Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

I) MTUME WA ALLAH AYAFIKISHIA MATAIFA UJUMBE WA ALLAH KUPITIA WAFALME WAO

 Faida

 

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipoazimia kuitekeleza kazi hii, alijitengezea muhuri wa fedha ulionakishiwa “Muhammadur-rasuulullah”. Na kisha akamuandikia barua rasmi kila mfalme akimlingania kumuamini Allah asiye na mshirika na akimkumbusha kwamba salama na mafanikio yako katika kumuamini Allah pekee. Na akimkalifisha kuufikisha ujumbe huo kwa raia wake, na iwapo atakengeuka na kupuuzia ujumbe huo basi atabeba dhambi zake mwenyewe na za watu wote walio nyuma yake. Akimaliza kuandika, ndipo barua hugongwa muhuri wake na kumtuma mmojawapo wa maswahaba wake kuifikisha kwa mlengwa. Akamtuma Dihyah Ibn Khaliyfah-Allah amuwiye radhi-kupeleka barua kwa Qayswar; mfalme wa Urumi. Abdullah Ibn Hudhaafah-Allah amuwiye radhi-akatumwa kwa Kisraa; mfalme wa Uajemi na Amrou Ibn Umayyah-Allah amuwiye radhi-akatumwa kwa Najaash; mfalme wa Uhabeshi. Akamtuma Haatib Ibn Abiy Balta’ah-Allah amuwiye radhi-kwa Muqauqis; kiongozi wa Waqibtw (Egyptian Coptics) na Shujaa Ibn Ibn Wahbi-Allah amuwiye radhi-akatumwa kwa Al-Haarith Al-Ghasaaniy; mfalme wa majimbo ya Shamu. Maswahaba sita hawa ndio wajumbe wa mwanzo wa Mtume wa Allah aliowatuma kwa wafalme waliomzunguka.

Ama mfalme wa Uhabeshi; Najaash baada ya kuupokea ujumbe wa Mtume alisilimu na akaichukua barua ile ya Mtume wa Allah na kuiweka machoni pake. Kwa kuitukuza barua ya Mtume akashuka kutoka katika kiti chake cha enzi na kukaa chini akasema: “Lau ningeliweza kumuendea (huko aliko), basi bila shaka ningelimuendea”. Kisha akamuandikia barua Mtume akimfahamisha juu ya kusilimu na kuamini kwake. Kisraa; mfalme wa Uajemi, huyo alionyesha jeuri na dharau kubwa, kwani aliichukua barua ya Mtume na kuichanachana. Kisha akamuandikia barua gavana wake aliyeko Yemen, akiitwa Baadhaan akimuamuru kutuma watu wakamletee huyu anayedai kuwa yeye ni mtume. Baadhaan akaipokea kwa utii amri ya mkuu wake, akawatuma wawili miongoni mwa watu wake mashujaa wakamlete mtume ili apelekwe kwa bwana wake. Walipofika Madinah kwa Mtume, alichukizwa mno na mandhari ya kike na ulainilaini waliokuwa nao wajumbe hawa wa Baadhaan, akawauliza: “Ni nani aliyekuamrisheni kuvaa hivyo?”, wakajibu: “Bwana wetu” – wakimkusudia Kisraa. Mtume akawaambia: “Mpelekeeni salamu huyo mtu wenu aliyekutumeni kwamba bwana wangu amemuua bwana wake Kisraa katika usiku huu wa leo”. Wapokezi wa Sira-Allah awarehemu-wanasema: Hakika usiku huo ulikuwa ni usiku wa kuamkia Jumanne, mwezi kumi Jumaadal-Uula (Mfunguo nne), mwaka wa saba wa Hijrah. Wajumbe wakarudi kwa Baadhaan na kumkhabarisha waliyoyasikia kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na haukupita muda mrefu tangu aelezwe khabari hiyo, ila ilimuwasilia khabari ya kuuawa Kisra kwa mkono wa mwanawe mwenyewe; Shiyrawaihi. Baadhaan akasilimu pamoja na Wafursi wote waliokuwa nae Yemen.

