|
Kama vita vya Khaybar vilivyoutamatisha utawala na ukaliaji wa Mayahudi katika
ardhi za Waarabu. Ndivyo hivyo hivyo vilivyoitoa jeuri na kibri cha Makureishi
na kuwaacha mbele ya nguvu ya Uislamu wakiwa wametoshewa na kuhemewa. Wakiwa
hawajui cha kufanya kuuelekea mwumbi huu mkokoto wa maji usioweza kuzuiwa na
nguvu yo yote. Hapo ndipo Makureishi na Waarabu wote kwa ujumla wao
wakalazimika kukubali na kukiri kwamba hawana tena ubavu wa kupambana na dini
hii. Wakawa hawana budi kusalimu amri na kuukubali uhalisia wa hali bila ya
hiari zao. Na tangu hapo hakupatikana tena mtu wa kuupiga vita Uislamu
miongoni mwa wakazi wa kisiwa cha Waarabu ila vikundi vidogo vidogo vichache
vya mabedui wa jangwani. Hawa wakawa wakilikinga wimbi hili kama
linavyokingama povu katika njia ya mumbwi. Ambapo mumbwi hulifagilia mbali
povu hilo na kuliacha likitawanyikia pembeni. Pakawa hapana budi kuadhibiwa
wakaidi wachache hawa wanaojaribu kushindana na nguvu ya Allah isiyoshindika.
Kwa ajili hii, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawa anatuma huku na
huko vikosi vya askari kwa lengo la kuhakikisha amani na usalama. Na kujenga
hali bora itakayowawezesha wana-da’awah (walinganiaji wa ujumbe wa Allah)
kuufikisha ujumbe wa Allah pande mbalimbali bila ya bughudha au kufanyiwa
khiana/usaliti.
SURA YA KUMI
BARUA KWA WAFALME
SOMO LA KWANZA.
i.
Dola za Uajemi na Urumi
ndizo zilizokuwa madola makuu ya wakati huo:
Muda mfupi
baada ya kumalizika kwa suluhu ya Hudaybiyah, Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akaanza kuwaandikia barua wafalme na watawala walio mzunguka.
Madhumuni ya barua hizi za Mtume kwa wafalme hawa, ilikuwa ni kuwalingania
Uislamu. Na dola kubwa za wakati huo zilikuwa ni Uajemi, Urumi na Uhabeshi.
Uajemi ilikuwa ni dola ya kimajusi inayofuata itikadi ya kuabudu moto na Urumi
na Uhabeshi zilikuwa ni dola zinazofuata itikadi ya Kinaswara. Palikuwa na
msuguano mkali na mapambano ya mara kwa mara baina yao, na kupokezana ushindi
na ushindwa. Hali iliendelea hivyo kwa miaka kadhaa mpaka pale walipofikia
maafikiano ya kuweka chini silaha. Ukiachilia mbali dola tatu hizi,
zilizobakia zilikuwa ni dola na himaya ndogo ndogo ambazo ama zilikuwa upande
wa Uajemi au ule wa Urumi. Na nyingine zilikuwa ni dola huru; zisizojihusisha
na upande wo wote. Dola za Yemen na Iraq zilikuwa chini ya uongozi wa Uajemi,
Shamu na Misri zilikuwa chini ya utawala wa Urumi. Na Yamaamah, Oman na
Bahrein zilikuwa ni falme huru zisizoegemea upande wo wote wa madola makuu
haya.
