|
SIRA NI NINI?
Sira ni fani
inayojishughulisha kuelezea maisha ya Nabii Muhammad tangu kuzaliwa mpaka kufa kwake,
ikiwa ni pamoja na malezi na makuzi yake, wasifu wake wa kimaumbile, tabia zake, harakati
zake katika kuufikisha ujumbe wa Uislamu kwa ummah, mahusiano yake na watu na mataifa
mbalimbali. Pia sira inaelezea hali ya ulimwengu kijamii na kiitikadi kabla na baada ya
kuja Nabii Muhammad, kadhalika inataja maisha na utawala wa Makhalifa waongofu baada ya
Mtume.
MADHUMUNI NA FAIDA ZA SIRA
Fani ya Sira inalenga kumfahamisha Muislamu:-
- Taswira na mfumo mzima wa Uislamu unatolewa na kutafsiriwa na maisha ya Mtume.
- Maisha ya Nabii Muhammad ndio kigezo na mfano mwema wa kuigwa na kufuatwa ili kuweza
kupata mafanikio Duniani na Akhera. Mwenyezi Mungu atuambia:-"BILA SHAKA MNAO MFANO
MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU
"(33:21)
- Muislamu apate katika maisha ya Nabii Muhammad kitu kitakachomsaidia kuifahamu Qur-ani
kwani aya nyingi za Qur-ani zinafasiriwa na kuwekwa wazi na matukio yaliyotokea katika
uhai wa Mtume.
- Sira inaonyesha ni njia na mbinu zipi alizozitumia Mtume mpaka akaweza kuusimamisha
Uislamu katika ulimwengu uliokuwa umefunikwa na kiza totoro cha ushirikina.
- Sira inaonyesha ni jinsi gani Mtume alivyoyatatua matatizo na vikwazo mbalimbali vya
ndani na nje alivyokumbana navyo katika kumfikisha ujumbe wa Allah kwa watu wote.
Hizi ni baadhi tu ya faida zinazopatikana katika kuisoma na kuifuata sira ya Bwana
Mtume.
SURA YA KWANZA
SOMO LA KWANZA
i )BARA ARABU WAKATI WA MTUME NA
WAKAZI WAKE
Bara Arabu lipo upande wa kusini wa Bara la Asia. Bara hili ndilo
makazi ya Waarabu tangu kale na mpaka sasa kinaishi humo kizazi cha Waarabu. Maelfu ya
miaka Waarabu wa kale wliishi maisha yaliyofanana na maisha yetu ya leo ukiondoa tofauti
chache zilizokuwepo. Walikuwepo miongoni mwao wakazi wa mijini waliostaarabika na
kuendelea.
Ama zile tofauti chache zilizokuwepo kati ya maisha ya Waarabu wale wa kale na maisha
yetu ya leo ni kwa upande wa kidini (kiitikadi) na kijamii. Waarabu wa kale waliishi
katika enzi/zama za viza zilizotawaliwa na itikadi potofu za kidini na desturi mbaya.
Baada ya kudhihiri Uislamu hali mbaya hizi zilibadilika na Waarabu wakaanza kuishi katika
zama za uchanuzi wa dini ya Kiislamu katika mji wa Makkah kisha ikaenea katika pande zote
za Bara Arabu Uislamu ulizibadilisha hali na kupigiwa mfano.
ii) NCHI YA HIJAZI NA KUANZISHWA MJI WA MAKKAH
Mji wa Makkah ndio kitovu na chimbuko la kuenea dini ya Kiislamu.
Mji huu upo katika nchi ya Hijazi, nchi ambayo imechukua eneo kubwa la Bara Arabu. Nchi
hii ya Hijazi ilikaliwa na makabila mengi ya Kiarabu, kabila mashuhuri zaidi lilikuwa ni
Qurayshi.
Historia ya mji wa Makkah na kuanzishwa kwake inaanzia pale alipofika katika mji huo
kwa mara ya kwanza Nabii Ibrahimu Amani na Rehma za Allah zimshukie -
akitokea nchi ya Palestina akiwa pamoja na mkewe Haajira na mwanawe Ismail. Wakati
huo mji wa Makkah ulikuwa ni jangwa tupu lililozungukwa na majabali. Nabii Ibrahimu
akamuacha mkewe na mwanawe katika jangwa hilo tupu lisilo na mimea na kurejea Palestina.
