Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Akhlaaq-Tabia  

"Hakika si vingine nimetumwa kuja kutimiza TABIA NJEMA" Hadith Tukufu

REHEMA/HURUMA                ...Inaendelea

Uislamu ni ujumbe wa kheri na salama/amani na upole kwa jamii yote ya wanaadamu. Na Allah Ataadhamiaye amekwisha mwambia Mtume wake: “NASI HATUKUKUTUMA ILA UWE NI REHEMA KWA WALIMWENGU WOTE”. [21:107]

Na sura zote za Qur-ani Tukufu zimeanzwa na “BISMILLAAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM” – Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Lakini mbwa mwitu walio jificha nyuma ya sura ya binaadamu, hawataki ila kuikingama rehema/huruma huru hii. Na wakaweka miamba katika mapito yake ili kuzuia mito ya rehema/huruma isiwafikie watu. Kwa minajili hiyo basi, watu waangamie katika mawanda ya udangana na ujaahili kutokana na kuyakosa maji ya mito ya rehema. Kwa ajili hiyo basi, ndio ikawa hapana budi kuviondosha vikwazo hivyo na kuwafanyia ugumu wadau wa vikwazo hivyo. Na siku utakapo katika upinzani na ukaidi wao huo, ndipo rehema hii jumuishi itakapo waenea. Na rehema hii haina mapungufu, lakini hakika si vinginevyo, mapungufu yako kwa yule aliye inyima nafsi yake fungu katika rehema hiyo. Hivi ewe ndugu msomaji mwema, huoni ya kwamba rehema ya Allah imevienea vitu vyote! Lakini pamoja na ukweli huo basi, rehema hiyo hatoipata mshirikina wala mkanusha Mungu: “...NA REHEMA YANGU IMEENEA KILA KITU. LAKINI NITAWAANDIKIA KHASA WANAO MCHAMNGU, NA WANAO TOA ZAKA, NA WALE AMBAO WANAZIAMINI ISHARA (aya) ZETU. AMBAO KWAMBA WANAMFUATA HUYO MTUME, NABII, ASIYE SOMA WALA KUANDIKA...”. [07:156-157]

Kama unavyo sema: Ukumbi huu una uwezo wa kuchukua watu elfu moja, lakini haruhusiwi kuingia humo ila tu yule aliye na tiketi. Basi baadhi ya watu watakao kataa kukata tiketi za kuingilia na hilo likapelekea wao kuzuiwa kuingia ukumbini, kwa sababu ya kutokuwa na tiketi. Wakabakia nje, kubakia kwao huko nje, hakuwi ni dosari katika ukunjufu (ukubwa) wa ukumbi.

Na mfano wa hilo, ni kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Umati wangu wote wataingia peponi, ila yule atakaye kataa. Wakauliza (maswahaba): Ni nani huyo atakaye kataa? Akajibu: Atakaye nitii, huyo ataingia peponi. Na atakaye niasi, huyo ndiye aliye kataa”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Na hupata kutokezea mara nyingine rehema ya kweli, ikavaa chapa ya ukatili, lakini kihakika si hivyo kabisa. Sote tumepata kushuhudia watoto wetu wakisindikizwa kwa bakora kwenda shule na wanahifadhi masomo yao kutokana na ukali wa mwalimu. Hili katika taswira yake ya nje linaweza kuonekana kuwa ni ukatili kwa watoto, ambao wanahitajia mno huruma ya wazazi na jamii kwa ujumla. Lakini sivyo kabisa, kwani lau watoto wetu hao wataachwa kufuata matashi na mapenzi yao hayo ya kitoto; yasiyo jua maslahi na manufaa yao. Basi bila ya shaka, wangeli angamizwa na pumbao na mchezo na wangeli fikia umri wa majukumu (ujana) wakiwa hawana walijualo si tu katika dini yao bali pia hata katika Dunia yao. Na tabibu pale anapo upasua mwili wa mgonjwa, hutumia kisu chake kikali ili kukata nyama. Na pengine hulazimika kuvunja mfupa na hata kukata kiungo. Hili nalo laweza kuonekana kuwa ni ukatili, lakini ukweli ni kwamba daktari hafanyi hivyo ila ni kwa kumuhurumia mgonjwa na kutaka arejewe na afya yake aliyo pokonywa na ugonjwa huo.

