|
i.
Vita hivi ndivyo
vilivyowapa amani waislamu dhidi ya shari ya mayahudi:
Naam, hivyo
ndivyo ilivyokuwa katika suala zima la kumtiisha na kumshikisha adabu adui
huyu mkubwa. Adui ambaye alifanya silaha yake kuwa vitimbi, khiana, uongo na
udanganyifu (ghushi) na kuleta uchochezi baina ya waislamu. Kuyatilia shaka
aliyoyateremsha Allah kwa Mtume wake na kugonganisha baina ya waislamu na
Uislamu wao pia ni miongoni mwa silaha hatari zilizotumiwa na adui huyu. Na
lengo lake kuu likiwa ni kuufuta Uislamu na waislamu juu ya uso wa sayari
dunia kwa njia yo yote iliyokuwa ndani ya uweza wake. Basi pale Allah
alipoikata nguvu yake, akaondosha mamlaka yake na kuidhalilisha jeuri yao,
hapo ndipo waislamu walipoaminika dhidi ya shari ya adui huyu. Kama
walivyoaminika dhidi ya shari ya Makureishi kwa kutimia mkataba wa suluhu ya
Hudaybiyah. Na yote haya ndio Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-aliyokuwa akiyatafuta kutokana na mapigano haya dhidi ya Mayahudi.
Kufuatia kushindwa vibaya huku kwa Mayahudi, Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaridhia Mayahudi kuendelea kuishi katika
ardhi ya Khaybar na kugawana nao nusu kwa nusu ya mavuno yatokanayo na
shughuli za kilimo. Mtume aliyafikia maridhiano haya baada ya Mayahudi hawa
kukubali kutolewa Khaybar na kuiacha mali yote na silaha ikiangukia ngawira
mikononi mwa waislamu. Kwa makubaliano haya, kukawa hakuna tena haja ya
kuwafukuza na kuwatoa Khaybar baada ya kusalimisha silaha zao na kuvunjwa
vunjwa nguvu yao. Kulikomaanisha kuwapatia amani waislamu dhidi ya adui yao
huyu.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaendeleza juhudi
zake za kutaka kuwepo na uhusiano mwema baina ya waislamu na mayahudi.
Uhusiano utakaojengwa juu ya misingi ya upendo, ukweli na ujirani mwema na
wala sio juu ya misingi ya uadui na chuki kama ilivyokuwa wakati huo. Ili
kulifikia lengo hili, akaamua kutumia mbinu ya kuunga nao udugu kwa kuoa kwao.
Akamteua katika wanawake wao Safiyah Bint Huyay na akampa khiari ya kuchagua
moja ya mambo mawili; ama amuache huru na kumuoa au amuache huru na kumrudisha
kwao. Bibi huyu akakhiari kuwa mke, Mtume akamuacha huru akamuoa na kuwa
miongoni mwa mama wa waumini. Kwa kukubali kwa khiari yake kuolewa na Mtume,
bibi huyu mwema akaisafisha nafsi yake na kuondosha uadui uliokuwamo humo
dhidi ya Mtume, Uislamu na waislamu. Mpaka imepokewa kwamba yeye alipata
kusema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa ni wa mbele katika
watu niliokuwa nikiwachukia kupindukia. (Kwa sababu) alimuua baba yangu na
mume wangu. Kwa ajili hiyo (Mtume) aliendelea kunitaka udhuru akisema: Hakika
baba yako alinikusanyia majeshi shirika ya Waarabu na akafanya akafanya...”,
mpaka hilo likatoka ndani ya nafsi yangu.
ii.
Mtume aishi na Mayahudi
kwa siasa ya urafiki na uadilifu:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa ni mpole kwa mahasimu wake hawa,
akipupia mno kutangamana nao kwa uadilifu. Akijitahidi kwa nguvu zake zote
kuondosha mioyoni mwao athari ya uadui huu, kwani uadui baina yao haukuwa
uadui binafsi. Hakika si vinginevyo, uadui huo ulitokana na tofauti za
itikadi/imani waliyo ibadilisha: “...KWA SABABU YA HUSUDA ILIYOMO NYOYONI
MWAO; (iliyowapata) BAADA YA KUWAPAMBANUKIA HAKI...” [2:109] Imepokewa kwamba
Sayyidina Bilali-Allah amuwiye radhi-alipita na Safiyah na binti ya ami yake
kwa wauliwa (maiti wa vita) wa Mayahudi. Yule binti ya ami yake na Bi. Safiyah
akapiga ukelele mkubwa, Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akaelezea kutopendezwa
kwake na kitendo alichokifanya Bilali. Akamuuliza: “Umetokwa na huruma wewe?
