Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

III. MAYAHUDI WAULIPA WEMA WA MTUME KWA USALIT/KHIYANA

 Faida

            Je, Mayahudi waliuthamini wema wote huu waliotendewa na Mtume? Na je, waliuhifadhi wema huu na kujua kwamba Mtume wa Uislamu hakuwadhamiria shari? Na kwamba misingi ya Uislamu imesimama juu ya haki, uadilifu na kuwaheshimu watu kama wanaadamu. Na kwamba Uislamu unawafanyia uadilifu maadui zake kama unavyowafanyia wapenzi na marafiki zake bila ya tofauti yo yote. Na je, Mayahudi walitambua kwamba Muhammad ni mkweli kuliko watu wote kwa kauli na mwingi wao kwa uadilifu? Na kwamba ni mtwaharifu wa moyo kuliko watu wote na ni mwenye matangamano mema?

Mayahudi hawakuthamini cho chote katika utu, uanadamu na wema huu mkubwa waliotendewa. Bali waliendelea kubakia na umbile lao la asili; dhamira chafu na kukanusha wema. Na nyoyo zao zikaendelea kutokota mifundo dhidi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Wakairejea ada yao ya tangu zama wakaanza kufikiria kumfanyia khiana Mtume na kula njama za kumuua. Wakamkabidhi jukumu hilo la kummaliza Mtume mwanamke mmoja, huyu akapanga hila kabambe katika kuitekeleza dhima hii chafu aliyopewa. Mwanasira; Ibn Ishaq-Allah amrehemu-anasimulia: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomakinika na kutulizana, Zaynab Bint Al-Haarith; mke wa Salaam Ibn Miksham alimletea zawadi ya mbuzi mzima wa kuchoma. Khabithi huyu alikuwa tayari amekwishauliza ni nyama ipi aipendayo mno Mtume wa Allah, akaambiwa anapenda sana mkono wa mbuzi. Basi akatia sumu nyingi sehemu hiyo na akamtia sumu mbuzi wote, kisha akamletea Mtume zawadi hii ya kifo. Alipomuweka mbele ya Mtume, akachukua mkono na kung’ata pande lakini hakutafuna. Na wakati huo Mtume alikuwa na swahaba wake; Bishru Ibn Al-Baraai Ibn Ma’aruur-Allah amuwiye radhi. Huyu nae akakata kipande pale pale alipokata Mtume wa Allah, akakitafuna na kukimeza. Ama Mtume yeye alikitema kipande alichokikata, kisha akasema: “Hakika mfupa huu unaniambia kwamba umetiwa sumu”, akamuita mwanamke yule kumuuliza nae akakiri. Mtume akamuuliza: Ni lipi lililokupelekea kufanya haya uliyoyafanya”, akajibu: “Umefikia kwa watu wangu daraja ya kutochelewa, basi nikajiambia akiwa ni mfalme (atakufa) nasi tutapumzika nae. Na akiwa ni Mtume kweli, basi ataambiwa”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-baada ya kumsikiliza, akamsamehe na swahaba wake; Bishru akafa kutokana na sumu ya kile kipande alichokula”.

    iv.          Makurayshi wazifuatilia kwa makini khabari za Khaybar:

            Ushindi wa Khaybar ulikuwa ni tukio adhimu lililowatikisa  Makurayshi na kuwafanya walifuatilie kwa karibu mno. Wakaanza kuangalia natija na kuitathmini tangu pale walipotambua kwamba Mtume ameelekea Khaybar. Katika kulielekea tukio hili, waligawika makundi mawili; kundi lililoangalia nguvu ya Mayahudi, uimara wa ngome zao na wingi wa idadi yao na zana zao za vita. Na kuangalia ushirika waliokuwa nao na Ghatwfaan, kwa maono yao haya wakisema: “Mayahudi na washirika wao wataibuka washindi”. Na kundi jingine likiangalia hali-kisogo (iliyopita) ya waislamu huko nyuma na nguvu na uthabiti wa nyoyo walio nao. Nidhamu na mipangp yao makini, ushirikiano wao mzuri na kuyaona kwao  mauti si kitu katika kuipigania itikadi/imani yao, kwa maono yao haya wakisema: “Muhammad na maswahaba wake wataibuka washindi”. Kila kundi likishikamana na maono yake mpaka wakafikia kuwekeana madau makubwa, wakawa wakifuatilia khabari za mambo yanavyojiri huko Khaybar kwa karibu mno. Na wakiyangojea matokeo kwa shauku kubwa kiasi cha kufikia kungojea kwenye njia kuu wakimuuliza kila ajaye hali ilivyo baina ya Muhammad na Mayahudi.