Haikuwa rehema ni hisia huba zisizo ambatana na akili na wala si upendo unao kinzana na uadilifu na nidhamu/utaratibu. La hasha! Si hivyo kabisa, hakika rehema ya kweli, ni zile hisia zinazo zichunga haki zote hizi. Bila ya shaka mandhari ya mtu aliye hukumiwa kunyongwa, akiwa ananing’inia manyongeoni ilhali mwili wake ukiwaya waya hewani. Na macho yake yaingiayo kiza yakiutamani mwanga na kutafuta uwokovu. Hayo ni mandhari yanayo vuta hisia za huruma, na lau hisia hizo zingeli itikiwa haraka na muuaji akaachiwa huru, basi kwa yakini ardhi ingeli jaa fujo/ghasia na uhovyo hovyo. Hiyo ndio huruma ya yale yanayo itwa mashirika ya kutetea haki za binaadamu, yanayo piga kelele za kufutwa kwa adhabu ya kifo. Hivi ni kweli binaadamu ana huruma zaidi kwa binaadamu mwenzake, kuliko Yule aliye waumba?! Hebu tuwe wakweli na tuwe huru, tusiongozwe na akili za viumbe kama sisi. Tukubali kuwa rehema/huruma ya kweli imo ndani ya kutozipa nafasi hisia kama hizo “MTAKUWA NAO UHAI MZURI KATIKA KULIPIZA KISASI ENYI WENYE AKILI, ILI MSALIMIKE”. [02:179]

Enyi wanaadamu! Hakika rehema ya Allah kwenu ni kubwa kwa hii hukumu ya kisasi. Kwa fadhila ya kisasi jamii yenu ina hakika kupata maisha ya amani na salama. Haya ni kwa kuwa mwenye kutaka kuua akijua kuwa naye atauawa, atajizuia kutenda alilo likusudia. Kwa hiyo yeye na yule ambaye angeli uawa wanahifadhika. Wenye akili na wazingatie faida ya sharia ya kisasi, hilo litawapelekea kuutambua upole wa Allah kwao kuendea njia ya uchaMngu, na kuzifuata amri za Allah.

Hakika ukatili unao laaniwa na kushutumiwa na Uislamu, ni ule ukavu/ugumu uliomo ndani ya nafsi ambao hauna mafungamano na mantiki wala uadilifu. Hakika ukatili huo ni maovu yaliyo jaa ubaya/uovu na adha/kero/bughdha, yanayo anzishwa na ubinafsi/umimi menyu na matamanio pofu. Ama rehema/huruma, hakika hiyo ni athari ya uzuri wa Kimungu, iliyo salia katika tabia/hulka/silka ya watu, inayo waongozea na kuwapelekea kwenye wema. Athari hiyo ndio inayo watunukia katika nyakati za mizozo songefu, upepo roho mwanana unao changamsha maisha na kuburudisha nyoyo. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Hakika Allah Ataadhamiaye siku alipo umba mbingu na ardhi, (pia) aliumba rehema mia moja. Kila rehema moja ni tabaka baina ya mbingu na ardhi. Akaweka katika ardhi rehema moja kutoka kwenye (tabaka) hilo. Katika hilo mzazi humuonea huruma mwanawe na mnyama mwitu na ndege (huoneana huruma) wao kwa wao”. Muslim-Allah amrehemu.