Kabla ya kufunga safari ya kurudi Palestina Nabii Ibrahimu alimuomba Mola wake Mtukufu
rehema zake ziyatawale maisha mapya ya mkewe na mwanawe jangwani hapo na Mola Muumba
aliipokea na kuikubali dua ya Mtume wake kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani. Mwenyezi Mungu
akamchimbulia mama Haajira na mwanawe Ismail chemchem ya Zamzam katika ardhi kame ya
jangwani.
Wasafiri wapitao njia ile walipokiona kisima cha Zamzam walikwenda mahala pale na
kuamua kuishi kandokando ya chemchem ile, hii ni kutokana na shida sugu ya maji jangwani.
Tangu wakati huo kitongoji hicho kikaanza kustawi mpaka kikawa ndio kitongoji mama cha
nchi ya Hijazi. Mtoto Ismail alipofikia umri wa kuoa alioa katika makabila yale ya Waarabu
waliokuja kukaa pale na kuuanzisha mji wa Makkah. Akajaaliwa kupata watoto.
Ibrahimu baba yake Ismail akawa anafanya ziara za mara kwa mara kujulia hali mkewe,
mwanae na wajukuu zake. Katika mojawapo ya ziara zake hizi ndipo Mwenyezi Mungu
alipompelekea wahyi wa kuijenga A-kaaba. Ibrahimu na mwanawe wakaitekeleza amri ya Mola
wao wakaijenga Al-kaaba. Mwenyezi Mungu akamuamrisha Nabii Ibrahimu awaite watu kuja
kuhiji na kufanya ibada katika nyumba yake hiyo tukufu. Ujenzi huu wa nyumba tukufu ya
Mwenyezi Mungu na ibada tukufu ya Hijjah ndivyo vilivyoufanya mji wa Makkah kuwa ni mji
mtakatifu. Hii ndio historia fupi ya kuasisiwa mji wa Makkah.
iii) KABILA LA QURAYSHI NA UTAWALA WAKE
Makabila mengi yalipatikana kutokana na kizazi cha Ismail mwana
wa Nabii Ibrahimu katika nchi ya Hijazi, kabila la Qurayshi ndilo lililokuwa mashuhuri
zaidi. Baadhi ya makabila haya yalikuwa yakimuabudu Mwenyezi Mungu kupitia mafundisho ya
dini ya Nabii Ibrahim- Amani ya Allah imshukie. Uongozi wa kidini na kibiashara
ulitawaliwa na Maqurayshi kwa sababu ya ushujaa na ufasaha waliokuwa nao, sifa hizi ndizo
zilizolipelekea kabila la Qurayshi kuyatawala makabila mengine yote. Mji wa Makkah na
Maqurayshi walizidi kupata utukufu pale Mzee Qusway Bin Kilaab-babu wa nne wa Mtume
aliposhika hatamu za uongozi wa mji wa Makkah. Mzee huyu alikuwa ni mtu mwenye busara,
fikra na hekima. Alianzisha mpango mji, bunge ili watu wote wa Makkah waweze kukutana humo
na kushauriana/kujadili mambo yao, pia aliijenga upya Al-Kaaba baada ya kuanza kuonyesha
athari za kubomoka. Kadhalika alianzisha utaratibu wa kuwasaidia masikini kwa kuwapa
chakula na maji. Baada ya kupita vizazi vingi, taratibu Maqurayshi walianza kuyatupa
mafundisho ya dini ya Nabii Ibrahimu na kuanza kuyaabudu masanamu yaliyotengenezwa na
mikono yao wenyewe. Ibada ya msanamu ilikuwa ni matokeo ya safari ya mmoja wa viongozi wa
Maqurayshi alipokewenda Shamu na kuwakuta watu wa huko wakiyaabudia masanamu na
akapendezwa na kuvutiwa na ibada hiyo. Akarejea Makkah na sanamu moja, akaliweka ndani ya
Al-kaaba na kuanza kuliabudia. Watu wa Makkah kuona hivyo nao wakamuiga kiongozi wao,
wakatengeneza masanamu yao wakayaweka ndani ya Al-kaaba na kuyaabudia na huo ukawa ndio
mwanzo wa kuiacha na kuitupa mila ya Nabii Ibrahimu.
|