Ama Muqauqis; kiongozi wa Waqibtw, yeye aliisoma barua ya Mtume na akasema maneno mazuri. Kisha akaihifadhi barua hiyo katika chombo kilichotengenezwa kwa meno ya tembo na akaigonga muhuri wake. Halafu akaandika barua kumjibu Mtume, akisema: “Ama baad, nimeisoma barua yako na nimeyafahamu uliyoyaandika na unachokilingania. Kwa yakini mimi najua kwamba kuna Mtume atakayekuja na nilikuwa nadhania kuwa atatokea pande za Shamu. Na nimempokea vema mjumbe wako na ninakuletea zawadi ya vigori wawili wenye heshima kubwa kwa Waqibtw. Na nimekupa zawadi ya nguo na nyumbu utakayemtumia katika usafiri, wassalaam”. Muqauqis hakwenda mbele zaidi ya hapo na Mtume akaipokea zawadi yake na kumfanya suria mmoja wa vigori wawili wale. Naye ndiye mama Maariah aliyemzaa Sayyidina Ibrahim; mmoja wa watoto watatu wa kiume wa Mtume.

 

           ii.          Qayswar apeleleza ukweli wa Mtume.

           Ama Qayswar; mfalme wa Urumi, huyu alitaka kupata ukweli na uhakika wa Mtume. Akatuma mjumbe kumuitia kundi la wafanyabiashara wa Kiarabu waliokuja Shamu kufanya biashara, wakaletwa mbele ya mfalme. Na miongoni mwao alikuwemo Abu Sufyaan Ibn Harb na wakati huo alikuwa bado hajasilimu. Akaanza kumuuliza khabari za Mtume, nae Abu Sufyaan akimueleza kwa ukamilifu kila anachokijua juu ya Mtume. Baada ya usaili wake huo, ikambainikia kwamba Muhammad ni mtume wa Allah kweli, akaupondokea Uislamu. Na akawaelezea khabari ya Uislamu wakubwa wa Urumi wanao mzunguka katika baraza yake, akaona kwao uchukivu mkubwa. Nae akajifanya kama kwamba alikuwa anataka kutahini imani yao na upeo wa kushikamana kwao na dini yao. Na tunafikiri kwamba si vibaya iwapo tutakuletea mapokezi ya Bukhaariy juu ya mazungumzo ya Qayswar na Abu Sufyaan. Kwani ndani yake kuna sura ya wazi ya uchunguzi yakinifu na mfano mzuri kwa kila mwenye kutaka kujua haki na ilivyo ndivyo/sawa katika mambo makubwa yanayompitikia. Imepokewa kutoka kwa Abdullah Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-“Kwamba Abu Sufyaan Ibn Harb alimkhabarisha kwamba Hiraqli alimtumia ujumbe akiwa pamoja na msafara wakifanya biashara Shamu. (Hii ilikuwa ni) katika kile kipindi cha masitisho ya vita (kipindi cha suluhu ya Hudaybiyah) baina ya Mtume na Makureishi. Basi wakamuitika akiwa Eliyaa, akawaita katika baraza yake iliyokuwa imezungukwa na wakubwa wa Urumi. Akamuita mkalimani wake, akasema: Ni nani kati yenu aliye karibu kinasabu na huyu mtu anayedai utume? (Abu Sufyaan anasema) nikajibu: Mimi ndio niko karibu nae kinasabu kuliko wengine wote hapa. Akaagiza nisogezeeni karibu mtu huyo na wasogezeni wenzake wakae kwa kumpa mgongo. Halafu akamwambia mkalimani wake: Waambie mimi ninamuuliza maswali mwenzenu huyu, akiniongopea mkadhibisheni. (Abu Sufyaan) anasema: Lau kama si kuona haya kukadhibishwa basi ningemuongopea. Kisha swali la mwanzo aliloniuliza likawa: Ikoje nasabu yake kwenu? Nikajibu: Yeye kwetu ni mtu mwenye nasabu njema. Akauliza: Je, ulipata kuwepo ufalme kwa wahenga wake? Nikajibu: Hapana, akauliza: Je, kuna mtu alipata kusema haya (ayasemayo) kabla yake? Nikajibu: Hapana, akauliza: Je, ni watu watukufu ndio wamfuatao au ni watu dhaifu (masikini)? Nikajibu: Watu dhaifu, akauliza: Je, wanazidi au wanapungua? Nikajibu: Wanazidi, akauliza: Je, kuna ye yote anayetoka katika dini yake kwa kuichukia baada ya kuingia? Nikajibu: Hapana, akauliza: Je, mlipata kumtuhumu uwongo kabla hajasema ayasemayo sasa? Nikajibu: hapana, akauliza: Je, anafanya khiana? Nikajibu: Hapana, nasi tumepeana nae muda wa kusitisha vita, hatujui atafanya nini ndani yake. Akauliza: Je, mmewahi kupigana nae? Nikajibu: Naam, akauliza: Yalikuwaje mapigano yenu nae? Nikajibu: Vita baina yetu nae ni kupokezana, anatushinda nasi tunamshinda. Akauliza: Anakuamrisheni nini? Nikajibu: Anasema muabuduni Allah peke yake na wala msimshirikishe na cho chote na acheni itikadi ya baba zenu. Na anatuamrisha kuswali, kusema ukweli, kuacha zinaa na kuunga udugu.

