|
Siku
ya Ijumaa na swala yake zina adabu na taratibu
zilizosuniwa, yatakikana kwa kila muislamu
kuzishughulikia na kuzoea kuzifanya, adabu na
taratibu hizo ni pamoja na:-
- Kukoga:
hili ni kwa mujibu wa hadithi ya Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-isemayo: “Anapoiendea mmoja wenu
Ijumaa basi na akoge”. Bukhaariy
(387) & Muslim (844).
Amri hii ya Bwana Mtume hapa inavuliwa kutoka katika hukumu ya uwajibu
kwenda katika usuna kwa mujibu wa ile hadithi
iliyopokelewa na Imamu Tirmidhiy: “Atakayetawadha
siku ya Ijumaa amefuata suna na hiyo ni suna
njema na atakayekoga, basi huko kukoga ni bora
zaidi”.
- Kuunadhifisha
mwili kutokana na taka (uchafu) na harufu
mbaya, kupakaza mafuta na kujitia manukato:
Muislamu anatakiwa kuyafanya yote haya ili asiwaudhi na kuwakera watu
wangine kutokana na uchafu na harufu yake mbaya.
Na badala yake awe katika hali na mandhari
ambayo watu watapenda na kuona raha kukaa karibu
yake. Na umekwishajifunza huko nyuma kwamba
miongoni mwa nyudhuru zinazompa mtu rukhsa
kutokuhudhuria swala ya jamaa ni kula kitu
chenye kutoa harufu mbaya inayowakera watu.
Imepokelewa kutoka kwa Salmaan Al-Faarisiy-Allah
amuwiye radhi-amesema: Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Mtu hakogi siku ya
Ijumaa na kujitwaharisha kiasi awezacho cha
twahara na kujipaka mafuta yake au kujitia
manukato ya nyumbani kwake. Kisha akatoka (kwenda
msikitini), hatenganishi baina ya watu wawili,
halafu akaswali alichofaradhiwa. Kisha akakaa
kimya Imamu atakapoanza kukhutubu ila
atasamehewa madhambi yaliyo baina yake na Ijumaa
ijayo”. Bukhaariy (843)-Allah amrehemu.
- Kuvaa
nguo nzuri:
Imepokelewa kutoka kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakayekoga
siku ya Ijumaa, kisha akavaa nguo zake nzuri
kabisa na akajitia manukato akiwa nayo. Kisha
akaiendea Ijumaa akiwa na utulivu na asimkeuke
ye yote na asimfanyie maudhi. Halafu akaswali
alichofaradhiwa, kisha akangojea mpaka aondoke
Imamu, atasamehewa madhambi yaliyo baina ya
Ijumaa mbili”. Ahmad (3/81) & wengineo-Allah
awarehemu.
Na ni bora zaidi ikiwa nguo nzuri hizo zitakuwa ni nyeupe, haya ni kwa
mujibu wa kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie: “Vaeni zilizo nyeupe katika nguo
zenu na wakafinini (wavisheni sanda) maiti zenu
katika hizo (nguo nyeupe)”. Tirmidhiy
(994) & wengineo-Allah awarehemu.
- Kukata
kucha na kutengeneza nywele:
Imepokelewa kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akikata
kucha zake na kupunguza sharubu zake siku ya
Ijumaa. Al-Bazaar-Allah amrehemu-katika
Musnadi yake.
- Kwenda
mapema msikitini:
Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakayekoga
siku ya Ijumaa mithili ya josho la janaba, kisha
akaenda mapema (msikitini) huwa kana kwamba
katoa sadaka ya ngamia. Na atakayekwenda katika
saa ya pili huwa ni kama aliyetoa sadaka ya
ng’ombe na atakayekwenda katika saa ya tatu
huwa ni kama aliyetoa sadaka ya kondoo mwenye
pembe. Na atakayekwenda katika saa ya nne huwa
ni kama aliyetoa sadaka ya kuku na atakayekwenda
katika saa ya tano huwa ni kama aliyetoa sadaka
ya yai. Imamu atakapotoka (atakapopanda
mimbarini) huhudhuria malaika kusikiliza dhikri
(khutba)”. Bukhaariy (841) & Muslim
(850)-Allah awarehemu.