Wanasema wana sira-Allah awarehemu: “Al-Hajaj Ibn Alaatw As-sulamiy-Allah amuwiye radhi-alikuwa amekwishasilimu na kuhudhuria Khaybar pamoja na Mtume wa Allah. Khaybar ilipoangukia mikononi mwa waislamu alisema: “Ewe Mtume wa Allah, hakika mimi ninayo mali Makah kwa mke wangu; Ummu Sheibah Bint Abiy Twalhah. Na mali yangu imetawanywa kwa wafanyabiashara wa Makah, basi nakuomba unipe idhini ewe Mtume wa Allah nikaikusanye”. Mtume akampa idhini, Al-Hajaaj akasema: “Sina budi kuzua uongo ewe Mtume wa Allah (ili niweze kutimiza azma yangu hii)”, Mtume akamwambia: “Sema”. Al-Hajjaaj anaendelea kusimulia: “Basi nikatoka hata nilipofika Makah nikawakuta watu katika Makureishi katika pande za jangwa la Thaniyah wakinusa khabari na kuulizia suala la Mtume. Na wakati huo ilikwishawafikia khabari kwamba Mtume ameenda Khaybar, waliponiona wakasema: “Wallah, Al-Hajaaj anazo khabari tuzitakazo”. – Anaendelea kusimulia – na walikuwa hawajui cho chote juu ya kusilimu kwangu, wakaniambia: “Hebu tupe khabari ewe babie Muhammad, kwani imetufikilia khabari kwamba mkata watu (wakimlenga Mtume) amekwenda Khaybar. Na hali ya kuwa huo ni mji wa Mayahudi na ni sehemu ya mashambani ya Hijaazi”. Nikawajibu: “Nami imekwishanifikia khabari hiyo na ninazo khabari zitakazokufurahisheni”. Walivyosikia hivyo haraka haraka wakamzunguka ngamia wangu na kusema: “Haya lete khabari ewe Hajjaaj”. Nikawaambia: “Muhammad ameshindwa vibaya mno haijapata kutokea na maswahaba wake wameuawa hamjapata kusikia katu na Muhammad mwenyewe amechukuliwa mateka. Wakasema Mayahudi sisi hatumuui tunampeleka huko Makah akauliwe na ndugu zake kulipa kisasi cha watu wao aliowaua”. Kusikia hivyo wakainuka na kupiga ukelele mkubwa wakisema: “Kwa yakini imekujilieni khabari, hakika si vinginevyo mnachongojea ni kuletewa Muhammad akauawa mbele yenu nyote mkishuhudia”. Nikawaambia: “Nipeni msaada wa kukusanya mali yangu kutoka kwa wadeni wangu wa Makah, kwani mimi ninataka kurudi Khaybar nilikute kundi la Muhammad, kabla sijatanguliwa huko na wafanyabiashara wengine”. Wakainuka na kunikusanyia mali yangu kwa haraka mno hujapata kusikia haraka kama hiyo. Nikamuendea mke wangu na kumuuliza: “I wapi mali yangu?, - kwani mimi nilikuwa na mali niliyoiwekesha kwake – ili nizipatilize fursa za biashara kabla sijatanguliwa na wafanyabiashara wengine”.

Anaendelea kusimulia Hajjaaj, Al-Abbas Ibn Abdul-Mutwalib alipoisikia khabari ile na kwamba imetoka kwangu. Akaja mpaka akasimama pembeni yangu nami nikiwa ndani ya mojawapo ya mahema ya wafanyabiashara, akasema: “Ewe Hajjaaj ni khabari gani hii uliyokuja nayo? Nikamuuliza: “Je, unaweza kuficha siri kwa nitakayokwambia?”, akajibu: “Naam”. Nikamwambia: “Basi ningojee mpaka nimalize”, nilipomaliza kukusanya kila kitu kilichokuwa changu pale Makah na nikaazimia kuondoka, nilikutana na Al-Abbas na nikamwambia: “Nifichie siri ewe Abul-Fadhli, kwani mimi ninachelea kutafutwa kwa siku tatu, baada ya hapo sema utakavyo”, akajibu: Nitafanya hivyo utakavyo”, ndipo nilipomwambia: “Basi wallah, hakika mimi nimemuacha mwana wa nduguyo akiwa ni bwana harusi kwa binti ya mfalme wao yaani Safiyah Bint Huyay Ibn Akhtwab. Na kwa yakini ameishinda na kuitia mikononi mwake Khaybar nzima na kuhodhi mali yote”. Akauliza: “Unasemaje ewe Hajjaaj?, nikamjibu: “Wallah ni kweli, lakini nifichie siri na kwa yakini mimi nimekwishasilimu na sikuja ila kwa ajili tu ya kukusanya mali yangu. Kwa sababu nachelea nisije kudhulumiwa, basi zikishapita siku tatu unaweza kulifichua hili ukipenda”.

Anaendela kuhadithia: “Nikaenda zangu hata ilipofika siku ya tatu tangu kuondoka kwangu, Al-Abbas akavaa mavazi yake rasmi, akajitia manukato na kuitia bakora mkononi. Kisha huyoo akatoka, akaenda zake mpaka kwenye Al-Ka’abah akatufu, Makureishi walipomuona wakamwambia: “Ewe babie Fadhli, huku wallah ni kustahamilia joto la msiba”, akasema: “Sivyo hivyo, ninaapa kwa Allah mnayeapa kwa jina lake, kwa yakini Muhammad ameifungua Khaybar. Na tena ameachwa akiwa bwana harusi kwa kumuoa binti ya mfalme wao na amehodhi mali zao na zimeangukia kuwa ni zake na maswahaba wake”. Wakamuuliza: “Ni nani aliyekuletea khabari hizi?”, akawaambia: “Ni yule yule aliyekuleteeni khabari alizo kuleteeni na ameingia kwenu akiwa tayari ni muislamu, akatwaa mali yake na kuondoka zake ili kujiunga pamoja na Muhammad na maswahaba wake”. Wakasema: “Ameponyoka adui wa Mungu, ama wallah lau tungelijua basi pangelikuwa na kazi baina yake nasi”. Na haukupita muda mrefu ikawajia khabari iyathibitishayo waliyoambiwa na Al-Abbas.

 



 | Tuandikie |