Akamwambia mkalimani wake, mwambie: Nimekuuliza juu ya nasabu yake, ukasema yuna nasabu njema kwenu, na hivyo ndivyo mitume walivyo, hutumwa katika nasabu za kaumu zao. Na nikakuuliza: Je, kuna mtu alipata kusema haya (ayasemayo) kabla yake? Ukajibu hapana, nikajisemea: Lau angelikuwepo aliyemtangulia kuyasema hayo, ningelisema: Ni mtu anaye yaendeleza yaliyosemwa kabla yake. Nikakuuliza: Je, ulipata kuwepo ufalme kwa wahenga wake? Ukajibu hapana, nikajisemea: Lau ungelikuwepo ufalme kwa wahenga wake, ningelisema: Huyo ni mtu tu anayetaka ufalme wa baba zake. Nikakuuliza: Je, mlipata kumtuhumu uwongo kabla hajasema ayasemayo sasa? Ukajibu hapana, basi nikajua kwamba yeye hawezi kuacha kuwaongopea watu, halafu akamuongopea Mungu. Nikakuuliza: Je, ni watu watukufu ndio wamfuatao au madhaifu wao? Ukasema kwamba madhaifu ndio wamfuatao na hao ndio wafuasi wa mitume. Na nikakuuliza: Je, wanazidi au wanapungua? Ukasema kuwa wanazidi na hivyo ndivyo lilivyo suala la imani mpaka litimie. Na nikakuuliza: Je, kuna ye yote anayetoka katika dini yake kwa kuichukia baada ya kuingia? Ukasema hapana, na hivyo ndivyo imani ilivyo inapoziingia nyoyo. Na nikakuuliza: Je, anafanya khiana? Ukasema hapana, na hivyo ndivyo walivyo mitume, hawafanyi khiana. Na nikakuuliza: Anakuamrisheni nini? Ukasema anakuamrisheni kumuabudu Allah na wala msimshirikishe na cho chote na anakukatazeni kuabudu masanamu. Na anakuamrisheni swala, kusema ukweli na kutokuzini. Ikiwa haya uyasemayo ni kweli, basi mtu huyo atamiliki mahala hapa ilipokanyaga miguu yangu miwili hii nami nilkuwa najua kuwa atatokea. Na wala sikudhania kwamba atatoka kwenu (Waarabu), basi lau mimi ningelimfikia ningelijikalifisha kukutana nae. Na lau ningelikuwa mbele yake, ningeliiosha miguu yake.

Ama Al-Haarith Al-Ghasaaniy, huyu aliisoma barua ya Mtume, kisha akaitupilia mbali na akaazimia kwenda kumuua Mtume. Qayswar akamuandikia barua ya kwamba asithubutu kufanya hivyo. Ama mfalme wa Yamaamah, yeye akadhania kuwa ni suala la ufalme na sio utume, akawa na tamaa na kupata sehemu ya ufalme huu. Akamuandikia barua Mtume akimwambia: “Eeh uzuri ulioje wa unayoyalingania, basi nipe sehemu ya jambo hili nitakufuata”. Mtume alipoisoma barua yake akasema: “Lau angeliniomba tende mbichi iliyoanguka chini nisingelimpa”.

Hawa wafalme sita ndio ambao Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwapelekea ujumbe katika mwaka wa saba. Na katika mwaka wa nane, alimtuma Al-Araai Ibn Al-Hadhwramiy kupeleka waraka wake kwa  Al-Mundhir Ibn Saawaa; mfalme wa Bahrein, huyu akaupokea vema ujumbe na akasilimu. Na akamtuma Amrou Ibn Al-Aaswi kwa wafalme wa Oman, nao pia wakasilimu. Akamtuma Al-Muhaajir Ibn Abiy Umayah kwa Al-Haarith Al-Humeiriy; mfalme wa Sanaa, nae akasilimu. Na akawatuma Abu Mousa Al-Ash-ariy na Muaadh Ibn Jabal kwenda kuulingania Uislamu Yemen, wakasilimu wengi wa watu wa huko. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamuandikia waraka Jabalah Ibn Al-ayham; mfalme wa Ghasaan akimlingania Uislamu, akasilimu. Kisha akaja kuritadi katika zama za ukhalifa wa Sayyidina Umar Ibn Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi.

 



 | Tuandikie |