa na kadhalika. Ni vema
kustanji, mtu akaanza kwa kutumia mawe/karatasi kisha ndio akamalizia na maji. Kufanya
hivyo ni kwa sababu mawe/karatasi huondosha juta (dhati) ya najisi na maji huondosha
athari ya najisi bila ya kuchangayika na juta lake. Ikiwa atatumia kimojawapo baina ya
mawe/karatasi na maji, basi ni bora akatumia maji kwani ndiyo pekee yenye uwezo wa
kuondosha juta (dhati) na athari ya najisi, kinyume na mawe na nduguze {karatasi, kitambaa
na kadhalika}.
Imepokelewa kutoka kwa Anas Ibn Maalik Allah amuwie Radhi amesema :
Mtume wa Allah alikuwa akiingia mahala pa kukidhi haja, mimi na kijana wa rika langu
tukimbebea chombo cha maji na fimbo/mkuki mfupi, basi akistanji kwa kutumia maji. Bukhariy
na Muslim.
Maelezo : Fimbo/Mkuki ulikuwa ukitumika kama sitara na alama wakati wa kuswali ili
mtu asiweze kupita mbele.
Imepokewa na Ibn Masoud Allah amuwie Radhi amesema : Mtume
Rehma na Amani zimshukie alienda kukidhi haja na akaniamrisha nimletee mawe matatu.
Al-Bukhariy.
USISTANJI kwa kutumia najisi nyingine iliyo kavu au kitu kilichonajisika tayari
kwani huenda kikaizidisha athari ya najisi badala ya kuipunguza. Kadhalika ni haramu
kustanji kwa kilicho chakula cha binadamu kama vile mkate au chakula cha majini kama vile
mifupa. Amesema Bwana Mtume Allah amshushie Rehma na Amani "Msistanji
kwa (kutumia) kinyesi cha wanyama wala mifupa kwani hiyo (mifupa) ni chakula cha ndugu
zenu majini" Tirmidhiy.
ADABU/TARATIBU ZA KUFUATA KATIKA KUKIDHI HAJA NA KUSTANJI (KUCHAMBA)
Sheria imeweka taratibu ambazo muislamu anapaswa kuzichunga na kuzifuata wakati wa
kukidhi haja na kustanji. Taratibu hizi tutazigawa katika mafungu/sehemu zifuatazo :
A. ADABU/TARATIBU ZINAZOFUNGAMANA NA MAHALA PA KUKIDHIA HAJA
Imemlazimu mkidhi haja, ajiepushe kukidhi haja katika :
- Njia ya watu au mahala wanapokaa, hii ni kutokana na kero na maudhi yatakayowapata.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah Allah amuwie Radhi kwamba Mtume
Rehma na Amani zimshukie amesema : "Yaogopeni mambo mawili yaletayo
laana" (Maswahaba) wakauliza : Ni yapi mambo mawili hayo ? (Mtume) akajibu : "Ni
yule ambaye anajisaidia katika njia ya watu au kivuli chao" Muslim.
- Tundu iliyopo ardhini au ufa wa ukuta/kiambaza. Hii ni kwa sababu ya kumlinda na
kumuepusha mkidhi haja na madhara yanayoweza kumpata. Kwani anaweza akawamo ndani ya
shimo/ufa mdudu mwenye kudhuru kama vile nge au nyoka, huyu akakerwa na haja akaamua
kumtokea mtu na kumdhuru. Imepokelewa kutoka kwa Abdillahi ibn Sarjisi, amesema :
Amekataza Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie kukojoa katika tundu.
Abuu Daawood.
- Chini ya mti utoao matunda. Hii ni kwa ajili ya kuyahifadhi na kuyalinda matunda
yadondokayo yasipatwe na najisi. Ni mamoja ikiwa matunda hayo yanaliwa au hayaliwi lakini
yana manufaa mengine kama dawa.
