|
UGOMBEZI WA NGAWIRA.
Ngawira walizozipata waislamu katika vita hivi zilikuwa ni
nyingi ikiwa ni pamoja na ngamia, vyombo, mabusati ya ngozi, nguo na ngozi
nyingi walizozichukua kwa ajili ya biashara. Ngawira hii ikawa ni fitna
inayokurubia kuwagawa maswahaba kutokana na mapenzi ya mali ambayo ni maumbile
ya kila mwanadamu. Wapiganaji waliokuwa katika medani ya vita wakipambana ana
kwa ana na adui wakiua na kuteka wakadai kwamba wao ndio wana haki zaidi ya
kupata ngawira hiyo. Wakusanyaji wa ngawira hizo wakati wapiganaji wakisonga
mbele nao wakadai kuwa na haki zaidi kuliko wengine. Walinzi wa Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-nao wakadai kuwa na haki zaidi ya kupata
ngawira hizo. Kutokana na kila kundi kudai haki zaidi ya kupata ngawira kuliko
jingine, wakaamua kulipeleka suala hilo kwa Mtume wa Allah ahukumu baina yao.
Bwana Mtume akaamuru kurudishwa kwa ngawira zote zilizomo mikononi mwa watu
ili kumpa fursa ya kuliamua suala hilo au Allah ashushe hukumu. Wakiwa katika
hali hii ya mzozo wa ngawira ndipo ikaja hukumu kutoka mbinguni:
“WANAKUULIZA JUU YA MALI YALIYOTEKWA (ngawira yagawiwe vipi?) SEMA: MALI
YALIYOTEKWA NI YA ALLAH NA MTUME WAKE (fuateni watakavyokugawieni). BASI
MUOGOPENI ALLAH NA SULUHISHENI MAMBO BAINA YENU, NA MTIINI ALLAH NA MTUME WAKE
IKIWA NYINYI NI KATIKA WANAOAMINI (kweli)”. [8:1] Haiwi kwa waislamu ila
kumtii Allah na Mtume wake, wakampa nafasi Mtume ya kuwa mgawaji wa ngawira
hizo. Bwana Mtume akawagawia mali hiyo ya ngawira na kila mmoja akaridhia kwa
kila alichopewa na Allah na Mtume wake.
Wanazuoni wa fani ya tafsiri wanazielezea sababu za
kukhitalifiana kwa maswahaba katika suala zima la ugawaji wa ngawira. Wanasema
kulikuwa na sababu kuu mbili zilizokuwa na athari kubwa katika mtafaruku huu
ambao kamwe haukutarajiwa kutokea. Haukutarajiwa kutokea si kwa Muhaajirina
ambao Allah alishuhudia kuwa wao ni waumini wa kweli kweli: “...AMBAO
WALIFUKUZWA KATIKA NYUMBA ZAO NA MALI ZAO (wakakhiari kuwacha hayo) KWA AJILI
YA (kutafuta) FADHILA ZA ALLAH NA RADHI (yake) NA KUINUSURU (dini ya) ALLAH NA
MTUME WAKE. BASI HAO NDIO WAUMINI WA KWELI”. [59:8] Wala kwa Answaar ambao
nao Allah aliwashuhudilia kwamba wao ndio waumini wa kweli: “...WAKAWAPENDA
HAO WALIOHAMIA KWAO, WALA HAWAPATI (hawaoni) DHIKI NYOYONI MWAO KWA HAYO
WALIYOPEWA (hao Muhajirina) NA WANAWAPENDELEA ZAIDI KULIKO NAFSI ZAO INGAWA
WENYEWE WANA HALI NDOGO...” [59:9]
Mojawapo ya sababu mbili hizo ni ya kiakili (kuwazika), kila
mmoja aliipupia kuipata katika ushindi huu wa kwanza dhidi ya batili.
Walifikiri ushujaa wa mtu katika uwanja wa mapambano utapimwa kwa kipimo cha
ngawira aliyopata. Kila mwenye ngawira nyingi huyo ndiye atakayeonekana kuwa
ni shujaa. Sababu ya pili ni ya kimaumbile kwamba ni maumbile ya kila binadamu
kupenda mali na kupenda kupata zaidi kuliko wenzake. Na pengine tunaweza
kusema kuwa hali ya dhiki na ufakiri waliokuwa nao waislamu wakati ule baada
ya kuporwa mali zao Makkah, inaweza kuwa ni sababu ya tatu iliyochangia mzozo
huu wa kugombea ngawira. Linalotupelekea kusema hivi ni ile riwaya
iliyopokelewa kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwatazama
maswahaba wake wakati wakitoka kwenda katika vita vya Badri, hali yao
ikamuathiri. Akawaombea Mungu, akasema: “Ewe Mola wa haki wee! Hakika waja
wako hawa ni pekupeku (hawana mnyama wa kupanda waendapo vitani) basi
(ninakuomba) uwabebe wewe (uwape mnyama wa kupanda). Hawana nguo, basi
(ninakuomba) uwavishe na wana njaa (ninakuomba) uwashibishe na ni mafakiri
basi (ninakuomba) uwakwasie (uwatajirishe) kutokana na fadhila zako”.
