|
i.
Kuanguka kwa Khaybar:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipokwishazifungua na kuzitia mikononi mwake
ngome za Mayahudi alizoziteka na kuhodhi mali zao kiasi alichohodhi. Mayahudi
wakawa hawana mahala pengine ila ngome mbili tu; Al-Watwiyh na Salaalim nazo
ndizo zilizokuwa ngome za mwisho za Khaybar. Mtume akawazingira kwa muda wa
siku kumi na kitu hivi, hata walipoyakinisha kuwa wataangamia wakamuomba Mtume
awakubalie kujisalimisha kwa sharti ya kutokumwagwa damu yao. Akateremka
kutoka ngomeni Kinaanah Ibn Rabee Ibn Abil-Huqayq, akasuluhiana na Mtume wa
Allah juu ya kutokumwagwa damu ya wapiganaji waliomo ngomeni na wakubaliwe
kuondoka Khaybar pamoja na familia zao. Nao wamuachie Mtume wa Allah ardhi,
mali, farasi na silaha zote walizokuwa wakimiliki. Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-akasema: “Na iwe mbali nanyi dhima ya Allah na ile ya Mtume wa
Allah iwapo mtanificha jambo/kitu cho chote”. Akaandikiana nao mkataba kwa
masharti hayo, kwa kuzisalimisha kwao ngome za Al-Watwiyh na Salaalim, Khaybar
nzima ikawa imeangukia mikononi mwa waislamu. Na waislamu wakapata humo
ngawira tele.
ii.
Suluhu baina ya Mayahudi
na waislamu:
Ilipotimia
suluhu baina ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na watu wa Khaybar.
Mayahudi hawakupenda kuhama na kuuacha mji wao huu wa Khaybar kama
walivyoahidi. Kwa hivyo wakamuomba Mtume awaache waitumie ardhi hiyo kwa
kilimo na wampe nusu ya mazao yatakayopatikana, wakamwambia: “Sisi tunaijua
zaidi ardhi hii kuliko nyinyi na tunaweza kuiendeleza”. Mtume akawakubalia
ombi lao hilo na kuwapa rukhsa ya kubakia Khaybar waendeleze kilimo. Na
akafunga nao suluhu kwa sharti ya kupata nusu ya mazao yatakayovunwa na kwamba
atakuwa na haki ya kuwatoa atakapotaka kufanya hivyo.
iii.
Mayahudi wa “Fadaka” na
wale wa “Waadil-Quraa” wataka amani:
Mayahudi wa
“Fadaka” walipoisikia suluhu iliyofikiwa baina ya Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-na watu wa Khaybar. Wakatia azma ya kuacha vita na wakaelekea
katika meza ya amani na wakamtumia ujumbe Mtume wakimtaka afanye nao suluhu
kama alivyofanya na watu wa Khaybar. Mtume akawaitika katika matakwa yao hayo
na suluhu ikapita baina yao bila ya kutokea mapigano. Khaybar ikawa ni ngawira
baina ya waislamu kwa sababu iliangukia mikononi mwao kwa matumizi ya nguvu.
Ama Fadaka hii ikawa ni ya Mtume pekee, kwa sababu haikupatikana kwa njia ya
vita. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomaliza kulishughulikia
suala la watu wa Khaybar, huyoo akashika njia kuelekea “Waadil-Quraa”.
Akawazingira watu wake kwa siku kadhaa mpaka wakasalimu amri na kutangaza
suluhu, Mtume akafunga nao suluhu kama alivyofanya kwa watu wa Khaybar. Ama
Mayahudi wa “Taymaa”, hawa walikubali kutoa kodi bila ya kupatikana vita wala
mapambano. Kwa hivyo basi, Mayahudi wote wakawa wamesalimu amri kwa Mtume na
mamlaka waliyokuwa nayo katika miji ya Waarabu yakafikia tamati. Waislamu sasa
wakawa na amani kwa upande wa Kaskazini mpaka Shamu kama walivyokuwa na Amani
upande wa Kusini baada ya suluhu ya Hudaybiyah.
iv.
Ugavi wa ngawira:
Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaipiga mafungu matano ngawira ya Khaybar
na kuanza kuigawa. Askari mwenda kwa miguu akampa fungu moja na mpandaji
akampa mafungu matatu. Na akampa kutoka katika khumsi (1/5) yake yeye Mtume
yule aliyemdhihirishia Allah kumpa; akawapa wakeze, akawapa wanaume na
wanawake wa ukoo wa Abdul-Mutwalib na akawapa pia mayatima na waombaji. Ama
watumwa na wanawake waliohudhuria Khaybar, hawa aliwamegea kitu kidogo na wala
hakuwatengea fungu maalum.
Wakati
waislamu wakiwa katika furaha ya ushindi wa Khaybar, walijiwa na Ja’afar Ibn
Abiy Twalib akiliongoza kundi la waislamu waliokuwa uhamishoni huko Uhabeshi
(Eritrea ya leo). Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akafurahishwa mno
na ujio wao, akamkumbatia Ja’afar, akambusu baina ya macho yake na kusema:
“Sijui nimefurahishwa na lipi zaidi kati ya mawili haya; ushindi wa Khaybar au
ujio wa Ja’afar?”.
|