- Maji yaliyotuama (yasiokwenda). Hii ni kutokana na kichefuchefu watumiaji wa maji
hayo yakiwa ni mengi yasiyoharibika na najisi na kuyanajisi yakiwa machache na hivyo
kuyafanya yasifae kutumika. Imepokelewa kutoka kwa Jabir Allah amuwie Radhi
kutoka kwa Mtume Rehema na Amani zimshukie kwamba (Mtume) amekataza kukojoa
katika maji yaliyotuama". Muslim.
Kunya ni aula zaidi kwa kukatazwa
B. ADABU/TARATIBU ZENYE KUFUNGAMANA NA UINGIAJI NA UTOKAJI MAHALA PA KUKIDHI
HAJA
Ni Vema kwa mwenye kutaka kukidhi haja, atangulize mguu wake wa kushoto wakati wa
kuingia chooni na mguu wa kulia wakati wa kutoka chooni, kama tulivyofundishwa na Mtume wa
Mwenyezi Mungu. Kadhalika asiingie na chochote chenye jina la Mwenyezi Mungu au jina
lolote tukufu kama vile jina la Mtume au aya ya Qurani Tukufu. Bali imemlazimu muislamu
kukivua kitu hicho wakati wa kuingia chooni. Pia imesuniwa kuleta dua wakati wa kuingia
chooni. Pia imesuniwa kuleta dua zilizothibiti kutoka kwa Bwana Mtume kabla na baada ya
kutoka chooni.
Aseme kabla ya kuingia chooni :
BISMILLAH ALLAHUMMA INNIY AUDHUBIKA MINAL KHUBUTHI WAL-KHABAITH. Al-Bukhariy na Muslim.
Na aseme baada ya kutoka :
GHUFRAANAKA AL-HAMDU LILLAHIL-LADHIY ADH-HABA ANNIYL-ADHA WA-AAFANIY. Abu Dawood,
Al-tirmidhi, Ibn Majah na Al-twabraniy.
C. ADABU/TARATIBU ZIFUNGAMANAZO NA UPANDE WA KUELEKEA WAKATI WA KUKIDHI HAJA :
Ni haramu kwa mwenye kukidhi haja kuelekea Qiblah au kukipa mgongo. Uharamu huu ni
iwapo anakidhi haja mwandani, wala hapana chenye kumsitiri wakati wa kukidhi haja yake. Na
imeshurutizwa sitara isiwe mbali nae zaidi ya dhiraa tatu za binadamu sawa na sentimeta
150 takriban. Ikiwa jengo analotumia limeandaliwa maalum kwa ajili ya kukidhia haja
(chooni), basi si haramu, bali inajuzu kuelekea na kulipa mgongo Qiblah kwa kuwa pana
sitara.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Ayyuub Al-Answariy Allah amuwie Radhi
kutoka kwa Mtume Rehma na Amani zimshukie amesema "mnapokwenda chooni
msielekee Qiblah wala msikipe mgongo kwa (kukidhi) haja ndogo au kubwa, lakini elekeeni
mashariki na magharibi". Al-Bukhariy na Muslim.
D. ADABU/TARATIBU ZINAZOFUNGAMANA NA HALI YA KUKIDHI HAJA :
Ni vema kwa mwenye kukidhi haja akategemea mguu wake wa kushoto na
kuusimamisha/kuunyoosha mguu wa kulia, hivi ndivyo anavyotakiwa akae wakati wa kukidhi
haja. Hekima ya ukaaji huu ni kuifanya haja itokee kwa wepesi kama vile unavyomimina
kilichomo ndani ya chupa kwa kuinamisha upande upande. Kadhalika anatakiwa wakati wa
kukidhi haja asiangalie juu, utupu wake wala kile kimtokacho. Pia ni karaha kuzungumza
wakati anakidhi haja.