- Kuswali
rakaa mbili wakati wa kuingia msikitini:
Imepokelewa kutoka kwa Jaabir-Allah amuwiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atakapokuja
mmoja wenu siku ya Ijumaa na ilhali Imamu
anakhutubu, basi na aswali rakaa mbili na
akhafifishe ndani yake (rakaa mbili hizo)”.
Muslim (875)-Allah amrehemu.
Hili la kuswali rakaa mbili ni iwapo khatibu hajafikia mwishoni mwishoni mwa
khutba. Na kama atakuwa amefikia mwishoni, basi
na asubiri tu kukimiwa kwa swala. Angalia rakaa
mbili hizi zitafutu kwa kukaa kwake kitako,
kwani akishakaa haitosihi kwake kuswali swala ya
suna tena. Bali kutamuwajibikia kuendelea kukaa
na kusikiliza khutba na kusubiri swala ikimiwe.
- Kukaa
kimya na kusikiliza khutba:
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Utakapo
mwambia mwenzako siku ya Ijumaa: Nyamaza, na
ilhali Imamu anakhutubu, hakika umefanya
porojo”. Bukhaariy (892), Muslim (851)
& wengineo-Allah awarehemu.
Na imekuja katika riwaya ya Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi: “Na
atakayefanya porojo, hana cho chote katika
Ijumaa yake”. Abuu Daawoud (1051)-Allah
amrehemu.
ADABU
NA TARATIBU JUMLA ZA SIKU YA IJUMAA:
Siku
ya Ijumaa ndio bora ya siku za juma (wiki) na
siku hii ina adabu na taratibu maalumu ambazo
muislamu anatakiwa kuzijua. Ili aweze kuzitia
vitendoni kiasi cha uweza wake na hizi hapa ni
baadhi yake:-
a.
Ni
suna kusoma Suratil-Kahfi (18) usiku wa kuamkia
Ijumaa na mchana mzima wa Ijumaa:
Imepokelewa
kutoka kwa Abuu Said Al-Khudriy-Allah amuwiye
radhi-kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Atakayesoma
Suratil-Kahfi siku ya Ijumaa, itamzagazia
(itamuangazia) nuru katika kipindi
kilicho baina ya Ijumaa mbili”. Nasaai-Allah
amrehemu.
b.
Kumesuniwa
kukithirisha kuomba dua usiku na mchana wake:
Imepokelewa
kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-aliitaja siku ya Ijumaa, akasema: “Umo
ndani yake muda fulani ambao mja muislamu
hauwafiki (haupati) na ilhali amesimama akiswali,
akamuomba Allah Mtukufu cho chote ila humpa”.-
Na Bwana Mtume akaashiria kwa mkono wake
akiudogesha; yaani akibainisha kwamba muda huo
ni kitambo kifupi. Bukhaariy (893) & Muslim
(852)-Allah awarehemu.
c.
Ni
suna kukithirisha kumswalia Bwana Mtume usiku na
mchana wake.
Suna
hii ni kwa mujibu wa ile hadithi ya Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-isemayo: “Hakika
miongoni mwa bora ya siku zenu ni siku ya Ijumaa,
basi kithirisheni kuniswalia ndani yake. Kwani
mimi ninaonyeshwa swala zenu (mnazoniswalia
ndani ya siku ya Ijumaa)”.
Abuu Daawoud (1047) & wengineo-Allah
awarehemu.
TANBIHI:
ü
Ni
haramu kuendelea kuuza na kununua baada ya
kuadhiniwa kwa ajili ya swala ya Ijumaa, hili ni
kufuatia kauli tukufu ya Allah: “ENYI
MLIOAMINI! KUKIADHINIWA KWA AJILI YA SWALA SIKU
YA IJUMAA, NENDENI UPESI KUMTAJA ALLAH NA
ACHENI BIASHARA...” [62:9]
ü
Ni
karaha ilekeayo katika uharamu kukeuka shingo za
watu siku ya Ijumaa kwa lengo la kwenda kukaa
mbele. Imepokelewa kutoka kwa Abdillah Ibn Yusri-Allah
amuwiye radhi-amesema: Alikuja mtu mmoja siku ya
Ijumaa akizikeuka shingo za watu na ilhali
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akikhutubu.
Mtume wa Allah akamwambia: “Kaa kitako, kwa
yakini umewaudhi (watu) na umechelewa”. Abuu
Daawoud, Nasaai, Ahmad & Ibn Khuzaymah
ameiweka katika daraja ya USAHIHI & wapokezi
wengineo-Allah awarehemu.
|