Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SOMO LA SABA

 Faida

 

             i.            Ushindi wa waislamu dhidi ya Mayahudi wa Khaybar wawabutwaisha na kuwastaajabisha mahasimu zao:

             Hivi ndivyo tukio la Khaybar lilivyotusha mshindo mkuu mioyoni mwa Makureishi na wala hapana shaka kwamba lilikuwa ni tukio hemezi na stushi. Kwani Makureishi hawakutarajia kabisa kwamba Khaybar itasamabaratika na kuangukia mikononi mwa waislamu kwa kasi kiasi hicho. Na hali Khaybar ndio Khaybar kwa ngome madhubuti na  watu mashujaa iliyokuwa nao. Na haikuwapitikia akilini kwamba Muhammad na maswahaba wake wanaweza kuishinda nguvu hiyo kwa haraka kiasi hicho. Ukweli ulivyo khasa, ushindi huu wa waislamu dhidi ya Mayahudi wa Khaybar unalazimisha kuleta fikra na mazingatio. Kwa sababu Mayahudi hawa walikuwa na nguvu kubwa mno kwa sura ambayo hawakuwa ni watu wa kushindwa. Kwanza idadi yao ilikuwa ni wapiganaji alfu kumi wenye umahiri wa vita na wao ndio waliokuwa kundi hatari katika medani ya vita kuliko Wana-Israeli wote. Isitoshe walikuwa na umahiri mkubwa katika urushaji wa mishale, mikuki na kuvurumisha mawe, tena walikuwa na ushujaa mkubwa katika uwanja wa mapambano. Halafu tena walikuwa wamezungukwa na ngome madhubuti zisizopenyeka kwa urahisi, si hivyo tu walikuwa na zana nzito za kivita ukilinganisha na waislamu. Walikuwa na chakula cha kutosha kujikimu kwa muda mrefu na walikuwa na kila sababu ya kuwatia mori vitani. Ikiwa ni pamoja na kulinda heshima/utukufu wao, kuuhami mji wao na kumfagilia mbali adui anayetishia maslahi yao. Wakati ambapo jeshi la waislamu halikuwa na zaidi ya wapiganaji alfu moja na mia sita tu. Na halikuwa na zana za vita zaidi ya majambia, mikuki na mishale, wala hawakuwa na ngome ya kuwakinga dhidi ya mashambulizi ya adui. Isitoshe walikuwa na uhaba wa chakula na hawakuwa na msaada pindi wangezidiwa.

Pamoja na tofauti hii kubwa na ya wazi kabisa katika idadi na zana baina ya makundi mawili haya, bado waislamu waliwashinda Mayahudi kwa ushindi wa kishindo. Je, hivi kweli hili si jambo linalolazimisha kuleta mazingatio na tafakari kina?! Hapana shaka kwamba ushindi huu wa kishindo walioupata waislamu uliwatunduwaza na kuwabutwaisha Makureishi. Kama ulivyowashtua Waarabu wote na wasio Waarabu katika pande zote za Peninsula ya Waarabu. Huenda pengine kule kujisalimisha Mayahudi wa Fadaka na Taymaa bila ya vita na kuporomoka kwa Waadil-Quraa haraka haraka, kulikuwa ni miongoni mwa athari za ushindi huu wa ajabu. Ushindi uliozihemeza akili za watu na kuzijaza khofu nyoyo zao kutokana na nguvu hii ya ajabu. Nguvu isiyoshindwa na wingi wa idadi/zana, isiyozuiliwa na ngome madhubuti wala haikengeushwi na cho chote katika kufikia malengo yake. Mayahudi wa Khaybar walijiaminisha kuwa wako salama na kamwe hawakudhania kwamba siku moja Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anaweza hata kuthubutu kuwashambulia seuze kuwashinda. Hii ndio hakika inayoelezwa na     Qur-ani Tukufu: “...NAO WALIDHANIA KUWA NGOME ZAO ZITAWALINDA NA (kufikwa na amri ya) ALLAH, LAKINI ALLAH ALIWAJIA KWA MAHALA WASIPOPATAZAMIA, NA AKATIA WOGA KATIKA NYOYO ZAO (wasiweze kupigana na waislamu walipokuja kupigana nao)...” [59:02]