Imepokelewa na Ibn Umar Allah amuwie Radhi kwamba mtu mmoja alipita
ilhali Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehma na Amani zimshukie akikidhi haja ndogo,
(mtu yule) akamtolea salamu, (Mtume) hakumjibu. Muslim.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Said Allah amuwie Radhi amesema ;
Nimemsikia Mtume Rehma na Amani zimshukie akisema : "Wasitoke watu
wawili wakaenda kukidhi haja, hali ya kufunua tupu zao huku wakizungumza, hakika Mwenyezi
Mungu Mtukufu hulichukia hilo" Abu Dawood na wengineo.
Maelezo : Inakisiwa/Inapimiwa juu ya maneno (mazungumzo) mambo mengine kama vile
kula, kunywa na kuchezeachezea utupu (uchi).
Kustanji/kuchamba kwa kutumia mkono wa kushoto : Anatakiwa mwenye kukidhi haja
atumie mkono wake wa kushoto kusafisha mahala ilipotokea najisi kwani ni karaha kutumia
mkono wa kulia.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Qatadah Allah amuwie Radhi kutoka kwa
Mtume Rehema na Amani zimshukie amesema : "Anapokojoa mmoja wenu, basi
asiishike dhakari yake kwa mkono wa kulia na wala asistanji/asichambe kwa mkono wa
kulia".
Kadhalika miongoni mwa adabu, anatakiwa mwenye kukidhi haja mawandani; nje ya
jengo lililoandaliwa kwa kukidhia haja (chooni), atafute mahala pa faragha palipo mbali na
watu. Watu wasimuone wala kusikia harufu ya choo chake au sauti ya mashuzi yake.
Imepokelewa kwamba Mtume Rehema na Amani zimshukie alikuwa anapotaka kwenda
kujisaidia huenda mbali mpaka mtu asiweze kumuona. Abu Dawood na Al-Tirmidhiy.
Vile vile anatakiwa asiisege/asiipandishe nguo yake ikiwa ni shuka/msuli mpaka
akurubiapo ardhi, sio anaanza kuvua nje kabla hajaingia ndani. Afanye hivyo kwa ajili ya
kuusitiri utupu wake, jambo ambalo limeamrishwa na sheria.
NYONGEZA : KATIKA KUTAJA HUKUMU ZA VYOMBO :
Vyombo ni vile vitu/vifaa ambavyo tunavyotumia katika kuwekea, kuhifadhia au kulia
chakula na vitu vingine viowevu (vimiminika) kama vile maji, maziwa, juisi na kadhalika.
Hivi ndivyo vyombo ambavyo tunavyokusudia kutaja hukumu ya utumiaji wake kwa mujibu wa
sheria. Tutavigawa na kuviweka vyombo katika mafungu manne, kama ifuatavyo :
1. HUKUMU YA UTUMIAJI WA VYOMBO VYA DHAHABU NA FEDHA:
Vyombo vya dhahabu ni vile vyombo ambavyo malighafi (material) iliyotumika
kuvitengenezea ni dhahabu halisi au fedha halisi. Vyombo hivi vinaweza kuwa ni vijiko,
sahani, bakuli na kadhalika, na siyo vitu kama mikufu, bangili, hirini, haya ni mapambo ya
wanawake na si vyombo.
Kwa mujibu wa sheria ni HARAMU kutumia vyombo vya dhahabu kwa aina zote za
matumizi, kama vile kuvitumia kwa ajili ya kutawadhia, kunywea, kulia chakula na matumizi
mengine kama haya. Mtu anaruhusiwa tu kutumia vyombo hivi kwa dharura, kama vile kukosa
kabisa chombo kingine kisichokuwa cha dhahabu. Kwa dharura kama hii anaweza kutumia chombo
cha dhahabu. Ruhusa hii ya dharura ni kwa mujibu wa msingi usemao :
DHARURA HUHALALISHA YALIYO HARAMU/YALIYOKATAZWA
Imepokelewa kwa swahaba Hudhayfah ibn Al-Yamaan Allah amuwie radhi
amesema : Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehema na Amani zimshukie
akisema : "Msivae hariri wala dibaji (aina ya nguo ya thamani za hariri) na wala
msinywee vyombo vya dhahabu na fedha, na wala msilie sahani zake (dhahabu na fedha) kwani
vyombo hivyo ni vyao (makafiri) duniani na ni vyetu akhera" Al-Bukhariy na Muslim.
