Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

MAJADILIANO NA WATU WA KITABU   Inaendelea...

  1. Kusema kwao ya kwamba Allah hakumteremshia mwanaadamu chochote, na Allah kumlakinia (kumfundisha) Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-jibu rejezi linalo ufedhehi uongo wao.

Allah Ataadhamiaye anasema: “NA HAWAKUMKADIRIA ALLAH KWA HAKI YA KADRI YAKE, WALIPO SEMA: ALLAH HAKUMTEREMSHIA MWANAADAMU CHOCHOTE. SEMA: NANI ALIYO TEREMSHA KITABU ALICHO KUJA NACHO MUSA, CHENYE NURU NA UWONGOFU KWA WATU. MLICHO KIFANYA KURASA KURASA MKIZIONYESHA, NA MENGI MKIYAFICHA. NA MKAFUNZWA MLIYO KUWA HAMYAJUI NYINYI WALA BABA ZENU? SEMA: ALLAH. KISHA WAACHE WACHEZE KATIKA POROJO LAO”. [06:91]

Wanazuoni wetu-Allah awarehemu-katika kuelezea sababu za kushuka kwa aya hii, wametaja riwaya nyingi. Miongoni mwazo, ni kwamba Maalik bin As-swaif; Muyahudi, huyu alizozana na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika mas-ala fulani. Mtume wa Allah akamwambia: Mimi ninamuapia Allah wewe hupati (aya) katika Taurati (inayo sema) kwamba Allah anamchukia mtu mzima mnene – na huyu Ibn As-swaif alikuwa ni mnene. Ndipo (Ibn As-swaif) akasema: “Allah hakumteremshia mwanaadamu chochote”. Baadhi ya wafuasi wake wakasema: Ole ni wako na wala si wa Musa. Ndipo Allah Ataadhamiaye akaiteremsha aya hii.

Maana ya aya:

Ni kwamba Mayahudi hawa hawakumuadhimisha Allah Ataadhamiaye ipasavyo kumuadhimisha. Na hawakumjua ipasavyo kumjua katika kuwaonea kwake upole na huruma waja wake. Lakini wao wakazinyongesha kwa kiwango kikubwa haki zake na hilo likawapelekea kupotea upotovu mkubwa, kwa kuwa wao walikanusha kuletwa kwa Mitume na kuteremshwa kwa vitabu. Ndipo wakayasema yale maneno yao mabaya, nayo si mengine ila ni kule kudai kwao ya kwamba Allah Ataadhamiaye hakumteremshia mwanaadamu chochote. Walilo likusudia kwa maneno yao haya mabaya: Ni kuutukana utume wa Nabii Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-na kuitukana Qur-ani kuwa haitoki kwa Allah.

Allah Ataadhamiaye akamuamrisha Mtume wake awajibu kwa majibu rejezi yatakayo zitia ububu ndimi zao, akasema: “SEMA: NANI ALIYO TEREMSHA KITABU ALICHO KUJA NACHO MUSA, CHENYE NURU NA UWONGOFU KWA WATU”. Yaani: Sema, ewe Muhammad! Waambie hao wanao dai ya kwamba Allah hajamteremshia mwanaadamu chochote. Basi hebu waulize ni nani aliye iteremsha Taurati, ambayo ni kitabu alicho kuja nacho Musa, kikiwa ni “NURU NA UWONGOFU KWA WATU”. Yaani: Ni mwangaza unao zagaza kutoka kwenye kiza cha ujaahili, tena ni uwongofu unao hifadhi dhidi ya batili na upotofu.

Kisha Allah-utakati wa mawi ni wake-akabainisha upotoshaji wa maana na ubadilishaji wa maana ulio fanywa na wapingaji kwenye vitabu vyake, akasema: “MLICHO KIFANYA KURASA KURASA MKIZIONYESHA, NA MENGI MKIYAFICHA”. Yaani: Mnakifanya kitabu hiki ambacho Allah Ataadhamiaye amekiteremsha kuwa ni nuru na uwongofu, mnakifanya kuwa kurasa kurasa zilizo tapanyika. Mnafanya hivyo ili mpate upenyo wa kukidhihirisha kile mnacho kitaka nyinyi kidhihirike na kifahamike na watu katika kurasa hizo. Na myafiche mengi katika kurasa hizo kwa mujibu wa matashi ya nafsi zenu zenye maradhi na matamanio yenu yenye madhambi.

Muradi/mapendeleo ya sentensi hii tukufu, ni kuwalaumu na kuwaumbua wale wanao badilisha vitabu vya Allah. Ambao makusudio yao ya nyuma ya pazia la upotoshaji/ubadilishaji huo, ilikuwa ni kuutukana utume wa Nabii Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Na kupata njia ya mkato ya kuyafikia matashi na matamanio yao.

Na kauli yake Allah “NA MKAFUNZWA MLIYO KUWA HAMYAJUI NYINYI WALA BABA ZENU”. Yaani: Na mkafundishwa kupitia ulimi wa Muhammad, yale ambayo nyinyi wala baba zenu hamkuwa mkiyajua. Mkafundishwa maarifa/elimu ambazo mtu mweledi hapati shaka kwamba elimu hizo ni uteremsho wa Mungu Mwenyezi.

Na kauli yake Allah: “SEMA: ALLAH. KISHA WAACHE WACHEZE KATIKA POROJO LAO”. Yaani: Sema ewe Muhammad, uwaambie hao wakanushaji: Allah Ataadhamiaye ndiye ambaye aliye mteremshia Musa kitabu. Kisha baada ya kuwaambia maneno hayo ya upambanuzi, waache katika batili yao wacheze na porojo lao.

Na Allah kumuamrisha Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-awajibu, amri hiyo inaleta hisia ya kwamba jawabu ni lazima na hakuna imkani ya njia nyingine. Na ni uzindushi ya kwamba wao wamepigwa na butwaa kiasi cha kushindwa kutoa jawabu.

Kwa maelezo haya basi, aya tukufu inakuwa imewarudi kwa jawabu madhubuti lifikishalo mno ujumbe. Jawabu lililo waacha wao katika utoshewa/udangani na lililo wafanya watu weledi kustaajabu kuipinga kwao hata Taurati ambayo Allah Ataadhamiaye alimteremshia Nabii Musa-Amani imshukie-kwa ajili ya kuwaongoza wao.

 

 | Tuandikie |