Ama Tihaamah, Hijaazi, Najid na Twaif na miji iliyozizunguka
katikati ya ghuba ya Kiarabu, hazikuunganishwa na madola mawili haya ila kwa
mahusiano ya kibiashara tu. Lakini hisia za kidini zilikuwa zikiyafanya
matamanio/mapenzi ya mushrikina kuwa pamoja na Uajemi. Na kuyafanya mapenzi ya
waislamu kuwa pamoja na Warumi, kwa hivyo wote kwa pamoja; waislamu na
mushrikina wakawa wakizifuatilia kwa makini na mapenzi makubwa khabari za vita
baina ya madola mawili makuu haya; Urumi na Uajemi. Kila kundi likishehenezwa
na mapenzi ya kutaka ushindi uwe ni fungu la washirika wao, mushrikina wote
wakipenda Uajemi iwashinde Warumi. Na waislamu wakipendelea ushindi wa Warumi
dhidi ya Waajemi, kwa kuwa wao ni watu wa kitabu. Mnamo mwaka 621 A.D.; mwaka
mmoja tu kabla ya Hijrah, ilitokezea Waajemi; washirika wa mushrikina
kuwashambulia Warumi; washirika wa waislamu na kuwashinda. Wakaendeleza wimbi
hilo la ushindi mpaka wakafika ndani kabisa ya Asia ndogo na kuusambaratisha
“Birantwiyah”; mji mkuu wa dola ya Urumi. Mushrikina wakafurahi mno na
kuushangilia ushindi huu wa washirika wao dhidi ya washirika wa waislamu. Kwa
ushindi huo, wakabashiri ushindi wa itikadi ya miungu wengi dhidi ya itikadi
ya Mungu mmoja (Tauheed ya waislamu). Hapo ndipo Allah Taala alipoziteremsha
aya za mwanzo za Suurat-Ruum akiwapa bishara njema waislamu ya kwamba Warumi
watawashinda Waajemi karibuni tu, akasema: “ALIF LAM MIYM. WARUMI WAMESHINDWA.
KATIKA NCHI ILIYO KARIBU (na nchi ya Arabu, nayo ni Shamu); NAO BAADA YA
KUSHINDWA KWAO, WATASHINDA. KATIKA MIAKA MICHACHE; AMRI NI YA ALLAH KABLA
(yake) NA BAADA (yake); NA SIKU HIYO WAISLAMU WATAFURAHI. KWA NUSURA YA ALLAH
(atakayowapa wao, nayo ni kuwashinda Makureishi siku hiyo). (Allah) HUMUNUSURU
AMTAKAYE; NAYE NI MWENYE NGUVU (na) MWENYE REHEMA. (Hii ni) AHADI YA ALLAH,
ALLAH HAVUNJI AHADI YAKE, LAKINI WATU WENGI HAWAJUI”. [30:1-6]
Na kwa yakini iliwathibitikia waumini ahadi ya Allah, Warumi
wakawashinda Waajemi mnamo mwaka 626 A.D. Na wakafanikiwa kuirejesha tena
mikononi mwao ardhi yao yote iliyokuwa imekaliwa kimabavu na waajemi. Siku
hiyo waumini waliifurahikia nusura ya Allah kwa kuwarudi Makureishi na
washirika wao.
ii.
Ulimwengu mzima ulikuwa
mithili ya wana-kondoo waliopotea, ukienda katika viza:
Hivi ndivyo
ilivyokuwa hali ya kisiasa ya ulimwengu wa Mashariki enzi hizo. Ama hali za
kimaadili na kijamii ndizo zilikuwa mbaya mno, tumetaja huko nyuma namna
maadili yalivyoporomoka na kufisidika kwa hali za kijamii. Na jinsi dhulma,
maasi na uovu vilivyokuwa ndio nembo ya jamii katika kila uma. Na namna gani
vurugu lilivyotawala itikadi na kuenea dini za kuabudu masanamu na imani isiyo
ya kweli kuzitawala fikra na akili za watu. Na vipi heshima zilivyovunjwa na
unyang’anyi, uporaji na uuaji vikawa ndio fakhri ya wenye nguvu. Na ulimwengu
wa magharibi haukutofautiana kiufisadi na ulimwengu huu wa mashariki. Jamii
ziliporomoka kimaadili mpaka kufikia tabaka ya chini kuliko wanyama na watu
kuwa mithili ya kundi la wana-kondoo lililopotea liendalo gizani.
Kwa hivyo basi, ilikuwa hapana budi kundi hili la wana-kondoo
wapotevu hawa liisikie sauti ya mchungaji ili liweze kuongoza njia. Na
ilikuwa lazima lipate kijinga cha moto ili liweze kuongozwa na muangaza wake.
Kwa hivyo basi mchungaji akaanza kuliswaga kundi ili lipate kuongoza njia na
kuliangazia ili lipate kuona njia. Na mchungaji huyu hakuwa mwingine zaidi ya
“Muhammad”; Mtume wa Allah kwa watu wote. Lilikuwa ni jukumu lake baada ya
kuisikizisha kaumu yake; Waarabu wenzake sauti yake, ayasikilizishe mataifa
yote. Hapo ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipoanza
kuyaandikia barua za ujumbe wa Uislamu kupitia kwa wafalme wao, ili awatoe
gizani kuwatia nuruni.
|