|
Kwanza kabisa
kabla hatujaanza kuzielezea haki hizi ni vema tukatambua kuwa haki za mume
kwa mkewe zinakomelea au ziko katika nafsi/dhati ya yule mke mwenyewe. Na
wala hazipindukii katika mali yake katika kipindi chote cha uhai wao kama
inavyokuwa kwa mke. Yeye mke ana haki ya nafsi na mali kwa mumewe lakini
mume ana haki ya nafsi tu kwa mkewe katika kipindi cha uhai. Haki ya mali
anaipata katika kipindi cha umauti wa mweziwe tu ambayo hiyo ndiyo
ijulikanayo kama haki ya mirathi. Haki hii inamuhusu kila mmoja wao
pindipo mwenziwe anapomtangulia katika maisha ya akhera. Hivi ndio kusema
kuwa mume ana haki nafsi tu kwa mkewe na wala hana haki mali kwa mujibu wa
sheria toharifu. Kwa mantiki hii mume hana haki na wala haimjuzii kisheria
kuchukua au kutumia mali ya mkewe ila kwa kibali na radhi ya mkewe huyo.
Mali ya mke kwa mume hukumu yake ni kama ilivyo mali ya mtu kando.
Kadhalika si halali mume kumlazimisha mkewe kujihudumia au kuihudumia
familia hata akiwa tajiri namna gani. Kwani katika uislamu hilo ni jukumu
la mume na sio la mke, mke afanye hivyo kwa mapenzi na matashi yake tu na
sio kwa njia ya uwajibu au kulazimishwa. Uislamu unamtaka mume kuelewa
kuwa mkewe ni mtu huru mwenye haki ya kuchuma, kumiliki na kuiendeleza
mali yake. Sambamba na kuitumia kwa maslahi yake binafsi yeye mwenyewe na
familia yake kwao anakotoka au na familia yenu wewe mume na yeye mke
katika mazingira ya khiari. Hakuna kabisa mafungamano yo yote baina ya
mume na mali ya mkewe katika kipindi cha uhai. Ndoa haimpi mume kibali cha
kuhodhi na kutumia mali ya mkewe bila ya ridhaa yake kwa njia yo yote ile.
Huu ndio uislamu, tukubali au tukatae utabakia hivyo hivyo na wala hauwezi
kubadilishwa na matashi au mazoea yetu.
Baada ya tanbihi
(uzindushi) hii, hebu sasa tuiangalie nafasi/thamani ya mwanamke katika
ulimwengu huu. Kisha ndio tuanze kuzielezea haki za mumewe zilizo juu
yake, yaani wajibu wake kwa mumewe huyo. Imepokelewa na Abdillah Ibn Amri
Ibn Al-Aaswi-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Dunia ni starehe na bora ya starehe zake ni mwanamke
mwema”.
Muslim &
Ahmad
Hadithi inamtaja
mwanamke mwema na wala haimtaji mwanamke mzuri wa sura/umbo kuwa ndio bora
ya starehe ya dunia. Wewe miliki nyumba nzuri, shamba, magari ya kifahari,
biashara kubwa , umaarufu au cheo, bado utakuwa haujastarehe kama
hukumpata mwanamke mwema. Sasa hebu tujiulize sote kwa pamoja, ni yupi
huyu mwanamke mwema aliyepewa hadhi hii kuu? Hapana shaka kama
tukitafakari pamoja kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya uislamu tutaelewa
kuwa mwanamke mwema ni yule anayezichunga haki za Allah Mola Muumba wake.
Na kuzipa nafasi ya kwanza kabla ya zile za mumewe hazijachukua nafasi ya
tatu baada ya haki ya Mtume wa Allah. Miongoni mwa sifa za wanawake wa
aina hii ni pamoja na:-
- Kulazimikiana na nyumba yake
ili aweze kupata fursa ya kutosha ya kulitekeleza jukumu na wajibu
wake kama mama na mlezi wa familia.
- Kutotoka hovyo nyumbani ila
kwa haja maalumu inayoambatana na idhini na ridhaa ya mumewe kama
kiongozi mkuu wa familia.
- Kuwa na moyo na ari ya
kutengenea kwa hali yake na hali ya familia sambamba na kuwa na mfumo
mzuri wa malezi ya watoto. Mfumo utakaozalisha wanajamii wema; baba na
mama wema wa kesho.
- Kuwa na pupa ya kuhakikisha
kuwa familia inaishi na kuifurahia hali na mazingira ya amani
yatakayoiletea ufanisi na mafanikio.
