|
Kabla
hatujaanza kuzielezea na kuzibainisha nguzo za udhu moja baada ya nyingine kama
zilivyotajwa ndani ya Qur-ani Tukufu, ni vema kujiuliza nguzo ni nini ?
Makusudio
ya neno Nguzo hapa ni yale mambo ambayo dhati na hakika ya udhu unayategemea kiasi ambacho
likikosekana au kupungua moja miongoni mwao, udhu huwa ni batili kisheria. Hiyo ndiyo
maana na muradi wa nguzo na zifuatazo sasa ndizo hizo nguzo za udhu kwa utaratibu; ambazo
ni sita :
1. NIA : Hii ndio
nguzo ya kwanza ya udhu. Neno nia lina maana mbili; maana ya kilugha na maana
ya kisheria. Nia katika lugha ya kawaida ni MAKUSUDIO na katika lugha ya kisheria ni
MAKUSUDIO YA KITU/JAMBO HALI YA KUAMBATANISHA KITU/JAMBO HILO NA KITENDO CHAKE. Na nia
hukaa moyoni mwa mtu. Dalili/ushahidi wa kufaradhiwa nia ni kauli ya Bwana Mtume
Rehema na Amani zimshukie Hakika (kusihi kwa) amali kumefungamana na
nia na kila mtu (atalipwa) kwa mujibu wa nia (yake)
Al-Bukhariy na
Muslim.
Kwa kuwa udhu ni ibada
na kwa kuwa nia ndiyo hupambanua baina ya ibada na ada; ikaonyesha kuwa hili sasa ni tendo
la ibada kama josho la wajibu na hili ni tendo la ada kama josho la unadhifu. Basi kwa
mantiki hii ikawa ni lazima udhu uambatane na nia. Namna ya nia ni mtu kusema moyoni mwake
:
Nawaytu
Fardhal-udhui au
Nawaytu Raf-al Hadath au
Nawaytu istibihatas-swalaat
Nia Huletwa
wapi na mawakati gani ? Nia huletwa wakati wa kuosha fungu/sehemu ya mwanzo ya uso, kwa
kuwa hapo ndio mwanzo wa udhu yaani udhu unaanzia hapo na yaletwayo kabla ya hapo
huhesabika kama maandalizi ya kuingia ndani ya udhu.
2. KUOSHA USO
MZIMA/WOTE kwa kufuata kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu : BASI OSHENI NYUSO ZENU
[5:6]
Kuosha uso mzima ndio
nguzo ya pili ya udhu. Uso huoshwa mara moja tu kwa kuitegemea kauli ya Mtume : Udhu
ni mara moja moja. Ama kule kuosha mara ya pili na ya tatu ni suna. Imethibiti
riwaya kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehema na Amani zimshukie alitawadha
mara moja moja na akasema : Huu ndio udhu ambao Allah haikubali swala ila kwao
Na akatawadha (tena) mara mbili mbili na akasema : Huu ndio wa wa mtu ambaye Allah
atampa ujira mara mbili Na akatawadha (tena) mara tatu tatu na akasema : Huu
ndio udhu wangu na udhu wa mitume kabla yangu, basi atakayezidisha (zaidi ya) hivi au
kupunguza, (huyo atakuwa) amechupa mipaka na kufanya dhuluma
Uso ni upi ? Kisheria
uso huanzia maoteo/mameleo ya nywele za kichwa mpaka chini ya kidevu, huo ni urefu, na
upana wake ni tokea ndewe moja ya sikio hadi nyingine. Eneo lote lililo katika mipaka
hiyo, ndio huitwa uso katika sheria. Na ni wajibu kuosha kila kilichoota ndani ya mipaka
hiyo kama nyusi, kope, sharubu na ndevu. Ndevu huoshwa nje na ndani zikiwa chache. Ama
zikiwa ni nyingi zilizoshindamana kiasi cha kutokuona ngozi basi inatosha kuosha juu yake
tu.