Kama ambavyo inavyo mea na kukua akili kwa kupata elimu/maarifa mbali mbali, ndivyo hivyo rehema hii nayo humea na kukua kwa njia mbali mbali na ikatanuka. Ama ikiachwa hivi hivi tu, basi hunyauka na hatimaye hufa na hapo ndipo mwenye nayo huwa kuni ya Jahannamu. Imepokewa kutoka kwa Sayyidna Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia ambaye yeye ni Mkweli; mwenye chumba hiki, Abul-Qaasimu-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Haiondolewi rehema ila kwa mtu muovu”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.

Na Uislamu umewatanabahisha Waislamu ya kwamba yapo makundi maalumu ya watu ambao jamii inatakiwa iwape ziada ya rehema/huruma na uangalizi. Miongoni mwao ni “Dhawil-Arhaam” – hawa ni ndugu wa umamani. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Wenye kuwahurumia (wenzao) watarehemewa na Allah Ataadhamiaye, waoneeni huruma walioko ardhini atakuhurumieni aliyeko mbinguni. Ar-rahimu – uzawa ni udugu utokanao na Rahmaani – Mwingi wa rehema. Atakaye uunga, ataungwa na Allah na atakaye ukata, naye atakatwa na Allah”. Tirmidhiy-Allah amrehemu.

Na ni wajibu wa muislamu kutekeleza haki za ndugu/jamaa zake na auimarishe udugu wake wa damu kwa mapenzi ya daima. Na wanao ustahiki mno wema wake na ambao wanatakiwa kupewa kipaumbele kabla ya watu wengine, ni wazazi wake wawili, Allah Ataadhamiaye anatuagiza: “NA WAINAMISHIE BAVU LA UNYENYEKEVU KWA KUWAONEA HURUMA. NA USEME: MOLA WANGU MLEZI! WAREHEMU KAMA WALIVYO NILEA UTOTONI”. [17:24]

Kisha wanao fuatia ni wanawe. Imepokewa kutoka kwa Al-Baraau, amesema: “Abubakar alikwenda kwa (binti yake) Aysha akiwa amepatwa na homa, akasema: Unajionaje ewe binti yangu na akambusu shavuni”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Na lionekanalo kwa watu mafedhuli ni kwamba hisia/mawazo yao hayachukui nembo hii ya upole na huruma, kwani katika hulka na maneno yao kuna ukavu karahishi. Imepokewa kutoka kwa Sayyidna Abu Huraira-Allah amuwiye radhi: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimbusu Hasan au Husein bin Aliy, akiwa na Al-Aqrau bin Haabis At-tamiimiy. Al-Aqrau akasema: Mimi nina watoto kumi na kamwe sijambusu yeyote miongoni mwao. Mtume wa Allah akamuangalia na kusema: “Asiye na rehema harehemewi”.

Na katika riwaya/upokezi mwingine alisema: “Mimi similiki kwako Allah kuondosha rehema moyoni mwako”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Na imepokewa kutoka kwa Sayyidna Anas-Allah amuwiye radhi: “Tuliingia pamoja na Mtume wa Allah kwa Abu Saifi muhunzi na alikuwa ni baba wa kunyonya wa Ibrahimu; mtoto wa Mtume wa Allah. Mtume wa Allah akamtwaa mwanawe akambusu na kumshumu. Kisha tukaenda tena nyuumbani kwake siku nyingine na Ibrahimu akiwa katika hali ya kukata roho, macho ya Mtume wa Allah yakaanza kububujika machozi. Ibn Auf akauliza: Ewe Mtume wa Allah, nawe (pia unalia)? – kama kwamba yeye aliona ajabu Mtume kulia – (Mtume) akasema: “Ewe mwana wa Auf! Hakika hayo (machozi) ni rehema”. Kisha akazidi kububujikwa na machozi na akasema: “Hakika jicho linatoa machozi na hakika moyo unanyenyekea. Na wala hatusemi ila yale yanayo mridhi Mola wetu na hakika sisi tuna huzuni kuu kutengana nawe, ewe Ibrahimu”. Muslim-Allah amrehemu.

  



 | Tuandikie |