Naam, ni kweli kabisa kwamba khofu aliyoitia Allah nyoyoni mwa Mayahudi ni miongoni mwa sababu muhimu zilizowapa waislamu ushindi huu mnono. Na amesema kweli Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anapoukiri na kuuthibitisha ukweli huu kupitia kauli yake: “...nimenusuriwa kwa khofu mwendo wa mwezi mzima...”

 

           ii.            Ushindi wa Khaybar wahitimisha ukaliaji na utawala wa Mayahudi katika nchi ya Hijaazi:

            Miongoni mwa natija za ushindi huu wa kishindo wa Khaybar ni kuvunjwa kabisa nguvu za kisiasa, kiuchumi na kidini walizokuwa nazo Mayahudi katika ardhi ya Hijaazi. Vivuli vyao vikaanza kufutika kidogo kidogo mpaka athari yao yote ikafutika na kutoweka kabisa. Kwa hiyo katika zama za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-mpaka anaondoka duniani, Mayahudi walibakia katika kipande kidogo cha ardhi wakiendesha shughuli za kilimo kwa makubaliano waliyofunga na Mtume wa Allah. Alipokufa Mtume na hatamu za uongozi wa waislamu kushikwa na Sayyidina Abu Bakri-Allah amuwiye radhi-aliendelea kuyaheshimu maamuzi na makubaliano yaliyofikiwa baina ya Mtume na Mayahudi mpaka anakufa. Sayyidina Umar-Allah amuwiye radhi-akashika hatamu za uongozi na kuyaendeleza na kuyaheshimu maamuzi ya Mtume na yale ya mtangulizi wake mwanzoni mwa ukhalifa wake. Kisha Sayyidina Umar akafikiwa na khabari kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisema katika maradhi-mauti yake: “Hazikusanyiki pamoja dini mbili katika kisiwa cha Waarabu”. Sayyidina Umar akazichunguza khabari hizo mpaka akapata ithibati kuwa ni za kweli, hapo ndipo alipowatumia Mayahudi ujumbe akisema: “Hakika Allah Taala ametoa idhini ya nyinyi kutolewa, kwani nimefikiwa na khabari kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisema: “Hazikusanyiki pamoja dini mbili katika kisiwa cha Waarabu”. Basi ye yote miongoni mwa Mayahudi aliyefunga ahadi na Mtume wa Allah, basi na aje nimtekelezee. Na ambaye hakufunga ahadi na Mtume wa Allah, basi na ajitayarishe kuondoka”. Baada ya tangazo hili, ndipo Sayyidina Umar-Allah amuwiye radhi-alipoanza zoezi rasmi la kuwahamisha Mayahudi wote ambao hawakuwa wamefunga ahadi na Mtume. Akawatoa katika ardhi za Waarabu Mayahudi wa Khaybar na Fadaka na akawa bakisha wale wa Taymaa na Waadil-Quraa, kwa sababu ardhi mbili hizo zimo katika mipaka ya Shamu. Nae Sayyidina Umar alikuwa anaona kwamba eneo lote lililo nyuma ya Waadil-Quraa mpaka Madinah ni sehemu ya Hijaazi. “Mayahudi wengi wakabakia Waadil-Quraa mpaka karne ya kumi na moja Miladia na makundi mengine madogo madogo yalikuwa pande za Taymaa mpaka karne ya kumi na mbili. Kisha wakaanza kutoweka kidogo kidogo katika ardhi ya Hijaazi mpaka wakachanganyika na kumezwa na makabila ya Kiarabu”. {Rejea TAARIKHUL-YAHUUD FIY BILAADIL-ARAB BITASWARUF} na {AL-BIDAAYAH WAN-NIHAAYAH}.

 



 | Tuandikie |