|
Swala
ya Ijumaa inasimama juu ya nguzo mbili ambazo
ndio msingi wa swala hii tukufu. Nguzo hizo ni:-
- KHUTBA
MBILI:
Hii ndio nguzo ya kwanza ya msingi miongoni mwa nguzo mbili zinazoijenga
swala ya Ijumaa. Nguzo hii inaambatana na sharti
kadhaa ambazo hujulikana kama “sharti za
khutba mbili” na sharti hizo ni kama
zifuatavyo:-
a.
Kusimama
na kutenganisha baina ya khutba ya kwanza na ile
ya pili kwa kitako kifupi.
Kumeshurutizwa
khatibu akhutubu ilhali akiwa kasimama ikiwa
anaweza huko kusimama na akishindwa kusimama
basi atakhutubu akiwa amekaa kitako. Kadhalika
anapaswa kukaa kitako kifupi ili kutenganisha
baina ya khutba ya kwanza na ile ya pili. Hivi
ndivyo alivyofanya mwenyewe Bwana Mtume.
Imepokelewa kutoka kwa Jaabir Ibn Samurah-Allah
amuwoye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-alikuwa akikhutubu khutba mbili akikaa
baina ya (khutba) mbili hizo. Na alikuwa
akikhutubu ilhali akiwa amesimama.
Muslim-Allah
amrehemu.
Imepokelewa
kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-amesema:
“Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alikuwa akikhutubu ilhali kasimama
kisha hukaa (baada ya khutba ya kwanza) kisha
huinuka (husimama tena kwa ajili ya khutba ya
pili) kama mfanyavyo nyinyi hivi sasa”. Bukhaariy
& Muslim-Allah awarehemu.
b. Khutba
ziitangulie swala.
Ni
sharti swala ya Ijumaa itanguliwe na khutba
mbili, zikimalizika ndio swala ikimiwe. Haiwi
kama inavyokuwa katika swala za Eid ambapo
hutangulia swala kisha ndio zikafuatia khutba
mbili. Sharti hii inatokana na eleweko jumuisho
la hadithi zilizopokelewa katika kutaja swala ya
Ijumaa na kwa Ijmaa ya
waislamu katika hili.
- Twahara
ya hadathi ndogo na kubwa na ya najisi
isiyosameheka katika nguo, mwili na mahala
pa kukhutubia na kusitiri tupu.
Kumeshurutizwa
kwa khatibu kuwa twahara; asiwe na hadathi ndogo
itakayompasishia udhu wala ile kubwa
itakayomuwajibishia josho. Pia inatakikana mwili
wake, nguo na mahala pa kukhutubia pawe twahara;
isiwepo najisi isiyosameheka kisheria. Kadhalika
kumeshurutizwa khatibu awe amejisitiri kwa
mujibu wa sheria.
Sharti
hii inatokana na kuichukulia khutba kuwa ni kama
swala ya Ijumaa. Ni kwa ajili ya msimamo huu
ndio khutba mbili zinakuwa ni badali ya zile
rakaa mbili za fardhi ya Adhuhuri. Kwa mantiki
hii khutba zikashurutiziwa sharti zote
zilizoshurutiziwa swala, kuanzia twahara na baki
ya sharti nyinginezo.
- Khutba
(nguzo) itolewe kwa lugha ya Kiarabu.
Kunampasa
khatibu kukhutubu kwa lugha ya Kiarabu hata kama
wanaokhutubiwa hawaijui lugha hiyo. Sharti hii
inazikhusu zile nguzo tano za khutba kama
tutakavyozitaja. Ama waadhi unaweza kutolewa kwa
lugha inayofahamika na watu wa mahala husika
kama yamivyoelezwa hayo katika vitabu vya Fiq-hi
pamoja na makindano ya wanazuoni juu yake,
zinduka!
- Kufululiza
baina ya nguzo za khutba, kufululiza baina
ya khutba ya kwanza na ile ya pili na baina
ya khutba ya pili na swala.
Kumeshurutizwa
kutokuwepo mwanya mkubwa baina ya nguzo na nguzo
fuatizi, baina ya khutba na khutba ambatizi na
hali kadhalika baina ya khutba na swala. Angalia
lau utakuwepo mwanya mkubwa baina ya khutba ya
kwanza na ile ya pili au mwanya huo ukawa ni
baina ya khutba mbili na swala, khutba hiyo
haitasihi. Ikimkinika kuidiriki kutawajibika
kuirudia na kama haikumkinika, basi swala hiyo
itageuka na kuwa Adhuhuri na sio Ijumaa tena.
- Kuwasikilizisha
nguzo za khutba watu arobaini
wanaofungamanikiwa na Ijumaa.
Kunampasa
khatibu kunyanyua sauti yake wakati wa kukhutubu
kiasi cha kuweza kusikiwa na wale anaowakhutubia
ambao hawana matatizo katika usikivu wao.
Hizi
ndizo shatri za khutba mbili kama zilivyotajwa
katika vitabu vya Fiq-hi kwa rejea za hadithi,
virejee utaziona.