Sababu yo yote itakayokuwa bado ukweli utabakia kuwa pale pale
kwamba tukio hili la mzozo wa ngawira liliwatia dosari waislamu. Kiasi cha
Allah kuwalaumu na kuwakaripia kutokana na tendo lao hilo lililotishia
kuuvunja umoja wa waislamu. Tukio hili kwa upande mwingine likawa ni darsa
iliyowafundisha maswahaba khasa na waislamu wote kwa ujumla namna gani
wanatakiwa kuwa waumini wakweli. Waumini wakweli wanatakiwa kuipenda zaidi
akhera yenye maisha ya milele na starehe za kweli kuliko dunia yenye kuondoka
na yenye starehe za muda mfupi zenye ghururi na khadaa: “HAKIKA WAUMINI WA
KWELI NI WALE AMBAO ANAPOTAJWA ALLAH NYOYO ZAO HUJAA KHOFU, NA WANAPOSOMEWA
ALLAH ZAKE HUWAZIDISHIA IMANI, NA WAKAMTEGEMEA MOLA WAO TU BASI. AMBAO
WANASIMAMISHA SWALA NA WANATOA KATIKA YALE TULIYOWAPA. HAO NDIO WAUMINI WA
KWELI WAO WANA VYEO (vikubwa) KWA MOLA WAO NA MSAMAHA NA RIZIKI BORA (kabisa
huko akhera)”. [8:2-4]
UGAVI (MGAWANYO) WA NGAWIRA.
Usiku ule wa mzozo wa ngawira, Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-alilala katika bonde la Badri. Kulipopambazuka akafunga safari
kuelekea Madinah pamoja na maswahaba wake wakiambatana na mateka wao na
ngawira waliyoipata kutoka kwa mushrikina. Akaenda mpaka katikati ya safari
akapiga kambi na akaanza kazi ya ugavi wa ngawira, akawagawia wote kwa usawa.
Akampa farasi aliyeenda vitani fungu moja na mpanda farasi fungu jingine, kwa
hiyo mwenye farasi akapata mafungu mawili; fungu lake binafsi na fungu
litokanalo na farasi wake. Fungu la mashahidi akawapa warithi wao. Kuna kundi
jingine la waumini hawakuweza kushiriki katika vita hivi kutokana na majukumu
mengine waliyopewa na Bwana Mtume. Mbali na kundi hili lililopewa majukumu,
lilikuwepo pia na kundi la watu wenye udhuru mkubwa usiozuilika na Mtume
alikuwa akilijua hilo. Makundi mawili haya pia Mtume aliyagawia mafungu sawa
na yale waliyopata wapiganaji.
Wapokezi wa sira-Allah awarehemu-wanasema: Baadhi ya maswahaba
walishangazwa na kustaajabishwa na ugavi huu wa ngawira uliomlinganisha sawa
mwenye nguvu na mnyonge. Wakashindwa kuvumilia, wakamuuliza Bwana Mtume ili
kupata ufafanuzi wa ugavi wake ule usio wa kawaida. Alisema Sa’ad Ibn Abiy
Waqaasw-Allah amuwiye radhi: “Nikauliza: Ewe Mtume wa Allah, hivi unampa
mpanda farasi ambaye anawaendesha mbio makafiri sawa na kile unachompa mtu
mnyonge (anayepigana kwa miguu)?” Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-akamwambia: “Afiliwe nawe mama yako, nyinyi hamnusuriwi (hampati
ushindi) ila kwa sababu ya wanyonge wenu”. Kama kwamba kwa kauli hii ya
Bwana Mtume alitaka kuzielekeza fikra za waislamu kwamba hili (ushindi) si
suala la nguvu tu. Kwani ingelikuwa hivyo basi waliokuwa na haki na nafasi ya
ushindi walikuwa ni makafiri kutokana na nguvu ya zana bora na idadi kubwa ya
watu, lakini mbona hawakushinda?! Ugavi wa Mtume wa Allah haukuzingatia nguvu,
bali ulilenga kujenga umoja na mshikamano baina ya waislamu kiasi cha kupewa
hata wasioshiriki vitani.
Baada ya kumaliza kazi ile ya ugavi na kuwakinaisha maswahaba
juu ya ugavi wake huo, Bwana Mtume akavunja kambi na kuendelea na safari ya
Madinah. Wakaenda mpaka wakafika mahala panapoitwa ‘Rauhaa’, Mtume
akalakiwa na waislamu waliokuja kumpongeza kwa ushindi alioupata. Na wengine
wakawa wanamueleza sababu za kutokushiriki kwao vitani.
|