- Kuishi ndani ya wigo wa
maadili ya dini yake kwa kutekeleza maamrisho yake na kuacha makatazo
ya Allah Mola Muamrishaji na Mkatazaji. Sambamba na kupanda mbegu hii
njema ya maadili haya ya kidini kwa familia yake.
- Kukinahi na kutosheka na
riziki waliyogawiwa na Allah, kwani tamaa ndio chanzo kikuu cha
matatizo katika dunia hii.
Ziada ya yote
haya, mwanamke hawezi kupata daraja na utukufu huu wa kuwa mwanamke mwema.
Mwenye thamani kuliko starehe zote za dunia mpaka kwanza azijue haki za
mumewe; mwenza na mwandani wake katika maisha. Hatua inayofuatia baada ya
kuzijua haki hizo ni kuzitekeleza ipasavyo. Tena bila ya kinyongo au kuona
vibaya huku akiamini kuwa huo ni wajibu wake umpasao kuutekeleza. Na
kwamba kuutekeleza wajibu wake huo ni kuitekeleza sehemu ya dini yake.
Miongoni mwa wajibu wa mke ambao kwa mume ni haki ni mambo yafuatayo:-
- Kuipa umbele haki ya mume
kuliko haki yake binfsi seuze haki za jamaa zake wengine. Hii ni kwa
sababu haki ya mume kwa mkewe iko juu ya haki nyingine zote: “...NA
WANAUME WANA DARAJA ZAIDI KULIKO WAO...” [2:228]
- Ajiandae na kuwa tayari wakati
wo wote kumpa mumewe haki yake ya unyumba atakapoihitaji ila katika
siku siku za hedhi au nifasi na katika hali ya maradhi. Haijuzu kabisa
kwa mwanamke muumini kumnyima mumewe haki yake hii nje ya mazingira
haya tuliyoyataja (hedhi/nifasi/maradhi). Kitendo cha kunyima mume
haki yake hii humpelekea mke kuwa katika hatia ya dhambi na kulaaniwa
na malaika. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye
radhi-amesema: Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“Mume atakapomuita mkewe kitandani, akakataa (mwanamke huyo)na mume
akalala katika hali ya kumghadhibikia. Hulaaniwa
(mwanamke huyo) na malaika mpaka kunapambazuka asubuhi”.
Bukhaariy &
Muslim.
Na imepokewa
kutoka kwa Twalqi Ibn Aliy-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mume atakapomuita mkewe kwa
ajili ya haja yake, basi na amuendee (amuitikie) hata kama akiwa kwenye
tanuri (jikoni anapika)”.
Tirmidhiy &
Nasaai
Ni dhahiri
shahiri kwamba haki hii; haki ya jimaa (unyumba) ni miongoni mwa haki
muhimu kabisa za mume kwa mkewe. Kitendo cha mke kuijali, kuishughulikia
na kisha kumkidhia mumewe haja yake hii ya kimaumbile kitandani. Ni
sababu kuu na nguzo muhimu kabisa ya ufanisi na mafanikio katika maisha
ya ndoa. Kwa upande wa pili kuzembea kwa mke na kuipuuzia haki hii ya
mumewe ni chanzo kikuu cha magomvi na mtafaruku. Ambao mara nyingi ndio
huwa sababu ya kutengana (talaka) kwa wawili hawa. Hawezi kuujua uzito
wa kadhia hii ila mwanandoa, asiye mwanandoa hawezi kuona wala kuujua
uzito na umuhimu wa suala hili. Tatizo hili huweza kusababisha mume kuwa
na nyumba ndogo au mke kuwa na “buzi” ikiwa mume hampi nafasi ya
kushibisha kiu yake ya kimaumbile (mapenzi).
- Kisheria mke hana haki ya
kujikurubisha kwa Mola wake kwa kufunga swaumu za suna, yaani
zisizokuwa Ramadhani au zile za nadhiri ila kwa idhini ya mumewe. Hii
ni kwa sababu swaumu hii itamnyima mume haki yake ya kustarehe na
mkewe wakati wa mchana. Kwa mantiki hii ni lazima ipatikane idhini ya
mume; idhini itakayoashiria kukubali kusamehe haki yake hii. Hivi
ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye
radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Haimuhalalikii mwanamke swaumu (ya suna) na ilhali mumewe yupo
(hayuko safarini) ila kwa idhini yake. Na wala asimkaribishe mtu
nyumbani kwake ila kwa idhini yake (mumewe)”.