NGUZO
ZA KHUTBA MBILI:
Baada ya kuangalia sharti za khutba, inatupasa tuelewe kuwa khutba ya Ijumaa
inazo nguzo ambazo hutambulika kama “nguzo
za khutba” hizi ni kama zifuatavyo:-
1)
Kumuhimidi
Allah kwa tamko lo lote lenye luleta maana ya
himda.
Kama
khatibu kusema: “Al-hamdulillah” au “Ahmadullah”
na mithili ya matamko haya.
2)
Kumswalia
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwa tamko
lo lote la swala ya mtume.
Imeshurutizwa
khatibu alitaje jina la Bwana Mtume kwa
ufumbulizo. Mithili ya kusema: “Nabiyyi”,
ama “Rasuuli”, au “Muhammad”,
kwani hakutoshi kutaja dhamiri
(kiwakilishi-pronoun) kama vile kusema: (Allaahumma
swalli alayhi) bila ya kutaja jina.
3)
Kuwausia watu kumcha Allah kwa tamko lo
lote lenye kubeba maana hiyo.
Mtihili
ya kusema: “Uuswiykumu bitaquwallaah”, au
“Ittaquwalaah” na kadhalika.
Nguzo tatu hizi; himda, swala ya Mtume na wasia wa kumcha Allah, ni nguzo
shiriki kwa kila mojawapo ya khutba mbili. Yaani
zinaletwa katika khutba zote mbili.
4)
Kusoma aya ya Qur-ani katika mojawapo ya
khutba mbili.
Imeshurutizwa
kuwa aya hiyo iwe ni yenye kufahamika na yenye
maana ya wazi na ni bora isomwe mwishoni mwa
khutba ya pili.
5)
Kuwaombea dua waislamu katika khutba ya
pili kwa tamko linaloweza kuitwa dua.
2.
KUSWALI
RAKAA MBILI KATIKA JAMAA:
Hii ndio nguzo ya pili ya
msingi ya swala ya Ijumaa kwa ushahidi wa
hadithi zifuatazo:-
ü
Imepokelewa kutoka kwa Sayyidina Umar-Allah amuwiye
radhi-amesema: “Swala
ya ya Ijumaa ni rakaa mbili (haya ni) kwa
ulimi wa Muhammad-Rehema na Amani zimshukie”. Nasaai-Allah amrehemu.
ü
Imepokelewa kutoka kwa Twariq Ibn Shihaab-Allah amuwiye
radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Ijumaa
ni haki ya wajibu kwa kila muislamu katika
jamaa...” Abuu Daawoud-Allah amrehemu.
Fungamano na kongamano la wanazuoni katika hili la kuswaliwa
rakka mbili za Ijumaa katika jamaa limejengeka
juu ya hadithi hizi.
Kumeshurutizwa katika kuidiriki (kuipata) jamaa kudiriki
rakaa moja ya Ijumaa. Mtu akiidiriki rakaa moja
hiyo, swala yake (Ijumaa) itasihi na kama
hakudiriki rakaa kutamuwajibikia kuihawilisha
(kuigeuza) Adhuhuri. Na ni wajibu maamuma
wanaounda jamaa ya Ijumaa ambao kwao Ijumaa
inafungamana isipungue idadi yao watu arobaini.
Kwa msingi huu, lau mtanguliwa (mtu
aliyechelewa) atakuja na akamfuata Imamu katika
rakaa ya pili, Ijumaa yake itasihi kutokana na
kule kuidiriki kwake rakaa moja ya swala
ya Ijumaa. Baada ya Imamu kutoa salamu, yeye
atapaswa kuinuka kuswali rakaa moja nyingine ili
kutimiza idadi ya rakaa mbili za Ijumaa. Ama
ikiwa huyu mtanguliwa atamdiriki Imamu baada ya
kuinuka kutoka katika rukuu ya rakaa ya pili,
haikutuka kwake Ijumaa. Kwa hivyo atawajibika
kumfuata Imamu hapo alipomdiriki kwa nia ya
Ijumaa na baada ya salamu ya Imamu atainuka na
kuitimiza Adhuhuri rakaa nne.
Ni kwa kuuzingatia msingi huu huu pia, lau maamuma
watamfuata Imamu katika swala ya Ijumaa na
wakatimiza pamoja nae rakaa moja. Kisha ikazuka
sababu inayowapelekea wote kumkhalifu Imamu au
baadhi yao. Wakamfariki na kila mmoja akatimiza
rakaa ya pili ya Ijumaa hali ya kuwa mpweke
(anaswali pekee), Ijumaa yao wote itakuwa ni
sahihi. Ama lau sababu hii ya mfaraka itazuka
kabla ya kumalizika kwa rakaa ya kwanza.
Wakamfariki, basi bila shaka yo yote Ijumaa yao
haitasihi na itageuka kwa upande wao kuwa
Adhuhuri. Maelezo na uchambuzi huu ni natija ya
riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah
awawiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atakayeidiriki
rakaa moja ya swala ya Ijumaa na swala
nyinginezo, basi na aiongezee nyingine na hakika
swala yake itakuwa imetimia”. Nasaai, Ibn Maajah &
Daaruqutwniy-Allah awarehemu.
|