3. KUOSHA MIKONO
HADI VIFUNDONI kwa kuitikia kauli ya Mola Mtukufu :
.NA (osheni) MIKONO YENU
MPAKA VIFUNDONI
[5:6]
Imelazimu maji yaenee
vema katika nywele na ngozi. Ukiwepo uchafu chini ya kucha ukayazuiliya maji kupenya ndani
au pete iliyobana isiyoruhusu kupenya maji, udhu hautasihi bali utakuwa ni batili.
Imepokelewa na Imam Muslim kwamba mtu mmoja alitawadha na akaacha (kuosha) sehemu ya kucha
mguuni. Mtume Rehema na Amani zimshukie akamuona na kumwambia : Rudi
ukatawadhe vizuri (kwa ukamilifu).
4. KUPAKAZA MAJI
SEHEMU YA KICHWA kwa kuitekeleza kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu :
NA MPAKE
VICHWA VYENU
[5:6]
Mapendeleo
ya kupakaza maji ni kuupitisha mkono uliorowa maji kichwani. Na namna ya kupakaza ni kama
ilivyothibiti katika hadithi sahihi iliyopokelewa na Abdallah ibn Zayd kwamba Mtume
Rehema na Amani zimshukie alipakaza (maji) kichwa chake kwa mikono yake, akaipeleka
mbele halafu akairudisha nyuma. Alianzia sehemu ya mbele ya kichwa chake kisha akaipeleka
kichogoni, kisha akairudisha pale mahala alipoanzia
5. KUOSHA MGUU HADI
VIFUNDONI kwa kulishika neno lake Mola Mtukufu
NA (osheni) MIGUU YENU MPAKA
VIFUNDONI
[5:6]
Inampasa
mwenye kutawadha ahakikishe anaosha sehemu yote iliyoainishwa katika sheria. Asiache
sehemu yeyote ile iliyo chini ya kucha. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar Allah awawie
Radhi amesema : Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie alibakia
nyuma yetu safarini, kisha akatudiriki, tukaanza kutawadha na kupaka maji miguu yetu.
Mtume akalingana kwa sauti ya juu : Adhabu kali ya moto itawathibitikia wenye kuacha
kuosha visigino, (akasema hivyo) mara mbili au tatu.
6. MPANGO/TARATIBU.
Kutungamanisha baina ya viungo hivi vinne vya udhu kwa namna ilivyokuja ndani ya Qur-ani
Tukufu, ndiyo nguzo ya sita. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema : ENYI MLIOAMINI!
MNAPOTAKA KUSWALI, BASI OSHENI NYUSO ZENU NA MIKONO YENU MPAKA VIFUNDONI, NA MPAKE (maji)
VICHWA VYENU, NA (osheni) MIGUU YENU MPAKA VIFUNDONI [5:6]
Utaratibu
ndio mojawapo ya faida tunazozipata kutokana na aya hii na pia utaratibu unapatikana
kutokana na utendaji wake Bwana Mtume kwani yeye hakutawadha ila kwa kuzitungamanisha
nguzo, moja ikifuatiwa na mwenziwe kama ilivyothibiti katika hadithi nyingi sahihi. Kwa
hivyo imempasa mwenye kutawadha mwenye kutawadha aanze na kuosha uso, kisha aoshe mikono,
halafu apakaze kichwa maji na amalizie na kuosha miguu.
Mambo
sita haya ndiyo yanayoitwa nguzo za udhu. Kusihi ama kutokusihi kwa udhu wa mtu
kunategemea sana utekelezaji wake. Akiyatekeleza yote kama itakiwavyo udhu wake ni sahihi
na akiacha mojawapo ya mambo sita haya, udhu wake ni batili. Udhu ukiwa batili basi kuwa
batili swala ni aula zaidi, kwa kuwa udhu ndio msingi wa swala.
|