Bukhaariy &
Muslim
- Mke hana rukhsa kutoa nyumbani
kwake cho chote kumpa yo yote ila kwa idhini ya mumewe. Hata kama huyo
anayempa ni jamaa yake huyo mume seuze jamaa zake yeye mke. Ikiwa mke
atatoa bila ya idhini ya mumewe, hata kama ni kwa nia ya sadaka. Hana
atakachokipata zaidi ya dhambi na ujira/thawabu za utoaji huo zitakuwa
ni katika fungu la mume. Naam, inamjuzia kutasadaki chakula cha mumewe
tu bila ya kufanya ubadhirifu. Hili ni kwa mujibu wa riwaya
iliyopokelewa kutoka kwa Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema:
Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Mwanamke
atakapotasadaki sehemu ya chakula cha mumewe bila ya israfu. Atapata
ujira wake (sadaka hiyo) na mumewe atapata ujira wa kukichuma (chakula
hicho)...”
Bukhaariy
- Mke hana haki ya kutoka nje ya
nyumba yake, kusafiri au kufanya kazi ila kwa idhini ya mumewe.
Kadhalika hana rukhsa ya kuchanganyika na kufanya ushoga na wanawake
wenziwe asiowapenda mumewe kutokana na tabia na mienendo yao mibaya.
- Mke akinahi na atosheke na
riziki aliyoruzukiwa mumewe na Allah Mola Mwenye kuruzuku bila ya
mkabala. Asimkorofishe wala asimuudhi mumewe kwa sababu tu ya dhiki ya
maisha au hali duni waliyo nayo. Bali anachotakiwa kufanya katika hali
hiyo ni kumuonyesha mumewe uvumilivu wake, akamsikizisha maneno mazuri
anaporudi nyumbani jioni akitokea kazini hali ya kuwa yu taabani. Ampe
mumewe ushauri wa nini cha kufanya ili kujikwamua na hali hiyo ya
dhiki iliyowagubika. Ni lazima mke aonyeshe kuithamini taabu na uchovu
wa mumewe katika kuitafuta riziki yao. Na ajiepushe kumkalifisha
mumewe zaidi ya uweza wake. Kwani kutokana na mapenzi ya mume kwake na
kwa kuchelea kumuudhi mkewe, mume anaweza kujitumbukiza katika chumo
la haramu kwa ajili tu ya kumridhisha mkewe. Mke ajitahidi kuishinda
nafsi yake ili asimfikishe mumewe mahala pabaya hapo. Na amuusie
kusubiri na kukinahi sambamba na kuzidisha juhudi katika kufanya kazi
huku akimuomba Allah amkunjulie na kuwawepesishia riziki yao.
Kadhalika mke asiache kumtahadharisha mumewe na kuchuma kwa kupitia
njia za haramu. Hii ndio iliyokuwa ada na dsturi ya wanawake wema wa
zama njema za uislamu-Allah awarehemu. Alikuwa mmoja wao akimwambia
mumewe anapotoka nyumbani kwake kwenda shughulini kwake: (Tahadhari na
chumo la haramu, kwani sisi tunaweza kusubiria njaa na dhara wala
hatuwezi kusubiri juu ya (kuingia) motoni (kutokana na kula/kuvaa
haramu).
- Ni wajibu wa mke kujihifadhi
na kujistiri na kutodhihirisha uzuri wa mwili wake kwa mtu asiye
maharimu yake ili kuchunga heshima yake, familia yake na hadhi ya
mumewe: “...BASI WANAWAKE WEMA NI WALE WENYE KUTII, WANAOJIHIFADHI
(hata) WASIPOKUWAPO (waume zao) KWA KUWA ALLAH AMEWAAMRISHA
KUJIHIFADHI...” [4:34]
Ni haramu
mwanamke kuonyesha sehemu ya mwili wake isiyotakiwa kuonekana kisheria
ila na mumewe au kumvulia nguo asiye mumewe. Huko ni kumnyima mumewe
haki yake na kumpa asiyestahiki. Jambo hili linausisha uvaaji wa nguo
fupi au nyepesi zinazoonyesha rangi ya mwili. Au zenye kubana mno
kiasi cha kuliacha umbo lake zuri kuonekana na kila mwenye macho. Ni
vema mke akatambua kwamba kitendo chake hiki ni chemchem kuu ya fisadi
na uharibifu katika ardhi. Imepokelewa kutoka kwa mama wa waumini
(mkewe Bwana Mtume); Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Asivue mwanamke
nguo zake katika nyumba isiyo ya mumewe ila atakuwa amevunja sitara
baina yake na Mola wake”-Yaani atakuwa amejifedhehesha na kuvunja
heshima na utukufu wake.
Ahmad,
Tirmidhiy & Abuu Daawoud
|