|
i.
Mtume kuwaandikia wafalme
wa nchi zinazomzunguka, ilikuwa ni dalili tosha juu ya kudhihiri kwa haki na
kushindwa kwa batili:
Pengine jambo
linalostaajabisha ni Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuwalingania
Uislamu wafalme hawa na ilhali Uislamu bado ni mchanga katika kisiwa cha
Waarabu. Na bado haujakuwa na mihimili ya nguvu na mamlaka ya kumuwezesha
kupambana na upinzani unaoweza kuonyeshwa na wafalme hawa wenye nguvu, utisho
na mamlaka. Lakini Mtume hakuyafikira yote hayo, yeye alikuwa na yakini ya
kutosha kwamba Allah Taala ataidhihirisha na kuipa ushindi dini yake na
ataliinua neno lake. Na kwamba hapana shala atamtekelezea ahadi ya nusra na
ushindi aliyompa na kwamba anachotakiwa yeye kukifanya ili Allah amtekelezee
ahadi yake ni kuufikisha ujumbe wake kwa watu wote kwa juhudi zake zote:
“...HAIKUWA JUU YAKO ILA NI KUFIKISHA (tu uliyoamrishwa)...” Ni kwa ajili hii
ndio Mtume-Rehema na Amani zimshukie-hakusita kuwandikia waraka wa ujumbe
wafalme hawa pamoja na ufalme mkubwa, mamlaka na nguvu walizokuwa nazo. Na
huenda pia aliuhisi ufadhaifu wa maswahaba wake katika kuitekeleza kazi hii
tukufu na msito wao katika kuziendea dola hizi zenye mali, nguvu na watu
wengi. Akawatokea siku moja na kuwaambia: “Kwa yakini Allah amenitumiliza kuwa
rehema kwa watu wote, basi nifikishieni (ujumbe wangu), Allah atakurehemuni.
Na wala msikhitilafiane nami kama wanafunzi walivyokhitilafiana na Issa mwana
wa Maryamu”. Wakauliza: “Ewe Mtume wa Allah, ikhtilafu yao ilikuwaje?”,
akawajibu: “Aliwaitia hili ninalo kuitieni nyinyi hivi sasa, basi ama yule
aliyemtuma eneo la karibu aliridhia na akasalimika (kufikwa na hukumu ya
kumkhalifu Mtume wa Allah). Ama yule aliyemtuma (kufikisha ujumbe) eneo la
mbali, akachukizwa na kujitia uzito (kama mfanyavyo nyinyi hivi sasa)”.
Mwachuoni Mulla Muhammad
Aliy-Allah amrehemu-anasema: “Yakini na imani ya Mtume ya kupata ushindi/nusra
haikutetereka na alikuwa na yakini thabiti kwamba Uislamu utaenea na kutawala
mpaka nuru yake itazagaza pande zote za ulimwengu. Pamoja na udhaifu wa
Uislamu kwa wakati huo, bado Mtume anawalingania kuingia katika dini yake
wafalme wenye nguvu. Hakuyafanya yote hayo ila ni yakini na imani yake juu ya
uwezo na nguvu zisizoshindika za Mola aliyemtuma kuifanya kazi hiyo. Hili ni
jawabu zuri kwa lile kundi la waislamu ambao wana mashaka juu ya kufanikiwa
kwa da’awah (wito/ujumbe) ya Uislamu katika ulimwengu wa Magharibi. Kwa hoja
kwamba leo Uislamu unahitajia nguvu za kidunia na himaya/dola kuu
litalalousaidia. Lakini hakika iliyo wazi ni kwamba Uislamu hauhitaji
kusaidiwa, kwani wenyewe ni nguvu itishayo isiyoshindika”.
ii.
Ukweli unaopasa
kuzingatiwa na waislamu:
Yawastahikia
mno waislamu hivi sasa kuuzingatia uhalisia huu wa mambo na hakika/kweli hii.
Kwamba ulimwengu wetu huu katika zama zetu hizi una kiu ya dini itakayo
mfikisha mkiu (mwenye kiu) kwenye kata-kiu halisi na baridi. Kwani nguvu za
kimaada zinazotakabari na kuufisidi ulimwengu katika zama zetu hizi,
hazitofautiana sana na nguvu-maada za ulimwengu ule ulipodhihiri Uislamu. Dola
kubwa za leo zinashabihiana na dola kubwa za enzi ya Mtume wa Allah; Urumi na
Uajemi. Kama zilivyo sambaratika katika muda wa mpepeso wa jicho mbele ya
nguvu za Uislamu. Basi hauko mbali wakati ambao Uislamu utapambana na Ulaya na
Amerika na madola yote hayo kusalimu amri na nguvu-maada zao kuporomoka. Kwani
dunia ni madola/nchi na historia hujirudia na zama ni mawimbi ya kiroho na
kimaada na ya imani na ukafiri yenye kufuatana. Huenda pengine hili wimbi la
mwamko na muasho linalosambaa kwa kasi ya moto nyikani katika ulimwengu wa
Kiislamu. Ni bishara njema kwamba wimbi la imani limeshaanza
kudhihiri/kuchomoza na kwamba wimbi la ustaarabu-maada lililoughuri ulimwengu
kwa zama kadhaa. Umefika wakati wake wa kuondoka na kutoa nafasi kwa wimbi la
imani kutawala: “...NA SIKU ZA NAMNA HII TUNAWALETEA WATU KWA ZAMU...” [3:140]
|