Hukadiriwa juu ya kula na kunywa matumizi mengine kama vile kunawia na kuhifadhia
chakula. Ni vema ikaeleweka kuwa uharamu huu wa utumiaji vyombo vya dhahabu unamuhusu
mwanamume na mwanamke.
2. HUKUMU YA UTUMIAJI WA VYOMBO VILIVYOTIWA KOWA LA DHAHABU AU FEDHA :
Tunamaanisha kwa neno KOA, ungo/muungo. Yaani chombo kisichotengenezwa kwa dhahabu
au fedha kilivunjika au kilikatika, kisha yakatumika madini ya dhahabu au fedha kukiunga
tena chombo kile ili kiweze kufaa kutumika.
Sheria imeharamisha kutumia chombo kilichotiwa koa la dhahabu kwa hali yeyote ile
iwayo. Ni mamoja koa lilikuwa kubwa au dogo. Ama utiaji wa koa la fedha, aangalie :
- ikiwa koa ni dogo kwa uungaji usio wa pambo, INAJUZU/IMERUHUSIWA.
- Ikiwa koa ni kubwa tena ni kwa ya pambo, basi ni HARAMU/IMEKATAZWA.
- Ikiwa koa ni kubwa kwa sababu ya haja au koa ni dogo kwa ajili ya pambo ni KARAHA.
Na dalili/ushahidi juu ya kujuzu koa kubwa la fedha ni ile hadithi iliyopokewa
kutoka kwa Aaswim Al-ahwaal amesema : niliiona bilauri ya Mtume Rehema na
Amani zimshukie kwa Anas bin Malik na ilikuwa imevunjika, akaiunga kwa (koa) la
fedha. Na Anas akasema : Nilimnyweshea Mtume wa Mwenyezi Mungu bilauri hii zaidi ya hivi
na hivi.
3. HUKUMU YA UTUMIAJI WA VYOMBO VILIVYOTENGENEZWA KUTOKANA NA MADINI YENYE THAMANI
KUBWA {PRECIOUS STONES}
Inajuzu kisheria kutumia vyombo ambavyo malighafi iliyotumika kuvitengenzea ni
madini yenye thamani kubwa kama vile almasi, lulu, marijani (coral), yaaquti (ruby) na
mengineyo. Kujuzu huku kunatokana na kutopokewa NASWI ya Qurani au hadithi kukataza vitu
hivi. Na Msingi wa Fiq-hi unasema :
(ASILI KATIKA VITU NI UHALALI) maadam haikupokewa dalili ya kuharamisha au
kukataza.
4. HUKUMU YA UTUMIAJI VYOMBO VYA MAKAFIRI :
Tunakusudia kwa ibara "Vyombo vya makafiri", vyombo vinavyomilikiwa na
makafiri yaani ni mali yao na wanavitumia kwa matumizi yao mbali mbali.
Sheria imeruhusu muislamu kutumia vyombo vya makafiri kwa matumizi mbali mbali.
Ruhusa hii ni kwa mujibu wa hadithi iliyopokelewa na Imam Bukhariy kutoka kwa Abu
Thaalabah Allah amuwie Radhi kwamba Mtume Rehema na Amani
zimshukie amesema : "Vikosheni na mvitumie kwa kulia chakula".
Maelezo : Amri hii ya Mtume juu ya kuviosha vyombo vya makafiri kabla ya kuvitumia
ni kwa ajili ya USUNA kwani inamkinika kuwa vimechafuliwa na wamiliki wake ambao ni
makafiri. Pengine wamevitumia katika kunywea pombe au kupikia na kulia nguruwe na
kadhalika. Inakadiriwa juu ya vyombo vitu vyao vingine kama vile nguo, samani(furniture)
na kadhalika.
|