Unampitisha binti kigori kushuhudia waliouliwa!!” Bilali akajitetea: “Ewe
Mtume wa Allah, mimi sikudhania kwamba wewe unalichukia jambo hilo na mimi
nilipenda aone maanguko ya kaumu yake”. Kisha akaapa kutorudia kutenda tena
kosa kama hilo. Kadhalika imepokewa kwamba Mayahudi walikwenda kumlalamikia
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwamba waislamu wanaingia mashambani
mwao na kuchukua mazao yao baada ya kupita kwa suluhu. Mtume alipowasilishiwa
rasmi malalamiko haya ya Mayahudi, akatoa amri waislamu wakusanyike.
Walipoitika wito, Mtume akasimama mbele yao, akamuhimidi Allah na kumsifia,
kisha akasema: “Hakika Mayahudi wamenishtakia kwamba nyinyi mnaingia katika
bustani zao na ilhali wao wamekwisha kuaminini juu ya mali na damu zao
zilizomo mikononi mwao katika ardhi yao. Na sisi tumechukua ahadi kwao kwamba
waendelee kuimiliki ardhi ( hii ya Khaybar kwa shughuli za kilimo) walime na
sisi tupewe nusu ya mazao yatakayovunwa. Kwa yakini hazihalaliki mali za
wafungiwa ahadi ila kwa haki yake”. Baada ya khutba hii ya Mtume, waislamu
wakawa hawachukui tena mboga za Mayahudi ila kwa kununua. Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawa anamtuma Abdullah Ibn Rawaahah-Allah
amuwiye radhi-kwa watu wa Khaybar. Kuwa mkadiriaji na mthamini wa mavuno baina
ya waislamu na mayahudi na kisha kugawa baina ya pande mbili hizi kwa mujibu
wa makubaliano ya suluhu. Wakati akiitekeleza dhima hii aliyokabidhiwa na
Mtume wa Allah, Mayahudi walipata kusema: “Umetufanyia uadui (umetudhulumu)”,
yeye akiwaambia: “Mkitaka gaweni nyini na mkitaka basi tutagawa sisi”. Hapo
Mayahudi husema: “Mbingu na ardhi zimesimama kwa uadilifu huu”.
Imamu Bukhaariy-Allah amrehemu-amepokea kwa sanadi ya Said
Al-Khudriy na Abu Hurayrah-Allah awawiye radhi. Kwamba Mtume wa Allah alimpa
ugavana wa mji wa Khaybar mtu mmoja. Gavana huyu akamletea Mtume tende bora
kabisa, Mtume akamuuliza: “Tende zote za Khaybar ndio ziko hivi?”, akajibu:
“Hapana ewe Mtume wa Allah, hakika sisi tunabadilisha pishi moja ya tende hizi
kwa pishi mbili za aina nyingine ya tende na pishi mbili kwa tatu”. Mtume
akasema: “Msifanye hivyo, ziuzeni zote kwa dirham kisha nunueni kwa dirham
mlizopata tende zenye kiwango hiki cha ubora”.
Na katika jumla ya ngawira walizozipata waislamu Khaybar ni
mbao za Taurati (vitabu), Mayahudi wakaja kuzidai, Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-akaamuru warudishiwe. Kulielekea hili Muisraeli Dr. Wilnson
anasema: “Tendo hili linaonyesha hadhi/daraja ya vitabu hivi iliyokuwemo ndani
ya nafsi ya Muhammad. Hili liliwafanya Mayahudi kumuona Muhammad kuwa ni
mjenzi (si mbomozi) na kumuheshimu kwa sababu hakuvitenda vibaya vitabu vyao
vitakatifu. Sambamba na hili wanayakumbuka yaliyotendwa na Warumi pale
walipouteka mji wa Jerusalem na kuutia mikononi mwao mnamo mwaka 70 K.K.
walivichoma moto vitabu vitakatifu na kuvikanyaga kwa miguu yao. Hii ndio
tofauti ya wazi baina ya wateka mji (washindi) tuliowataja na Mtume wa
Uislamu”. Mwisho wa kunukuu.
|